ad

ad

USIKU WA KIGODORO - 10


Endelea kulike: www.facebook.com/2jiachie
Tembelea: www.2jiachie.com

ILIPOISHIA :Mimi sijawahi kumwona ila kuna wakati Semi alikuwa anafukuzia mkopo mkubwa benki, Lina alikuwa mmoja wa watu wanaotakiwa kutia sahihi kwenye fomu. Kwa sababu tulikuwa tukienda benki kila siku nikalizoea hilo jina.
“Halafu juzi nadhani, nilikwenda kuchukua mzigo wangu ofisini kwa huyo Lina aliuacha mumewe, huyo Semi…”
JIACHIE SASA…

“Kindaundau,” aliita James akiwa na sura yenye mshangao...
“Naam bosi.”
“Unasema?”

“Ndiyo hivyo, jaribu kuchunguza nini kinaendelea kati yenu.”
James alikuwa kama ameganda kwa muda akiwaza, akaangalia juu, kulia na kushoto kisha akamwangalia Kindaundau…

“Kuna mambo unayasema kama yana ukweli fulani. Mfano, unalitaja jina la Semi, naamini kama ni Lina mke wangu, amemsevu kwa jina la Bro Semi…lakini hebu nikuulize Kindaundau…wewe ndiye ulikwenda kuchukua huo mzigo kazini kwa Lina halafu ulimkuta mlinzi?”
“Ndiyo.”

“Halafu uliongea kwa simu na Lina akiwa hayupo kazini?”
“Ndiyo mimi. We umejuaje kwanza? Halafu umenikumbusha kitu James…baada ya mimi kuongea na Lina tu, wewe ukanipigia simu.”

“Ndiyo! Nilikuwa naye mimi alipomuuliza jina lako mlinzi akalitaja la Kindaundau nikakukumbuka na yeye Lina nilimwambia huyo mtu Kindaundau namjua na namba zake ninazo ndiyo maana nikakupigia.”
“He! Kumbe!”

“Mimi nashukuru sanasana ndugu yangu Kindaundau kwa kunihabarisha hili japokuwa nimeumia sana. Lina! Mke wangu, kumbe  ana mume mwingine? Ina maana mimi si mume halali? Siamini hata kidogo. Da! Nitaua mwaka huu Mungu nasema, siwezi kuwa mwanaume bwege mimi.”
“James acha jazba.”

“No Kindaundau. Mimi ni mtu na pesa zangu. Anapotokea mwanamke anakufanyia hivi unadhani nini kitatokea hapo?”“Ni kweli kinaweza kutokea kikubwa. Lakini mimi nakushauri…”

“Unanishauri nini Kindaundau, we umeshaniambia niachie mimi. Kwanza huyo Lina kaniambia anakwenda kumwona mama yake Korogwe anaumwa. Kuna uwezekano hajasafiri…hebu mpigie huyo Semi muulize kiaina ujue mkewe yuko wapi?”

“Da! Bwana James, unavyodhani inawezekana kweli nikamuuliza swali kama hilo?”
“Naamini ukiongea naye mawili matatu atasema jambo ambalo litakupa mwanga.”
“Sawa, ngoja nijaribu.”
Kindaundau alimpigia simu Semi akiwa ameweka loud speaker…
“Hujambo bwana Semi?”

“Sijambo, vipi Kindaundau? Mzima wewe?”
“Mimi mzima bwana. Uko nyumbani nini? Maana wakubwa kama nyinyi si ajabu uko nyumbani na shemeji mnakula bata tu.”

“Nipo mkoa bwana, maisha haya bila kutafuta huwezi kuyamudu kaka.”
“Shemeji vipi? Umesafiri naye?”
“Hamna, yuko kazini saa hizi.”
“Poa, nilidhani upo Dar nikupe dili, basi ukirudi nitafute tuongee.”
“Sawa mkuu.”

Baada ya kukata simu, Kindaundau na James walitazamana…
“Kazini hayupo maana mimi nimetokea huko,” alisema James…
“Basi atakuwa amesafiri kweli?” alisema Kindaundau…

“Haiwezekani asafiri halafu huyo Semi asijue, ni ngumu.”
“Mh! Mpigie basi umuulize aliko.”
“Hapana, nitamshtua mapema sana. Mimi nataka niende naye polepole hadi aingie kwenye kumi na nane yeye mwenyewe.”

