ad

ad

A JOURNALIST IS BACK (MWANDISHI AMERUDI) - 13


MWANDISHI: NYEMO CHILONGANI
Endelea kulike: www.facebook.com/2jiachie
Tembelea: www.2jiachie.com

   “Lakini kumbuka kwamba ulinisaliti. Yaani upendo wote ule niliokuonyeshea, malipo yake yakawa ni usaliti. Unakumbuka kama ulinisaliti?” Dominick aliuliza huku tabasamu pana likionekana usoni mwake. Bwana Ombeni hakujibu kitu chochote kile, alibaki kimya huku akimwangalia Dominick.
   “Swali gumu hilo, inaelekea haukumbuki kitu chochote kile” Dominick alimwambia Bwana Ombeni.
   “Nakumbuka” Bwana Ombeni alimwambia Dominick.
   “Safi sana. Unakumbuka kwamba ulinisababishia kidonda kikubwa maishani mwangu?” Dominick aliuliza, tayari uso wake ukabadilika, tabasamu lote ambalo lilikuwa likionekana kabla likapotea.

   Bwana Ombeni hakujibu chochote kile, alibaki akimwangalia Dominick usoni. Dominick akaifuata droo yaa kitanda na kutoa bastora yake ndogo na kisha kuanza kuiangalia. Bwana Ombeni akazidi kutetemeka zaidi.
   “Unakumbuka?” Dominick aliuliza kwa sauti ya taratibu. Bwana Ombeni hakujibu chochote kile.
   “Unakumbuka?” Dominick aliuliza kwa sauti iliyojaa ukali huku akimgusisha bunduki ile kichwani.
   “Nakumbuka” Bwana Ombeni alijibu.
   “Safi sana. Ulimuua mtoto wangu na mke wangu. Najua hao sitoweza kuwapata tena. Uliiteketeza nyumba yangu kwa moto, na fedha hizi ambazo umeniletea ndizo ambazo nitazitumia kununulia nyumba nyingine. Chagua nikufanye nini siku ya leo?” Dominick alimuuliza Bwana Ombeni.
   “Naomba unisamehe”
   “Ningekusamehe kama tu usingeiangamiza familia yangu” Dominick alimwambia Bwana Ombeni.
   “Naomba unisamehe”
   “Nitakupiga risasi nne za miguuni ili usitembee tena, nitakutoboa macho yako ili usione tena na kuukata ulimi wako ili usiongee tena. Utakapoulizwa chochoe juu yangu, hautoweza kujibu wala kuona. Na pia nitavikata vidole vyako ili usiweze kuandika chochote. Nitakufanya uishi katika maisha ya mateso kipindi chote cha maisha yako” Dominick alimwambia Bwana Ombeni na kuendelea.
   “Ila nitafanya hivyo kama hautotaka nikuue” Dominick alimwambia Bwana Ombeni.
   “Ni adhabu kali Dominick….naomba unisamehe” Bwana Ombeni alimwambia Dominick.
   Dominick akachukua mto kutoka katika kitanda kile na kisha kuuweka mbele ya bunduki yake. Bwana Ombeni akabaki akiendelea kuomba msamaha huku akilia kama mtoto mdogo.
   “Nililia hata zaidi ya unavyolia sasa, nikaumia sana” Dominic alimwambia Bwana Ombeni na kisha kubonyeza kitufe cha kuruhusu risasi.
   Risasi tano zikatoka, mwili wa Bwana Ombeni ukatobolewa kwa risasi, damu zikatapaa kitandani pale alipokuwa amekaa. Akaangukia kitandani, miguu na mikono yake wala haikutulia, aliendelee kuirusha huku na kule, baada ya sekunde chache, akatulia.
   Dominick hakutaa kuendele kubaki ndani ya cumba kile, alichokifanyani kuvaaa nguo zake pamoja na ndevu zake za bandia, akachukua brifukesi ile na kisha kuondoka chumbani mule.
   Safari yake ilikuwa ni kwenda nyumbani kwa rafiki yake Edmund na kumuelezea kila kitu ambacho kilikuwa kimeendelea baada ya kuondoka nyumbani kwake mwaka mmoja uliopita kwa ajili ya kutekeleza kile ambacho alikuwa amekipanga kukitekeleza.
   “Nimefanikiwa. Najiona kuwa amani kwa sasa” Dominick alimwambia Edmund.
   “Safi sana. Vipi kuhusu brifukesi hiyo?”
   “Kuna kiasi cha shilingi milioni mia moja” Dominick alimwambia.
   “Umezitoa wapi tena”
   “Aliniletea yeye mwenyewe. Sikiliza Edmund, nitahitaji kuondoka kueleke nchini Congo” Dominick alimwambia Edmund.
   “Congo! Kufanya nini tena?”
