ad

ad

MOYO WANGU BADO UNAVUJA DAMU - 03


Endelea kulike: www.facebook.com/2jiachie
Tembelea: www.2jiachie.com

Baada ya miezi kadhaa, mvulana Walter akawa miongoni mwa wanafunzi ambao walikuwa wamehamia shuleni hapo. Walter alionekana kuwa mvulana wa tofauti sana, hii iltokana na uwezo mkubwa wa kifedha ambao walikuwa nao wazazi wake.
   Kila siku shuleni alikuwa akipelekwa kwa gari lakini baada ya muda fulani, alikuwa akiendesha gari yeye mwenyewe. Shule nzima, gari la Walter aina ya Harrier ndilo ambalo lilikuwa likionekana katika uwanja wa shule hiyo. Walter akaonekana kujivunia maisha ya kifahari ambayo alikuwa akiishi, shuleni alikuwa aambiwi kitu chochote kile, fedha za wazazi wake zilimtia wazimu.
   Walter hakuwa na heshima kwa walimu wake, alifanya kitu chochote ambacho alijisikia kukifanya. Matumizi yake makubwa ya fedha shuleni yaliwafanya wasichana wote waliokuwa na tamaa kuanza kumbabaikia akiwemo Beatrice.

   Walter hakutaka kuchelewesha, kitu cha kwanza alichokifanya ni kuanza uhusiano wa kimapenzi na Beatrice. Beatrice hakuonekana kuwa mgumu kwa Walter na wala hakutaka muda wa kujifikiria zaidi ya siku hiyo hiyo kuanza mahusiano ya kimapenzi.
   Mara kwa mara walikuwa pamoja huku Beatrice akitumia fedha za Walter kadri alivyotaka. Beatrice alijiona kumpata mvulana ambaye kila siku alitamani kuwa nae. Kila walipokuwa wakiitwa ofisini, walikuwa wakijitetea kwamba walikuwa katika uhusiano wa kawaida tu, kaka na dada.
   Uhusiano ule ulikuwa ukimuumiza sana Simon lakini hakutaka kukata tamaa. Bado alijiona kuwa na nafasi kubwa ya kuwa na Beatrice ambaye kwa wakati huo alikuwa amezama katika penzi la dhati na Walter ambaye kila siku alikuwa akitaka kuitwa jina la ‘Bosi mtoto’ shuleni hapo.
   “Mbona haunielewi wewe mtu! Kila siku najaribu kukwambia kitu kimoja...SIKUTAKI” Beatrice alimwambia Simon.
   “Beatrice naomba unielewe. Wewe ndiye msichana ambaye kila siku nilikuwa nikikuota. Unasema haunitaki
kwa kuwa sistahili, kumbuka kwamba mapenzi ya dhati hayajali utajiri wala umasikini. Sistahili kuwa na wewe kwa sababu tu mimi ni masikini, nakuomba Beatrice uwe wangu. Ninakupenda sana. Umasikini ni hali tu ambayo kila mtu anaweza kuwa nayo ila kumbuka kuwa mapenzi ya dhati ni hisia ambazo si kila mtu anazo moyoni mwake”Simon alimwambia Beatrice.
   “UNANUKA..” Beatrice alimwambia Simon, akatema mate chini na kuondoka.
   Simon akashindwa kuvumilia, machozi yakaanza kumtoka hapo hapo alipokuwa amesimama. Alimwangalia Beatrice mara mbili mbili, moyo wake ukatengeneza chuki kubwa na umasikini ambao alikuwa nao. Simon akageuka nyuma kwa ajili ya kuondoka kuelekea darasani kwao, akashtuka, zaidi ya wanafunzi hamsini walikuwa wakimwangalia.
   Simon akainamisha kichwa chini, bado machozi yalikuwa yakimtoka kwa uchungu. Katika maisha yake, hakuamini kama kuna siku mapenzi yangeweza kumuumiza namna ile. Kwa haraka haraka Violeth ambaye alikuwa miongoni mwa wanafunzi wale akaanza kupiga hatua kumfuata Simon ambaye alikuwa akielekea darasani.
