MOYO WANGU BADO UNAVUJA DAMU - 09
Akatoka darasani na kisha kuanza kurandaranda katika maeneo kadhaa ya chuoni pale huku lengo lake likiwa ni kuwatafuta Walter na Nuru. Aliendelea kuwatafuta zaidi na zaidi lakini hakufanikiwa kuwaona katika mazingira ya chuoni hapo.
Akili yake haikubadilika hata kidogo, kwake aliona kukosa mapenzi ilikuwa ni sawa na kukosa pumzi ambapo baada ya muda fulani angepoteza maisha yake. Kichwani hakufikiria jela wala kifungo chochote cha maisha kama tu angediriki kuua, kitu ambacho alikuwa akikijali kwa wakati huo ni kufanya mauaji tu.
Kwake ikaonekana kuwa kama bahati mara baada ya kuliona gari la Walter likiingia katika eneo la chuoni hapo. Kwa mwendo wa taratibu na wa kujificha uso wake akaanza kusogea kule lilipokuwa limesimama kwa kuamini kwamba Nuru alikuwa ndani ya gari lile.
Akakichukua kisu chake kutoka katika mfuko wa madaftari yake na kuendelea kuwasogelea. Mapigo yake ya moyo yalikuwa yakimdunda kwa kasi, woga ukaanza kumuingia moyoni mwake, akaupiga moyo wake konde na kuzidi kuwasogelea.
Walter na Nuru hawakuwa na hili wala lile, walikuwa wakienndelea kusogea kule kulipokuwa na madarasa. Walikuwa wameshikana mikono huku wakionekana kutokujua kitu chochote kama msichana ambaye alikuwa akija kwa mwendo wa taratibu mbele yao alikuwa Beatrice.
Kilikuwa ni kitendo cha ghafla na cha kushtukiza, Beatrice alipoona amewafikia, akaupeleka kisu kile tumboni mwa Nuru. Kwa bahati nzuri wakati kisu kikielekea tumboni mwake, kidogo Nuru akayumba jambo ambalo lilisababisha kile kisu kumchuna ubavuni mwake na kuacha jeraha kubwa.
“Ahhhhh...!” Ilikuwa ni sauti iliyosikika kutoka kwa Nuru.
Walter akamwangalia Nuru ambaye alikuwa ameinama chini akilia. Walter hakujua ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea, alipoagalia nyuma, alimuona msichana ambaye alikuwa akimfahamu kwamba ni Beatrice akikimbia.
Walter akamuinamia Nuru pale chini, Nuru alikuwa akilia kama mtoto mdogo huku ubavu wake wa kulia ukionekana kutokwa na damu zilizokuwa zimeloanisha fulana ambayo alikuwa ameivaa. Walter akaonekana kuchanganyikiwa, akaipandisha fulana ya Nuru na kuanza kuangalia kujua ni kitu gani kilikuwa kimetokea.
Alama ya kuchanwa na kisu iikuwa inaonekana vizuri huku nyama ya ndani nyeupe ikionekana. Walter hakutaka kupoteza muda, akamuinua Nuru na kisha kuanza kwenda nae ndani ya gari. Nuru alikuwa akiendelea kulia kwa maumivu makali.
Hakukuwa na mtu yeyote ambaye alikuwa ameliona lile tukio ambalo lilikuwa limetokea, ni Walter tu ndiye ambaye alijua kwamba aliyefanya vile alikuwa Beatrice. Njia nzima Nuru alikuwa akilia kwa maumivu makali,Walter alikuwa akiendesha gari kwa kasi huku lengo lake likiwa ni kufika haraka katika hospitali ya Hindu Mandal.
Mara baada ya kufika, akamteremsha Nuru ndani ya gari na kuanza kuelekea ndani ya hospitali ile. Bado Nuru alikuwa akiendelea kulia kwa maumivu makali, kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo alizidi kupoteza damu nyingi.
Manesi wakamchukua na kumpeleka katika chumba maalumu na kisha kumlaza. Walter alibaki akiwa benchini huku akionekana kama mtu aliyechanganyikiwa, kadri ambavyo alivyokuwa akimkumbuka Beatrice, hasira zilikuwa zikimpanda kichwani.
Hakumpenda tena Beatrice, tena kitendo kile ambacho alikuwa amekifanya ndicho ambacho kilionekana kumkasirisha kupita kawaida. Hapo alikuwa akitaka kuona ni kitu gani ambacho kingemtokea Nuru, kile ambacho kingemtokea Nuru na ndicho ambacho angekwenda kukisababisha katika mwili wa Beatrice.
Kitu kingine kikaja kichwani mwake, alikuwa akijiuliza kama lilikuwa jambo zuri kuwataharifu wazazi wa Nuru au la. Jibu alilokuja nalo lilikuwa ni kuwapa taarifa ili wajue ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea.
Hapo hapo akaichukua simu yake na kisha kuanza kuangalia majina ambayo yalikuwepo ndani ya simu ile na kisha kulitafuta jina la mzee Brown na kumpigia. Simu ikaanza kuita, wala haikuchukua muda mrefu, sauti nzito ya mzee Godson ilikuwa ikisikika.
“Hujambo Walter!” Mzee Godson alimsalimia.
“Sijambo mzee. Shikamoo”
“Marahaba. Mwenzako hajambo?” Mzee Godson aliuliza swali ambalo lilisababisha ukimya a muda.
“Hapana. Kuna tatizo limetokea. Hili ni tatizo kubwa ambalo linanifanya kuwahitaji sana mje Dar e Salaam mara moja” Walter alimwambia mzee Godson.
“Tatizo gani?”
“Halielezeki. Naomba mje haraka, akili yangu imechanganyikiwa sana” Walter alisema na siku kukatwa.
Walter akakiinamisha kichwa chake chini, kwa mara ya kwanza machozi yakaanza kutoka kwa ajili ya msichana, moyo wake ulikuwa umemuuma kupita kawaida, kila alipokuwa akikumbuka mambo mengi ambayo alifanya na Nuru, alionekana kuumia.
Mara kwa maraalikuwa akiupiga ukuta ngumi na wala hakusikia maumivu yoyote yale. Alimchukia sana Beatrice kiasi ambacho alitamani sana akutane nae na kumfanyia kitu kibaya ambacho asingeweza kukisahau katika maisha yake yote.
“Nitamuua...nitamuua huyu msichana na kama nitamkosa kosa kumuua, nitamfanya kuwa mlemavu maisha yake yote” Walter alisema.
Kila dokta ambaye alikuwa akiingia ndani ya chumba kile na kutoka alionekana kuwa bize, Walter hakujua ni dokta yupi ambaye alitakiwa kumuuliza juu ya hali ya Beatrice ambayo alikuwa akiendelea nayo.
