ad

ad

USIFE KWANZA MPENZI WANGU - 06

ILIPOISHIA
Jioni Levina aliwahi sana kurudi nyumbani, akamkuta mama yake sebuleni, baada ya kumsalimia akamwambia...
“Mama nilipata sms yako ya mchana, nimeanza kuifanyia kazi, ndani ya siku tatu tutapata mtu mwingine.”

“Oh! Usijali binti yangu, ameshapatikana kijana mwingine kutoka Bagamoyo, atakuja kuanza kazi kesho.”
Uso wa Levina ukasawagika kwa huzuni.
Sasa endelea...

KWA sekunde kumi na tano, Levina alikuwa ameganda akimwangalia mama yake, ni kama hakusikia vyema maneno yale, hata kama aliyasikia vizuri lakini yalionekana kuwa magumu sana kupenyeza kwenye ngoma za masikio yake.

Anamwangalia mama yake kwa macho yanayozungumza jambo fulani, ingawa haijulikani moja kwa moja kuwa anazungumza nini. Mama yake aliweza kugundua tofauti aliyonayo mwanaye haraka sana.

“Vipi Levina mwanangu, mbona kama hujafurahia?”
“Siyo hivyo mama?”
“Bali nini tena?”
“Nimeshangaa, maana tayari nilishaanza taratibu za kumpata huyo mtu.”

“Kwani umeshampata?”
“Kuna dada mmoja ameniambia kwamba jioni ya leo atakwenda kuzungumza naye. Yupo kaka mmoja amesema anaishi Mburahati, kwahiyo akionana naye atajaribu kumweleza.”
“Ni mfanyakazi au yupo tu, nyumbani?”

“Anafanya kazi!”
“Sasa atawezaje kutoka?”
“Kasema atamshawishi, maana hata pale halipwi mshahara mkubwa, lakini pia atamwambia mazingira ya kazi ni mazuri.”
“Sawa, ngoja tuone.”


“Na huyo mwingine uliyesema?”
“Huyo kila kitu kipo tayari, nimeshafanya naye mawasiliano na tumekubaliana aje kesho!”
“Sasa itakuwaje? Maana sitaki kuonekana mwongo kwa rafiki yangu.”

“Kesho tutapata majibu kamili, kama akija huyo wa Bagamoyo sawa, asipokuja basi utanijulisha makubaliano ya huyo kijana mwingine atakayezungumza na rafiki yako leo usiku.”
“Sawa mama, mimi nipo ndani,” akasema Levina.
“Sawa mama.”

Levina akajikongoja mpaka ndani akionekana kuwa na uchangamfu kidogo, bado alikuwa akiomba sana huyo kijana wa Bagamoyo asitokee ili Deo apate nafasi ya kuingia kwao.
“Itawezekana tu, maadamu moyo wangu umempenda, naamini itakuwa hivyo,” akawaza Levina.

Baada ya kubadili nguo, aliingia bafuni kuoga, alipotoka alionekana kuwa na nguvu kidogo, akachukua simu na kumpigia Deo.
“Uko wapi?”
“Nipo njiani naelekea nyumbani.”

“Umefika wapi sasa hivi?”
“Ndiyo nakaribia kushuka Mwembechai!”
“Ok! ukishuka naomba unisubiri!”
“Kwani wewe uko wapi?”
“Nipo home, lakini natoka sasa hivi nachukua taxi nakuja.”

“Basi jitahidi ufanye haraka!”
“Usijali, sina muda mrefu sana nitakuwa hapo.”
“Poa.”
Levina akabadili nguo haraka na kutoka. Alipopita sebuleni alimkuta mama yake akiwa amekaa pale pale!

“Haya wapi tena?”
“Natoka kidogo mama!”
“Ila saa hizi ni usiku na baba yako hapendi kabisa utoke usiku.”
“Mama siendi mbali, nakwenda hapo Mwembechai mara moja.”
“Unatoka na gari?”

“Hapana, sitaki baba ajue nimeenda mbali kama akirudi mapema, ni bora alione gari atajua nipo jirani!”
“Kumbe hutakuwa jirani siyo?”
“Mama...!!! Mwembechai si mbali, lakini ni mbali pia mama. Kwa baba kule ni mbali!”

Mama Levina akacheka.
“Uwahi kurudi,” akasema mama Levina akiendelea kutabasamu.
“Nakuahidi mama.”
Levina akaondoka zake.