   “Simon.....utauumiza moyo wako mpaka lini?” Violeth alimuuliza Simon.
   Simon hakujibu kitu chochote ile, aliendelea kupiga hatua kuelekea darasani huku uso wake akiwa ameuinamisha chini. Bado Violeth alikuwa akiendelea kumfuata kwa hatua moja nyuma yake.
   “Simon....Simon....Jaribu kuitambua thamani kubwa ya chozi lako” Violeth alimwambia Simon na kuondoka.
   Simon akafika darasani na kutulia kitini, moyo wake ulikuwa unamuuma kupita kawaida. Akakiinamisha kichwa chake juu ya meza yake ya kusomea. Akaanza kuafikiria maneno ambayo alikuwa ameambiwa na Beatrice. Neno ‘Unanuka’ ndilo lilikuwa limeemuumiza zaidi. Akajaribu kulinusa shati lake, hakuwa akitoa harufu yoyote ile.
   “Hii ni dharau ila kamwe sitokoma, nitaendelea kumfuata mpaka pale atakapokuwa wangu. Msichana atabaki kuwa msichana kila siku. Ipo siku ataulegeza tu moyo wake” Simon alijisemea.
                                                                   ***********
                                                                         4
   Bado kila siku Simon alikuwa akiendelea kumfuatilia Beatrice ambaye alikuwa akimkatalia kila siku. Simon hakuonekana kujali, aliwajua wasichana vilivyo kwamba siku za mwanzoni huwa wagumu lakini baadae mambo huwa mazuri.
   Hakutaka kuacha kumfuatilia Beatrice, bado alikuwa akimuona kuwa msichana yule ambaye alikuwa amemuota katika kipindi cha nyuma. Alijua fika kwamba pale ndipo ambapo kulikuwa na maendeleo yake katika maisha yake ya baadae. Hakujua namna ambayo maendeleo yangepatikana kwa kupitia kwa Beatrice ila kitu ambacho alikifanya ni kuiheshimu sauti ile ambayo alikuwa ameisikia ndotoni.
   Sura ya msichana yule ambaye alikuwa amemuona katika ndoto yake ilikuwa ngeni kabisa machoni mwake. Ni kweli alikuwa akimfuatilia Beatrice kutokana na uzuri ambao alikuwa nao lakini alikuwa na uhakika kwamba msichana yule ambaye alikuwa amemuona ndotoni hakuwa Beatrice yule.
   Kila siku alikuwa akijifikiria juu ya msichana yule ambaye urembo wake ulimchanganya kupita kawaida. Kila siku maombi yake yalikuwa ni kutaka kuonana na msichana huyo, kuwa nae na hatimae kufunga nae ndoa. Kamwe hakutaka kupingana na ndoto ile kwani alijua fika kwamba ndoto ile ilikuwa ni ndoto ya kweli ambayo ingeweza kutokea katika maisha yake.
   Kila siku Simon aliendelea kuumia, kitendo cha kumuona Walter akiwa na msichana ambaye alikuwa akimpenda moyoni mwake kilimuumiza kupita kawaida. Mapenzi yakaonekana kumuumiza kupitakiasi, mara kwa mara alikuwa akitumia kuandika katika karatasi juu ya jinsi ambavyo alikuwa akiumia moyoni mwake.
   Hakumpenda Walter, alimchukia kuliko mvulana yeyote katika maisha yake, sababu kubwa ambayo ilitengeneza chuki moyoni mwake ni kwa sababu tu alikuwa akitembea na msichana ambaye alikuwa akimhitaji. Alijua fika kwamba Beatrice alikuwa amemkubali Walter kwa kuwa tu alikuwa katika familia iliyokuwa na fedha, fedha ambazo zilikuwa na uwezo wa kutatua shida zake zote alizokuwa nazo.
