USIFE KWANZA MPENZI WANGU - 05
Like: www.facebook.com/2jiachie
Web: www.2jiachie.com
Mpango wa kumtoa Rashid nyumbani kwao unaendelea, nia hasa ya Levina ni kumwingiza Deo nyumbani kwao.
Lakini moyoni aliumia sana, maana machozi ya Rashid yalikuwa yanamuuma sana!
Ni kweli alimsingizia. Nini kitatokea? Endelea kuisoma...
LEVINA aliumia ndani kwa ndani, alikiri kabisa kwamba Rashid hakuwa anahusika na chochote katika mchezo ule. Kitu pekee kilichomsukuma kufanya vile ni mapenzi yake ya dhati pekee, hakuwa na kitu kingine ndani yake zaidi ya hivyo.
Tangu Rashid alipoondoka kwenda chumbani kwake kukusanya mizigo yake, alijisikia mkosaji sana.
Mwenye roho mbaya sana!
Alijihisi kama si binadamu kabisa!
Sifa zote mbaya akajipa yeye!
Mama yake aliweza kugundua tofauti aliyokuwa nayo mwanaye, akaona njia pekee ya kugundua kilichokuwa kikimtatiza mwanaye ni kumuuliza tu!
“Nini tatizo tena mwanangu?”
Levina akabaki kimya!
“Levina...” mama yake akaita.
“Abee...” Levina akaitikia kwa kushtuka kidogo.
Ni kama alikuwa amegutuka kutoka katika usingizi mzito, lakini ukweli haukuwa huo. Levina alikuwa na mawazo ya usaliti. Kusema uongo na kumnyanyasa Rashid kwa sababu ya mapenzi.
“Una nini mama?!!”
“Inaniuma sana mama...” Levina akasema machozi yakidondoka machoni mwake, ni kama alikuwa akiumizwa na meseji za Rashid, lakini ukweli halisi haukuwa huo.
Ndani ya nafsi yake alikuwa akiumizwa na kitendo cha kumsingizia na si kufanyiwa kama ambavyo alitaka kutengeneza.
“Lakini ndiyo nimemtimua hivyo.”
“Amekosa adabu kabisa, yaani siku zote hizo naishi naye kama kaka yangu halafu anakuja kuniambia maneno machafu kiasi hicho? Hana adabu kabisa...” akasema Levina lakini kichwani mwake kukiwa na kitu kingine.
Moyoni mwake alihifadhi kitu tofauti kabisa, alikuwa na siri nzito sana, ambayo hakutakiwa kumwambia mtu yeyote, ilikuwa ni siri ambayo alitakiwa kuijua yeye na moyo wake pekee.
“Potelea mbali, kama ni kazi anaweza kupata mahali pengine, lakini nitapata wapi mwanaume kama Deo, lazima nifanye hivi, sina namna!” Akazidi kuwaza kichani mwake.
“Usijali mwanangu, nimeshamtimua huyu mwanaharamu. Hutakiwi kuwa na mawazo mwanangu na mimi mama yako nipo. Tena subiri...wewe Rashid, unasubiri nini? Kwani una mizigo gani mingi ya kuchukua muda mrefu kiasi hicho?” Akasema mama Levina akisimama kumfuata chumbani kwake.
Mama Levina alikuwa amevimba kwa hasira, akafika chumbani kwa Rashid na kumwita kwa sauti kubwa...
“Si naongea na wewe, hebu toka haraka nyumbani kwangu.”
“Natoka mama,lakini siku moja utakuja kugundua ukweli, siwezi kufanya mambo ya ujinga kiasi hicho mama, lakini kwakuwa wewe umeamua kumuamini Levina sawa!”
“Tena funga domo lako kabisa wewe mwanaharamu, inaonekana unataka kunigombanisha na mwanangu, unataka kuniambia mwanangu anaongopa?”
“Ndiyo mama!”
“Kwa lipi hasa?”
“Sijui mama, lakini ukichunguza utagundua ukweli.”
“Tena ishia hapo hapo kuniita mama, anayeruhusiwa kuniita mama ni yule anayeheshimu wanangu na kuwachukulia kama dada zake, si wewe mpumbavu!”
“Hapana mama!”
“We’ mwendawazimu, sina muda wa kubishana zaidi na wewe. Paki vitu vyako, nakwenda kukuchukulia pesa zako uondoke!”
Rashid akabaki kimya.
Mama Levina akaenda ndani haraka na kuchukua fedha alizokuwa akidaiwa na Rashid kisha akarudi na kumkuta tayari ameshajiandaa.