***
Levina alifurahi sana kukutana na Deo, moyo wake ulikuwa ukisisimka sana kila alipokutanisha macho yake na Deogratius.
Alikuwa mwanaume pekee ambaye aliweza kuutetemesha moyo wake.
“Nina habari njema Deo!”
“Juu ya nini?”

“Unakumbuka mara ya mwisho nilizungumza nini na wewe?”
“Ndiyo, nakumbuka vizuri sana.”
“Ilikuwa ni nini?”
“Kuhusu kazi nyingine!”
“Halafu?”
“Kusoma.”

“Safi sana, kumbe unakumbuka vizuri sana, sasa tunaanza na kimoja baada ya kingine. Kama nilivyokuambia sisi ni marafiki na nitakuwa tayari kutumia kila njia nihakikishe nakufurahisha!”
”Nimefurahi kusikia hivyo.”
“Nimekupatia kazi, tena nyumbani kwetu kabisa.”

“Unasema kweli?” Deo akauliza akiwa haamini kabisa alichoambiwa na Levina.
“Kwanini isiwe kweli?” Levina akauliza akitabasamu.

Tabasamu lililomchoma Deo moyoni, kwa mara ya kwanza alikiri kumuona Levina akiwa ameachia tabasamu zuri zaidi kuliko siku zote!
Uzuri wa Levina ukawa hadharani!
DEOGRATIUS akagundua kitu kipya kabisa kutoka kwa Levina, aligundua kwamba alikuwa msichana mzuri kupindukia! Tabasamu lake lililoacha sehemu kubwa ya meno yake nje, lilisababisha aone vijishimo vidogo mashavuni mwake na hivyo kuzidisha urembo wake.

Alihisi moyo wake kama umepigwa na shoti ya umeme, alikuwa amesimama mbele ya mwanamke mrembo sana tofauti na matarajio yake. Levina alikuwa mzuri zaidi ya alivyofikiria.
Kwanini anamsaidia sana?

Kwanini anakuwa naye karibu sana? Hayo yaliendelea kuwa maswali ambayo hayakuwa na majibu ya moja kwa moja kichwani mwake. Alibaki ameganda akimwangalia Levina ambaye sasa aliamua kucheka kabisa. Furaha ya Levina ilikuwa ni kuona jinsi Deo anavyomkubali yeye.

Hakujali umasikini wake, alichojua yeye ni mapenzi tu. Moyo wake ulianguka kwake, alitamani sana awe mpenzi wake wa dhati ndani ya moyo wake.

“Deo!” Levina akaita kwa sauti tamu sana.
“Naam!”
“Vipi?”
“Poa.”

Levina akacheka.
“Mbona unanicheka?”
“Sijakucheka Deo!”
“Bali!”

“Nimecheka. Unajua kuna tofauti kubwa sana kati ya kucheka na kumcheka mtu. Mimi nimecheka, sijakucheka. Umeona tofauti hiyo?”
“Haya mama wa Kiswahili, siwezi kushindana na wewe, hapo umenishinda.”
“Enhee stori nyingine?”

“Sina!”
“Basi poa, acha mimi nirudi zangu home, si unajua tena dingi hajaingia, sasa akija na kunikuta sijafika nyumbani mpaka saa hizi haitakuwa sawa!”

“Sawa basi. Enhee niambie, naanza lini kazi?”
“Una hamu eeh!”

“Sasa kumbe ningefanyaje?”
“Subiri kidogo, mpaka kesho nitakupa jibu kamili la lini utaanza kazi rasmi.”

“Sawa.”
“Usiku mwema.”
“Nawe pia!”

Deo akaondoka, Levina akaendelea kumkazia macho mpaka alipoondoka. Baada ya hapo akavuka upande wa pili, akachukua taxi nyingine na kurudi zake nyumbani. Kwa bahati nzuri, baba yake alikuwa bado hajafika nyumbani.
“Una bahati, baba yako hajafika!”

“Acha tu mama!”
“Enhee vipi, mambo yanaendaje?”
“Huyo kijana yupo mama, hata kesho anaweza kuja!”

“Sawa basi, lakini naomba tusubiri hadi kesho, kama yule wa Bagamoyo hatakuja basi atakuja huyo, unajua tayari nilishamuahidi na huyo mtu alimuhangaikia sana!”
“Sawa mama,” Levina akasema kwa sauti ya chini lakini ndani ya moyo wake akiumia sana.

