VITILIVYOGO (PAPA NA MUHOGO) - 15
MTUNZI: DK. AMBE
Endelea kulike ==>www.facebook.com/2jiachie
Muda wote alikuwa ajiuliza jioni itakuwaje kikao chake na shoga yake kipenzi aliyegeuka mbogo na kutaka kumpa kipigo cha mbwa mwizi.
Alijiuliza huo ushahidi anaotaka kuutoa ni upi? Picha? Alikataa na kuamini hajawahi kupiga picha na Shaka pia hata kukutana kwao mazingira hayakuwa rahisi kuwatilia mashaka na mtu. Alijipa moyo kusubiri jioni ifike ili atoe ushahidi unaoonesha yeye na Shaka ni wapenzi.
Shaka na Stella wakiwa wanaelekea msalani Stella alimwita Shaka.
“Shaka.”
“Unasemaje?”
“Ukitoka msalani nisubiri.”
“Poa.”
Shaka aliingilia msalani akiwa anajindaa kujibu maswali ya Stella huku akijipanga kupinga shutuma zote atakazoambiwa. Alipotoka msalani alimsubiri pembeni ya choo baada ya muda Stella alitoka na kumsogelea.
“Vipi baby?” Shaka alimuwahi Stella.
“Shaka nimekukosea nini?”
“Kivipi baby?”
“Shaka unadiriki kunizunguka kwa shoga yangu?” Stella alianza tena kulia.
“Stella nimekueleza toka zamani maneno ya watu yatatugombanisha.”
“Si maneno ya watu bali nina ushahidi kumbe jana hukwenda kwenu ulikuwa na Diana.”
“Si kweli, jana nimewahi nyumbani na kutumwa na mama mjini kwenda kumnunulia matunda ya juisi.”
“Sasa jana Diana alienda wapi?”
”Stella hilo swali la kuniuliza mimi?”
“Sasa nimuulize nani?”
“Kwa hiyo mambo ya Stella ushindwe kujua shoga yake nijue mimi hiki si kioja?” Shaka alijifanya kushangaa.
“Si kioja bali unajua kila kitu Shaka,” Stella alianza kulia.
“Stella mambo gani tena haya mpenzi?”
“Shaka kwa nini huridhiki na mimi?”
“Kivipi baby.”
“Mwalimu wewe wanafunzi wewe, kwa nini lakini?”
“Tatizo lako kila mwanafunzi wa kike nikimchekea unajua mpenzi wangu.”
“Sawa ukweli jioni utajulikana.”
“Hakuna tatizo japo naamini sina kosa.”
“Sawa Shaka,” waliongozana mpaka darasani bila kusemezana huku Stella akifuta machozi.
“Usilie baby,” Shaka alimsogelea na kumnong’oneza sikioni.
“Kwa mtindo huu nitaendelea kulia na mwisho nitakunywa sumu.”
“Stellaaa maneno gani hayo!”
“Wewe si unaona raha kunitesa.”
“Basi jioni tutazungumza.”
“Shaka,” sauti ya mwalimu Rose iliwashtua na kufanya wageuke.
“Mnafanya nini?”
“Wewe unataka tufanye nini?” Stella alimjibu mwalimu kwa hasira.
“Stella usimjibu hivyo mwalimu,” Shaka alimzuia.
“Nisimjibu yeye nani? umbeya tu unamsumbua.”
“Stella unamwambia nani?” mwalimu Rose alimuuliza.
“Kwani hapa nazungumza na kima?”
“Stella, Stellaaa!” mwalimu Rose alisema huku akimfuata Stella alipokuwa amesimama.
“Mwalimu acha bwana,” Shaka alimuwahi mwalimu.
“Shaka mwache aje nimwoneshe malaya mkubwa.”
“Mimi malaya?” mwalimu Rose alijitahidi kutoka katika mikono ya Shaka iliyokuwa imemshikilia madhubuti.
“Shaka mwachiee, ukimshika unampa kichwa.”
Bahati nzuri mwalimu Monika alifika kuamua ugomvi ule.
“Jamani mbona aibu kuna nini tena mwalimu na mwanafunzi?”
“Si huyu mtoto.”
“Mimi si mtoto kama unavyofikiria mi mkubwa mwenzako,” Stella alijibu kwa maneno ya nyodo.
“Stella kwa nini lakini, kama hunisikilizi tusijuane,” Shaka alichimba mkwara.
“Nimekusikia Shaka lakini mwambie na mwalimu aache kunifuatafuata mimi si mke mwenzie.”
“Nini?” mwalimu Rose aliyekuwa amepandwa na hasira alitaka kujitoa kwenye mikono ya mwalimu Monika amfuate.