   Kila siku Simon alikuwa na majonzi ambayo yalikuwa yakimpelekea kulia, shuleni kwake ikaonekana kuwa kama jehanamu, sehemu ambayo ilikuwa na mateso makubwa. Hakuwa na furaha tena kama katika miaka iliyopita, kila siku alikuwa na huzuni kubwa moyoni mwake.
   Alitamani Beatrice ajue ni kwa jinsi gani alimpenda moyoni mwake, alitamani kila siku Beatrice aijue thamani kubwa ambayo alikuwa amemuwekea katika moyo wake. Kila siku Beatrice alikuwa akimletea dharau ambazo zilikuwa kama chachu katika kuendelea kumfuatlia.
   “Beatrice....” Simon aliita kwa sauti ndogo.
   Beatrice ambaye alikuwa mbele yake akasimama na kugeuka nyuma, macho yake yalipogongana na macho ya Simon, Beatrice akaonekana kukasirika. Moyoni mwake hakumpenda sana Simon, alimchukia kupita kiasi.Kila siku alikuwa akiongea maneno mengi ya dharau lakini Simon hakuonekana kuelewa kabisa.
   “Unasemaje?” Beatrice alimuuliza Simon huku akionekana dhahiri kukasirika.
   Simon akaanza kupiga hatua kumfuata Beatrice, alipomfikia, akaanza kumwangalia usoni. Simon akaonekana kuchanganyikiwa, siku hiyo Beatrice alionekana kuwa mzuri zaidi ya siku zote. Simon akabaki akimkodolea macho Beatrice ambaye japokuwa alikuwa amekasirika kupita kiasi lakini mbele ya macho ya Simon, alionekana kuwa mzuri kupita kiasi.
   “Unasemaje?” Beatrice aliuliza swali lile kwa mara ya pili mara baada ya kumuona Simon akimwangalia tu pasipo kusema chochote kile.
   “Macho yangu yanaeleza kila kitu” Simon alimwambia Beatrice.
   “Kwa nini hautaki kuuheshimu uamuzi wangu Simon? Kwa nini unaendelea kunifuatilia? Nimekwishakwambia kwamba sikutaki. Yaani sikutaki na sifiirii kama kuna siku nitakutaka katika maisha yangu. SIKUTAKI” Beatrice alimwambia Simon.
   Hata kabla Simon hajaongea kitu chochote kile, Walter akatokea mahali hapo. Simon bado alikuwa akimwangalia Beatrice ambaye alikuwa akizidi kumvutia kupita kawaida. Walter hakuonekana kuelewa ni kitu gani ambacho kilikuwa inaendelea mahali hapo, alibaki akiwaangalia wote wawili.
   “Beatrice, naomba unielewe” Simon alimwambia Beatrice.
   “Hapana Simon. Sikutaki, ninakuchukia....kila ninapokuona huwa ninakuchukia tu” Beatrice alimwambia Simon huku akipiga hatua kumfuata Walter ambaye alikuwa amesimama pembeni.
   Simon hakuonekana kuelewa chochote kile, akaanza kupiga hatua kumfuata Beatrice na kusimama karibu yao. Bado alikuwa akihitaji kuongea zaidi na Beatrice, hakujali kama Walter alikuwa mahali hapo, kitu ambacho alikuwa akihitaji kukiongea ni juu ya hisia zake kwa Beatrice.
   “Naomba unielewe Beatrice...ninakupenda” Simon alimwambia Beatrice ambaye tayari alikuwa pembeni mwa Walter.
   Beatrice alibaki akimwangalia Simon huku uso wake ukiwa na tabasamu pana. Akayaamisha macho yake kutoka kwa Simon na kumwangalia Walter ambaye nae alikuwa akimwangalia Simon huku akitoa tabasamu pana.
   “Mbona unamtesa hivi?” Walter alimuuliza Beatrice huku akitabasamu.
   “Nimekwishamwambia simtaki. Anang’ang’ania huyo....yaani kama ruba” Beatrice alimwambia Walter.
   “Mkubalie bwana. Hauoni anavyolia kama mtoto. Muonee huruma Beatrice” Walter alimwambia Beatrice huku tabasamu likiendelea kuonekana usoni mwake.
