ad

ad

USIKU WA KIGODORO - 13


Endelea kulike: www.facebook.com/2jiachie
Tembelea: www.2jiachie.com

ILIPOISHIA: “Bro za tangu sana, kama nakukumbuka,” alisema James ambaye kiti alichokaa aliweza kuonana na Semi moja kwa moja wakati kiti alichokaa Lina alimpa mgongo kwa hiyo Semi alimwona kwa nyuma.
Kabla hajaitika salamu ya James, Semi alikaza macho kwa Lina, akashangaa, akasimama na kumfuata…
“Lina,” aliita huku akimwangalia usoni na kumshika begani…
SASA JIACHIE…
Lina alishtuka sana, aligeuka kumwangalia Semi, akaanguka chini na kupoteza fahamu…
“Kwani ni nini mkuu?” aliuliza James…
“Huyu ni mke wangu, kaniambia yupo saluni nashangaa namemkuta hapa. Kwani ndugu yangu huyu ni nani kwako?” aliuliza Semi huku akimkazia macho James…
“Huyu mimi ni mke wangu,” alisema James kwa kujiamini.
“Mke wako?”
“Ndiyo kaka. Kwani vipi?”
“Lina mke wangu mimi unasema mkeo?” alishtuka Semi.
“Ama, Lina ni mke wangu, nimefunga naye ndoa kanisani kabisa.”
“Kaka acha utani. Kwanza wewe jana si ulikuja ukakaa hapa?”
“Ndiyo.”
“Mbona nilikuwa naye mimi kama ni mkeo. Acha mambo ya utani bwana. We unaniibia mke wangu, nimekufumania.”
“Sijakuibia na jana hakuwepo.”
“Alikuwepo, ulipokuja wewe alikwenda chooni,” alisema Semi.
Kwa mbali James alipata picha kwamba, huenda Lina hakusafiri kama ni hivyo. Pia alianza kuyaamini maneno ya Kindaundau kwamba Lina ana mume wake.
Wateja walianza kujaa kwenye meza a kujua nini kimetokea. Wengine waliuliza, wengine walitumbua macho tu.  Mzee mmoja mwenye busara zake aliingilia kati baada ya kusikia mazungumzo ya James na Semi. Aliwataka watulize munkali kwanza, wahakikishe Lina anazinduka halafu mambo mengine yaendelee…
“Hivi we mzee unajua inavyouma ukimfumania mke wako? Nina miaka naye minne sasa” alisema kwa hasira Semi.“Umemfumania nani wewe? Mimi Lina nimeshasema ni mke wangu.”
“Una cheti cha ndoa wewe?” yule mzee alimuuliza James baada ya kumsikia Semi akisema ana miaka naye minne.
“Ninacho ndiyo,” alijibu kwa kujiamini sana James.
“Basi kama nilivyowaambia, mwacheni kwanza azinduke mambo mengine yatafuata,” mzee alisema tena.
Semi aliinama kumtingisha Lina na James naye akafanya hivyohivyo…
“Lina…Lina,” aliita Semi…
“Baby…mke wangu,” aliita James naye akimtingisha. Semi alitaka kumrushia ngumi James lakini akajizuia.
Kwa mbali Lina alionekana kushtuka, akafumbua macho na watu wakaombwa kutawanyika ili aweze kupata hewa safi.Walipoona Lina amezinduka walimsimamisha wote na kumkalisha kwenye kiti…