   “Usijali. Nitataka kuonekana kama nilitekwa na kupelekwa nchini Congo. Nitarudi huku na kujifanya nimerudi nyumbani. Unauonaje mpango huo?” Dominick aliuliza.
   “Uko safi. Utasema ulikuwa wapi uko Congo?”
   “Katika msitu wa Bwambiro kwamba nilikaa mateka chini ya waasi. Kila kitu kitakuwa safi, ila ninachokihitaji ni msaada wako. Sitoweza kwenda Congo kwa ndege, nitata nisafiri kwa basi mpaka Kigoma ambako nitaonganisha mpaka Congo kwa kutumia meli pale ziwani Tanganyika” Dominick alimwambia.
   “Sawa. Nitakwenda kukata tiketi kesho” Edmund alimwambia Dominick.
   Kama jisi ilivyopanga ndivyo ilivyofanyika, moja kwa moja siku iliyofuata Dominick akaingia katika basi la Shibobo na kisha safari ya kuelekea mkoani Kigoma kuanza. Safari ilichukua siku moja na nusu na ndipo gari likaanza kuingia katika kitu cha mabasi cha Mwandiga ambako akateremka na kuanza kuelekea katika hoteli ya Mamboleo iliyokuwa katika mtaa wa Mwanga. Siku iliyofuata, akapanda meli ambayo ilikuwa ikielekea nchini Congo.
                                                           *************
Taarifa hii ilikuwa ni zaidi ya mshtuko mkubwa nchini Tanzania. Kila mtu ambaye alikuwa ameisikia alionekana kuogopa, amani ikaonekana kupotea muda wowote ule. Watu wakaanza kuhuzunika kupita kawaida, Waziri wao ambaye walikuwa wakimpenda hakuwa nao tena, alikuwa ameuawa ndani ya hoteli ya Caspian.
Mapolisi walikuwa wamekusanyika nje ya hoteli ile huku wengne wakiwa wameelekea katika chumba kile ambacho kilikuwa kimetokea mauaji. Bwana Ombeni alikuwa chini huku damu zikiwa zimetapakaa chumbani mule.
Wapelelezi wengine kutoka katika kitengo cha polisi walikuwa wakipiga picha za tukio lile kwa ajili ya kwenda kuzihifadhi katika ofisi zao. Kila mtu ambaye alikuwa akiiangalia maiti ile, alibaki akihuzunika.
Siku iliyofuata, asilimia tisini ya magazeti yalikuwa yameandika taarifa ile ambayo ilikuwa imeshika sana hisia za watu nchini. Kila mtu alitaka kuisoma habari ile kwa undani zaidi na kutaka kujua chanzo cha mauaji yale.
Mpaka inafika saa saba mchana, hakukuwa na gazeti lolote mtaani ambalo lilikuwa na habari ile, magazeti yote yalikuwa yamenunuliwa. Hiyo ndio ilikuwa habari ambayo ilishika sana katika masikio ya kila mtu ambaye aliisoma na kuisikia.
“Mapolisi walisema amepigwa risasi ngapi?” Jamaa mmoja aliwauliza wenzake
“Tano. Ila si unajua mapolisi wetu wanavyoficha, unaweza kukuta kapigwa hata risasi hamsini” Jamaa mwingine alijibu.
                                                               *******
Edmund alikuwa akionyesha uso uliojaa mshtuko, wafanyakazi wote ambao walikuwa ofisini pale walionekana kumshangaa, hawakujua sababu ambayo ilimfanya Edmund kuwa katika hali ile. Wafanyakazi wengine wakaanza kuendelea na kazi zao kama kawaida ila wengine wakaanza kumsogele karibu.
“Dominick…!” Edmund alisema kwa mshtuko.
Wafanyakazi wote wakashtuka, jina lile bado lilikuwa katika kumbukumbu zao. Wote wakajikuta wakianza kumsogelea, tayari wakaona kuna kitu ambacho kilikuwa kikiendelea mahali hapo. Edmund alikuwa ameishika simu yake, kila mfanyakazi alitamani aiachie simu ile na kuwaelezea kitu ambacho kilikuwa kinaendelea juu ya jina lile ambalo alikuwa amelitaja.
“Kuna nini?” Mfanyakzi mmoja aliwauliza wenzake.
“Subiri kwanza”
Mara baada ya muda wa sekunde kadhaa, Edmund akaitoa simu yake sikioni na kuanza kuwaangalia wafanyakazi ambao walikuwa wamemzunguka katika meza ile. Kwa mbali tabasamu likaanza kuonekana usoni mwake.
“Kuna nini?” Mfanyakazi mmoja alimuuliza.
“Dominick….Dominick yupo hai….!” Edmund aliwaambia wafanyakazi wenzake.