   Walter akaanza kutoa kicheko kilichojaa dhihaka, kicheko ambacho kilimuumiza sana Simon ambaye alikuwa akiendelea kumwangalia Beatrice. Hasira zikamkamata moyoni mwake, kadri Walter alivyozidi kucheka na ndivyo ambavyo hasira zilipozidi kumshika zaidi. Akayaamisha macho yake kutoka kwa Beatrice na kumwangalia Walter.
   “Kweli una mapenzi ya kweli” Walter alimwambia Simon ambaye dhahiri alikuwa akionekana kuwa na hasira.
   Alichokifanya Walter ni kumshika mkono Beatrice na kisha kumuingiza garini. Simon alibaki mahall pale akiwaangalia kwa macho yaliyojaa hasira, hakufurahia kabisa kila alipokuwa akimwangalia Walter akiwa na msichana ambaye alikuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati.
   Gari likawashwa na kisha kuondoka katika eneo hilo, Simon alibaki kimya huku akiiangalia gari lile ambalo lilikuwa na vioo visivyoruhusu mtu wa nje kuona ndani. Simon alibaki mahali pale akiwa ameumia kupita kiasi. Akajikuta akikosa nguvu, akakaa chini huku machozi yakianza kuonekana machoni mwake.
   Mapenzi yalionekana kumuumiza kupita kawaida, kila siku alikuwa akiumia kupita kawaida. Hakujua ni wapi pa kuanzia mpaka Beatrice amkubali na kumpa moyo wake. Kila siku alikuwa akiuchukia umasikini ambao alikuwa nao katika maisha yake. Alijiona kuwa na kila sababu ya kupigana maishani mwake kwa ajili ya kuutoa umasikini ambao ulikuwa katika maisha yake na mama yake pia.
   “Nitapigana kufa na kupona. Sitouhitaji umasikini tena. Ni lazima nipate fedha na kumchukua Beatrice” Simon alijisemea.
                                                                              ***********
                                                                                  5
   Bado mapenzi yalikuwa yakimuumiza Violeth kupita kawaida. Kila siku alikuwa akitamani kuwa na mvulana ambaye alikuwa akimpenda kuliko mvulana yeyote katika maisha yake, Simon. Hakujua ni wapi alitakiwa hasa kuanzia, alitamani kumwambia ukweli juu ya kile ambacho kilikuwa kikiendelea moyoni mwake kwa wakati huo.
   Kila alipokuwa akimuona Simon akizidi kumfuatilia Beatrice, moyoni mwake alikuwa akiumia kupita kiasi. Alijua fika kwamba yeye ndiye ambaye alikuwa na makosa makubwa kwa kuamua kukaa kimya pasipo kumwambia Simon neno lolote kuhusiana na mapenzi.
   Kila siku alipokuwa kitandani, alikuwa akimfikiria Simon ambaye alikuwa akiendelea kumfuatilia Beatrice, msichana ambaye alikuwa aambiwi wala hasikii chochote kile juu ya Walter. Violeth akaonekana kujipanga kwa wakati huu, hakutaka tena kuutesa moyo wake kwa kukaa kimya, alijiona kuwa na kila sababu za kumwambia Simon kila kitu.
   Asubuhi hii alifika shuleni mapema sana. Akaingia darasani na kutulia. Baada ya muda, gari aina ya Harrier ilikuwa ikionekana katika uwanja wa shule ile likiingia ambapo baada ya muda, Walter na Beatrice kuteremka. Vioeth akaonekana kukunja uso wake kwa hasira, hakumpenda Beatrice hata mara moja, alikuwa akimchukia kuliko mtu yeyote shuleni pale.
   Mara moyo wake ukashtuka baada ya kumuona Simon akiingia shuleni pale. Violeth akabaki akitabasamu, alijisikia faraja sana mara baada ya kumuona mvulana ambaye alikuwa akimpenda kuingia shuleni pale. Mara tabasamu lake likapotea mara baada ya kuona Simon akianza kumwangalia Beatrice ambaye alikuwa pamoja na Walter ambao walikuwa wakielekea darasni.
