A JOURNALIST IS BACK (MWANDISHI AMERUDI) - 03
MWANDISHI: NYEMO CHILONGANI
Endelea kulike: www.facebook.com/2jiachie
Tembelea: www.2jiachie.com
“Mnataka nini? Mnataka nini jamani?” Mzee Mrisho aliuliza huku hofu ikizidi kuongezeka.
Hata kabla mwanaume yule hajajibu chochote juu ya kile walichokuwa wakikitaka, Bi Sikujua akatokea sebueni pale. Akaamriwa anyamaze kimya, sauti yoyote kutoka kwake isisikike. Mwanaume mmoja alimsogelea na kumvuta katika upande aliokuwa mzee Mrisho.
“Tunamuhitaji mtu wetu” Mwanaume yule alimwambia mzee Mrisho
“Mtu gani jamani? Mbona mnanichanganya” Mzee Mrisho aliuliza.
“Unakumbuka nilichokuambia? Unakumbuka nilikwambia nini nilipoingia hapa?” Mwanaume yule aliuliza huku sauti yake ikisikika kama mtu aliyekasirika.
“Ndio. Ninakumbuka”
“Basi tunamuhitaji mtu wetu, hatuna muda mwingi wa kukaa mahali hapa” Mwanaume yule alimwambia mzee Mrisho.
SONGA NAYO....
“Jamani, mtu gani ambaye mnataka mimi niwape?” Mzee Mrisho aliuliza huku hofu ikiongezeka kadri muda ulivyozidi kwenda mbele.
“Tunamuhitaji mwandishi wa habari. Mwandishi yule mbeya” Mwanaume yule alimwambia.
“Mwandishi gani jamani?”
Yule mwanaume hakuongea kitu, mpaka muda huo tayari aliona kama anafanyiwa mzaha, akaivuta bunduki yake kwake na kuikoki hali iliyoonyesha alikuwa tayari kumfyatulia risasi mzee Mrisho. Bi Sikujua alikuwa akilia tu, hakuamini kama muda huo walikuwa wamewekwa chini ya ulinzi na watu ambao walionekana hatari, watu waliokuwa wameshika bunduki.
“Moja... niambie. Mbili.... niambie. Ta...”
“Subiri baba. Mimi nitakwambia ukweli” Bi Sikujua alimwambia.
“Ukweli gani?”
“Juu ya huyo mnayemtafuta”
“Tuambie yuko wapi?”
“Chumbani. Yuko chumbani. Naomba mmuache mume wangu” Bi Sikujua alimwambia.
“Chumba gani?”
“Chumba cha tatu koridoni upande wa kushoto” Bi Sikujua aliwaambia.
“Una bahati sana, mkeo ameokoa maisha yako” Mwanaume yule alimwambia mzee Mrisho.
Hawakutaka kupoteza muda, wote wakaanza kuelekea katika korido ile na kisha kuanza kuufuata mlango wa chumba kila. Walipoufikia, wakajaribu kuufungua, mlango ulikuwa mgumu hali iliyoonyesha kuwa ulifungwa kwa ndani. Wakaanza kuugonga kifujo fujo lakini mlango wala haukufunguka.
“Tuuvunjeni” Mwanaume yule aliyeonekana kuwa kiongozi aliwaambia wenzake na hatua za kuuvunja mlango kuanza.
Ni ndani ya dakika moja tu, mlango ukavunjika. Wakawasha tochi ambazo walikuja nazo mahali hapo na kuanza kumulika ndani ya kile chumba alichokuwa Dominick.
“Yule pale kitandani” Mwanaume mwingine aliwaambia wenzake na wote kuanza kumfuata Domonick kitandani huku bunduki zao zikiwa tayari.
***********
Kikao cha dharura kilikuwa kinaendelea kufanyika ndani ya chumba kimoja ambacho kilikuwa miongoni mwa vyumba vizuri vilivyokuwa katika nyumba ambayo ilikuwa ikiheshimiwa sana, nyumba ya kifahari iliyojengwa katika mtaa wa kifahari wa Osterbay.