Masaa mawili yaapita na ndipo Bwana Godson na mkewe, Bi Catherine kuingia katika hospitali hiyo. Macho yao yakagongana na macho ya Walter ambayo yalikuwa yamevimba kwa sababu ya kulia sana. Wote wakajikuta wakiishiwa nguvu.
“Vipi Walter. Kuna nini?” Bwana Godson aliuliza huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Nuru....”
“Amefanya nini?”
“Alichomwa kisu” Walter alijibu.
Jibu lile likaonekana kumshtua kila aliyelisikia, Bi Catherine akakosa nguvu, akajiweka benchini, tayari machozi yalikuwa yakimtoka, hakuamini kile ambacho alikuwa amekisikia kutoka kwa Walter. Kilio kikaanza kusikika kutoka kwa Bi Catherine, aliumia kupita kiasi.
“Kwa sasa sihitaji ushauri wala huruma. Ni lazima niue. Ni lazima niue” Bwana Godson alisema kwa hasira.
“Hapana mzee. Hii kazi hautakiwi kuifanya wewe” Walter alimwambia Bwana Godson.
“Hapana. Nimeumia sana”
“Najua. Ila hii kazi acha niifanye mimi. Sitomuua ila nitamfanya kuwa kilema katika maisha yake yote. Kila atakapokuwa akijiangalia basi ataweza kunikumbuka maishani mwake” Walter alisema huku akionekana kuumia.
“Hapo bado unamuonea huruma”
“Hiyo dio njia nzuri. Nataka kuziharibu kumbukumbu zake milele. Niachie mimi na kila kitu kitakuwa salama” Walter alisema.
Bwana Godson hakuwa na jinsi, kila alivyokuwa akimwangalia Walter na maneno yale ambayo alikuwa akiyaongea yalionekana kumaanishwa. Hakutaka kumjua mtuambaye alikuwa amesababisha yale yote kwani aliamini kama angemfahamu basi hata masaa manne hasingechukua.
Muda wa kuona wagonjwa ulipofika, wakaingia ndani ya chumba kile. Macho yao yakatua usoni mwa Nuru ambaye alikuwa amelala kimya huku dripu ya maji ikiwa inaning’inia juu yake. Kila mmoja alionekana kuumia kupita kawaida. Ubavuni mwake alikuwa na bandeji kubwa ambayo kwa mbali damu zilikuwa zikionekana. Nuru alikuwa kimya huku akionekana kuwa kama mtu ambaye alikuwa amekwishakata roho.
“Haiwezekani. Ni lazima nifanye kitu sasa hivi” Walter alisema kwa hasira, akatoka chumbani mule na kuelekea nje ambapo akaingia garini mwake na kisha kuondoka mahali hapo huku lengo lake ikiwa ni kutaka kumfanyia kitu Beatrice ambacho asingekuja kukisahau katika maisha yake yote.
************
Walter alikuwa akiliendesha gari lake kwa mwendo wa haraka ambao ulionyesha dhahiri kwamba alikuwa akiwahi kitu fulani. Kichwa chake kilikuwa na mawazo juu ya mpenzi wake, Nuru huku akiwa na hasira kali juu ya mpenzi wake wa amani ambaye alitokea kumchukia, Beatrice.
Hakukuwa na kitu kingine alichokuwa akikifikiria kichwani mwake zaidi ya muaji tu. Mikono yake ilikuwa na hamu kubwa ya kufanya mauaji katika wakati huo. Kwake hakuonekana kujali kitu chochote, alikuwa radhi kufungwa kifungo cha maisha jela lakini si kumuacha Beatrice aendelee kuishi.
Breki ya kwanza akaifungia nje ya geti lao, kama steringi akaufungua mlango na kutoka ndani ya gari lile na kuanza kuelekea ndani ya eneo la nyumba yao. Mlinzi wao akaonekana kushangaa, hakuwahi kumuona Walter akiwa katika hali ile hata siku moja. Aliamani kuuliza lakini akaamua kukaa kimya kwa kuepuka kuanzisha zogo mahali hapo.
Walter akaingia ndani ya nyumba yao na kisha kuanza kuelekea chumbani kwake. Wala hakukaa sana, akatoka huku akiwa na ufunguo mwingine ambao ulikuwa wa akiba. Akaufuata mlango wa chumbani kwa wazazi wake na kisha kuufungua.
Akaingia na kuanza kutafuta kitu fulani. Akaanza kufungua katika droo ya kitanda, alichokuwa akikitafuta wala hakukiona. Akaendelea zaidi na zaidi, akafungua kabati la nguo na kuanza kukitafuta kitu hicho mahali humo. Akafungua droo ya kabati lile, macho yake yakatua katika kitu ambacho alikuwa akikitaka, bastola, akaichukua.
Akaiweka kiunono na kuifunika na fulana ambayo alikuwa ameivaa na kisha kuanza kutoka nje. Wala hakutaka kuongea kitu chochote na mlinzi, alichokifanya ni kuingia ndani ya gari lake na kisha kuondoka mahali hapo huku mlinzi akibaki akishangaa tu.
Kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo hasira zaidi zilipozidi kumkamata. Foleni ya magari ambayo ilikuwa barabarani ndio ambayo ilikuwa ikizidi kumkasirisha kupita kawaida, alitamani gari lake lingekuwa na uwezo mkubwa wa kutoa mabawa ili alipaishe na kufika chuoni haraka ambako huko ndipo alipanga kukamilisha kila kitu bila kuogopa macho ya watu.
Foleni ilikuwa ikisogea taratibu jambo ambalo lilimfanya kukasirika kupitakawaida. Magari yalitembea kwa sekunde thelathini lakini yakasimama kwa dakika tatu. Honi mbalimbali za magari zilikuwa zikipigwa barabarani, kila dereva alionekana kuwa na haraka katika kipindi hicho.
Magari ya upande wao yakaendelea na safari baada ya dakika kumi, Walter alikuwa amevimba kwa hasira kupita kawaida. Kutoka hapo mpaka chuoni alitumia dakika ishirini, akaingia chuoni hapo ambapo akaliki gari lake katika sehemu ya maegesho na kisha kuanza kuelekea katika daraa alilokuwa akisoma Beatrice.
Japokuwa wanachuo walikuwa wakiendelea na masomo yao, Walter akaingia darasani mule na macho yake kuanza kumwangalia kila mtu darasani mule. Kila mwanachuo alionekana kumshangaa Walter lakini yeye hakuonekana kujali.
“Shiiit....Hayupo” Walter alijisemea na kutoka darasani hapo.
