ad

ad

USIFE KWANZA MPENZI WANGU - 03


Like: www.facebook.com/2jiachie
Web: www.2jiachie.com
Cleopatra analia mbele ya kitanda cha Deogratius, ambaye alikuwa amelazwa baada ya kupigwa risasi. Zilibaki wiki tatu tu, kabla ya ndoa yao. Machozi machoni mwa Cleopatra yaligoma kabisa kufutika!
Dokta akamtoa nje, akimbembeleza na kumpa moyo kwamba asijali, mgonjwa wake angepona. Cleopatra haamini hilo, anazidi kulia kwa uchungu, mawazo tele kichwani mwake yakizidi kumzonga.
Alichowaza yeye ni ndoa tu! Atafungaje wakati mpenzi wake alikuwa amelazwa wodini? Endelea kufuatilia...

AKIWA katika mawazo ya kumuumiza moyo, simu yake ikaita. Akaangalia jina la mpigaji akakutana na jina lililoandikwa ‘My Mumy’. Alikuwa ni mama yake mzazi akimpigia. Kwa muda akaiangalia ile simu akijishauri kupokea, lakini alisita.

Alijua sababu ya simu ya mama yake, kwa vyovyote vile, angetaka kujua kuhusu Deo, jambo ambalo aliamini lingeweza kuamsha machozi upya, kitu ambacho hakutaka kabisa kitokee. Lakini baadaye akaamua kupokea...

“Patra uko wapi?” Ndiyo neno alilokutana nalo baada ya kupokea simu ya mama yake.
“Hospitalini!”

“Upo sehemu gani, maana na mimi tayari nimeshafika hapa Muhimbili!”
“Nipo huku MOI mama!”

“Nakuja!”
Muda mfupi baadaye, mama yake akatokea. Cleopatra alipokutanisha uso na mama yake, machozi kama maji yakaanza kumwagika machoni mwake. Akamkimbilia na kumkumbatia.

“Mama Deo wangu anakufa mama...” akasema kwa hisia za uchungu sana.
“Hapana mwanangu, hutakiwi kuwaza hayo mama...yupo wapi?”
“Wodini!”
“Twende...”

“Hawaruhusu kwenda sasa hivi, muda wa kuwaona wagonjwa umepita!”
“Tatizo ni nini hasa lakini?”
“Amepigwa risasi!”
“Na nani?”

“Hawajulikani mama.”
“Wapi?”
“Mjini. Daktari anasema aliletwa na wasamaria wema baada ya kumuokoa!”

“Maskini, ana hali mbaya sana?”
“Haongei mama, amepigwa risasi ya bega, lakini dokta anasema imekuwa vizuri maana haijatokeza upande wa pili.”
“Mungu ni mwema mwanangu.”

“Namuomba sana amponye ili tufunge ndoa yetu kwanza.”
“Sote ndiyo dua yetu!”
Kwakuwa muda ulikuwa umeshapita wakaondoka kwa ahadi ya kurudi jioni kumuona.

****
Saa 11:00 jioni, Cleopatra na mama yake walikuwa wanaingia katika wodi aliyolazwa Deo. Hawakuamini walipofika kitandani mwake na kumuona akiwa amefumbua macho yake. Cleopatra akalia kwa furaha.
“Pole sana sweetie!”

“Ahsante!” Deo akajibu kwa sauti ya taratibu sana.
“Shikamoo mama...” Deo akasalimia.

“Marahaba mwanangu, pole sana!”
“Ahsante mama!”
“Ilikuwaje?” Cleopatra akauliza akiketi kitandani kwa Deo.

“Hata sielewi, nakumbuka nilikuwa kwenye lifti, nilipofika ghorofa ya tatu lifti ikasimama, wakaingia wanaume watatu, tukaanza tena kushuka hadi ghorofa ya pili, ikasimama tena. Ghafla nikasukumwa nje, kilichofuata ilikuwa ni mlio wa risasi.

“Nikashtuka sana na kupoteza fahamu. Nilipozinduka, nikajikuta nipo hapa hospitalini.”
“Unaweza kumkumbuka kwa sura hata mmoja wao?”
“Hapana.”
“Pole sana, lakini unajisikiaje sasa?”

“Siwezi kujielezea, nahisi maumivu ya mkono na bega, lakini sielewi hali yangu hasa!”
“Pole sana, utapona usijali,” mama yake Cleopatra akasema.
“Nashukuru sana mama.”