“Na kweli, ni wazo zuri sana. Ukifanya papara unaweza kupoteza ushahidi lakini ukienda naye polepole itafika mahali kila kitu kitakuwa kweupe.”

Baada ya hapo, waliagana lakini James hakutaka kuondoka na kumruhusu Kindaundau kuanza kutoka. Nyuma, James alizama kwenye kumfikiria Lina kama habari alizozipata ni za kweli!

“Mimi nahisi Kindaundau amechanganya majina. Siku hizi majina yanafanana sana. Unaweza kuwapata Lina Joseph Ambakucha hata saba, tatizo liko wapi? Na kama kweli ni Lina mke wangu, kwa nini amsevu mumewe kwa jina la Bro Semi…

“Halafu, mpaka nifunge ndoa na mke wake, yeye Semi alikuwa wapi? Tena ndoa ilitangazwa kwa siku ishirini na moja kanisani. Itakuwa si kweli.”

Hata hivyo, nyuma ya mawazo yake hayo, James alipata mawazo mengine yanayompa ushahidi kuwa ni kweli Lina aliyemsema Kindaundau ndiyo Lina wa Semi.

“Lakini si nilimsikia Lina akizungumza na mlinzi wa kazini kwake na akamtaja Kindaundau? Inawezekana ikawa ni Lina huyu kweli. Hata mahudhurio yake kwenye fungate hayakuwa mazuri, lakini ninavyojua mimi mwanamke akishafunga ndoa kukaa honeymoon ni kazi ndogo, sasa yeye kila siku alikuwa akitoa sababu.”

***
Lina alitoka kazini jioni na kurudi nyumbani kwake kwa Semi lakini huku akiwa na wasiwasi kwamba, endapo James atampigia simu na kutaka kuzungumza na mama yake atampa nani, maana mama mpika chai alikuwa ameshaachana naye.