   Uso wa Simon ulikuwa ukionyesha hasira hali iliyomuonyeshea kwamba hakufurahishwa kabisa na ukaribu wa Walter na Beatrice. Simon akaanza kupiga hatua mpaka darasani na kuuweka mfuko wake wa madaftari katika meza yake ya kusomea.
   Simon akatulia kitini na kisha kuuinamisha uso wake chini. Simon alionekana akilia mahali pale. Kila mwanafunzi ambaye alikuwa darasani alikuwa akimwangalia Simon ambaye bado uso wake alikuwa ameiiinamisha kichwa chake juu ya meza yake.
   Kila mmoja alikuwa akimuonea huruma Simon. Walijua ni kwa jinsi gani mvulana huyo alikuwa na mapenzi ya kweli kwa msichana yule. Simon aliinama kwa dakika kadhaa, akauinua uso wake. Wanafunzi wote ambao walikuwa wakimwangalia wakayaamisha macho yao na kuanza kuangalia pembeni isipokuwa Violeth.
   Macho ya Simon yalikuwa mekundu, alionekana kuwa na hasira kupita kawaida. Violeth ambaye alikuwa pembeni kabisa ya darasa lile akaanza kupiga hatua kumfuata Simon mahali pale alipokuwa na kisha kuvuta kiti na kutulia pembeni yake.
   Simon akayapeleka macho yake usoni mwa Violeth. Violeth alionekana kuwa na majonzi usoni mwake, hakuonekana kuifurahia hali ambayo alikuwa nayo Simon katika kipindi kile. Akajisogeza karibu zaidi, Simon alibaki kimya akimwangalia Violeth.
   “Mbona uko hivyo Simon?” Violeth alimuuliza Simon.
   Simon hakuongea kitu chochote kile. Alijiona kutokuwa na jibu la kumpa Violeth kwani aliamini kwamba msichana huyo alikuwa akifahamu kila kitu ambacho kilikuwa kinaendelea juu yake na msichana Beatrice. Alibaki akimwangalia tu.
   “Mbona uko hivyo Simon?” Violeth alilirudia swali lake.
   “Mapenzi. Kila kitu kinachonitokea kinasababishwa na mapenzi Violeth” Simon alimwambia Violeth.
   “Nafahamu Simon. Beatrice haonekani kama ana penzi lolote kwako. Usitake kuumiza moyo wako kila siku, ni bora ujinusuru, haujui Mungu Amepanga nini katika maisha yako. Achana nae tu” Violeth alimwambia Simon.
   Simon akayageuza macho yake na kuanza kumwangalia Violeth. Usoni alionekana kukasirika, hakutegemea hata mara moja kama Violeth angeweza kuyatamka maneno yale ya yeye kuachana na Beatrice na wakati ndiye alikuwa msichana ambaye alikuwa akimpenda kuliko msichana yeyote yule.
   “Usinikasirikie Simon. Huwa sipendi kukuona kila siku ukiwa katika hali hii. Wewe ni rafiki yangu ambaye ninakupenda sana, huwa sijisikii furaha kabisa kuwa katika hali hiyo. Unanihuzunisha kila ninapokuona katika hali hiyo” Violeth alimwambia Simon.
   “Najiona kumpenda sana Beatrice” Simon alimwambia Violeth.
   “Nafahamu ni kwa jinsi gani unampenda. Hebu jifikirie Simon, unampenda vipi msichana asiyekupenda. Unamuhitaji vipi msichana asiyekuhitaji?” Violeth alimuuliza Simon.
   “Kila siku utaendelea kuumia. Mapenzi yataendelea kukutesa kila siku kama tu hautotaka kuwa makini. Kumbuka kuwa Beatrice hakupendi, anakuchukia kuliko mvulana yeyote” Violeth alimwambia Simon.