“Mwacheee aje malaya mkubwa umekosa walimu wenzio unafuata wanafunzi.”
“Jamani hebu mwalimu tuondoke wanafunzi wameanza kujaa,” mwalimu Monika alimshika mwenzie na kumpeleka nyuma ya shule kukimbia mkusanyiko wa wanafunzi walioanza kujaa. Naye Shaka alimchukua Stella aliyekuwa akilia kwa hasira na kumtoa eneo la tukio.
Stella pamoja na watu kuondoka alikuwa bado na hasira na kujikuta akishindwa kuzuia hasira zake na kuendelea kulia. Shaka alimfuata na kumbembeleza:
“Stella mambo gani haya?”
“Mambo gani wakati unafurahi.”
“Mi nimefanya nini tena jamani?”
“Hujui? Bila wewe ningetukanana na shoga yangu na mwalimu?”
“Stella hutaki kunisikiliza ungenisikiliza yote haya yasingetokea.”
“Shaka sina moyo wa chuma nina moyo wa nyama naumizwa na matendo yako.”
“Lakini lini ulinikamata na mwanamke?”
“Shaka najua mambo yako mengi jioni utajua nakufahamu vipi?”
“Naomba ujizuie na hasira unakoelekea kubaya, tunaweza kufukuzwa shule.”
“Kwa hili nipo tayari kufukuzwa shule, ina maana wamekuona baada ya kuwa na mimi, kabla yangu wao walikuwa wapi? Huyo Diana mshenzi mkubwa si ndiye alikuwa ananinanga kuwa natembea na mtu asiye hadhi yangu leo ndiyo umekua hadhi yao?”
“Lakini Stella, Diana sina uhusiano naye ni shemeji yangu tu.”
“Narudia tena kukueleza kukuvulia nguo si kwamba sina akili, nina akili zangu timamu kwa vile mapenzi hayana cheo bali kupata kiupacho furaha moyo wako.”
“Ni kweli lakini kuhusu wote unaonifikiria vibaya ni mazoea tu wala sina uhusiano nao wa karibu.”
“Shaka kwa nini umekuwa malaya wa kiume?”
“Stella utanionea bure, heri niache shule maana nina wasiwasi wa kukuharibia muda uliobakia.”
“Shaka tatizo si kuacha shule bali kujiheshimu, wewe si mtoto mdogo usiyejua zuri na baya lipi linafurahisha na lipi linaumiza.”
“Najua unaumia, lakini bado unajiumiza mwenyewe kujiingiza katika mateso ya kujitakia.”
“Shaka unadiriki kusema hivyo? Sawa..sawa jioni ndo utajua najitesa au unanitesa.”
“Sawa, jioni si itafika? Nimekueleza muda mrefu ukifuata ya watu tutatengana huku tunapendana.”
“Si kutengana bali kumkomesha mmoja katika hao wadokozi ili liwe onyo kwa wengine, kwani wanaume wamekwisha mpaka wakufuate wewe?”
“Basi Stella tutazunguza jioni.”
Stella alikwenda kwenye bomba na kunawa uso kisha alirudi zake darasani, Edna alipata nafuu baada ya kuona shoga yake kama kachanganyikiwa kugombana ovyo na kuamini huenda siku ile aliamka vibaya.
Stella akiwa mwingi wa hasira alichukua kitabu chake na kutulia kwenye dawati lake akisoma bila kuelewa kilichokuwa kimeandikwa. Taratibu hasira zake zilianza kushuka na kujikuta akitabasamu baada ya kukumbuka kitu.
Shaka naye alirudi darasani akiwa na msimamo wake wa kutokukubali kuwa ana uhusiano na Edna kwa kujua Stella hajui lolote zaidi ya kubahatisha na jioni angeweza kutoa ushahidi wa maneno ambayo hayana nguvu kwa vile kukutana kwao kulikuwa kwa siri sana.
Kwa hiyo hakuwa na wasiwasi wowote kuhusiana na tuhuma za kutembea na Edna na kujua jioni Stella angeona aibu.
***
Stella aliisubiri jioni kwa hamu, ilipotimu alimuagiza Edna kama kawaida atangulie na Shaka japokuwa moyo ulikuwa ukimuuma lakini aliamini siku ile ndiyo shoga yake angemjua yeye ni nani. Shaka akiwa ametangulia na Edna walipata muda wa kubadilishana mawazo kabla hajafika.
“Shaka mbona Stella anajiamini hivyo ana ushahidi gani?” Edna aliuliza.
“Hana ushahidi wowote zaidi ya kushuku, wewe na mimi ni kukataa kwa nguvu zote.”
“Mmh! Kile kikaratasi nilichokuwa kipo wapi?”