Alitamani sana huyo kijana asitokee ili Deo wake aweze kwenda nyumbani kwao. Hiyo ilikuwa dua yake kubwa.
“Mimi naingia chumbani mama.”

“Sawa, bado nipo hapa naendelea kuangalia taarifa ya habari.”
Muda mfupi baada ya Levina kuingia chumbani kwake, simu ya Mama yake ikaita. Namba hakuzijua, lakini mara moja akapokea!
“Nani mwenzangu?” Ndiyo neno la kwanza mama Levina kutamka mara baada ya kupokea simu.

“Mama Happy wa Bagamoyo...samahani mama Levina, nimekupigia na namba ya kibandani, simu yangu haina chaji!”
“Usijali, vipi za huko?”
“Bwana wangu, si salama.”

“Kuna nini tena?”
“Yule kijana amefiwa na mama yake, kwahiyo anatakiwa kwenda kwao Morogoro kesho, kurudi ni baada ya wiki mbili!”
“Duh!”

“Ndiyo mwenzangu, matatizo yamemfika kijana wa watu, kwa jinsi alivyokuwa na hamu na hiyo kazi, yaani amechanganyikiwa kabisa!”
“Poleni mwaya, umpe pole na yeye, hakuna jinsi, maana nilikuwa na shida ya haraka sana na kijana wa kazi, sasa nalazimika kutafuta mwingine.”

“Hakuna shida, haikuwa riziki yake!”
Wakakata simu zao. Muda ule ule mama Levina akamwita binti yake, ambaye alifika baada ya muda mfupi sana.

“Levina nimepigiwa simu na Happy sasa hivi, yule kijana amepatwa na matatizo. Amefiwa na mama yake, kwahiyo hataweza tena kuja labda mpaka baada ya wiki mbili, nimemwambia mama Happy kwakuwa nina haraka, nalazimika kutafuta mwingine kwahiyo basi zungumza na huyo rafiki yako, yule kijana aje kesho aanze kazi mara moja!”

“Sawa,” Levina akajibu kwa sauti ya chini sana, akionekana kuwa na huzuni lakini ndani ya moyo wake alikuwa akishangilia kwamba Deo wake alikuwa anakwenda kuwa karibu naye.

****
Levina alivyoingia tu chumbani kwake, kitu cha kwanza ilikuwa kuchukua simu yake na kumpigia Deo haraka sana.
“Vipi?”

“Habari njema zaidi ya zile za saa ile!”
“Zipi tena Levina?”
“Unatakiwa kuanza kazi kesho, vipi utaweza?”
“Nitaweza!”
“Kweli?”

“Kweli kabisa.”
“Basi fanya juu chini, kesho tukutane saa 3:00 asubuhi!”
“Sawa.”
Wakaagana.

****
Kama walivyokubaliana, siku iliyofuata walikutana Mwembechai, Deo akiwa na begi lake, tayari alikuwa ameshaacha kazi alipokuwa akifanya mwanzoni na akawa tayari kwenda kuanza kazi kwa akina Levina.

Wakaingia sebuleni na kukutana na mama yake Levina akiwa anamsubiria kwa hamu...

“Karibu mwanangu!” Mama Levina akamwambia Deo.
“Ahsante mama!”
“Jisikie uko nyumbani!”

“Ahsante mama.”
“Nina imani maelekezo yote umeshapewa na Levina, kama bado atakupa. Acha mimi niwahi kazini, nawatakieni siku njema,” akasema mama Levina akisimama na kupiga hatua za kuondoka.

“Ahsante!” Deo akajibu akiona haya.
Mama Levina akaondoka zake, akawaacha Deo na Levina tu nyumbani. Levina aliposikia muungurumo wa gari la mama yake nje, akajua tayari ameshaondoka. Akamkazia macho Deo, aliyekuwa amesimama kama mlingoti!

Mara ghafla akamsogelea na kumkumbatia kwa nguvu! Kilikuwa kitendo cha haraka na ghafla sana, kilichomshtua sana Deo. Akabaki ameduwaa akimwangalia bila majibu!
Je, nini kitatokea? Usikose kufuatilia Jumatatu

No comments

Powered by Blogger.