Alichokifanya ni kuanza kumtafuta Beatrice katika sehemu mbalimbali chuoni hapo. Katika kila kona ambayo alikuwa akipita, Beatrice hakuwa mahali huko. Walter alionekana kukasirika zaidi, akaanza kulifuata gari lake huku lengo lake likiwa ni kuelekea nyumbani alipokuwa akiishi Beatrice.
Bado hasira kali zilikuwa zikizidi kumshika kupita kawaida. Hakuyakumbuka mapenzi mazito ambayo alikuwa nayo juu ya Beatrice katika miezi michache iliyopita, kitu ambacho alikuwa akikifiria katia kipindi hicho ni kufanya mauaji tu.
Foleni za barabarani zikaonekana kuanza kumkasirisha tena, hizi za sasa hivi zilikuwa kubwa kuliko zile za mwanzo hasa katika barabara ya Salender Bridge. Walter alionekana kukasirika kupita kawaida, kadri muda ulivyokuwa ukienda mbele, alikuwa akikasirika zaidi.
Alikaa katika foleni zaidi ya dakika arobaini na ndipo safari ilikuwa ikiendelea. Kila wakati alikuwa akipiga usukani kwa hasira, foleni zile ambazo zilikuwa zimemchelewesha zilionekana kuanza kumharibia kila kitu.
Alitumia muda wa dakika mia na ishirini mpaka kufika katika nyumba aliyokuwa akiishi Beatrice, akateremka na kuanza kuelekea ndani ya nyumba hiyo. Kadri hatua zake zilipokuwa zikienda mbele na ndivyo ambavyo hasira zilivyozidi kumpanda zaidi na zaidi.
Mlango ulikuwa wazi hali ambayo akaufungua moja kwa moja na kuingia ndani. Nyumba ilionekana kuwa kimya, akaanza kupiga hatua kuelekea katika chumba cha Beatrice, napo hakuwepo humo. Alichokifanya ni kuanza kuelekea sebuleni. Kwa mbali akaanza kuisikia sauti ya Beatrice ikiimba bafuni.
Alikuwa na uhakika kwamba mtu huyo alikuwa Beatrice, alichokifanya ni kuanza kuelekea chumbani na kutulia. Baada ya dakika kadhaa, mlago ukafunguliwa na Beatrice kuingia ndani. Beatrice akaonekana kushtuka mara baada ya kuuona mdomo wa bunduki ukiwa umemlenga.
“Mama yangu!” Beatrice alisemakwa mshtuko huku taulo likimvuka.
“Unashangaa! Unashangaa nini? Unafikiri kile ulichokifanya kwa mpenzi wangu nitakuacha hai!” Walter alimwambia Beatrice.
“Naomba unisamehe Walter” Beatrice akaanza kuomba msamaha, mdomo wa bunduki ambao ulikuwa umemuelekea uliokuwa ukimtisha.
“Haiwezekani hata kidogo. Umeuumiza moyo wangu Beatrice. Kwa kitendo ambacho ulikuwa umekifanya, hakika sitoweza kukuacha hai” Walter alimwambia Beatrice.
Walter hakuonekana kutania hata kidogo, alikuwa tayari kabisa kukibonyeza kitufe kile cha kuruhusu risasi. Huku akiwa amejiandaa kukibonyeza kitufe kile, mara ghafla mlango ukafunguliwa kwa nguvu na wanaume watatu waliokuwa na miili iliyojazia kuingia.
Wote wakajikuta wakiwekwa chini ya ulinzi. Walter hakuwa akiwaelewa watu wale ila alichokifanya ni kuiweka bunduki yake chini na kunyanyua mikono yake juu. Beatice alionekana kuchanganyikiwa, hakuwahi kuwaona watu wale ambao walikuwa wameingia ndani ya nyumba ile, akaambiwa avae nguo zake kwani walikuwa na kazi nae.
Bila ubishi wowote ule, Beatice akaanza kuvaa nguo zake na kisha kutulia huku akisubiri kuambiwa ni nini kilikuwa kikifuatia. Wanaume wale wakamchukua Beatrice na kuanza kutoka nae nje hali ambayo ilionekana kumshangaza Walter.
“Wewe si muuaji. Yaani unaishika bunduki huku mnamrembea. Ngoja tukuonyeshe jinsi wauaji tunavyofanya kazi” Mwanaume mmoja alikwambia Walter.
Walter akaachwa ndani ya chumba kile huku akiwa hajui ni kitu gani ambacho alitakiwa kufanya kwa wakati huo. Kwa haraka haraka nae akatoka nje na kuingia ndani ya gari lake na kuanza kulifuatilia lile gari la wale vijana ambalo lilikuwa limembeba Beatrice.
Alikuwa akilifuatilia zaidi na zaidi. Gari likachukua barabara ya Bagamoyo na kuanza kuelekea Bagamoyo. Bado Walter alikuwa akiendelea kulifuatilia. Mpaka wanafika katika daraja la Mafinga bado Walter alikuwa akiendelea kuwafuatilia.
Walter akajiona kuwa na bahati mbaya hasa mara baada ya kulimaliza daraja hilo, gari lake likaanza kupunguza mwendo huku alamu ya kuashiria kwamba mafuta yalikuwa yameisha ikianza kulia. Kuanzia hapo gari lilitembea kwa umbali wa hatua thelathini tu, likasimama.
“Dah! Basi tena” Walter alisema huku akiliangalia lile gari likienda kwa mwendo wa kasi.
*********
Simon alikuwa na presha kubwa katika kipindi ambacho treni lilikuwa likiingia katika stesheni hiyo ya Dar es Salaam. Kiu yake kubwa ilikuwa ni kutaka kumuona mpenzi wake ambaye hakuwa ameonana nae kwa muda wa miaka sita.
Alisimama katika sehemu ambayo watu waliokuwa wakiwasubiri wageni wao walipokuwa wamesimama. Mkononi mwake alikuwa na maua ambayo alipanga kumgawia mpenzi wake, Violeth mara tu atakapomuona kwa mara nyingine.
Kijasho chembamba kikaanza kumtoka, kwa mbali mwili wake ulikuwa ukitetemeka hasa katika kipindi ambacho treni lilipofunga breki na kusimama. Abiria wakaanza kuteremka, watu ambao walikuwa wakiwasubiria wageni wao wakaanza kusogea huku nae Simon akisogea pia.
Abiria wakaanza kuteremka na kuanza kutoka nje ya kituo kile. Kila mtu ambaye alikuwa akimwona ndugu au rafiki yake alikuwa akionekana kuwa na furaha. Simon alibaki kimya huku akiangalia huku na kule. Abiria walikuwa wengi kiasi ambacho kumuona mpenzi wake, Violeth ilikuwa ngumu.