Pia alishangaa sana kwani James hakumpigia simu kwa muda mrefu wakati si kawaida yake.
Alifika nyumbani kwa Semi na akili moja tu kwamba, James akipiga simu asipokee kesho yake akienda kazini ndiyo atampigia na akitaka kuzungumza na mama yake atampa mama wa chai.
***
Ilikuwa usiku wa saa tano Lina akiwa kitandani kwake na kanga moja tu, James hakumpigia simu. Akaingiwa na wasiwasi, akampigia akiamini kwamba kama atataka kuongea na mama yake atamwambia amashalala. Simu ya James iliita mara nane bila kupokelewa…
“Mh! Kuna kitu,” alisema Lina akianza kuogopa. 
Usiku ulipita lakini Lina hakupata usingizi kwani kila wakati alikuwa akishtuka na kuiangalia simu yake kama ataona missed calls au meseji za James…
“Hivi huyu ana nini? Mbona si kawaida yake?” alijiuliza Lina huku akiwa na mawazo kibao kichwani mwake.
***
Kulikucha,  Lina alitoka kitandani huku mwili ukikataa kwani hakuwa amepata usingizi mzuri usiku uliopita kwa kumuwaza James.
Alijiandaa kwenda kazini huku akili ikimwambia ni siku nyingine ya mpambano ambapo itabidi atumie akili sana kuwepo kazini ili asibambwe na James.
Alipofika kazini tu, alipitiliza hadi kwenye chumba cha mama mpika chai…
“Shikamoo mama nanihi…”
“Marhaba, mbona leo upo kama umechoka sana?”
“Ni kweli kabisa. Yaani sijalala.”
“Kisa?”
“Kisa ni James. Toka jana hajanipigia simu wala kunitumia meseji, nimempigia simu hajapokea. Mpaka kunakucha hajawasiliana na mimi.”
“Unahisi nini?”
“Nahisi kuna kitu.”
“Kitu kama kipi?”
“Nahisi ameambiwa mchezo na mtu.”
“Mchezo gani?”
“Si kunioa mimi wakati nina ndoa nyingine?”
Lina hakutaka kujadili sana na mwanamke huyo, akatoka kwenda kwenye meza yake ambapo alikaa akitupa macho getini. Uzuri wake, meza yake akikaa alikuwa akiliangalia geti kwa mbele hivyo, mtu yeyote aliyeingia ilikuwa lazima amuone.
Aliwasha kompyuta lakini ile anaanza kushika makaratasi tu, James aliingia getini, Lulu akatoka mbio hadi kwenye chumba cha mama mpika chai…
“Kaja…kaja, ndiyo anaingia…”
“Nani?”
“Si James!”
“Kwa hiyo?”
“Naomba uende mama. Mpaka atakapoondoka ndiyo urudi.”
“Chai?”
“Nitapika mimi.”
Mama huyo alitoka, akamkuta James ndiyo anaingia mapokezi…
“Karibu sana.”
“Asante. Za kazi?”
“Kazi nzuri.”
“Naona bibie hajarudi.”
“Ee, bado.”
“Oke. Meneja yupo?”
“Yupo ofisini kwake.”
James alipitiliza hadi ofisini kwa meneja huyo.
Baada ya dakika tano, meneja alitoka peke yake na kwenda hadi kwenye chumba cha jiko…
“Lina yuko huku?” aliuliza akifungua mlango.
“Nipo bosi, nakunywa chai.”
“Leo chai unanywea huku?”
“Nimeona ninywee huku bosi.”
“Kuna mgeni kule kwangu, mletee maziwa ya moto bila sukari wala kitafunwa,” alisema bosi huyo huku akitoka. Lina alitazamana na mwanamke huyo kisha akasema…
“Siri inafichuka sasa. Nifanyaje mama nanihi?”
“Mh! Sijui mwenzangu. Na wageni wa kwa mabosi wewe ndiyo unayetakiwa kuwapelekea mahitaji yao, nikienda mimi si itakuwa balaa? Si unakumbuka siku ile nilipeleka kahawa kwa mhasibu wakaniwakia?”
Lina alianza kulia. Aliandaa maziwa huku machozi yakimchuruzika mashavuni, moyoni aliilaani sana siku ya kwanza kukutana na James ambapo ilikuwa kwenye ofisi hiyohiyo.
Alibeba maziwa hayo yaliyokuwa katika kikombe cha dongo na kukiweka kwenye sinia na kwenda nayo. Alipofika mlangoni alisimama, akasali kwa muda kisha akafungua mlango na kuzama ndani.
James alikuwa ameinama akisoma Gazeti la Daily News ambalo ni pana sana hivyo alilishika pembe ya kulia na kushoto kiasi kwamba hakuinua macho kumwangalia Lina.
Lina aliweka sinia na kutoka haraka sana na wakati anafunga mlango akageuka kumwangalia James, bado alikuwa amezama kwenye kusoma gazeti hilo.
Hakuondoka, akasimama na kuchungulia ndani kupitia tundu za funguo kwenye kitasa, akamwona James akiweka gazeti mezani na kupeleka mkono kwenye kikombe cha maziwa.
“Kwa hiyo ile fedha iliyozidi nikupe wewe au mista Brown?” aliuliza James, Lina akaondoka zake. Aliingia kwenye chumba cha chai na kumkuta mama mpika chai akimsubiri kwa hamu kubwa.
“Enhe? Imekuaje?”
“Huwezi amini, nimeshinda mtihani mmoja, bado wa pili. Nimeingia, nimeweka maziwa, nimetoka James hajaniona. Kainama anasoma gazeti.”
“Kweli?”
“Kweli kabisa, sasa nasubiri kwenye kutoa sinia na kikombe.”
“Kwanza unatakiwa urudi mapokezi, uliona bosi amekuja huku ina maana amekupigia simu sana mapokezi hukupokea.”
“Mh! Huo ni mtihani mwingine,” alisema Lina akionekana ana wasiwasi kupita kawaida.
Baada ya nusu saa akiwa bado kwenye jiko, alisikia simu ya mapokezi inaita…
Endelea kulike: www.facebook.com/2jiachie
Tembelea: www.2jiachie.com
 

ITAENDELEA SIKU YA KESHO

No comments

Powered by Blogger.