Kitanzi, Kisu au Bastola - 11

ILIPOISHIA :
“Madam Flaviana, amekuja kunifuata mimi au?” alijiuliza Salima kwa shauku kwani zilikuwa zimepita siku nyingi bila kuonana naye.
ENDELEA…
Salima aliingia ndani na kusimama kwa furaha baada ya kumuona Madam Flaviana pembeni ya Madam Bernadeta.
Moyoni aliamini Madam Flaviana atakuwa na habari mpya kuhusu mpenzi wake, Dedan. Akahisi huenda atakuwa amepatikana.
“Caro, nina habari nzuri na mbaya, ipi nianze kukwambia kwanza?” Madam Flaviana alimuuliza Salima bila uso wake kuonesha alama yoyote ya furaha.
“Aaah…anza na habari njema kwanza,” Salima aliongea kwa wasiwasi hasa baada ya kumsikia Madam Flaviana naye akimuita kwa jina la ‘Caro’ na si Salima kama ilivyokuwa zamani.
Kauli ya habari nzuri na mbaya ilizidi kumtia hofu Salima.
“Baada ya wiki mbili kutoka sasa, kuna ugeni kutoka Uarabuni utafika nchini kwa ziara binafsi ya kibiashara na kampuni yetu. Kwa niaba ya ‘Serenity’ tumekuchagua wewe kuwa mwenyeji wao kipindi chote watakapokuwa katika ziara yao… Hongera sana Caro,” alisema Madam Flaviana akirudia tena kutumia jina hilo Caro badala ya lile la Salima, akaachia tabasamu pana huku Madam Bernadeta na Julieth wakimpigia makofi.
Kipindi chote hicho Salima alitulia kimya, maswali mengi kuhusu uhusika wake kwenye hiyo ziara yalitawala akilini mwake huku akishangazwa kwa jinsi gani hiyo ilikuwa habari nzuri!
“Usiwe na wasiwasi hautakuwa peke yako. Kipindi chote utakuwa na shoga yako Julieth. Mwenzako ana uzoefu sana,” Madam Flaviana alisema huku akimwangalia Julieth ambaye alikuwa amesimama nyuma ya Salima huku uso wake ukiwa umejikunja kwa kutajwa kama msindikizaji wa Salima.
“Na habari mbaya ni ipi?” Salima aliuliza kwa hofu akimtazama Madam Flaviana machoni kana kwamba alitegemea kusoma macho yake zaidi ya kusikiliza.
“Jamani naomba mtupishe,” aliongea Madam Flaviana, mara moja Julieth na Madam Bernadeta wakatoka nje na kumuacha yeye (Madam) na Salima.
Madam Flaviana alijua fika kuwa lazima abuni uongo mpya ambao Salima hatoweza kuugundua kwa haraka kwa kuwa, awali yeye ndiye aliyemdanganya Salima kwamba Dedan alikuwa amechukuliwa na Caro jambo ambalo halikuwa sahihi.
Mbaya zaidi Salima alishaongea na Caro mwenyewe, kwa hiyo isingekuwa rahisi kumdanganya Salima kuwa Dedan bado alikuwa kwa Caro.
“Habari mpya ni kuhusu Dedan,” alianza kuongea Madam Flaviana kwa umakini mkubwa.
“Dedan! Vipi amepatikana?” Salima alijikuta akiuliza kwa hofu kwani tayari kichwani mwake alishajiwekea kuwa hiyo ndiyo habari mbaya kama alivyotahadharishwa.
“Ndiyo amepatikana na ni mzima wa afya, lakini…”Madam Flaviana alinyamaza kidogo na kumtazama Salima kwa kuibia akitarajia kumuona akiwa ameanza kuchanganyikiwa jambo ambalo lilikuwa sahihi.
“Siku zote tulizodhania alikuwa kwa Caro kumbe alikuwa na mwanamke mwingine anayeitwa Sonia. Kibaya zaidi ni kwamba, Sonia ndiye mke wake wa ndoa na wana watoto wawili siku nyingi.
“Kwa kifupi Dedan alikuwa na uhusiano na wanawake wawili, ambao mmoja tu ndiye uliyemtambua, yaani Caro.” alisema Madam Flaviana kwa umakini mkubwa ili asije kukosea.
Siku zote msema uongo hupaswa kuwa na kumbukumbu nzuri ili asije akajisahau na kuchanya madawa. Kwa hilo, Madam Flaviana alijipanga kutofanya makosa kwani alishakariri kila neno alilopanga kumwambia Salima na kuhakikisha analirudiarudia kabla ya kukutana na Salima siku hiyo.