Alibaki akiangalia huku na kule. Abiria wakaanza kupungua na mwisho wa siku, Simon akajikuta akipigwa na mshtuko ambao hakuwahi kuupata katika maisha yake hasa mara baada ya macho yake kutua kwa msichana ambaye alikuwa na uhakika kwamba alikuwa amekwishawahi kumuona sehemu fulani.
Kwa haraka haraka akaanza kuzivuta kumbukumbu zake kichwani, akakumbuka vizuri na kupata jibu. Msichana ambaye alikuwa amemuona akija alikuwa amekwishawahi kumuona sehemu, ALIKUWA MSICHANA ALIYEMUONA NDOTONI miaka sita ilyopita. Alikuwa na uhakika kabisa kwamba msichana yule ndiye ambaye alikuwa akimfikiria sana katika maisha yake huku akiwa na hamu ya kumuona siku moja.
Siku hiyo ndio ilikuwa siku yenyewe, msichana ambaye alikuwa amemuota ndotoni mwake miaka sita iliyopita alikuwa mbele yake akipiga hatua kuelekea kule alipokuwa amesimama na watu wengine. Macho yake hayakutoka usoni mwa msichana yule ambaye alikuwa akisogea huku akilivuta begi lake.
Simon hakumfikiria tena mpenzi wake, Violeth ambaye alikuwa amekuja kumpokea mahali hapo. Akaanza kupiga hatua kumfuata msichana yule huku lengo lake likiwa ni kuongea nae na kumwambia kwamba alikuwa amekwishawahi kumuota miaka sita iliyopita na kwamba yeye ndiye alikuwa mke wake wa halali ambaye alitakiwa kuwa nae.
Huku akizidi kumsogelea msichana yule, nae msichana yule akaanza kumsogelea huku uso wake ukionekana kujaa tabasamu. Ghafla msichana yule akaanza kumkimbilia kwa furaha. Simon akabaki akiwa ameshtuka, maswali kibao yakaanza kujikusanya kichwani mwake kama kweli msichana yule alikuwa akimfahamu au nae alikuwa ameoteshwa ndoto kwamba alikuwa mvulana wake ambaye alitakiwa kumuoa.
Mara baada ya kumfikia, akamkumbatia na kumng’ang’ania kwa nguvu zote. Simon hakuwa na jinsi, nae akamkumbatia na kumng’ang’ania kama alivyofanyiwa. Bado Simon hakuonekana kuwa na amani, kichwa chake bado kilikuwa kikimfikiria mpenzi wake, Violeth ambaye angekuja mahali hapo na kumkuta amekumbatiana na msichana mwingine.
“Ndiye mwenyewe....” Simon alisema moyoni huku akimwangalia msichana yule usoni.
“Nimekukumbuka mpenzi. Nimekukumbuka Simon” Msichana yle alisema maneno ambayo yalionekana kumshtua Simon.
“Nimekumiss mpenzi” Msichana yule alisema na kisha kumkumbatia tena.
Simon akapigwa na mshtuko, kwake, tukio lile likaonekana kuwa kama ndotoni ambapo baada ya muda fulani angeamka na kujikuta akiwa kitandani. Akaanza kumfikiria msichana yule kama alikwishawahi kuona katika sehemu nyingine zaidi ya ndotoni, jibu alilokuja nalo, lilikuwa HAPANA.
“Uliwahi kuniona wapi?” Simon alimuuliza yle msichana huku akionekana kumshangaa.
“Unasemaje mpenzi? Mimi ni mpenzi wako......VIOLETH” Msichana yule alitoa jibu ambalo lilimfanya Simon kutaka kuzimia pale alipokuwa amesimama.
*******
Miaka sita ambayo walikuwa mbalimbali pasipo kuonana ilionekana kumbadilisha Violeth kabisa kiasi ambacho ingekuwa ngumu sana kujua kama Violeth huyu ndiye alikuwa Violeth yule ambaye aliachana na Simon miaka sita iliyopita.
Kila wakati Simon alikuwa akimwangalia Violeth huku akionekana kutokuamini kama yule msichana ambaye alikuwa amemuota miaka sita iliyopita alikuwa msichana huyu ambaye alikuwa mbele yake na tena ambaye alikuwa katika uhusiano nae kwa miaka sita.
Ingawa alikuwa akiendesha gari kuelekea nyumbani lakini bado macho yake yalikuwa yakimwangalia Violeth. Hakujua ni kwa jinsi gani angemweleza mama yake juu ya Violeth ambaye alikuwa msichana ambaye alikuwa akimfikiria katika kipindi kirefu.
Alijiona akiendesha gari kwa mwendo mdogo hali iliyomfanya kuongeza kasi. Kutoka stesheni mpaka nyumbani iliwachukua dakika arobaini na tano. Wote wakateremka na kisha kuanza kuelekea ndani. Muda wote huo Simon alikuwa akitabasamu tu, hakujua ni maneno gani ambayo alitakiwa kuongea ili aielezee furaha ambayo ilikuwa moyoni mwake.
“Karibuni” Bi Martina aliwakaribisha.
“Asante” Violeth aliitikia.
Siku hiyo ilikuwa ni furaha kwa kila mmoja, kuwa tena pamoja kwa mara nyingine kulionekana kuwafurahisha kupita kawaida. Hawakutaka kuficha kitu chochote kile, muda wote walikuwa wakiyaonyesha mapenzi yao ya dhati hadharani.
Hawakuwa wakimuogopa mtu yeyote yule, kila mmoja kichwani mwake alikuwa akifikiria kwamba tayari walikuwa wamekwishfunga ndoa na kuwa mume na mke. Chakula kikaandaliwa na kula pamoja, baada ya saa moja wakaingia chumbani kwa ajili ya kulala.
Usingizi wala haukupatikana, walikuwa wamekaa kitandani huku wakiangaliana tu. Kama kawaida yao, michezo ya kupigana na miito ikaanza kitandani pale. Walicheza kwa zaidi ya dakika thelathini na kujikuta wakikumbatiana tu.
Wakaanza kuangaliana kama simba ambao walikuwa wakitaka kupigana. Simon akamkaribia Violeth zaidi na kisha kuubusu mdomo wake. Miili yao ikaanza kuwasisimka kupita kawaida, wakajikuta wakianza kupapasana na hatimae baada ya muda wakajikuta wakiwa watupu.
Kwa mara ya kwanza wakafanya mapenzi kitandani hapo. Lilikuwa ni tendo ambalo liliwapa furaha na kufanya kwa nguvu zote kana kwamba wasingeweza kufanya tena baada ya hapo. Walimaliza baada ya saa moja na nusu kuisha na ndipo wakainuka na kueleka bafuni kuoga.
Bafuni walikuwa wakisuguana tu kiasi ambacho kikaifanya miili yao kutamaniana tena, mchezo ukarudiwa kule kule bafuni. Walikuwa wakiendelea kufanya kwa nguvu zote huku kila mmoja akijitahidi kumuonyeshea mwenzake ufundi wake.