   “Nafahamu. Nafahamu Violeth. Ila kumbuka kuwa yeye ni msichana. Siku za kwanza anakuwa mgumu lakini mwisho wake atakuja kukubaliana na ombi langu kwake” Simon alimwambia Violeth.
   “Usifikirie hivyo. Si kila msichana yupo kama unavyofikiria. Mwingine uamuzi wake huwa wa moja kwa moja. Kumbuka kuwa Beatrice anachokitaka ni fedha na wala si mapenzi” Violeth alimwambia Simon
   “Nitatafuta fedha. Nitakapozipata, nitamtafuta tu, nafikiri atanikubalia tu” Simon alimwambia Violeth.
   “Una akili sana Simon na wala sikudhania kama siku moja ungeweza kuwaza kitu kama hicho. Usitake kumpenda mtu asiyekupenda katika kipindi ambacho haukuwa na fedha. Kama ukiwa nae katika kipindi hicho, amini kuwa katika kipindi ambacho zitaondoka basi nae ataondoka pia. Mfuate msichana mwenye mapenzi ya kweli ambaye unaamini ataweza kuwa nawe katika hali yoyote ile. Beatrice si msichana wa kuwa nawe” Violeth alimwambia Simon.
   Simon akaonekana kuelewa lakini upande mwingine wa moyo wake ukaonekana kuwa mgumu kukubaliana na Violeth. Asingeweza kumuacha Beatrice, alihitaji sana kuwa na Beatrice kuliko msichana yeyote yule. Kila siku alikuwa akiifikiria ndoto ile ambayo alikuwa ameiota katika miaka iliyopita, alijua fika kwamba msichana yule hakuwa Beatrice ila akili yake pia ikapingana na mawazo yake kwamba msichana yule alikuwa Beatrice.
   “Kama nitashindwa....acha nishindwe ila sitoweza kumuacha Beatrice. Ni lazima nitaendelea kumfuatilia” Simon alimwambia Violeth.
                                                                         *************
Harakati za Simon kuendelea kumfuatilia Beatrice hazikuisha kabisa. Mara kwa mara alikuwa akiendelea kumfuatilia pasipo kukata tamaa. Aalikuwa akionyeshea dharau za kila aina lakini wala Simon hakuonekana kukubali, bado moywake uliamini kwamba siku moja Beatrice angekuwa wake na kuishi nae katika maisha ya raha hapo baadae.
   Violeth hakutaka kukaa kimya tena, akaamua kumwambia Simon juu ya jinsi aivyojisikia. Simon akaishia kutabasamu tu. Alimwangalia Violeth mara mbili mbili. Simon alionekana kujua kwamba kuna siku Violeth angekuja na kutamka maneno yale ambayo alikuwa ameyatamka mbele yake kwa wakati huo.
   Ni kweli Violeth alikuwa rafiki yake ambaye walikuwa wamezoeana sana hata zaidi ya watu wengine lakini kuingia katika mapenzi na msichana huyo kilikuwa ni kitu ambacho wala hakuwa akikihitaji kwa wakati huo. Mt ambaye alikuwa akimuhitaji alikuwa Beatrice pekee ambaye wala hakuwa akionyesha penzi lolote kwake.
   “Nimekuelewa Violeth. U msichana mrembo sana lakini nasikitika kukwambia kwamba moyo wangu haupo kwako hata mara moja” Simon alimwambia Vileth.
   Violeth akabaki kimya. Moyo wake ukaumia kupita kawaida. Hakuamini kama Simon alikuwa amemkataa kwa sababu tu alikuwa akimpenda Beatrice. Violeth akabaki kimya huku akitamani kutoa machozi mbele ya Simon ambaye wala hakuonekana kabisa kuwa na mapenzi ya kweli kwa Violeth.
   “Ni kweli haunipendi Simon?” Violeth aliuliza huku macho yake yakianza kujaza machozi.
   “Ninakupenda. Ninakupenda sana lakini sijui kwa nini sijisikii kuingia katika mapenzi pamoja nawe” Simon alimwambia Violeth.