Cleopatra akamlisha chakula huku akimwambia maneno matamu ya kumtia moyo! Kidogo Deo akaanza kujisikia vizuri baada ya kupata faraja kutoka kwa mpenzi wake. Muda wa kuwaona wagonjwa ulipopita wakaondoka zao.

“Ugua pole dear, kesho asubuhi nitakuja kukuona.”
“Ahsante sana mpenzi wangu, nakupenda sana. Ahsante kwa kujali kwako!”
“Ni wajibu wangu...utapenda kula chakula gani asubuhi?”
“Chochote tu baby!”

“Chagua mwenyewe mpenzi wangu!”
“Nadhani mtori utanifaa zaidi.”
“Ok! lala salama, ugua pole, you will be okay!”
“Thank you baby!”

Cleopatra na mama yake wakaondoka, wakamuacha Deo akiwa ametulia kimya kitandani, akisikilizia maumivu yake ya bega. Mpaka wakati huo, hakuelewa ni kwanini watu wale walimpiga risasi, maana hakuwa na fedha na wala hawakumwibia! Hilo liliendelea kuzunguka kichwani mwake bila kupata majibu.

***
Anahisi kama ameguswa na mkono wa mtu, anajaribu kuyafumbua macho yake kwa shida kidogo kutokana na mzigo wa usingizi aliokuwa nao! Alilala sana siku hiyo. Uchovu na usingizi ulisababishwa na mambo mawili; Deo alikuwa hajalala usiku mzima kwa maumivu ya bega, ndiyo kwanza asubuhi hiyo alianza kuhisi usingizi.

Dawa alizokunywa, zilikuwa kali na zilimchosha sana mwili wake. Hayo yalitosha kabisa kumfanya, saa moja hii ya asubuhi, macho yake yaendelee kuwa mazito. Anajaribu kuyafumbua kwa shida na kumtazama mtu huyo!
Akashtuka sana!

Hakutegemea kukutana na sura hii hospitalini. Nani amemwambia kwamba amelazwa? Ni jana tu, alipata matatizo, leo hii amejuaje? Nani amempa taarifa za yeye kuumwa? Yalikuwa maswali yaliyofumuka mfululizo kichwani mwake, bila kupata majibu stahiki!
Anazidi kumwangalia mwanamke huyu ambaye naye amesimama kama ameganda...

“Pole Deogratius...pole sana kwa matatizo!” Mwanamke huyo akatamka kwa sauti ya taratibu sana.
Deo hakuitika!

“Maskini Deo, najua ni kiasi gani unaumia, najua kwamba ni jinsi gani ndoa yako itakavyokuwa na ugumu wa kufungwa. Bila shaka mmebakiza wiki tatu tu, sidhani kama utaweza kupanda madhabahuni ukiwa katika hali hii...pole sana...ni majaribu tu ya shetani,” akatamka kwa yakini, akiongea kwa mpangilio mzuri sana.
Deo hakujibu neno!

“Huyu vipi? Amejuaje nipo hapa? Amejuaje natarajia kufunga ndoa? Amejuaje mambo yangu?...amejuaje?” Akazidi kujiuliza Deo, lakini majibu hakuwa nayo.

“Nakupa pole huitiki, kwanini? Au hujapenda mimi kuja hapa?” Mwanamke yule akasema, akionekana kusononeka na mapokeo ya Deo.

Kwa ghafla sana, macho ya Deo yakaanza kupatwa na unyevunyevu, baadaye machozi yakaanza kuchuruzika machoni mwake. Ubongo wake ukasafiri miaka kumi nyuma. Akayatupa macho yake juu ya dari, kisha kumbukumbu zote za maisha yake yaliyopita zikaanza kumjia kama anatazama sinema ya kusisimua...

Sinema ya maisha yenye kila aina ya machafuko na mataabiko. Mateso, dhiki na kuonewa. Masimango, kutukanwa na kudhalilishwa. Ilikuwa sinema mbaya, lakini yenye mwisho mzuri wa kupendeza, mwisho ambao baadaye uliingia shubiri.
Ikawa chungu!
Sinema ikaanza...

Oktoba 22, 1999 – Dar es Salaam
Ni siku nyingine ya pilikapilika, kama ilivyokuwa kwa siku zilizotangulia, leo pia Deo ameamka saa 11:00 alfajiri kama kawaida yake. Alipoamka kitu cha kwanza kufanya ni kumwagilia maji maua, kufanya usafi wa mazingira na kuwapeleka watoto shule.