Watu watatu ambao walikuwa wazee wa makamo ndio ambao walikuwa wamejikusanya ndani ya chumba hicho. Bado ajenda ambayo walikuwa wakiizungumzia katika kipindi hicho haikupatiwa muafaka kabisa. Kwa wakati huo, kila mmoja alionekana kuchanganyikiwa.
Dada waliyemtuma katika kufanya kazi ya kumuita Dominick katika hoteli ya New Africa alifanya kazi kama vile ilivyotakiwa kufanywa. Wasiwasi wao bado ulikuwa juu ya vijana wale ambao waliondoka na Dominick kuelekea katika msitu wa Nyakipande.
Bado hawakupata taarifa yoyote juu ya kilichoendelea msituni. Mara kwa mara walikuwa wakijaribu kuwapigia simu, simu hazikuwa zikipokelewa zaidi ya kuita mpaka kuzima. Mambo haya yote yakaonekana kuwatia wasiwasi.
Kikao kikaendelea zaidi na zaidi hadi kufikia muafaka wa kuwatafuta vijana wengine ambao wangeanza kufuatilia ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea msituni. Kutokana na usiku kuwa umekwenda sana, wakaahirisha kikao ambacho kilitarajiwa kufanyika tena kesho.
Siku iliyofuata vijana watatu wakatafutwa na kupewa mavazi ya kipolisi pamoja na kuwa na mbwa mmoja ambaye angetumika katika kunusa nusa ndani ya msitu ule. Safari ya kuelekea katika msitu wa Nyakipande ikaanza mara moja.
Mara baada ya vijana wale kuingia msituni wakaanza kuwatafuta watu wale ambao walikuwa wametumwa kuifanya kazi waliyopewa jana usiku. Walitembea sana msituni huku wakiongozana na mbwa ambaye alikuwa makini kunusa katika kila njia.
Hakukuwa na dalili zozote za kuwapata vijana wale kitu ambacho kiliwapelekea kumfuata mbwa kila sehemu alipotaka waelekee. Mbwa aliendelea kunusa ardhini huku akipita katika kila njia ambazo aliziona kuwa sahihi kwake. Ni ndani ya dakika tano tu, wakafika katika eneo ambalo lilikuwa na nyasi fupifupi.
Wote wakaanza kuangalia katika eneo hilo, miili ya watu watatu iliyokuwa na michirizi ya damu ilikuwa ikionekana vizuri machoni mwao. Kwa haraka wakapiga simu kwa wazee wale ambao walikuwa wamewatuma na kuwapa taarifa juu ya kile walichokuwa wamekiona.
“Kama ni hivyo, basi rudini” Sauti ya mzee mmoja iliskika.
“Turudi pamoja nayo?”
“Nini?”
“Hii miili”
“Hapana. Iacheni, hatuna kazi nayo”
“Sawa mkuu”
“Kuna bunduki walizokuwa wanazitumia mahali hapo?”
“Ndio”
“Hizo njooni nazo”
“Sawa” Kijana yule alijibu na kisha kukata simu.
Wazee walionekana kuchanganyikiwa, kitendo cha vijana wao kupigwa risasi na kisha Dominick kutoweka kilionekana kuwachanganya zaidi. Kila wakati walikuwa wakijiuliza ni kwa jinsi gani Dominick aliweza kupambana na vijana wao watatu waliokuwa na bunduki na kuwashinda nguvu.
Walichokifanya baada ya vijana wao kurudi ni kuwapa kazi ambayo vijana wale wengine walishindwa kuifanya. Dominick hakutakiwa kuwa hai tena, tayari alionekana kuwa hatari katika maisha yao kama tu wangemwacha aendelee kuvuta pumzi ya dunia hii.