Walipomaliza wakarudi chumbani ambako huko napo mchezo ukaanza upya. Walijikuta wakifanya mpaka saa kumi na mbili na ndipo wakapumzika huku kila mmoja akionekana kuchoka.
“Sitaki kuchelewa mpenzi, ni lazima nikatoe barua wiki ijayo” Simon alisema.
Alichokisema ndicho ambacho alikifanya, barua ikaandikwa na kupelekwa kwa wazazi wa Violeth na baada ya muda fulani mahari kutolewa. Kila kitu kilikuwa kimeendelea katika mpangilio mzuri, miezi miwili ilipokwisha, wawili hao wakaoana mbele ya umati wa watu hasa madaktari ambao ndani ya kanisa la Praise And Worship.
Hapo ndipo wakaanza maisha ya ndoa, kila mmoja alikuwa akimpenda na kumuhitaji mwenzake. Mambo mengi mabaya yenye vituko ambayo walikuwa wamepitia katika maisha ya nyuma yalikuwa yamebaki kama historia, hawakutaka kukumbuka mabaya.
*******
Nuru alionekana kuumia kupita kawaida mara baada ya kushambuliwa na Beatrice chuoni. Alitamani kumwambia baba yake juu ya Beatrice lakini kitu alichokifanya ni kuwaeleza kisiri pasipo Walter kufahamu kitu chochote kile.
Mbele ya Walter, Nuru alionekana kuwa na moyo uliojaa msamaha na kutokujali ila moyoni mwake alikuwa ameumia kupita kawaida. Katika maisha yake hakuwahi kumchukia msichana yeyote kama ambavyo alivyomchukia Beatrice.
Alichokifanya mara baada ya kumwambia baba yake ni kuanza kuona ni kitu gani ambacho kingetokea. Wala hazikupita siku nyingi na ndipo alipochomwa kisu ubavuni. Mzee Godson alipokuja kuligundua hilo, moja kwa moja akajua kwamba Beatrice ndiye ambaye alikuwa amefanya tukio lile.
“Ni lazima nimfanyie kitu” Mzee Godson alijiseme.
Kitu cha kwanza alichokifanya kabla ya kuondoka Kilimanjaro kuja jijini Dar es Salaam ni kuwasiliana na vijana wake na kuwaambia kila kitu kilichotokea. Kitu ambacho waliamua kufanya vijana wale ni kuanza kuelekea chuoni hapo na kuanza kumuulizia Beatrice.
Wala haikuwa kazi kubwa, wakaambia darasa analosoma mpaka mahali anapokaa. Kila mmoja akaonekana kuridhika, ni kazi moja ambayo ilikuwa ikisubiriwa kufanyika. Vijana wale wakajikusanya sehemu na kuanza kupanga mipango ya kumfuata Beatrce nyumbani kwao.
“Tumuueni huko huko au?” The Killer aliuliza.
“Hapana. Bosi hakutoa amri ya kumuua” Zinja alijibu.
“Yeye alitoa amri gani?”
“Tumfanye kitu chochote ambacho kitamfanya kujuta maishani kwa kumgusa mtoto wa mwenye pesa” Zinja alijibu.
“Sawa”
Mipango ikapangwa kama ambavyo ilitakiwa kuwa. Mara ya mwisho walipompigia simu mzee Godson na kumueleza kwamba walikuwa wakienda kuanza kazi ambayo alikuwa amewapa, aliwaonya kuhusu kitu kimoja.
Mzee Godson alifahamu kwamba Walter alipoondoka mahali hapo basi ilikuwa ni lazima alikuwa akielekea nyumbani kwa kina Beatrice. Akawaambia kwamba hawakutakiwa kumjeruhi mwanaume yeyote ambaye wangemkuta kule hata kama angekuwa katika hali gani.
Hakukuwa na ubishi wa mtu yeyote kupinga, wakaanza kuelekea huko ambako wakamkuta Walter akiwa amemuelekezea bunduki Beatrice. Walichokifanya ni kuwaweka wote chini ya ulinzi na kisha wao kuondoka na Beatrice ambaye walikuwa na shida nae.
Gari lao bado lilikuwa likielekea Bagamoyo huku likiwa katika mwendo wa kasi. Hakukuwa na mtu ambaye alikuwa akifahamu kama Walter alikuwa akiwafuata. Wakapita katika daraja la Mapinga kwa mwendo wa kasi.
Muda wote Beatrice alikuwa akilia huku akiomba msamaha pasipo kufahamu ni kitu gani alikuwa amekifanya. Tayari mbele yake alikuwa amekwishaona hatari kubwa ambayo ingeweza kupoteza hata maisha yake.
Kilio cha kuomba msamaha bado kilikuwa kikiendelea kusikika lakini hakukuwa na yeyote ambaye alioekana kujali, bado walionekana kuwa na hasira na Beatrice. Gari lile wala halikufika Bagamoyo mjini, likaanza kuingia porini ambako baada ya mwendo fulani wakalipaki na kumshusha Beatrice.
“Chagua tukuue kwa kukupiga risasi za wapi?” Zinja aliuliza.
Beatrice hakujibu kitu chochote kile zaidi ya kuendelea kulia huku akiomba msamaha wa kuachiwa. Hakukuwa na mtu ambaye alikuwa akimsikiliza na kumuelewa.
“Tatizo unawachokoza wenye hela. Yaani unamchokoza mtu pasipo kumjua huyo ni nani” Zinja alisema huku akiwa amemuelekezea bunduki Beatrice aliyekuwa chini akilia.
Hakukuwa na sababu ya kuendelea kupoteza muda, hapo hapo zinja akaachia risasi nne ambazo zilikwenda kupenya katika miguu ya Beatrice. Yalikuwa ni maumivu makali ambayo wala hakuwahi kuyapata kabla, Beatrice alibaki akilia huku akiiangalia miguu yake.
Damu zilikuwa zikimtoka katika miguu yake, risasi zile zilipenya na kutoboa miiguu ya mifupa yake. Zinja na wenzake hawakutaka kuendelea kubaki mahali pale, walichokifanya ni kuingia ndani ya gari lao na kisha kuondoka mahali pale huku wakimuacha Beatrice akilia kama mtoto kwa maumivu makali.
*******
Bado Beatrice alikuwa akilia kwa maumivu makali kutokana na risasi ambazo zilikuwa zimepenya katika miguu yake na kuisaga mifupa yake. Alikuwa porini kiasi ambacho kila alipokuwa akilia, hakukuwa na mtu yeyote ambaye alikuja kumsaidia kutoka kule alipokuwa.