Kila mmoja akaonekana kushtuka, hawakuyaamini maneno yale ambayo Edmund alikuwa ameyaongea, kila mmoja akaonyesha mshtuko wa wazi. Ilionekana kuwa ngumu sana kwa Dominick kuwa hai katika kipindi hicho na wakati Tanzania nzima ilikuwa inajua kwamba aliuawa na tayari alikuwa amezikwa.
“Unasemaje?”
“Ndio hivyo. Amesema anakuja, yuko njiani kutoka mkoani Kigoma” Edmund aliwaambia.
Siku iliyofuata, wafanyakazi hawakutaka kuwepo maofisini mwao, wote walikuwa katika kituo cha mabasi cha Ubungo kwa ajili ya kumpokea Dominick ambaye hawakuwa wamemuona kwa muda wa mwaka mzima.
Mara baada ya basi la Zainabu kupaki sehemu husika, Dominick akaanza kuteremka. Kila mmoja alionekana kutokuamini, mwili wake ulikuwa umepungua sana kuonyesha kwamba alikuwa katika kipindi kikubwa cha matatizo.
Ilionekana kuwa shangwe kwa kila mfanyakazi ambaye alikusanyika kituoni hapo. Moja kwa moja baada ya kumkumbatia, wakaanza kuelekea katika gari la kampuni ambal walikuwa wamekuja nalo na kisha kuanza kuelekea ofisini.
“Tuambie nini kilitokea?” Bosi wa kampuni hiyo alimuuliza Dominick mbele ya wafanyakazi wake.
“Ni habari ndefu sana. Kuna siku nilipigiwa simu niende kuchukua habari pale Africa Hotel. Nilipofika pale, nilitekwa na kupelekwa mkoani Kigoma ambako huko safari ilionganishwa mpaka nchini Congo katika msitu mmoja ambao ulikuwa ukitisha sana” Dominick aliwaambia.
“Mungu wangu! Ni watu gani hao ambao walikuwa wamekuvamia?” Bosi aliuliza.
“Siwafahamu, walikuwa wamevalia kofia kubwa za kihuni. Nilipata mateso sana nchini Congo, kwa kifupi ni kwamba walitaka kuniua kwa kifo kilichojaa maumivu makali” Dominick alisema.
“Pole sana. Ilikuwaje sasa mpaka wakakuachia?”
“Hawakuniachia, nilitoroka mara baada ya majeshi ya serikali kuvamia kambi ile ya waasi. Mateka wenzangu wengi waliuawa kwa kupigwa risasi ila mimi walikuwa wakiniacha kwa kusema kwamba mtu ambaye alikuwa amewapa maagizo alitaka kuniua kwa mkono wake mwenyewe” Dominick aliwaambia.
“Mtu gani huyo?”
   “Mpaka naondoka, sijamjua ni mtu gani” Dominick alijibu.
   “Karibu sana nyumbani”
   “Asanteni sana. Vipi kuhusu upelelezi wa mauaji ya familia yangu?” Dominick aliuliza huku akionekana kutojua chochote kile. Wafanyakazi wote wakaanza kuangaliana.
   “Bado hatujajua. Yaani kuna matukio kadhaa ya mauaji yalitokea, nafikiri mapolisi walikuwa bize wakiyashughulikia”
   “Mauaji? Mauaji gani?”
   Kila kitu ambacho kilielezewa mahali hapo kilionekana kuwa kama kipya kwa Dominick, muda wote alikuwa akitingisha kichwa chake kushoto kulia hali iliyoonyesha kuhuzunika. Hakukuwa na mtu yeyote ambaye alikuwa akifahamu juu ya kila kilichoendelea zaidi ya Edmund ambaye nae alikuwa akijifanya kutokuelewa kitu chochote kile.
   Siku iliyofuata, magazeti yalikuwa yakiandika taarifa juu ya ujio wa Dominick, taarifa ile ilionekana kuwa kama muujiza ambao ulikuwa umemtokea Dominick. Wananchi wakawa na furaha kwa kuwa mwandishi ambaye alikuwa akionekana kuwa shujaa alikuwa amerudi tena kazini baada ya kipindi cha mwaka mzima kupita.
   Wiki nzima, sura ya Dominick ndiyo ambayo ilikuwa ikionekana katika magazeti mbalimbali. Magazeti hayo yote yalikuwa yakinunulika sana mitaani, ujio wa Dominick ukaonekana kuwa kitu kikubwa ambacho kila siku alitakiwa kumshukuru Mungu kwa kumuokoa kutoka katika mikono ya waasi.
   “Kuna mwanaume anataka kukuona” Msichana mmoja alimwambia Dominick.
   “Mwanaume gani?”
   “Simfahamu, ila amesema ametoka kituoni” Mwanamke yule alimwambia Dominick.
