ad

ad

MOYO WANGU BADO UNAVUJA DAMU - 02

   Muda wa mapumziko, Simon hakuwa akila kitu chochote kile, alikuwa akishinda bila kula kitu chochote shuleni mpaka katika kipindi ambacho alikuwa akirudi nyumbani. Siimon hakuwa na idadi kubwa ya marafiki shuleni, na hata hao ambao alikuwa nao katika kipindi hicho walikuwa nae kwa sababu tu uwezo wake darasani ulikuwa mkubwa.
   Maisha ya kimasikini ambayo alikuwa akiishi kamwe hakuyapenda hata kidogo, alitamani kuishi maisha mazuri ambayo yangemfanya kula chakula katika muda wa mapumziko au kununua kitu chochote cha kupoza njaa ambayo mara kwa mara ilikuwa ikimuuma.
   Simon aliitambua hali halisi ya nyumbani kwao, alijua ni kwa jinsi gani mama yake, Bi Martina alivyokuwa akihangaika usiku na mchana kwa ajili ya kutafuta fedha za kumpeleka shuleni pamoja na kumnunulia mavazi mbalimbali.
   Simon hakupata upendo kutoka kwa watu wengine, mtu pekee ambaye alikuwa akimuonyeshea upendo mkubwa alikuwa mama yake pekee. Mara kwa mara alikuwa akifarijika kila alipokuwa akirudi shuleni na kumkuta mama yake, tabasamu ambalo mara kwa mara alikuwa akiliona kutoka kwa mama yake lilikuwa likimpa sana furaha.
   Kutokana na uwezo wake kuwa mkubwa darasani, Simon alikuwa akifaulu masomo yake yote na kuwaongoza wanafunzi wote wa kidato cha kwanza. Mpaka mwaka unaisha na mwaka wa pili kuingia, hakukuwa na mwanafunzi ambaye alikuwa akifanya vizuri kama Simon.
   Simon alionekana kuwa na akili za tofauti na wanafunzi wengine. Shuleni hakuwa akigusa madaftari ya somo lolote lile zaidi ya Biblia ambayo kila siku alikuwa akienda nayo shuleni. Lakini pamoja na hayo yote, Simon bado alikuwa akiongoza darasani hali iliyowapelekea wanafunzi hadi walimu kugundua kwamba Simon alikuwa na akili za kuzaliwa.
   Mwaka wa pili ulipomalizika na mwaka wa tatu kuingia, marafiki wakaanza kuongezeka kwa Simon. Wanafunzi wengi waliokuwa kidato cha tatu wakaanza kuwa karibu na Simon kwa kuwa walikuwa wamegundua kwamba mvulana huyo alikuwa na kitu cha ziada.
   Simon hakuwa mtu wa majivuno, kila mwanafunzi ambaye alikuwa akitaka kufndishwa, alimfundisha pasipo kujali kitu chochote kile. Ukaribu wa wanafunzi wengine na Simon ukaongezeka lakini kwa msichana Violeth, ukaribu ulikuwa mkubwa zaidi.
   Kila siku Violeth alitamani kuwa karibu na Simon, hakuwa akijisikia furaha katika kipindi ambacho Simon alikuwa mbali nae. Tofauti na kutaka kufundishwa, tayari kuna kitu ambacho kilikuwa kikimsumbua moyoni mwake, MAPENZI.
   Kila Siku moyo wake aliuona kuwa wa tofauti sana kila alipokuwa akimwangalia Simon. Mapenzi ambayo yalikuwa moyoni mwake juu ya Simon yaikuwa yakizidi kuongezeka kadri siku zilivyozidi kwenda mbele. Ni kweli alikuwa akisoma na Simon darasa moja lakini kamwe hakuwahi kumtamkia Simon neno lolote kuhusiana na jinsi alivyojisikia, aibu ilikuwa imembana.
   Simon hakuwa akifikiria mapenzi, kila siku alikuwa karibu na dini yake. Kusali ndio ikawa sehemu ya maisha yake. Kila siku alikuwa akimuomba Mungu afanye miujiza katika maisha yake. Hakutaka kumuona mama yake akipata tabu kama zile ambazo alikuwa akizipata, alitamani mama yake aishi katika maisha ya raha kama watu wengine walivyokuwa wakiishi.
   “Ndoto...” Simon alijisemea.
