PLUIJM AKATAA KUSAINI YANGA
UONGOZI wa Yanga umeamua kumrejesha kikosini kocha aliyewapa mafanikio kwa muda mfupi, Mholanzi, Hans van der Pluijm ambaye inadaiwa ataanza kazi rasmi Jumatatu wiki ijayo baada ya kumfungashia virago Mbrazili, Marcio Maximo.
Wakati Yanga wakifikia maamuzi hayo, habari za ndani, zinadai kuwa Pluijm amekataa kusaini mkataba mpaka kwanza uongozi umalizane na Maximo. Mholanzi huyo pia amezungumza juu ya taarifa ya bifu kati yake na kiungo wa timu hiyo, Haruna Niyonzima.
Taarifa za ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa baada ya kuzungumza naye juu ya kumkabidhi timu, kocha huyo amesisitiza kutosaini mpaka kwanza Yanga imalizane na Maximo kila kitu kisha yeye ndiye atasaini na kuanza kazi.
“Wameshazungumza kila kitu na uongozi na wamekubaliana, nafikiri watampa mkataba wa miaka miwili, ndivyo wamekubaliana, lakini tatizo bado ni moja tu juu ya sharti la kuwataka wamalizane na Maximo,” alisema mtoa taarifa na kuongeza:
“Hataki kujiingiza kwenye mgogoro wa kimaslahi, nafikiri kama Yanga wakikamilisha kila kitu ataanza kazi Jumatatu ijayo.”Alipoulizwa juu ya taarifa hizo, Pluijm aligoma kuzungumzia suala hilo na kutaka mwandishi awasiliane na uongozi.
“Ni kweli bado sijasaini, viongozi wameamua kwanza wamalizane na kocha (Maximo) kisha ndiyo nisaini. Nadhani kati ya leo (jana) ama kesho (leo) tutakutana kwa ajili ya kumalizana,” alisema.
CHANZO: GPL
Post a Comment