   Dominick akaonekana kushtuka, hakujua ni mwanaume gani huyo ambaye alikuwa amefika ofisini hapo na kumuulizia, alichokifanya ni kumwambia yule mwanamke kumruhusu mwanaume huyo.
   Bugabu akaanza kuingia ndani ya ofisi ile. Shati lake jeupe pamoja na tai yake nyekundu vilimfanya kupendeza kupita kawaida. Moja kwa moja baada ya kuingia ndani ya ofisi ile, akakaa katika kiti kimoja kilichokuwa wazi.
   “Karibu”
   “Asante sana” Bugabu alijibu na kujitambulisha kwamba alikuwa mpelelezi kutoka katika kituo cha polisi.
   Maongezi yalianzia hapo, walizidi kuongea mambo mengi sana na ya kawaida kabisa. Mpelelezi Bugabu akaonekana kutaka kujua kitu fulani kutoka kwa Dominick ambaye alikuwa akijibu kila swali ambalo alikuwa akiulizwa kiufasaha kabisa.
   “Wewe ndiye muuaji Dominick. Wewe ndiye uliyewaua Mawaziri wote hawa” Bugabu alimwambia Dominick ambaye alionekana kushtuka.
   “Unasemaje?”
   “Usishtuke. Mimi ni mpelelezi na kila siku nilikuwa nikiendelea na upelelezi wangu. Wewe ndiye muuaji. Nimepeleleza kwa kipindi kirefu sana. Nimegundua kwamba Mawaziri hawa waliiteketeza familia yako. Usitake kuuliza nimejua vipi, kumbuka kwamba mimi ndiye mpelelezi na nimefanya kazi kwa muda mrefu sana. Nilikwenda makaburini, makaburi ya familia yako yalikuwa yakiwekwa maua mara kwa mara lakini kaburi lako halikuwa likiwekwa maua, hii ilinionyesha kwamba wewe ndiye ulikuwa akifanya yale. Nimegundua mengi, niliyaangalia maneno yale yaliyoandikwa ukutani siku ile familia yako ilipoangamizwa, nikafuatilia majina ya Mawaziri waliouawa, nikagundua kwa asilimia mia moja kwamba ni wewe, ninaamini kwamba ulifanya hivi kwa ajili ya kulipa kisasi” Mpelelezi Bugabu alimwambia Dominick ambaye alikuwa kimya huku akionekana kuwa na wasiwasi tele.
   “Nakuunga mkono kwa vyote ulivyofanya, hata kama ningekuwa mimi, ningeziteketeza familia zao na kuwamaliza wao pia. Hongera kwa kazi kubwa. Hautakiwi kujali hata kidogo. Kila kitu kipo ofisini mwangu, nakuhakikishia kwamba hakuna atakayefahamu hili. Nimeamua kuja kukueleza kwa kuwa tu nilitaka ujue kwamba mimi ni mpelelezi wa kimataifa na huwa hakuna upelelezi unaonishinda. Nakutakia kazi njema na hongera Dominick” Mpelelezi Bugabu alimwambia Dominick.
   Bugabu akainuka, Dominick akashusha pumzi ndefu na kuipeleka mikono yake mezani. Baada ya sekunde chache nae akainuka na kupeana mikono na Bugabu ambaye wala hakutaka kuendelea kukaa ofisini pale zaidi ya kuaga na kuondoka.
   “Asante Mungu” Dominick alijikuta akijisemea na kuegemea kiti chake.
   Maisha mapya ya Dominick yakaanza, kiasi cha fedha cha shilingi milioni mia moja alikuwa amekwishazitumia kwa kununua nyumba kubwa iliyomgharimu milioni sitini huku milioni arobaini akifanyia biashara nyingine.
   Mara kwa mara alikuwa akielekea katika makaburi ya Kinondoni na kuyaangalia makaburi ya familia yake na kisha kuweka maua. Kila siku ambazo alikuwa akiendelea kuishi katika dunia hii ambayo ilionekana kujaa mambo mengi, alikuwa akiikumbuka familia yake.
   Baada ya miaka miwili, Dominick akaamua kumuoa msichana mrembo Magreth. Magreth ndiye ambaye akaonekana kuanza kuyabadilisha maisha yake, hakuwa mtu wa mawazo tena kama ilivyokuwa siku za nyuma. Alimpenda mkewe Magreth na kumthamini katika maisha yake yote.
   Baada ya mwaka mmoja, wakafanikiwa kupata mtoto wa kiume aliyempa jina la Ibrahim, jina ambalo alikuwa amempa marehemu mtoto wake. Alifanya hivi kuwa kama ishara maalumu ya kumkumbuka mtoto wake ambaye alikuwa akimthamini kuliko mtu yeyote.


                                                                                             MWISHO

No comments

Powered by Blogger.