   Tayari ndoto ambayo aliiota miaka miwili iliyopita ikaanza kujirudia. Aliikumbuka sana ndoto ile ambayo alikuwa ameiota na kumfanya kukurupuka kutoka kitandani. Aliyakumbuka vizuri maneno yale ambayo yalikuwa yamesikika katika ndoto ile, pia alimkumbuka sana msichana yule mrembo ambaye alikuwa amemuona katika ndoto.
   Kila siku alikuwa akijiuliza juu ya msichana yule ambaye wala hakuwa akimfahamu. Maana ya ile ndoto ilikuwa ikimsumbua sana akilini mwake. Alisali usiku na mchana ili kujua maana halisi ya ndoto ile lakini hakupata chochote kile. Siku zikazidi kusonga mbele na hatimae msichana Beatrice Sebastian kuhamia shuleni hapo.
   Beatrice alikuwa msichana mrembo kuliko wasichana wote shuleni pale. Kila mvulana ambaye alikuwa akimwangalia Beatrice, alijikuta akisema kwamba alifanikiwa kukutana na msichana mrembo kuliko wasichana wote maishani mwake.
   Beatrice alikuwa mwembamba, hipsi zake zilikuwa kubwa kiasi ambacho kila alipokuwa akivaa shati la shule ambalo lilikuwa likimbana, hipsi zake zilikuw zikionekana vizuri. Beatrice hakuwa mweusi, ngozi yake ya maji ya kunde nayo ilikuwa chachu kubwa sana kwa wavulana kuvutiwa nae.
   Uso mwembamba wa Beatrice uliotengenezwa vizuri na vishimo vidogo viwili mashavuni ulikuwa ukimvuta kila mvulana ambaye alikuwa akimwangalia. Beatrice hakukubalika kwa wavulana tu bali hata wasichana wenzake walikuwa wakiukubali uzuri wake.
   Mwendo wake ulikuwa wa taratibu uliojaa mapozi na kama ingetokea kumuona basi ungeweza kusema kwamba Beatrice hakustahili kukanyaga ardhi ya dunia hii kwa kuwa haikuwa hadhi yake kwa jinsi ambavyo alivyokuwa.
   Miguu yake ndiyo ambayo ilikuwa imejaa mvuto zaidi. Kila mvulana ambaye alikuwa akiiangalia miguu ya Beatrice alikuwa akitamani kulala pamoja na msichana huyo. Miguu yake ilijaa mvuto mkubwa, kutokana na kujua uzuri wa miguu yake, alichokifanya Beatrice ni kuanza kuvaa sketi fupi ambazo zilijaa mitego kuanzia kwa wanafunzi hadi kwa walimu wake.
   Wavulana hawakutaka kutulia. Hawakuona sababu ya kutulia na wakati shuleni pale kulikuwa na msichana mzuri kiasi kile. Kitu ambacho walichokifanya wakati huo ni kuanza kumfuata Beatrice na kila mtu kujaribu bahati yake. Kila mvulana ambaye alikuwa akimfuata Beatrice hakuwa akifanikiwa kwani Beatice alikuwa akiwakataa.
   Ingawa Simon alikuwa mtu wa dini lakini kwa Beatrice akashindwa kuvumilia. Akaanza kumnyemelea Beatrice japokuwa hakuwa na uhakika kama angeweza kukubaliwa na msichana huyo ambaye alionekana kujaa mapozi kupita kawaida.
   Kila siku Simon alikuwa akitafuta nafasi ya kuongea na Beatrice ambaye alionekana kuwa bize kupita kiasi. Simon hakujua aanzie wapi, hakuwa tayari kumuacha Beatrice apite katika himaya yake, aliona ni bora amfuate kuliko kujiumiza kila siku kimawazo.
   “Unasemaje?” Beatrice alimuuliza Simon huku akionekana kushtuka.
   “Nakupenda Bearice” Simon alimwambia Beatrice.
   Beatrice akatoa tabasamu na kisha kutoa kicheko kilichojaa dharau. Akaanza kumwangalia Simon kuanzia juu mpaka chini na kisha kuanza kumwangalia tena kuanzia chini mpaka juu, kicheko kile cha dhihaka kikaongezeka zaidi.
   “Unanipenda! Hebu jiangalie kwanza. Hauna mvuto wowote ule na wala sifikirii kama mimi ni hadhi yako. Kama ningekuwa na ratiba ya kutembea na wavulana shuleni hapa, basi katika ratiba hiyo ungekuwa wa mwisho. Yaani hapo namaanisha kwamba ningetembea na wanafunzi, walimu, walinzi hadi wauza vyakula na wewe kuwa wa mwisho” Beatrice alimwambia Simon.