“Nilikitupa.”
“Ulikitupia wapi?”
“Nakumbuka kilikuwa mfukoni naweza kuwa kimefuliwa kwenye kaptula.”
“Msiwe mlikwenda kwenye mambo yebu akakiona ikiwa kimbembe,” Edna alimtaadhalisha Shaka.
“Walaa wasiwasi wako, kuhusu kile kikaratasi ondoa hofu kabisa.”
Wakiwa katika ya mazungumzo walikatisha mazungumzo baada ya kumuona Stella akija kwa mbele. Walipofika walikaa mkao wa kumsikiliza, ilikuwa tofauti alikuja na tabasamu tofauti na walivyofikiria patachimbika, alipofika aliwauliza:
“Jamani vinywaji vipi?”
“Tulikuwa tunakusubiri wewe.”
“Agizeni basi.”
Waliagiza na kuanza kunywa kukiwa kimetawaliwa na kimya, Stella alikuwa wa kwanza kumwita mpenzi wake.
“Shaka.”
“Naam.”
“Huyu ni nani yako?” alimuonesha Edna.
“Semeji yangu.”
“Kwa nani?”
“Kwako.”
“Vizuri, na Edna unamfahamu vipi Shaka?”
“Namfahamu kama mwanafunzi mwenzangu pia shemeji yangu.”
“Shemeji yako kivipi?”
“Kupitia kwako.”
“Vizuri, unamfahamu vipi Shaka zaidi?”
“Kumfahamu zaidi kivipi?” swali lilimchanganya kidogo.
“Unavyomfahamu nje ya ushemeji?”
“Simjui vyovyote nje ya ushemeji kupitia kwako.”
“Eti Shaka?”
“Eti kuhusu nini?”
“Kufahamiana na Edna, ni ushemeji tu au kuna zaidi?”
“Ni shemeji tu.”
“Sasa sikilizeni, huenda mnaniona kama mtoto mdogo mnaweza kunila akili.”
“Kivipi?” Shaka aliuliza.
Stella hakusema kitu alichukua mkoba wa shule na kufungua zipu kisha alitoa kikaratasi na kukisoma kwanza kisha alimpa Edna aliyekipokea alipokitupia jicho moyo ulimpasuka baada ya kukuta ujumbe aliomtumia Shaka upo mikononi mwa shoga yake. Stella aliuona mshtuko wa Edna baada ya kusoma ule ujumbe.
Baada ya ukisoma alitulia wakati huo Shaka tayari aliishagundua nini kimetokea, wakati huo Stella alitembeza macho kwa kila mmoja kumuangalia amepokeaje taarifa ile. Alimuona shoga yake akishusha pumzi nzito kuonesha alishtushwa na ujumbe ule aliomtumia Shaka uliosema: Sasa leo itakuwaje? Si unajua zamu yangu..
“Mpe na Shaka,” Stella alisema kwa sauti ya kistaarabu.
Edna akiwa ametota kama mwanga aliyekamatwa mchana alimpa Shaka kikaratasi kile. Shaka baada ya kukipokea alitulia kusikiliza Stella anataka kusema nini baada ya ushahidi ule.
“Nina imani ujumbe ulioandikwa mmeuona?”
“Ndiyo,” alijibu Shaka, Edna midomo ilikuwa mizito.
“Hebu nielezeni hiki kikaratasi kaandika nani na kilikuwa kinaenda kwa nani?”
Kabla hajapata jibu simu ya Stella iliita alipoangalia ilikuwa inatoka kwa mama yake, alisogea mbali kidogo na kina Edna ili azungumze na mama yake ile ikuwapa nafasi ya kulaumiana.
“Shaka sasa umefanya nini?” Edna alikuwa wa kwanza kuuliza.
“Yaani siamini naona kama mazingaombwe.”
“Mazingaombwe wapi, wakati umefanya makusudi.”
“Nifanye makusudi ili iweje?”
“Ili unigombanishe na Stella.”
“Huwezi kuamini kikaratasi nilikuwa nacho mfukoni nashangaa Stella amekipataje?” Shaka naye alishangaa.
“Ulikaa nacho cha nini, ulishajua kila kitu kwa nini uliendelea kuwa nacho?” Edna aliendelea kumlaumu Shaka.
“Bahati mbaya.”
“Sasa tumelikoroga sijui itakuwaje?”
“Ataamua atakavyo hamtishi mtu,” Shaka alisema kwa kujiamini.
“Kwako hutishiki lakini kwangu msala mzito na wewe ndiye umeniponza,” Edna aliendelea kumlaumu Shaka.
“Umejiponza mwenye bado una mapenzi ya kizamani ya kuandikiana barua ungekuja hata kwa wakati wako si ningekuelewa,” Shaka alijitetea.