Aliporudi, alitoka nyumbani kwa bosi wake Mburahati, akaenda sokoni Tandale, kilometa zaidi ya kumi na tano kwa miguu. Hapo ndipo anapofanya kazi ya kuuza mchele hadi saa 11:00 jioni, anapoanza safari nyingine ya kurudi nyumbani kwa miguu.

Siku yake humalizika kwa kufunga mifuko ya barafu hadi saa sita za usiku anapopata muda wa kupumzika, kabla ya kukurupushwa tena alfajiri inayofuata.
Hayo ndiyo maisha yake!

Deogratius Mgana, kijana mchapakazi, hajawahi kupumzika hata siku moja tangu alipoanza kazi katika nyumba ya mzee Maneno, miaka mitatu iliyopita. Alikuja Dar es Salaam, akitokea nyumbani kwao Kiomboi Singida kwa lengo moja tu, kutafuta maisha. Mshahara wake ukiwa ni shingili elfu arobaini na tano tu, kwa kazi zote anazofanya.

Akiwa ametulia kwenye ubao wake sokoni, anatokea dada mmoja mrembo sana. Si mgeni machoni mwake, ni mteja wake wa kila siku, ambaye amekuwa akimhudumia mchele karibu mara mbili au tatu kwa wiki!
“Mambo kaka?” Dada yule akamsalimia.

“Poa, karibu!”
“Ahsante, nipimie kilo tano!”
“Usijali!”

Deo akampimia mchele aliohitaji na kumuwekea kwenye mfuko, kisha akampa. Yule msichana akalipa na kuondoka...baada ya hatua nne, akarudi tena.

“Samahani kaka, nimeshakuwa mteja wako wa kudumu sasa, nadhani ni vizuri kujua jina lako. Mimi naitwa Levina, wewe je?”
“Deogratius, lakini wengi wanapenda kuniita Deo!”
“Nashukuru kukufahamu, sasa nimeridhika, kwaheri!”
“Poa!”

Deo alimwangalia Levina hadi alivyoishilia, namna alivyokuwa akitembea, namna alivyokuwa akiongea vilimpa picha ya tofauti sana. Alianza kuhisi eti huenda Levina anampenda, lakini alijishangaa, maana lilikuwa jambo gumu kidogo!

Levina ampende yeye?
Muuza mchele?
Mbona alikuwa anawaza mambo makubwa sana? Lakini bado hakutaka kuuhakikishia ubongo wake moja kwa moja juu ya hilo. Aliamini kwamba lazima kulikuwa na kitukinaendelea. Kwanini atake kujua jina lake? Ana umuhimu gani hasa?

“Au zali la mentali nini? Si kawaida mteja kutaka kujua jina langu bila sababu za msingi. Lazima kuna kitu kinaendelea, lazima....” akawaza Deo akiwa anamwangalia mpaka anavyoishilia mbali.

Akabaki akiwa na mawazo mengi kichwani mwake, tayari hisia za mapenzi dhidi ya Levina zilianza kumuingia, lakini aliwaza sana namna ya kumuingia, hakuwa na hadhi ya kutoka na Levina.

****
“Mambo Deo?”
“Poa Levina, mzima?”
“Nipo poa!”
“Za nyumbani?”
“Salama kabisa.”

“Ngapi leo?”
“Pima kilo kumi!”
“Wewe kwani mna sherehe?”
“Hapana ni bajeti tu!”

Deo akapima mchele alioagizwa, akamimina kwenye mfuko na kumkabidhi Levina, aliyeupokea huku akiachia tabasamu mwanana kabisa.
“Ahsante sana Deo!”
“Nashukuru pia!”
“Samahani Deo, naweza kupata namba zako za simu?” Levina akamwuliza.

“Simu?”
“Ndiyo!”
“Mimi sina, labda nikupe namba za nyumbani!”
“Hapana, nataka namba zako mwenyewe!”
“Sina.”

“Kwanini?”
“Maisha Levina!”
“Ok! basi chukua zangu...ukimaliza kazi zako nipigie kwenye kibanda cha simu, nahitaji kuzungumza na wewe!” Levina akasema akiandika namba na kumkabidhi Deo akiambatanisha na noti ya elfu tano.
“Ahsante sana Levina, nitakupigia!”
“Usiache tafadhali, ni muhimu sana!”
“Sawa.”

Levina ni nani hasa? Anataka kumwambia nini Deo? Fuatilia inayofata endelea kushare atakaye ongozaKU-SHARE atatumiwa simulizi hii ya mbele kabla ya muda.
..

No comments

Powered by Blogger.