Wakawatuma mitaani kuhakikisha Dominick anapatikana na kuuawa. Miezi miwili ilipita na ndipo taarifa za Dominick kufa zikaanza kutapakaa. Wazee wa hawakutaka kukubali kabisa. Ukweli waliujua kwamba Dominick hakuwa amekufa kama ilivyotangazwa, alikuwa hai akiwa amejificha sehemu fulani.
“Mtafuteni katika kila sehemu, ila Mbezi ndio muitolee macho sana” Mzee mmoja aliwaambia vijana wale.
“Sawa mkuu”
Dominick akaanza kutafutwa katika maeneo mengi ya Mbezi. Kazi haikuwa nyepesi hata kidogo, katika kila kona ambayo walikuwa wakifika, Dominick hakuwa akionekana kabisa. Siku ziliendelea kukatika lakini bado Dominick alionekana kuwa adimu kupatikana.
“Kuna tetesi zinasikika kuwa kuna nyumba ina mgeni ambaye hutoka nje usiku sana” Mmoja wa vijana wale waliotumwa na wazee wale, Pius aliwaambia wenzake.
“Nyumba gani?”
“Bado sijaifahamu, ila inatubidi tuendelee kuchunguza”
Uchunguzi wa kuigundua nyumba hiyo ukaanza mara moja, mara kwa mara walikuwa wakiwaaita vijana mbalimbali na kuwauliza swali juu ya nyumba hiyo.
“Hata mimi nimesikia. Ila si unajua umbea, kwanza mtu atakaaje na mtu pasipo kumtoa nje. Huo uzushi” Kijana mmoja alimwambia Pius.
“Kwani nyumba yenyewe ipi?”
“Kwani wewe mgeni maeneo haya? Hata nyumbani kwa mzee Mrisho haupafahamu?” Kijana yule alimuuliza Pius huku akionekana kumshangaa.
“Simjui yeyote huku. Bado mimi ni mgeni, nakaa hapo mtaa wa nyuma. Unamjua mzee Ally Mangushi?” Pius alisema na kuuliza swali.
“Yule mzee mfupi mwenye upara?”
“Ndio. Nyumbani kwake ndipo nilipopanga” Pius alimwambia kijana yule.
Pius hakutaka kuacha kuzungumza na kijana yule, muda wote alikuwa akiongea nae kama njia mojawapo ya kutafuta mazoea. Kijana yule akaonekana kumzoea Pius kana kwamba alikuwa rafiki yake wa muda mrefu.
“Ulisema nyumba ipi?”
“Kwa mzee Mrisho. Mzee mwindaji. Subiri akipita nitakuonyeshea”
“Hapana. Usifanye hivyo, kwani nyumba yenyewe iko wapi?”
“Kule mbele, nyumba yenye bucha kwa nje”
“Nimekwishaikumbuka. Kumbe pale ndipo anapokaa?”
“Ndio hapo hapo”
Pius hakutaka kuendelea kukaa mahali hapo, tayari alikwishaonekana kupata kile ambacho alikuwa akitaka ukipata kwa wakati huo. Moja kwa moja akaanza kuwasiliana na wazee ambao walikuwa wamemtuma na kuwapa taarifa juu ya kile kinachoendelea kwa wakati huo.
“Msimcheleweshe. Mkimpata muueni”
“Sawa. Ila hamtaki hata kiungo kimoja kutoka mwilini mwake?”
“Kama itawezekan, tuleteeni kichwa”
Mipango ikaanza kufanyika usiku huo. Pius akawaita wenzake na kuwaambia kila kitu ambacho kilikuwa kinaendelea. Hawakutaka kupoteza muda, walitaka kumtia mikononi Dominick hata kabla siku nyingine haijafika.
Wakapanga mpango mzima na hatimae wazo la kuzima umeme wa nyumba ile kupewa kipaumbele. Walitaka kuzima kwanza umeme wa nyumba ile kutoka katika chuma la umeme la nyumba ile kwa kutoruhusu umeme kuingia ndani na kisha ndipo wavamie.