   “Ninakupenda Simon. Ninatamani tuwe zaidi ya marafiki. Wewe ni mvulana ambaye kila siku unaonekana ndotoni mwangu. Kwa nini usinikubalie Simon?” Violeth alimwambia Simon na kumalizia na swali.
   “Najua kwamba kila siku unaniota, nimezoea kusikia juu ya ndoto zako mara kwa mara. Nisikilize Violeth, najua ni kwa jinsi gani mtu unaumia kumuona mtu unayempenda anampenda mtu mwingine. Najua unaumia sana moyoni mwako kila unaponiona namfuatilia Beatrice. Hakuna jinsi Violeth, Beatrice ni msichana wa ndoto. Nimemuota, ni lazima niwe nae” Simon alimwambia Violeth.
   “Una uhakika kwamba huyo msichana ni yeye?” Violeth aliuliza.
   “Sidhani kama hilo unapaswa kulifahamu. Ninachotaka kukwambia ni kwamba ninampenda sana Beatrice. Itakuwa vigumu sana kukukabidhi moyo wangu ambao uko kwa mtu mwingine” Simon almwambia Violeth.
   Violeth akauhisi mwili wake ukipigwa ganzi, kibaridi kikaanza kumshika, akajihisi kuanza kutetemeka. Bado hakuendelea kuamini kama kweli Simon angeweza kumkatalia namna ile. Alijua fika kwamba Beatrice ndiye ambaye alikuwa amesababisha yote hayo, moyo wake ukaendelea kumchukia Beatrice hata zaidi ya alivyomchukia Shetani.
   “Na mimi nitamng’ang’ania, najua kuna siku atauegeza moyo wake. Ninampenda sana Simon” Violeth alijisemea huku machozi yaliyokuwa yamejaa machoni mwake yakiwa yameanza kutiririka mashavuni mwake.
                                                                     **************
   Mama yake Beatrice, Bi Imelda hakuonekana kabisa kuwa upande wa Walter. Mara kwa mara alikuwa akimuonya binti yake juu ya kuwa na Walter ambaye alikuwa akitumia kiasi kikubwa cha fedha katika kuhakikisha Beatrice aondoki mikononi mwake.
   Beatrice hakuonekana kuelewa kitu, akili na moyo wake tayari ulikuwa umetekwa na fedha alizokuwa nazo Walter kiasi ambacho mapenzi yalikuwa yakiendelea kukua moyoni mwake. Beatrice akawa aambiwi kitu chochote kile juu ya Walter, alikuwa akimpenda kuliko mvulana yeyote yule.
   Kila alipokuwa akimwangalia Simon, aimdharau huku akimuonyeshea chuki za waziwazi. Alimchukia Simon na wala hakutamani kumuona machoni mwake. Kila siku Simon aipokuwa akimfuatili, Beatrice alikuwa akikereka na kila alipokuwa akimwambia Beatrice, Simon hakuonekana kuelewa kitu chochote kile.
   Miezi iliendelea kukatika na hatimae mwaka mwingine kuingia. Wote wakaingia kidato cha nne huku Simon akiendelea kuongoza kama kawaida yake.
   Mwaka huu usumbufu ulikuwa mkubwa zaidi. Simon alijua fika kwamba kama asingefanikiwa kumuingiza Beatrice katika himaya yake mwaka huo basi ingekuwa vigumu sana kuonana nae kama tu wangefanya mitihani ya Taifa.
   Beatrice hakutulia, mara kwa mara Simon alikuwa akimfuata na kuendelea kumwambia juu ya jinsi alivyokuwa akijisikia moyoni mwake. Beatrice hakuwa akielewa zaidi ya kuendelea kumwonyeshea dharau Simon ambazo zilionekana kama kumhamasisha.
   “Kwa nini usiwe na Violeth?” Beatrice alimuuliza Simon.
   “Hapana Beatrice. Ninakupenda wewe tu” Simon alimwambia.
   “Kwangu haitowezekana. Si unajua nina mtu?”
