BINGO: MAN UNITED KUILIPA ZAIDI MADRID KWA DI MARIA
ALIWAZALO mjinga ndilo linalomtokea. Na kama kweli likitokea, basi Real Madrid itajipatia mabilioni ya pesa zaidi endapo Angel Di Maria atashinda tuzo ya mwanasoka bora wa dunia katika kipindi cha maisha yake ya soka Manchester United.
Real Madrid wameingiza kipengele cha mkataba wa mauzo ya Di Maria kwenda Old Trafford kwamba endapo mwanasoka huyo atachaguliwa kuwa mwanasoka bora wa dunia akiwa na Manchester United basi klabu hiyo italazimika kuipa Real Madrid Pauni 4 milioni kama asante kwa kuuziwa kipaji hicho.
Di Maria, 26, aliuzwa kutoka Madrid kwenda Old Trafford kwa dau la Pauni 59 milioni katika dirisha lililofungwa hivi majuzi, lakini kama akifanikiwa kung’ara zaidi Old Trafford basi Real Madrid itaendelea kunufaika zaidi.
Labda kutokana na kiu yao ya kumnasa Di Maria, inadaiwa kuwa viongozi wa Manchester United hawakuona hatari kuingiziwa kipengele hicho huku pia wakiamini endapo Di Maria atafikia makali hayo basi atakuwa amethibitisha ukubwa wa dau lake ambapo kwa sasa ndiye mwanasoka ghali zaidi Ligi Kuu ya England.
Wakati huo huo, Di Maria ameendeleza bifu lake na Real Madrid kwa kuishambulia klabu hiyo kutokana na kitendo chake cha kujaribu kumzuia kucheza pambano la fainali ya Kombe la Dunia kati ya timu yake ya Argentina dhidi ya Ujerumani.
“Kulikuwa na barua kutoka Madrid, iliwasili saa tano asubuhi siku ya mechi. Na mechi yenyewe ilikuwa saa kumi jioni. Wakati huo nilikuwa nimeweka barafu katika mguu wangu ili nicheze fainali.” alisema Di Maria.
“Niliichana barua hapo hapo pindi nilipopewa na
wala sikujali. Sikujali ambalo lingetokea. Lakini kutopangwa ulikuwa
uamuzi wa kocha Alejandro (Sabella),” aliongeza staa huyo wa zamani wa
Benfica.
“Sikuhitaji lolote kutoka kwake, lakini pia sikutaka kuicha timu yangu ikiwa pungufu katika mechi hiyo muhimu,” Aliongeza Di Maria.
Kabla la pambano hilo, ambalo Argentina ililala
bao 1-0, Di Maria alikuwa nje kutokana na majeruhi ya paja na hakuweza
pia kucheza katika fainali hiyo iliyopigwa katika dimba la Maracana
jijini Rio de Janeiro.
CHANZO: MWANASPOTI
CHANZO: MWANASPOTI

Post a Comment