“Sina haja ya huyo mkewe wala watoto wake, Dedan yupo wapi?” Salima aliuliza kwa hasira kidogo kwani alishaanza kuhisi kuumizwa na kila neno ambalo Madam Flaviana alikuwa akiliongea kuhusu Dedan.
“Ubaya ni kwamba mimi mwenyewe nilijitahidi kumtaka Dedan angalau aongee na wewe yeye mwenyewe, lakini alikataa na kusema kuwa hakufahamu na mbaya zaidi amenipa ujumbe huu akitegemea kuwa baada ya kuusoma, hautamsumbua tena,” aliongea Madam Flaviana huku akimkabidhi Salima bahasha ndogo.
***
Baada ya kushinda siku nzima ya jana yake wakiwa na uchovu uliopindukia, siku hiyo waliamka wakiwa na nguvu kama kawaida. Kwa mara ya kwanza Sonia naye alianza kuhisi maumivu shingoni mwake, akajua kwamba Madam Flaviana hakutania kuhusu kuwawekea vipandikizi ndani ya miili yao.
Akageuka na kumtazama msichana aliyejitambulisha kwa jina la Caro na kumuongelesha.
“Caro, unamfahamu Dedan?” aliuliza Sonia kimasihara baada ya kuhisi huenda Caro aliyewahi kusimuliwa na Side alikuwa ndiye huyo.
“Ndiyo namfahamu. Nafahamu pia kuhusu Salima msichana aliyekuwa akiishi naye baada ya wewe kumsababishia Dedan matatizo.”
“Jamani Dedan wangu ana matatizo gani! Yupo wapi?” alinong’ona Caro kwa simanzi kubwa huku machozi yakianza kumtiririka.
“Tulitekwa wote na kuletwa hapa, lakini sijui amewekwa sehemu gani!”
“Unataka kusema Dedan yupo hapa Serenity! Alipatwa na matatizo gani?”
“Kwani wewe hujui? Nimeambiwa alikuwa zezeta, lakini alipona akiwa kwa huyo Salima ambaye naye nimesikia ameletwa hapa Serenity kama msichana wa kuuzwa.”
“Unasemaje! Dedan alikuwa zezeta?” alihoji Caro huku machozi yakimtiririka kwa kasi, safari hii yakifika hadi mashavuni mwake. Hakutegemea kama Dedan angefikia hali hiyo baada ya kummwaga enzi zile.
Akakosa hoja na kubaki akijilaumu kwa yote aliyomfanyia Dedan, hata hivyo alitamani kupata nafasi ili amuombe msamaha kwa kitendo alichomfanyia na kuamini angesamehewa kwani alijua alikuwa na sababu ya msingi ya kufanya vile.
***
“Umefanya kazi nzuri sana Madam,” Mr. Chakos alimpongeza Madam Flaviana huku akimmiminia ‘wine’ kwenye glasi yake.
“So nini kinafuata?” aliongea Madam Flaviana huku akiipokea glasi kutoka kwa Mr. Chakos na kuonja kidogo.
“Njoo uangalie, nilichokigundua,” Mr. Chakos alimvuta Madam Flaviana mpaka upande wenye kompyuta moja kubwa na kuicheza video aliyorekodi muda mfupi uliopita. Kwenye video ile, Salima alionekana akitembea kwenye korido huku macho yake yakiziangalia kamera zilizotegwa kwenye dari kana kwamba alikuwa akifahamu uwepo wa vifaa hivyo.
“Angalia na hii,” Chakos alibofya ‘kipanya’ cha kompyuta yake na kuicheza video nyingine ambapo ndani yake walionekana Caro na Sonia wakiongea kwa kunong’ona kana kwamba walikuwa wakijua uwepo wa kinasa sauti ndani ya chumba chao.
“Dirty bitch (mbwa jike mchafu)! Lazima Caro alimwambia Salima kuhusu jambo hili, si unakumbuka siku ile Caro ndiye aliyeongea naye mara ya mwisho kwenye simu?” alifoka Madam Flaviana.
***
Ndani ya chumba chake, Salima alikuwa amejifungia kimya akitafakari jinsi gani Dedan aliweza kufanya mambo hayo yote kwa muda mfupi. Ujumbe aliopewa ulijieleza vizuri kama Madam Flaviana alivyomwambia, lakini hakuamini moja kwa moja kama maneno hayo yaliandikwa na Dedan mwenyewe.