   Simon akajihisi mwili ukipigwa ganzi. Alitamani muda huo huo ardhi ipasuke na kutumbukia ndani. Dharau ambayo alikuwa ameonyeshewa na Beatrice ilimuuma kupita kawaida. Alimwangalia Beatrice mara mbili mbili, hakuamini kama kweli Beatrice huyo ndiye ambaye alikuwa ametamka maneno yale.
   Akayaamisha macho yake kutoka kwa Beatrice na kisha kujiangalia yeye mwenyewe. Ni kweli maneno ambayo alikuwa akiongea Beatrice aliyaona kuwa sahihi kabisa, hakuwa na hadhi ya kutembea na Beatrice hata mara moja. Akayaamisha macho yake na kumwangalia Beatrice usoni.
   “Beatrice, ninakupenda. Kila siku umekuwa msichana wa ndotoni mwangu. Kila siku nimekuwa nikikuota hata kabla haujaja shuleni hapa” Simon alimwambia Beatrice kwa sauti ya taratibu.
   “Ndotoni mwako? Umekuwa ukiniota? Hebu jiangalie jinsi ulivyo, yaani haustahili Simon. Mimi sio hadhi yako, tafuta daraja lako” Beatrice alimwambia Simon na kuanza kuondoka.
   Simon akajiona kupoteza nguvu za miguu yake, akachuchumaa chini huku akiaendelea kumwangalia Beatrice ambaye alikuwa akiondoka. Moyoni aliumia, aliumia kupita kawaida. Hakutaka kukata tamaa, alijua kwa vyovyote vile ni lazima baadae Beatrice atamkubali tu na kuiona ndoto ile aliyoiota kuwa kweli.
   “Wewe ndiye nilikuwa nikikuota kila siku. Sitotaka kukucha kwani naamini wewe ndiye njia ya mafanikio yangu” Simon alisema.
                                                             *************
                                                                   
   Katika kipindi ambacho Simon alikuwa akiongea na Beatrice, Violeth alikuwa pembeni akiwaangalia. Violeth alijisikia kuumia kupita kiasi kila alipokuwa akimwangalia Simon. Kwa jinsi muonekano wa Simon ulivyokuwa ukionekana mahali pale, alijua moja kwa moja kwamba Simon alikuwa akiongea na Beatrice kuhusu mapenzi.
   Alipomuona Beatrice ameanza kuondoka, Violeth akaanza kupiga hatua kumfuata Smon mahali pale alipokuwa na kisha kuanza kumwangalia. Simon alionekana kutia huruma, alionekana dhahiri kuumia moyoni mwake, alichokifanya Violeth ni kumfuata na kumshika bega pale chini alipokuwa amechuchumaa.
   “Simon....” Violeth aliita huku akimshika begani.
   Simon akageuka nyuma, macho yake yakatua kwa Violeth ambaye alionekana dhahiri kutokuipenda hali ile ambayo alikuwa ameiona mahali pale. Simon akasimama juu na kuanza kuangaliana na Violeth usoni.
   “Kuna nini? Mbona umejiinamia halafu unaonekana hauna raha?” Violeth alimuuliza Simon huku akimwangalia usoni.
   “Naomba uniangalie Violeth” Simon alimwambia Violeth ambaye alikuwa akimwangalia.
   “Kuna nini? Mbona sikuelewi” Violeth aliuliza
   “Hivi sistahili kupendwa na msichana kama Beatrice?” Simon aliuliza, tayari macho yake yalikuwa yamebadilika na kuwa mekundu.
   “Unastahili”
   “Mbona yeye ananiambia sistahili? Kwa nini ameniambia hivi? Hivi hajui ni kwa kiasi gani ninampenda na kumuhitaji?” Simon alimuuliza Violeth maswali ambayo yalikuwa mwiba mkali moyoni mwa Violeth.
   Violeth hakujibu kitu chochote kile, ni kweli alimpenda sana Simon, maswali yale yalikuwa yamemuumiza sana kiasi ambacho nae macho yake yakaanza kuwa mekundu. Hakumpenda Beatrice kwa kuwa tu alikuwa amemuumiza mvulana ambaye alikuwa akimpenda lakini katika upande mwingine aliona ni afadhali Simon alivyoumizwa vile ili yeye apate nafasi.