Alilia kwa muda wa dakika zaidi ya arobaini, alipoona kwamba hakukuwa na msaada wowote uliokuja kwake akaamua kuanza kutambaa. Ilikuwa ni kazi kubwa iliyojaa maumivu lakini Beatric hakutaka kujali, aliendelea kutambaa.
Mahali alipokuwa kulikuwa na umbali mkubwa mpaka kufika katika barabara ya lami, alitambaa kwa takribani danina kumi, akaamua kupumzika huku damu zikiendelea kutoka miguuni mwake. Yalikuwa ni maumivu makali ambayo hakumbuki kama alikwishawahi kuyapata mwilini mwake katika maisha yake yote.
Bahati ikaonekana kuwa kwake hasa mara baada ya kusikia sauti za watu ambao walikuwa wakitembea kupita njia ile ambayo alikuwa karibu nayo. Hapo hapo akaanza tena kupiga kelele za kuomba msaada hali ambayo ikawafanya wapita njia hao kuja mahali pale alipokuwa.
“Mungu wangu!” Mwanamme mmoja alisema huku akionekana kushtuka.
“Nisai...dieee...niii..” Beatrice alisema huku akionekana kusikia maumivu makali.
Hakukuwa na cha kupoteza mahali hapo, tayari walikwishona kwamba Beatrice alikuwa kwenye hali mbaya, walichokifanya ni kumbeba na kuanza kuondoka nae kuelekea barabarani. Kila mmoja alikuwa na mawazo kichwani juu ya hali ambayo alikuwa nayo Beatrice wakati ule. Hawakuwa na muda wa kuuliza swali lolote lile, walichokiona kukifanya kwa kipindi hicho ni kumsaidia Beatrice.
Ulikuwa ni mwendo wa dakika kumi mpaka kuifikia barabara ya lami ambapo wote wakatulia chini na kuanza kuyapungia magari kuomba msaada. Magari yalikuwa yakipita kwa kasi huku hali ikionyesha madereva wengi walikuwa wakihofia kusimamisha magari porini.
Msamaria mwema mmoja ambaye alikuwa akiendesha gari aina ya Pick Up akalisimamisha gari lake na kisha kuteremka chini. Hali ambayo aliikuta kwa Beatrice ilikuwa imemshtua kupita kiasi. Alionekana kutokuamini kile ambacho alikuwa akikiona kwa Beatrice. Miguu yake ilikuwa ikionekana kuwa kwenye hali mbaya huku wakati mwingine ikionekana kama kutaka kun’goka kutokana na mifupa kuvunjika vunjika.
“Mmmmhh! Nini kimetokea tena?” Dereva yule ambaye alikuwa mzee wa makamo aliuliza kwa mshangao.
“Hata sisi hatujui. Tumemkuta porini akiwa katika hali hii” Mwanaume mmoja alijibu.
Beatrice akapakizwa ndani ya gari lile pamoja na wale wanaume na kisha safari ya kuelekea katika hospitali ya Mwenge kuanza. Safari ilikuwa ndefu, muda wote Beatrice alikuwa akilia kwa maumivu makali. Kwake alipaona hospitali kuwa mbali sana, alitamani afike haraka iwezekanavyo ili apewe tiba.
Walitumia dakika arobaini mpaka kufika katika hospitali ya Mwenge ambapo machela ililetwa na kisha kupakizwa. Kila nesi ambaye alikuwa akiiangalia miguu ya Beatrice alikuwa akisikitika na kuogopa kuiangalia kwa mara nyingine.
Bado kilio cha Beatrice kilikuwa kinaendelea kusikika, alikuwa katika maumivu makali kupita kawaida, akapelekwa katika chumba maalumu kwa ajili ya kufanyiwa mattibabu kwani hali yake ilionyesha kuhitajika kupewa matibabu ya haraka sana.
Kutokana na hali yake kuwa mbaya sana, madaktari wakafanya mpango wa kumpeleka katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako huko ndiko kulikuwa na madaktari wengi waliokuwa na utaalamu na magonjwa mengi.
Gari la wagonjwa likafika hospitalini hapo na kisha kumchukua na safari ya kuelekea Muhimbili kuanza. Risasi ambazo zilikuwa miguuni mwake tayari zilikuwa zimekwishatolewa na kidogo alikuwa akisikia nafuu japokuwa miguu yake ilikuwa katika hali mbaya kupita kawaida.
Magari yote ambayo yalikuwa yakisikia ving’ora vya gari lile la wagonjwa walikuwa wakiyaweka magari yao pembeni kulipisha gari lile la wagonjwa ambalo lilikuwa likipita kwa kasi kuwahi hospitalini.
Gari likaingia ndani ya eneo la hospitali ile na machela kuletwa, Beatrice aakateremshwa na kisha kupandishwa juu ya machela na kisha kuanza kusukumwa kuelekea ndani ya jengo la hospitali ile.
******
Madaktari zaidi ya watatu walikuwa wamemzunguka Beatrice katika kitanda ambacho alikuwa amelalia. Wote walikuwa wakionekana kuwa na jambo ambalo walikuwa wakitaka kulizungumza mahali hapo, walichokifanya ni kutoka nje ya chumba kile.
Beatrice alionekana kuwa na wasiwasi kwani tangu afikishwe ndani ya chumba kile hakuwa ametibiwa zaidi ya kuangaliwa na madaktari ambao walikuwa wakimwangalia huku wakionekana kuwa na wasiwasi.
“Kwa hiyo itakuwaje?”
“Haina jinsi. Mifupa imevunjika sana na haitoweza kuunganika tena” Dokta Edward alisema.
“Kwa hiyo tufanye nini?”
“Hakuna cha kufanya zaidi ya kuikata. Tukiiacha hivi hivi itamletea matatizo makubwa baadae” Dokta Edward alisema na hapo ndipo walipoingia ndani ya chumba kile.
Hawakutaka kumficha, walichokifanya ni kumueleza Beatrice ukweli kuhusiana na hatua ambayo walikuwa wameifikia ya kuikata miguu yake kutokana na mifupa kuvunjia kupita kiasi. Kilikuwa ni kilio kilichojaa masikitiko kwa Beatrice, alitamani kuwaambia wasiikate lakini kila alipoambiwa madhara ya kuiacha miguu hiyo, aliona hakuna jinsi zaidi ya kukubaliana nao.
Huo ndio ukawa mwisho wa kuwa na miguu katika maisha yake, huo ndio ukawa mwisho wa kutembea na kukimbia katika maisha yake na huo ndio ukawa mwisho wa kuvaa viatu katika maisha yake.
Beatrice akaanza kuishi maisha yaliyojaa majonzi, marafiki zake ndio ambao walikuwa wakifika nyumbani hapo na kumsaidia kazi mbalimbali za mahali hapo. Mapenzi yakaonekana kuharibu ndoto zake zote ambazo alikuwa amejiwekea zamani.