Akiwa na hasira zilizochanganyika na wivu, Salima alifikiria jambo moja tu ambalo ni kuondoka ndani ya jengo la Serenity na kuhakikisha anamsaka Dedan popote alipo ili angalau amsikie akitamka maneno hayo kwa kinywa chake mwenyewe.
Akasimama na kuweka nguo zake kwenye begi bila kujali kamera iliyokuwa ikimmulika.
Baada ya kumaliza zoezi hilo, akafungua mlango wa chumba chake na kuanza kutembea kwa kujiamini akielekea kwenye korido na hatimaye kuteremka kwa lifti mpaka chini na kufika nje.
Akavuka vizingiti vyote na kutembea kuelekea kwenye geti kubwa lililotenganisha ulimwengu wa nje na mle ndani.
Kwa hasira alizokuwanazo, hakujali chochote, akazidi kukaribia geti hilo, lakini ghafla kitu mfano wa sindano kikamchoma mgongoni, Salima akajikuta akilegea ghafla na kudondoka chini kama mzigo, ‘puuh’.
***
Kufanya kazi kwa bidii ndiyo sababu iliyomfanya Mkuu wa Upelelezi amkabidhi kesi ile Afande John. Alijua baada ya siku chache watuhumiwa watakuwa wamepatikana kwa kuwa alimuamini sana kijana wake huyo tofauti na maaskari wengine.
Bila hiyana, Afande John naye alilichukua jukumu hilo na kuanza kulifanyia kazi ambapo kwa muda mfupi tu alifanikiwa kupata taarifa za watu wawili ambao ni: Henry ‘Ze Deader’ yaani yule muuaji wa Side, na mtu mwingine ambaye alionekana mara moja tu akiwa na marehemu, wakimaanisha Dedan.
Kwa maelezo ya watu wachache aliowafanyia mahojiano, Afande John alifanikiwa kufika hadi kwenye kichaka ambacho awali alifungiwa Dedan na Sonia na kugundua kamba zikinin’ginia kwenye magome ya miti miwili. Baada ya kuchunguza, aligundua kuwa mahali hapo watu wawili walikuwa wamefungwa kabla ya kuhamishwa ama kutorokea sehemu nyingine.
Kama kawaida yake, Afande John akatoa kitabu chake na kuchora michoro aliyoifahamu yeye mwenyewe.
Ghafla wazo likamjia. Kwa kasi ya ajabu akairukia pikipiki yake na kuiwasha kana kwamba alikuwa akiwahi jambo fulani alilolikumbuka. Akiwa njiani, aliiacha barabara ya lami na kuingia ya vumbi ambayo haikuwa ikielekea sehemu yoyote nyingine zaidi ya kwenye jengo moja kubwa la ghorofa lenye fensi ya ukuta mrefu kupindukia.
Akasimamisha pikipiki yake na kuificha mita chache karibu na jengo lile. Akaitoa mfukoni ile kadi aliyoichomoa kwa yule mhalifu aliyekurupushana naye usiku wa jana yake na kujaribu kuifananisha na alama iliyopo kwenye kadi hiyo na ile aliyoiona kwenye lile geti. Akaitazama na kubaini kuwa alama zile zinafanana.
“Kumbe herufi ‘s’ ni kifupi cha neno ‘Serenity’!” Afande John alistaajabu kimoyomoyo. Moja kwa moja akatambua kuwa kwa vyovyote yule mtu aliyekurupushana naye alikuwa akifanya kazi ndani ya jengo hilo. Kwa kutumia simu yake ya kisasa akaandika neno ‘Serenity’ akidhamiria kutafuta maana yake kwenye mitandao akiamini huko atapata maelezo sahihi kuhusu kampuni hiyo na shughuli zake.
Baada sekunde chache za kuperuzi kwenye kurasa za ‘google,’ alibaini kuwa jengo hilo lilijihusisha na masuala ya kukuza vipaji vya urembo na lina matawi mengi duniani.
Alipojaribu kuchimba zaidi kuhusu watu wanaoiendesha kampuni hiyo, kurasa ziligoma kufunguka na kuhitaji anuani ya barua pepe na ‘pasiwedi’ ili kuweza kufunguka.
“Kwani kuna siri gani humu!” alijisemea Afande John huku akiingiza anuani yake ya barua pepe na ‘pasiwedi’ akijaribu kama kurasa hizo zingefunguka.