   “Usihuzunike Simon. Wewe ni mvulana na pia unaweza kufanya maamuzi mengine. Kulalamika kamwe hakuwezi kukusaidia” Violeth alimwambia Simon.
   “Hata kama Violeth. Mimi ni mwanaume japokuwa masikini, ninahitaji kuzielezea hisia zangu kwa mtu yeyote yule. Nimehuzunika sana Violeth lakini kamwe sitoweza kuacha kumfuatilia Beatrice, najua huu ni mwanzo tu, hapo baadae moyo wake utageuka” Simon alimwambia Violeth na kisha kuondoka mahali hapo.
   Machozi yakaanza kumlenga Violeth na baada ya muda yakaanza kumtoka. Moyoni alikuwa ameumia kupita kawaida, hakuamini kama mvulana ambaye alikuwa akimpenda alikuwa akimpenda msichana mwingine. Alibaki akimwangalia Simon huku mashavu yake yakiwa yameanza kuloanishwa na machozi yake.
   Alijuta kwa nini hakumwambia Simon ukweli tangu katika kipindi ambacho Beatrice hakuhamia shuleni pale. Hakuona dalili kama angeweza kuubadilisha moyo wa Simon na kumkubalia yeye katika kipindi ambacho ataamua kumwambia ukweli.
   Simon hakujisikia raha. Maneno ambayo alikuwa ameambiwa na Beatrice yalikuwa yamemuumiza kupita kawaida. Mara baada ya kufika nyumbani, moja kwa moja akajilaza kitandani. Simon akaanza kulia, kadri alivyokuwa akiyafikiria maneno ambayo alikuwa ameambiwa na Beatrice, alionekana kuumia kupta kawaida.
   Simon akaendelea kuuchukia umasikini kwa kuamini kwamba ulikuwa ni sababu moja wapo ambayo ilimfanya kukataliwa na Beatrice. Simon hakuona maana yoyote ile kuwa na akili nyingi darasani halafu yule msichana ambaye ulikuwa ukimtaka kukukataa.
   Kila siku Simon alikuwa akijipa moyo kwa kuamini kwamba ni lazima siku moja angekuwa na Beatrice ambaye alikuwa ameuteka moyo wake kupita kawaida. Aliwafahamu viivyo wasichana kwamba katika kipindi cha kwanza huwa wagumu lakini baadae huruma huwaingia na kujikuta ukiwachukua kirahisi.
   Kwa kuwa Beatrice alikuwa msichana basi alijua fika kwamba nae alikuwa kama wasichana wengine ambao mara baada ya kuwasumbua kwa muda mrefu basi hulegeza msimamo wao na kukubali kile ambacho kila siku ulikuwa ukimwambia.
   Kila siku shuleni, Simon hakuwa na raha. Kila alipokuwa akimwangalia Beatrice, maneno yale ambayo alikuwa amemwambia yalikuwa yakijirudia kichwani mwake. Bado maumivu makali yalikuwa moyoni mwake, lakini alijiona radhi kuendelea kupata maumivu kuliko kumuacha Beatrice.
                                                                   ******
   Baada ya miezi kadhaa, mvulana Walter akawa miongoni mwa wanafunzi ambao walikuwa wamehamia shuleni hapo. Walter alionekana kuwa mvulana wa tofauti sana, hii iltokana na uwezo mkubwa wa kifedha ambao walikuwa nao wazazi wake.
   Kila siku shuleni alikuwa akipelekwa kwa gari lakini baada ya muda fulani, alikuwa akiendesha gari yeye mwenyewe. Shule nzima, gari la Walter aina ya Harrier ndilo ambalo lilikuwa likionekana katika uwanja wa shule hiyo. Walter akaonekana kujivunia maisha ya kifahari ambayo alikuwa akiishi, shuleni alikuwa aambiwi kitu chochote kile, fedha za wazazi wake zilimtia wazimu.
   Walter hakuwa na heshima kwa walimu wake, alifanya kitu chochote ambacho alijisikia kukifanya. Matumizi yake makubwa ya fedha shuleni yaliwafanya wasichana wote waliokuwa na tamaa kuanza kumbabaikia akiwemo Beatrice.
INAENDELEA HAPA HAPA SIKU YA LEO

No comments

Powered by Blogger.