Kwa upande mwingine Beatrice alijikuta akijuta kwa kile ambacho alikuwa amekifanya kwa mvulana Simon, alijua fika kwamba mambo yote ambayo yalikuwa yametokea katika maisha yake yalikuwa kama laana kutoka kwa mvulana huyo ambaye hadi muda huo hakujua mahali alipokuwa.
***********
Beatrice alikuwa amelala kitandani, akaamka na kisha kutulia kitako. Muda ulikuwa umekwenda sana kwani saa yake ya ukutani ilikuwa ikionyesha kwamba tayari ilikuwa saa tisa usiku. Uso wake ulionekana kuwa katika majonzi makubwa hasa katika kipindi ambacho alikuwa akiviangalia vipisi vya miguu yake.
Moyo wake ulikuwa ukimuuma kupita kiasi. Alijiona ni bora kama angekuwa katika hali hiyo toka alipokuwa mtoto mdogo kuliko kuwa katika hali hiyo katika kipindi hicho. Alikaa katika hali ya mawazo kwa dakika kadhaana ndipo alipoinuka na kuanza kukifuta kibaiskeli chake na kisha kukikalia na kuanza kukisukuma mpaka karibu na meza na kisha kuchukua daftari kubwa na kuchana karatasi.
Alikuwa akitaka kuandika kitu, aliiangalia karatasi ile kwa sekunde kadhaa na ndipo akaichukua kalamu iliyokuwa pembeni na kisha kuanza kuandika kile ambacho alikuwa akitaka kukiandika kwa wakati huo.
Mama Mpendwa.
Najua kwamba mlinionya mara kwa mara juu ya uamuzi ambao niliuchukua wa kuwa na mtu ambaye alionekana kwangu kuwa si sahihi, sikutaka kusikia kitu chochote kutoka kwenu, kila siku nilijisikia kufanya kile ambacho nilitamani kukifanya hata kama kilikuwa si sahihi.
Kila kitu ambacho kilitokea katika maisha yangu, sitoweza kumlaumu mtu yeyote zaidi ya kujilaumu mimi mwenyewe. Nilijiona kuwa katika mapenzi mazito, nilijiona kuthaminiwa zaidi ya mtu yeyote yule ingawa kwa sasa nimefahamu kwamba kule nilipokuwa, kamwe haikuwa sehemu yangu sahihi.
Sikuwa mtu wa furaha, huzuni ndio ilikuwa sehemu ya maisha yangu, kila siku nilikuwa mtu wa kuumia, furaha ikapotea katika maisha yangu. Nilijuta na milele nitaendelea kujutia uamuzi ambao niliamua kuuchukua wa kuishi na mwanaume ambaye nina uhakika hakuwa mwanaume wangu sahihi.
Namkumbuka Simon ambaye siku zote alitamani sana kuwa pamoja nami, nilifahamu kwamba Simon alikuwa na mapenzi ya dhati kwangu na kila siku alikuwa akinihitaji kuliko kitu chochote kile. Pamoja na mapenzi yake yote aliyokuwa nayo, nilimkataa kwa kumuona hanifai.
Kila siku Simon alikuwa akilia mbele yangu, alilililia penzi langu ambalo kamwe sikutaka kumpa. Niliijua hali yake ya maisha ambayo alikuwa akiishi, hakuwa akiishi katika familia iliyokuwa na fedha za kutosha kama ilivyokuwa familia ya Walter.
Sikutaka kuwa na Simon japokuwa alinionyeshea ni jinsi gani alikuwa akinihitaji tangu kipindi kile shuleni, sikutaka kabisa kuwa na Simon. Alijitahidi kuniletea maua ambayo nilikuwa nikiyatupa katika pipa la takataka tena mbele ya macho yake. Nakumbuka vizuri sana hadi zile siku ambazo alikuwa akijitahidi kuniletea kadi mbalimbali za mapenzi, sikuona thamani yoyote ile zaidi ya kuzitupa na nyingine kuzichoma moto.
Sikumuhitaji Simon kabisa na wala sidhani kama kulikuwa na msichana yeyote ambaye alikuwa akimuhitaji pale shuleni zaidi ya msichana Violeth ambaye kila siku nilikuwa nikimuona mjinga. Sikujua alikuwa akimpendea nini mvulana yule ambaye nilimuona kutokuwa na mvuto wowote ule.
Sikuwa nikitaka kusikia kitu chochote kile kutoka kwa mtu yeyote juu ya Walter ambaye alinionyeshea mapenzi ya kweli ambayo kwa sasa ninaamini kwamba yalikuwa feki. Alinichezea alivyotaka, nilimkabidhi kila kitu katika maisha yangu, kwa sasa NINAJUTA.
Nilimuonea huruma Simon ambaye kila siku alikuwa akiendelea kunifuatilia kila sehemu nilipokuwa, nilikuwa nikimchukia sana katika kipindi kile, nilikuwa nikimletea dharau kila siku lakini hakutaka kunielewa, kila siku alikuwa akiendelea kunifuatilia.
Ninajuta na kila siku nitaendelea kujuta katika maisha yangu. Nilipoteza bahati ambayo sidhani kama itaweza kurudi tena maisha mwangu. Sidhani kama Simon ataendelea kunipenda kama tu atakuja kuniona kwa jinsi nilivyokuwa sasa.
Miguu yangu mizuri ambayo nilikuwa nikiiringia haipo tena, mataili ya baiskeli yangu ndio yamekuwa miguu yangu. Sidhani kama uzuri wa uso wangu upo tena, tindikali imeuharibu uso wangu wote. Ninaonekana kuwa kama kinyago. Sitaki tena kutoka nje, kila siku ninajifungia chumbani kwangu nikilia, sijui nifanye nini tena.
Namkumbuka sana Simon, nakumbuka mara ya mwisho kuonana nae, alikuwa mbele yangu pamoja na Walter. Simon alikuwa amepiga magoti chini akiendelea kulilia penzi langu. Muda wote nilikuwa nikimwangalia kwa dharau, sikutaka kusikia kitu chochote kutoka kwake.
Simon alikuwa akizielezea hisia zake kali juu yangu, nilijikuta nikipata moyo wa ujasiri kumkataa kwa mara nyingine tena. Muda wote kicheko cha dharau kilikuwa kikisikika kutoka kwa Walter ambaye sidhani kama kuna siku ilitokea kumpenda Simon.
Namchukia Walter na sidhani kama kuna siku nitakuja kumpenda au kumsamehe kwa haya ambayo amenifanyia, nimekuwa binadamu mpya, nimekuwa mtu nisiyejiweza tena. Kila siku nikimkumbuka Simon, bado moyo wangu unaendelea kujuta kwa kutokumpa kile ambacho alikuwa akikililia kila siku kutoka kwangu.