Taratibu kurasa mpya ilianza kufunguka kwenye simu yake huku zikionekana baadhi ya picha za wasichana kadhaa warembo wakiwa katika pozi tofauti. ‘Akazidownload’ haraka picha hizo na kuzihifadhi ndani ya simu yake, lakini zaidi ya hapo hakufanikiwa kupata kitu chochote ndani ya kurasa hizo, aliona maandishi mekundu yaliyosomeka: MEMBERS ONLY (Wanachama pekee)!
Baada ya jitihada za kuzifungua kurasa zile kugonga mwamba, Afande John aliketi hapo kwa muda kidogo akiangaza kila kona ya jengo hilo lililokuwa kimya sana.
Kwa kujificha akapiga picha chache na kupotea eneo hilo moyoni akiweka azma ya kufuatilia zaidi namna kampuni hiyo inavyoendeshwa.
***
Salima akiwa hajielewi alibebwa na kukokotwa na mabaunsa walioonekana kujizatiti katika kazi yao. Wakapita naye karibu kabisa na mahali walipofungiwa akina Sonia.
Moja kwa moja wakambwaga juu ya kitanda cha chumba ambacho ndani yake walionekana Madam Flaviana na mzee mmoja wa Kizungu aliyejulikana kwa jina la Dr. Church kisha wakaondoka.
Haraka Dr. Church alifungua begi lake na kuchukua sindano, kisha akaifyonza dawa iliyokuwa ndani ya chupa moja wapo na kumchoma Salima kwenye mshipa wa kiganja chake na kutulia kwa muda.
“Itasaidia kweli?” aliuliza Madam Flaviana ambaye kipindi chote hicho alikuwa kimya akimwangalia Dr. Church alipokuwa akifanya vitu vyake.
“Hii ni moja kati ya dawa zangu chache zilizonigharimu sana katika ugunduzi wake, nimeipa jina la ‘Ecstacy 33’ kutokana na uwezo wake wa kumfanya mtu asahau mambo yote ya awali na kukubali kila kitu atakachoamrishwa kufanya. Sibahatishi katika hili, kama utakuwa tayari tutamjaribu mtu wako baada ya saa moja.” alisema Dr. Church kwa kujiamini tena kwa Kiswahili fasaha.
Kwa maelezo yake, dawa hiyo aliigundua kwa kutumia dawa za kulevya aina ya ‘Ecstasy’ ambayo ina uwezo wa kumfanya mtu asahau mambo na kumchangamsha saa zote.
Dr. Church alichoweza kukifanya ni kuiweka dawa hiyo katika kiwango sahihi cha dozi huku akiichanganya na kemikali nyingine zilizokuwa na uwezo wa kumfanya mtu kuwa katika hali hiyo kwa muda mrefu tofauti na ‘ecstasy’ ya kawaida.
Kwa hiyo, baada ya muda mfupi ujao, dawa hiyo ingeweza kumfanya Salima amsahau Dedan na kukubali kufanya kila kitu atakachotumwa na Madam Flaviana hasa wakilenga kufanikisha kumtumia katika ziara ya Prince Khalfani kutoka Falme za Kiarabu.
***
“Caro, kwa nini kila mara ukiongea unataka tuzungumze kwa sauti ya chini kwani kuna nini?” aliuliza Sonia kwa kunong’ona baada ya kila mara kuzuiwa na Caro kuongea kwa sauti ya kawaida.
“Shh! kuna vinasa sauti na kamera ndani ya jengo zima,” alijibu Caro bila kumtazama Sonia.
Bado moyo wake ulikuwa na donge zito kwa aliyoyasikia muda mfupi kuhusu Dedan. Ghafla wakasikia vishindo vya watu vikipita karibu na chumba walichomo, kwa sauti za hatua zao Caro aligundua mara moja kuwa watu hao walikuwa wakielekea upande wao, jambo ambalo lilikuwa sahihi. Kufumba na kufumbua wanaume watatu wenye miraba minne waliingia ndani ya chumba hicho. Kwa uoga Sonia alijikuta akimkumbatia Carolina.
“Tufuateni mara moja!” alitoa amri mmoja wa wanaume hao aliyeonekana kama kiongozi wao.
Bila kukaidi, Caro alisimama na kuanza kutembea akiwafuata watu wale huku Sonia naye akifuatia kwa nyuma kama vile mbwa amfuatavyo chatu hali akijua hatoweza kupona.
INAENDELEA
Post a Comment