“Chukua pesa zako, tena nimekuongezea na elfu thelathini zikusaidie, ondoka kwangu!”
“Ahsante mama, lakini Mungu mwenyewe ndiye anayejua ukweli wa haya yote!”
“Hayo mahubiri yako huwa nakutana nayo kanisani, sasa sioni kama hata hapa nyumbani kwangu panafaa kuhubiriwa!”
“Siyo mahubiri mama, ni ukweli kabisa kutoka ndani ya moyo wangu!”
“Ukweli wa nini?”
“Sijamtumia zile meseji mimi mama.”
“Hivi wewe una akili? Zile namba ni zako au za nani?”
“Zangu.”
“Sasa kama ni zako, kwanini unaruka?”
“Unajua mama...juzi...” mama Levina hakumpa nafasi ya kumalizia utetezi wake.
“Hebu toka kwangu haraka tafadhali, sidhani kama bado nina nafasi ya kuendelea kuusikiliza utumbo wako, ondoka tafadhali!”
Rashid alikuwa anataka kumweleza mama Levina kwamba kuna siku alimuazima simu yake, lakini hakupewa nafasi hiyo.
Rashid akaondoka analia, mama Levina akiendelea kufoka huku akirusha mikono. Alikuwa amekasirika sana. Pamoja na utendaji kazi wake kuwa mzuri kwa muda mrefu aliokuwa akikaa naye, lakini siku aliyasahau yote hayo kwa meseji iliyoonekana kutumiwa mwanaye.
****
Mto wote ulikuwa umelowana kwa machozi, Levina alikuwa na uchungu sana ndani ya moyo wake. Usiku huo ulikuwa mgumu sana kwake, aliteswa na watu mawili; DEO NA RASHID!
Alifanya dhambi ya kumsingizia Rashid kwamba amemtongoza na akafukuzwa kazi. Hilo lilimuuma, lakini lingepoa kama kweli Deo angekubali kuwa naye. Lakini aliteseka sana, akiwa hana uhakika kama kweli Deo atamkubalia.
LEVINA aliumia sana ndani ya moyo wake, akaona ni vyema kama angenyanyua simu yake na kumpigia Deo. Alitaka kujua hisia zake zina nini juu yake. Hakutaka kufanya mambo kwa hasara!
Akachukua simu na kwenda moja kwa moja kwenye Menu, akabonyeza Contacts kisha akaanza kutafuta jina la Deo, alipolipata akabonyeza kwenye kitufe cha kijani ili kuruhusu upigwaji simu.
Punde tu, sauti ya Deo ikasikika...
“Vipi Levina mbona usiku sana?”
“Nina matatizo Deo!”
“Matatizo gani?”
“Naomba nikuulize kwanza maswali yangu!”
“Uliza.”
“Mimi ni rafiki yako?”
“Ndiyo!”
“Unaniamini?”
“Ndiyo!”
“Unanipenda?” Levina akauliza kwa sauti ya taratibu, lakini iliyochanganyikana na kilio cha kwikwi kwa mbali.
Deo hakupata shida sana kugundua kwamba Levina alikuwa analia. Pengine hilo si neno sana, lakini kwanini amemuuliza kama anampenda? Hata kama anampenda, ndiyo alie?
Kwanini analia?
Hakujua!
Kimya cha muda mfupi kikapita, Deo akiwa ametulia kwenye simu na Levina akiendeleza kilio chake cha chini chini huku kwikwi zikisikika kwa mbali.
“Levina,” baadaye Deo akaita.
“Bee!”
“Nini tatizo?”
“Si tatizo, napenda kusikia ukinijibu!”
“Uliuliza nini?”
“Nilikuuliza kama unanipenda?”
“Ni kweli nakupenda Levina, wewe ni rafiki yangu na umekuwa msaada kwangu kwa kila kitu, lazima nieleze ukweli, nakupenda, kwani wewe hunipendi?”
“Swali gani hilo Deo?”
“Samahani kama nimekuudhi, lakini ndani ya moyo wangu natambua kwamba tunapendana, mimi nafahamu hilo, naamini hata wewe ni kama mimi.”
“Kweli.”
“Lakini ni kwanini unalia?”
“Silii ila sauti yangu leo haipo vizuri sana.”
“Unakohoa?”
“Ndiyo!”
“Pole sana.”
“Ahsante.”
“Nina swali lingine kwako Deo!”
“Uliza.”
“Lakini kabla sijauliza, nataka unihakikishie kwamba utajibu ukweli wako wote na hutanidanganya jambo lolote.”