   “Nafahamu Beatrice”
   “Kwa hiyo unataka niachane nae ili niwe nawe?” Beatrice alimuuliza Simon. Swali lile likaonekana kuwa gumu, Simon akabaki kimya.
   “Kwa hiyo unataka nimsaliti?”
   “Hapana. Ila kama nimeonekana kukuonyeshea mapenzi ya kweli, haina budi kufanya hivyo” Simon alimwambia Beatrice.
   “Walter ananipenda sana. Ananipenda hata zaidi ya unavyonipenda” Beatrice alimwambia Simon.
   “Zaidi ya ninavyokupenda? Hapana. Nina penzi la dhati moyoni mwangu juu yako” Simon alimwambia Beatrice.
   ‘SIKUTAKI” Beatrice alimwambia Simon na kisha kuondoka mahali hapo.
   Simon aliumia, neno lile lilikuwa likimuumiza kuliko maneno yote ambayo alikuwa akiyatamka Beatice mbele yake. Kila siku alikuwa akiumia lakini siku hiyo alionekana kuumia zaidi na zaidi. Hakuamini kama kweli tayari ulikuwa umefika mwaka wa pili lakini wala Beatrice hakuonekana kuvutiwa nae.
   Miezi ikaendelea kukatika huku Simon akiendelea kukataliwa na Beatrice. Mwaka huo ukazidi kuwa mbaya zaidi kwake kuliko miaka yoyote. Violeth hakutaka kukata tamaa, nae alikuwa akijaribu kumfuatilia Simon kama kawaida yake kwa kumwambia maneno mengi yaliyojaa mapenzi lakini Simon hakuonekana kukubaliana nae.
   Simon akaanza kufikiria njia nyingine nyingi ambazo akaamua kuzitumia ili kuufikisha ujumbe wake kwa Beatrice. Kitu alichokifanya kwa wakati huu ni kununua maua mazuri mekundu ambayo aliamini kama angempa Beatrice, basi angejua ni kwa jinsi gani alikuwa akimaanisha kile alichokuwa akimwambia kila siku.
   “Umeniletea maua?” Beatrice alimuuliza Simon huku akiyachukua maua yale.
   “Hizi ni hisia zangu kwako Beatrice” Simon alimwambia Beatrice.
   “Nashukuru” Beatrice alimwambia Simon.
   Simon akaonekana kufarijika hasa mara baada ya kuliona tabasamu pana la Beatrice. Moyo wake ukaamini kwamba kwa wakati huo tayari alikuwa ameanza kufanikiwa katika harakati zake za kumuingiza Beatrice katika himaya yake ya mapenzi.
   Beatrice alibaki akiyaangalia maua yale mazuri ambayo alikuwa ameletewa na Simon. Alichokifanya ni kuanza kupiga hatua hadi lilipokuwa pipa dogo la takataka na kisha kuyatupa maua yale.
   Simon akaonekana kushtuka. Hakuamini kama kitu kile kingeweza kutokea. Tabasamu la Beatrice lilimfanya kuona kwamba kila kitu kilikuwa kinakwenda kuwa kama alivyotaka kiwe. Kitendo cha kumuona Beatrice akiyatupa maua katika pipa la takataka lilionekana kuwa tukio baya ambalo wala hakulitegemea.
   “Mbona unafanya hivi Beatrice? Nimejinyima kwa ajili yako. Nimetunza fedha zangu za shule mwezi mzima kwa ajili ya kukununulia maua. Umeyatupa? Tena katika pipa la takataka!” Simon alimwambia Beatrice huku machozi yakianza kumtoka.
   “Ulitaka nifanye nini? Niyapokee?” Beatrice aliuliza huku akionekana kukasirika.
   “Hicho ndicho nilichokitaka Beatrice”
   “Hauna nafasi kwangu. Ninakuchukia sana Simon. Kama ungejua jinsi ninavyokuchukia, usingejaribu kunifuata katika maisha yako yote” Beatric alimwambia Simon.
ITAENDELEA SIKU YA KESHO IJUMAA

No comments

Powered by Blogger.