MOYO WANGU BADO UNAVUJA DAMU kwa maumivu makali ambayo yametokea kuumiza moyo wangu. Sijui kama itatokea siku nitakuwa katika hali ya kawaida. Kila ninapoyakumbuka mambo mengi yaliyotokea katika kipindi changu cha nyuma, nabaki nikilia huku nikiendelea kumlaumu Walter ambaye alinitelekeza porini.
Sijajua mahali ambapo Simon atakuwepo kwa sasa, sijajua ni kwa jinsi gani nitaweza kumuona. Na kama nikibahatika kuonana nae, nitahitaji sana kuzungumza nae kwa kirefu, nitahitaji kumuomba msamaha juu ya yote ambayo nilikuwa nimemtendea katika maisha ya nyuma. Najua kwa sasa anaweza kuwa na msichana ambaye atakuwa anampenda, ila kama atakuwa na Violeth, moyo wangu utafurahi sana kwani naamini yule alikuwa msichana pekee ambaye ana mapenzi ya kweli kwake.
Nimejaribu kuandika barua hii ndefu kwako mama kwa sababu nilitamani sana ufahamu mambo ambayo yalinitokea katika kipindi ambacho mlihama na kuelekea mkoani Shinyanga. Kwa sasa sijiwezi ila kumbukeni kwamba Walter ndiye alikuwa chanzo cha haya yote.
Kama itatokea nikapata msaada wowote ule, basi naamini nitakuja huko kukaa nanyi mpaka pale kifo kitakaponikuta. Najua utakuwa umeshtuka sana kuyasoma haya ambayo nimekuandikia, ila amini kuwa hii ndio hali halisi niliyokuwa nayo na kamwe sitotakiwa kupingana nayo.
Wasalimieni watu wote huko, msisahau kumsalimia mdogo wangu Paula, naomba umwambie mambo mengi kuhusiana na mapenzi ili yasimtokee haya ambayo yamenitokea.
Nawapenda sana.
Ni mimi
Beatrice Sebastian.
Beatrice alimaliza kuandika barua ile, machozi yalikuwa yameyaloanisha mashavu yake kupita kawaida. Hakuonekana kuridhika, akaanza kuirudia kuisoma zaidi na zaidi, kila alivyozidi kuisoma na ndivyo alivyozidi kuumia zaidi.
Karatasi ya barua ile ikaanza kuloanishwa na machozi yake ambayo yalikuwa yakimtoka. Akaanza kuikunja karatasi ile na kisha kuiweka ndani ya bahasha na kuanza kukisukuma kibaiskeli chake mpaka karibu na kitanda huku bahasha ile akiwa ameiacha mezani.
Alitumia muda wa dakika nzima mpaka kupanda kitandani. Akajifunika shuka na kuanza kulia. Kila alipokuwa akikumbuka maisha yake ya nyuma, moyo wake ulikuwa ukimuuma zaidi na zaidi. Miguu yake ambayo ilikuwa ikisifika kwa kila aliyekuwa akimwangalia wala haikuwapo tena zaidi ya kubaki vipingili tu.
“MOYO WANGU BADO UNAVUJA DAMU” Beatrice alibaki akijisemea kitandani pale.
Huo ndio ukaonekana kuwa mwisho wa kila kitu. Hali ambayo alikuwa nayo alishindwa kabisa kuivumilia. Ilikuwa imepita miezi mitatu tangu akatwe miguu lakini mateso ambayo alikuwa akiyapata yalimfanya kujiona kama alikuwa amekaa katika hali hiyo kwa miaka kumi.
Ingawa katika barua hiyo aliandika kwamba angekwenda kumuona mama yake pamoja na mdogo wake mkoani Shinyanga lakini jambo hilo aliliona kutokutokea tena katika maisha yake. Alichokifanya ni kuanza kujivuta mpaka katika droo ya kitanda na kisha kukifungua na kutoa vidonge kadhaa.
Akajitahidi kujinyoosha mpaka pale alipoifikia ndoo ya maji ambayo wala haikuwa mbali kutoka pale ilipokuwa na kisha kuchukua kikombe na kuchota maji. Kilichofuatia mahali hapo ni kuangalia darini kama mtu ambaye alikuwa akitaka kufanya maombezi na kisha kunywa vidonge vile.
Historia ya maisha yake ikaishia hapo na ukurasa unaohusu maisha yake kufungwa. Siku iliyofuata, ni mwili tu ndio ambao ulikuwa ukionekana. Mama yake pamoja na mdogo wake wakapewa taarifa juu ya kile ambacho kilikuwa kimetokea na hivyo kuja jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mazishi.
Uzuri wa Beatrice bado ulikuwa umebakia katika kichwa cha kila mwanaume ambaye alikuwa amewahi kukutana nae. Ingawa alikuwa amekatwa miguu lakini kamwe uzuri wake haukuweza kupotea.
**********
“Nimeifungisha ndoa hii kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amen” Ilikuwa ni sauti ya mchungaji Stefano ambayo ilikuwa ikisikika kutoka katika kanisa la Mtakatifu Luka ambalo lilikuwa mkoani Kilimanjaro.
Nuru hakuamini kama kweli siku alikuwa akianza kuitwa mke wa Walter. Muda wote Bwana Godson na mkewe, Catherine walikuwa wakionekana kuwa katika nyuso za furaha, kuolewa kwa binti yao kulionekana kuwafariji kupita kawaida.
Walter hakuamini kama kweli katika kipindi hicho Nuru alikuwa mke wake halali ambaye alitakiwa kumpenda na kuishi nae mpaka pale kifo kingewatenganisha. Mpaka kufikia hapo, hakutakiwa kukumbuka kitu chochote ambacho kilikuwa kimepita katika maisha yake.
Hapo ndipo walipoanza kuishi maisha ya ndoa huku wakikabidhiwa kila kitu kilichokuwa kikimilikiwa na Bwana Godson kwa ajili kukviendesha. Ingawa alikuwa ametoka katika familia ya kitajiri kama mke wake lakini utajiri ambao alikuwa ameukuta kwa Bwana Godson ulikuwa mkubwa.
Akilini mwake hakumkumbuka tena Beatrice na wala hakuwa na taarifa zozote kama msichana huyo alikuwa amejiua mara baada ya kujiona akiteseka kitandani.
“Nitakupenda katika maisha yangu yote mke wangu” Walter alimwambia Nuru.
“Hata mimi pia” Nuru alisema na wote kukumbatiana kwa furaha.
Endelea kulike: www.facebook.com/2jiachie
Tembelea: www.2jiachie.com
MWISHO

Post a Comment