YAYA TOURE MPYA WA YANGA EMERSON DE OLIVEIRA ATUA BONGO
Emerson akiwa na Meneja wa Yanga SC, Hafidh Saleh kulia baada ya kuwasili JNIA leo
YANGA imeamua kuachana na mshambuliaji Geilson Santana ‘Jaja’ aliyeamua kubaki nchini kwao Brazil, lakini inaziba pengo kwa kumsajili kiungo Emerson De Oliveira Roque.Uongozi wa Yanga umethibitisha ujio wake, kupitia Katibu Mkuu, Beno Njovu, ukaeleza kuwa Emerson anakuja kufanya majaribio lakini kwa kiwango chake, kupitia mechi mbalimbali zilizorekodiwa kwenye video moja, Mbrazili huyo mwenye sifa saba zinazofanana na kiungo Yaya Toure wa Manchester City ya England, lazima atasajiliwa na Yanga.
Ujio wa Emerson ambaye anatua leo mchana akitokea Bonscusessco FC ya Brazil, umekuwa gumzo, wengi wakitaka kujua atafanya nini baada ya Jaja ‘kuachia’ basi njiani.Emerson ni mchezaji asiye na papara, karibu kila mpira anaopokea anautuliza na anapenda kufanya mambo kwa uhakika.
Kiungo huyo, ana sifa saba zinazofanana na za Yaya Toure ambazo ni kumiliki mpira, kupiga pasi fupi, kupiga pasi ndefu, kuokoa mipira kwa kulala ‘takolin’ na uwezo mkubwa wa kuokoa kwa kupiga kichwa, usisahau pia ni mzuri kwa mabao kwa kichwa.
Pasi:
Hapa ana sifa mbili, moja ni kupiga pasi fupi na ndefu za chinichini kwa uhakika kama ambavyo umekuwa ukimuona Yaya Toure.Ukiangalia video hiyo ya ‘action zake’, utaona anavyotelezesha mipira, kwa pasi za chini za karibu na mbali. Sifa ya pili, anapiga zile pasi ndefu za juu na kweli zinafika.
Takolin:
Hapa ndiyo utampenda, ukiweka mguu, yeye anaweka mguu na nguvu alizonazo amekuwa akiiwahi mipira kwa kulala, anaokoa.
Nguvu:
Emerson ana nguvu za miguu, hivyo kumfanya awe bora katika ukabaji, iwe isiwe, Mbuyu Twite atalazimika kumpisha kwenye nafasi hiyo.
Vichwa:
Ukiangalia video hiyo, utaona ndiye mchezaji anayepiga vichwa vingi vya kuokoa kwenye timu yake. Hivyo mipira mingi inayokwenda langoni mwake anaitoa.
Mabao:
Ndiyo, Emerson anafunga mabao hasa kwenye mipira ya adhabu inayochongwa langoni au kona. Uwezo wake ni kufunga kwa kichwa na amekuwa akifanya hivyo.
Mipira ‘iliyokufa’:
Maximo atalazimika kumpa nafasi, ili agawane na Coutinho namna ya kupiga mipira ya adhabu ndogo maarufu kama ‘mipira iliyokufa’. Ana uwezo wa kufunga kama ambavyo umekuwa ukimuona Yaya.

Post a Comment