“Hilo wazo zuri sana. Tufanyeni hivyo hivyo” Kimbetu alimwambia Pius.
Usiku ulipoingia, kazi ikaanza mara moja Wakaelekea katika duka la vifaa mbalimbali na kununua plaizi kwa ajili ya kukata waya wa umeme ambao ulikuwa ukipitisha umeme katika nyumba ya mzee Mrisho. Mara walipopata kila kitu walichokuwa wakikihitaji, wakajiandaa na kazi.
Usiku ulipoingia, wakasubiri mpaka ifike saa mbili. Muda ulipotimia, moja kwa moja wakaanza kupiga hatua kuelekea katika eneo ilipokuwa nyumba ile.
“Kwa hiyo tunaanza kukata waya?”
“Ndio”
“Basi msitake kupoteza muda, mtakapoona umeme umezimika, pigeni hodi” Jonas aliwaambia.
“Poa” Pius aliitikia na kisha yeye na Kimbetu kuanza kuelekea mlangoni.
Jonas akaanza kupanda katika ukuta wa nyumba ile mpaka pale alipolifikia chuma la umeme na kisha kuchukua plaizi na kuukata waya uliokuwa ukipitisha umeme ndani ya nyumba ile. Umeme ndani ya nyumba ile ukakatika.Pius na Kimbetu hawakutaka kupoteza muda, wakaanza kugonga mlango.
*********
Dominick alikuwa amechoka kukaa sebuleni, kila kitu ambacho kilikuwa kinaendelea katika vituo mbalimbali vya televisheni aliviona kuwa kama vikimpotezea muda. Akainuka katika kochi alilokuwa amekalia na moja kwa moja kuelekea chumbani huku akimwacha mzee Mrisho sebuleni pale.
Dominick akapanda kitadani, hata kabla hajachukua muda mrefu kitandani pale, akaanza kusikia minong’ono kutoka nje ya nyumba ile karibu kabisa na dirisha la chumba kile. Kwa kasi ya ajabu, Dominick akainukana kufungua pazia kuchungulia nje.
Vijana watatu walikuwa wamesimama nje karibu kabisa na dirisha la chumba chake. Dominick hakutaka kujiuliza watu wale walikuwa ni wakina nani, moja kwa moja akatoka nje ya chumba kile na kuelekea koridoni ambako akaanza kupiga hatua kuelekea jikoni.
Alipofika jikoni akaufungua mlango na kisha kutoka nje. Dominick akaanza kukimbia kuelekea mbali kidogo na nyumba ile, alipofika umbali fulani, akasimama kwa kujificha katika ukuta wa nyumba moja na kuanza kuchungulia kuona ni kitu gani ambacho kilikuwa kinaendelea.
Kwa mbali akamuona mwanaume mmoja akipanda katika ukuta ambao ulikuwa karibu na chuma lililokuwa limeshikiria nyaya iliyokuwa ikiingia ndani ya nyumba ile. Wala hazikupita hata sekunde ishirini, umeme ndani ya nyumba ile ukakatika.
Vijana wawili wakaanza kupiga hatua kuufuata mlango wa kuingilia sebuleni ambako baada ya kuufikia, wakaanza kugonga. Wala haukupita muda mrefu, mzee Mrisho akaufungua mlango ule.
Kila kitu ambacho kiliendelea baada ya vijana wale kuingia ndani ya nyumba ile wala Dominick hakuwa akikifahamu. Alibaki pale katika kiambaza cha ukuta huku akiendelea kuangalia kule ilipokuwa nyumba ya mzee Mrisho.
Wala hazikupita dakika nyingi, akawaona wanaume wale wakitoka nje ambako mmoja wao akatoa amri wajitawanye mahali hapo.