“Hilo kabla hujauliza, naamini unatambua kabisa jinsi nilivyo mkweli.”
“Umewahi kuona mtu akilia?”
“Mara nyingi sana, hata leo kuna mtoto nimemuona akilia.”
“Siyo mtoto, nazungumzia mtu mzima.”
“Ndiyo, kwenye misiba huwa wanalia sana, nimeshaona mara nyingi, kwani kuna nini, mbona unaniacha na maswali?”
“Lakini vipi kama ukiona mtu mzima analia?”
“Nitajisikia vibaya sana.”
“Umeshawahi kumuona mtu akilia kwa ajili yako?”
“Hapana.”
“Utapenda siku moja hilo likitokea?”
“Hapana.”
“Basi usiku mwema.”
“Kwanini?”
“Nimekutakia usiku mwema Deo.”
“Lakini sijakuelewa kabisa. Mbona leo maneno yako yamekuwa magumu sana kuingia kichwani mwangu? Kwani kuna nini kimetokea?”
“Hakuna...nilitaka kujua tu unachowaza kichwani mwako!”
“Nikuambie kitu Levina?”
“Nakusikiliza.”
“Nitalala nikiwa na mawazo sana leo. Maneno yako yananiacha na maswali mengi yasiyo na majibu kabisa. Mpaka sasa sijajua maana ya kauli yako.”
“Siku moja utajua....”
“Usiku mwema.”
“Na wewe pia!”
Wakakata simu zao.
Deo akapata wakati mgumu sana wa kuwaza mambo kichwani mwake bila kupata majibu. Alikuwa katika wakati mgumu sana wa kujaribu kuwaza kilicho kichwani mwa Levina kitu ambacho kwa hakika kisingekuwa rahisi kuelewa.
“Sijajua anamaanisha nini? Anyway itajulikana baadaye!” Akawaza na kujifunika shuka kisha akaishilia usingizini.
****
Siku nzima ilikuwa kama wiki kwa Levina, kichwa kilikuwa kinamuuma mawazo mengi yakimsumbua. Hakuwa na kitu kingine kilichomtesa zaidi ya Deo, aliendelea kuwaza namna ya kumsogeza karibu yake.
“Nampenda sana Deo, ni kweli kwamba nampenda sana, lazima nitumie kila njia, nihakikishe anakuwa wangu. Hilo lazima nitalifanya,” akawaza Levina akiwa kazini kwake Posta.
Levina baada ya kumaliza kidato cha sita, wazazi wake walimkabidhi moja ya maduka yao yaliyopo mjini, Levina alipewa duka la simu lililopo Posta Mpya jijini Dar es Salaam.
Alichojua yeye ni kwamba alikuwa msimamizi wa duka lile kubwa, lakini wazazi wake walipanga kumwachia moja kwa moja kama lake. Walimfanya msimamizi mkuu, akishughulikia kila kitu, mpaka mishahara ya wafanyakazi, walichokifanya wao ni kukagua mahesabu ya fedha zinazoingia na kutoka benki.
Mali ikipungua dukani, ilikuwa ni kazi ya Levina kuagiza au kwenda nje ya nchi kununua mzigo mwingine wa dukani.
Akionekana mwenye mawazo tele kichwani mwake, simu yake ikatoa mlio wa ujumbe mfupi wa maneno, mara moja akaufungua na kusoma.
Ilikuwa meseji kutoka kwa mama yake, alijikuta anarudia kusoma zaidi ya mara mbili ile meseji akiwa haamini kabisa alichokiona.
Ujumbe ule ulisomeka; “Levina ni wiki moja sasa tangu Rashid ameondoka, hatuna house boy, sasa kama unaweza ni vizuri ukashughulikia hilo, tukapata mtu mwingine haraka.”
Levina akatabasamu.
Ilikuwa nafasi nzuri kwake ya kumwingiza Deo nyumbani kwao.
“Yes, mambo yanakwenda kama nilivyopanga, afadhali,” akasema kwa sauti ya taratibu akiachia tabasamu.
***
Jioni Levina aliwahi sana kurudi nyumbani, akamkuta mama yake sebuleni, baada ya kumsalimia akamwambia...
“Mama nilipata sms yako ya mchana, nimeanza kuifanyia kazi, ndani ya siku tatu tutapata mtu mwingine.”
“Oh! Usijali binti yangu, ameshapatikana kijana mwingine kutoka Bagamoyo, atakuja kuanza kazi kesho.”
Uso wa Levina ukasawagika kwa huzuni.
Endelea kuisoma...

Post a Comment