“Kwa hiyo umeamua kunikomoa siyo?” Edna alizidi kumlaumu Shaka.
“Edna kuwa muelewa kama ningeamua kukukomoa nisingemdanganya Stella na kukubali mwaliko wako.”
“Sasa tutafanyaje?”
“Wewe ikane hii karatasi kwa nguvu zote, mimi nitaikubali na kumtafuta msichana yeyote kumbambikia lakini kwako nitakuruka.”
“Fanya hivyo la sivyo hali ni tete.”
Walinyamaza baada ya kumuona Stella amesogea karibu, alipofika alisimama kusubiri kupewa jibu la kuhusu kile kikaratasi. Shaka na Edna walibakia kimya wakimtazama. Stella baada ya kutembeza macho kwa wote aliwauliza:
“Jamani mbona mnageuka mabubu naomba jibu langu?”
“Sasa tukujibu nini?” Shaka aliuliza.
“Hamna jibu siyo?” aliuliza huku amewakazia macho.
“Kwangu sina jibu labda Edna,” Shaka alijifanya kujitoa.
“Eti Edna ujumbe huu ulikuwa unamwandikia nani?”
Edna kabla ya kujibu alikifungua tena kile kikaratasi na kukisoma upya kama kigeni machoni mwake. Baada ya kukirudia zaidi ya mara kumi alinyanyua mdomo wake na kusema:
“Kwa kweli sijui lolote.”
“Huu mwandiko wa nani?”
“Siujui,” Edna aliukana mwandiko wake.
“Eti Shaka kikaratasi hiki kakuandikia nani?” Stella alimgeukia Shaka.
“Mi sikijui,” Shaka alijifanya naye kuruka futi mia sita.
“Sasa mimi nimekitoa wapi?”
“Mi nitajuaje, tukuulize wewe?” Shaka alijifanya kumgeuzia kibao Stella.
“Edna wewe ni shoga yangu mkubwa, nimekufanya kama ndugu yangu katika shida na raha, siamini kama unaweza kunifanya hivi. Siku ile tukiwa break niliokota kikaratasi hiki ambacho sikukitilia maanani, wakati nakwenda darasani mnilimuona Shaka anarudi eneo lile kitu kile kilinishtua sana juu ya kile kikaratasi, lakini niliporudi sikukikuta.
“ Japo nilikuwa na wasiwasi na Shaka bila kuelewa kile kikaratasi kinamaanisha nini, baada ya kukikosa nilipuuza yale mawazo japo sikuwaza kama utakuwa shoga yangu kipenzi. Lakini siku ile nilipokipata kikaratasi hiki kwa Shaka na kukichunguza nilishtuka kuona mwandiko wa Edna moyo uliniuma sana.
“Pia hata uondokaji wenu ambao mwanzo niliona wa kawaida nilipata jibu la hiki kikaratasi kukikuta kwa Shaka na mwandiko wako. Pia hata jioni nilipokuja kwenu kukujulia hali sikukuta na kesho yake ulikuwa hujambo kabisa...Shaka kwa nini unanisaliti?” Stella alimgeukia Shaka.
“Kikaratasi hicho umekitoa wapi?” Shaka alijifanya hakijui.
“Kwako.”
“Umekitoaje?”
“Shaka wewe si mtoto wa kiniuliza maswali ya chekechea, leo umetoka kunigombanisha na mwalimu Rose kwa ajili ya umalaya wako. Wakati huohuo unanisaliti na shoga yangu kipenzi?” Stella alimjia juu Shaka.
Mara simu ya Edna iliita alipotaka kwenda kupokelea pembeni Stella alimzuia.
“Pokelea hapahapa hutoki bila kunieleza sababu ya kunigeuka, wewe si ndiye uliyekuwa kimbelekimbele cha kutaka mi na Shaka tuachane kwa vile Shaka ni mtoto mdogo kuwa naye nilikuwa najiaibisha?”
“Sawa ngoja basi nipokee dada ananipigia”
”Pokea,” Stella alijibu huku amekunja uso na kumsimamia mbele kama jini la kutumwa.
Edna aliona maji yamefika shingoni baada ya kila kitu kuwa wazi kama vazi la kahaba. Huku kijasho cha kuumbuka kikimtoka alipokea simu ya dada yake.
MTUNZI: DK. AMBE
Endelea kulike ==>www.facebook.com/2jiachie
ANGALIZO: ITAENDELEAMPAKA MWISHO HAPA KAMA SHARE ZITAFIKA 3,000 NA COMMENT 2,000 VINGINEVYO MTAMALIZIA KATIKA KITABU

Post a Comment