“Pole sana, unajisikiaje sasa?” aliuliza James huku akimshika.
Lina hakujibu akaanza kuporomosha machozi sasa huku akiangalia chini. Alichojua ni kwamba amepoteza ndoa zote mbili.
Semi alimsimamisha ili waende hospitali, James akasema anampeleka yeye. Ukatokea mzozo mwingine tena na walitaka kuzichapa. Yule mzee akaingilia tena kati, akamuuliza Lina aliyeonesha kukosa nguvu bado…
“Eti, kati ya hawa wawili nani ni mume wako?”
Lina alijiinamia, machozi yakamtoka tena…
“Unajua binti, wewe ndiye mwenye uwezo wa kumaliza hili tatizo hapa, sasa kama utashindwa kuwa muwazi sijui itakuwaje leo.”
Lina aliendelea kulia, wasiwasi ulimtawala. Kwa muda huo alitamani ardhi ipasuke ili aingie ndani yake na kufia huko.
“Lina, nini umenifanyia?” aliuliza Semi. Swali hilo likazidi kuchochea kilio cha Lina, sasa alilia kama mtoto ikabidi uongozi wa eneo hilo kumuita mlinzi na kuwataka akina Semi kuondoka na Lina wao…
“Mkamalizane majumbani mwenu bwana, hapa ni eneo la biashara, mke wangu mimi mke wangu mimi, basi huyo mwanamke atakuwa kiboko, ndoa mbili,” alisema mfanyakazi mmoja wa eneo hilo.
Mwngine akadakia…
“Hata huyo mume wa kwanza naye kiboko. Mkeo mpaka anafunga ndoa wewe uko wapi? Kwani kama mlipofunga ndoa mlikwenda fungate?” aliuliza mfanyakazi huyo aliyedakia…
“Yeah! Tulikuwa honeymoon ya siku kama tatu hivi, tukaenda kuishi nyumbani kwangu Mbezi,” alipasua James…
“Hamna, mimi mke wangu hajawahi kukosekana nyumbani siku tatu,” alidakia Semi. Kauli zao ziliwakoroga sana watu waliokuwa wakisikiliza.Lina alisimama na kuanza kutembea kuondoka eneo hilo huku akizomewa. Semi na James walimfuata kwa nyuma lakini hawakumkuta kwa vile alishatoka kwenye geti na kuchukua Bajaj.
Kazi ilikuwa moja kwa Lina, anakwenda wapi? Na huko anakokwenda ataishi mpaka lini? Je, atasema nini kwa wazazi wake? Semi atamuelewaje? Lakini hata James atamuelewaje?
“Wapi dada?” aliuliza dereva wa Bajaj…
“We twende tu.”
***
James aliingia kwenye gari lake, Semi naye alifanya hivyohivyo. Lakini kabla James hajaondoa gari, alishuka akamkimbilia Semi na kugonga kioo cha gari…
Semi akafungua kioo nusu…
“Unasemaje?”
“Nipe namba  yako bro. unajua kuna uwezekano ishu si sisi ila ni huyu mwanamke. Muhimu sisi kama wanaume tukutane,” alisema James.
Semi akiwa hana amani, alizitaja namba zake za simu kisha naye James akamtajia za kwake. Wakaagana na kuondoka.
Semi alisema moyoni kwamba hatampigia simu Lina mpaka atakaposema mwenyewe lolote na pia kama ni kweli alifunga ndoa na James, yeye basi! 

Lina alikwenda kupiga kambi nyumbani kwa shoga yake, Eg ambapo alipofika tu na jinsi alivyokuwa akihema, Eg alijua kuna ishu nzito sana imetokea. Walipokutana macho, Lina akaanza kuporomosha machozi palepale…
“Lina, nini kimetokea?” aliulia kwa mshtuko Eg…
“Nimenaswa leo Eg, sijui itakuaje?” alisema Lina huku akilia.
“Umenaswaje? Hebu nisimulie.”
“Nilikwena Mlimani City na James, Semi alisafiri kwenda Zanzibar jana na alisema angerudi leo. Sasa nashangaa kumbe kaamua kurudi leo, akaja Mlimani City akanikuta nimekaa na James.”
“Mmmh!” alishtuka sana Eg. Aliliona tatizo kweli ni zito.
“Ikawaje sasa?” aliuliza Eg.
“Yaani Eg, amenikamata hivi nimekaa na James,” kabla hajamaliza kusema, Lina alilia tena. Ilibidi Eg atumie nguvu kubwa sana kumtuliza.
“Naomba utulie kisha uendelee kunisimulia,” alisema Eg akimkumbatia Lina.
Lina alitulia kwa muda kisha akasema…
“Yaani Eg iko hivi. Nilikaa na James Mlimani City, tena kwa kujiachia nikijua Semi si yupo Zanzibar anarudi kesho, kumbe karudi leo. Akaja Mlimani City, alinipigia simu nikamwambia nipo saluni, alipokuja pale kanikuta. Akanishika geba na kusema Lina.
“Yaani huwezi amini shoga nilianguka nikazimia palepale. Nilipokuja kupata fahamu nikakimbia. Aibu iliyoje?”
“Da! Pole sana shoga…sasa?”
“Sijui lolote. We unadhani naweza kwenda kwa nani kati yao?” aliuliza Lina.
“Mh! Uchaguzi ni wako.”
“Hamna Eg. Nikienda kwa Semi atanishangaa sana, kwa James pia. Hapa sijui wao wameachanaje! Kama walizungumza kila mmoja akajieleza kwa mwenzake mwisho wa siku si mimi nitaonekana wa ajabu sana?”
“Sana. Mi nadhani tumtafute mtu mzima mmoja ili asaidie busara zake,” alisema Eg…
“Eg, nilishaongea na watu wazima wote walishtuka na kuonesha dalili kwamba, mzigo ni wangu mwenyewe.”
“Mh!”
***
James baada ya kufika nyumbani kwake aliingia chumbani, akampigia simu Semi. Semi naye alikuwa chumbani kwake amelala ubavuubavu akishangaa kilichotokea…
“Haloo,” Semi alipokea simu…
“James hapa bwana.”
“Ndiyo kaka, tunaweza kukutana muda huu?” aliuliza James…
“Mi nadhani itakuwa muhimu. Wapi sasa?”
“Tukutane popote pale.”
“Wewe njoo nyumbani kwangu, nitakuelekeza ukifika.”
James alitoka, aliendesha gari akiwa amempigia simu Semi akampa maelekezo mpaka nyumbani kwake. Aliposhuka, alichukua bastola na kuisunda sehemu fulani ya nyuma, akampigia simu  Semi kwamba ameshafika.
Alitoka, akampokea na kumkaribisha ndani. Ile anakaa tu James, macho ya kwanza yakatua kwenye ukuta na kukutana na picha kubwa ya siku ya ndoa ya Lina na Semi…
“Kumbe kweli,” alisema moyoni.
Baada ya salamu ya muda huo, James alianza kwa kuelezea alivyokutana na Lina na alivyomuuliza kama ameolewa, akamjibu hana mume na alivyojitosa yeye kufunga naye ndoa…
“Ina maana umefunga ndoa kweli na Lina?”
“Kabisa.”
“Kanisani?”
“Ndani ya kanisa kabisa na honeymoon tulikwenda.”
Semi alianza kuunganisha matukio, akaanza kukubali moyoni mwake kwamba, Lina alifunga ndoa na kijana huyo.
“Inawezekana kweli, maana naanza kukumbuka kwamba kuna wakati amekuwa na safari nyingi za hospitali na wakati mwingine kulala hukohuko,” alisema Semi kwa sauti iliyojaa majonzi…
“Hata kwangu, kuna wakati alikuwa na safari nyingi na kusema anakwenda kulala kwa mgonjwa wa rafiki yake mmoja anaitwa…”
Kabla James hajamaliza kumtaja jina, Semi akamtaja…
“Eg?”
“Ee Eg. Huyohuyo.”
Semi alizidi kuvuta picha na kukumbuka siku moja Lina alipomwambia anakwenda kwenye sherehe ya Eg. Akakumbuka siku hiyo alikuwa  na safari ya gafla ikabidi amfuate Lina kwa Eg ambapo alimkuta amependeza sana.
Kifupi aliunganisha matukio na kukumbuka mambo mengi sana yaliyoonesha uhalisia.
“Hivi mimi leo ninavyojua ametoka safarini kwao, Korogwe, Tanga ambapo alisena anakwenda mama yake ni mgonjwa,” alisema James.
“Wewe jana si ulikuja pale Mlimani City?” aliuliza Semi.
“Nilikwenda kumpokea Ubungo maana alisema anarudi. Kufika napiga simu haipokelewi, ndiyo nikaamua kuja hapa.
“Kufika hapa, nakaa kidogo tu, akanitumia meseji kwamba ameingia Ubungo alikuwa amelala, lakini simu yake inaisha chaji, ndiyo maana nilitoka mbio.
“Kufika kule sikumpata tena hewani, nikaenda nyumbani naingia na yeye anaingia na bodaboda na ana mizigo.”
“Ana mizigo kabisa?” aliuliza kwa kuhamaki Semi…
“Kabisa.”
“Da! Huenda alinunua vitu sokoni ili ujue alisafiri kweli. Mimi nilikaa naye Mlimani City, wakati umekuja alikuwa chooni. Nahisi alikuona ndiyo maana akakutumia meseji ya kukwambia umefika ili uondoke. Maana ulipoondoka tu, akaja tukaondoka,” alisema kwa kirefu Semi.
Endelea kulike: www.facebook.com/2jiachie
Tembelea: www.2jiachie.com

No comments

Powered by Blogger.