“Atakuwa yupo karibu na hapa. Mtafuteni” Sauti ya Pius iliskika na vijana wale wawili kutawanyika kumtafuta Dominick ambaye waliamini kwamba hakuwa mbali na mahali hapo.
Dominick hakutaka kuendelea kubaki mahali hapo, tayari alikwishaona kuwa wanaume wale hawakuwa na amani hata kidogo. Kwa kasi ya ajabu nae akaanza kukimbia kuelekea mbele zaidi ya mtaa ule.
Dominick alipofika katika barabara ya lami, akasimamisha taksi moja ya kukodi na kuingia ndani. Kutokana na mwanga hafifu uliokuwepo ndani ya gari lile, dereva hakuweza kumjua kama mteja ambaye alimpakiza alikuwa Dominick, mwandishi ambaye alisemekana kufa miezi mitatu iliyopita.
Taksi ilisimama nje ya nyumba moja ambayo ilikuwa imezungushiwa ukuta pamoja na kuwa na geti kubwa la rangi nyeupe. Dominick akaingiza mkono mfukoni na kutoa kiasi ambacho kilihitajika na dereva yule kisha kuteremka na kuanza kuugonga mlango.
Mlinzi alisikika akielekea getini pale ambako akafungua geti na moja kwa moja kuingia ndani. Mlinzi akamsimamisha Dominick huku akionekana kukasirika na kitendo kile cha kuingia moja kwa moja katika eneo la nyumba ile pasipo hata ruhusa.
“Mbona unaingia moja kwa moja hata bila kuuliza?” Mlinzi alimuuliza Dominik aliyeonekana kuchanganyikiwa.
“Samahani sana. Akili yangu haiko sawa kabisa. Edmund yupo?” Dominick alimuuliza mlinzi.
“Mbona usiku sana. Wewe nani?”
“Rafiki yake, ninafanya kazi pamoja nae”
“Namba yake ya simu si unayo hapo, kwa nini usimpigie?”
“Hapana. Simu yangu haina chaji. Naomba ukaniitie mara moja” Dominick alimwambia mlinzi ambaye pasipo kuuliza swali jingine akaanza kuufuata mlango na kubonyeza kengele.
Wala haikupita hata dakika moja, mlango ukafunguliwa na mfanyakazi wa ndani. Mlinzi akaanza kumuelezea mfanyakazi yule juu ya Dominick. Msichana yule wa kazi akaondoka na kuelekea ndani ambako baada ya muda, Edmund akatokea.
“Kuna mgeni gani?” Edmund alimuuliza mlinzi.
“Mimi hapa”
“Wewe nani?”
“Sogea karibu”
Edmund akaanza kupiga hatua kumfuta Dominick. Edmund hakuamini macho yake mara baada ya kumfikia Dominick. Hofu ilimjaa moyoni huku mapigo yake ya moyo yakiongeza kasi ya udundaji. Mtu ambaye alikuwa akionekana mbele yake, walikwishamzika miezi mitatu iliyopita, kwake, Dominick alionekana kuwa kama mzimu.
“Dominick!” Edmnd aliita huku akionekana dhahiri kutaka kukimbia.
“Ndio mimi, Edmund”
Edmund akapiga hatua zaidi, alipomfikia Dominick, akamkumbatia kwa furaha. Macho yake hayakuamini kabisa, alijiona kuwa kama ndotoni ambako muda mchache ujao angeamka na kujikuta yuko kitandani.
Wote wakaanza kuelekea ndani ambako wakakaa kochini na kisha Dominick kuanza kumuelezea Edmund kila kitu ambacho kilitokea baada ya kupotea kwake. Edmund alibaki akishangaa, hakuamini kama duniani kulikuwa na mtu aliyekuwa na bahati kama aliyokuwa nayo Dominick.
“Kwa hiyo unamaanisha hauwafahamu kabisa watu wanaokutafuta?”
“Hadi sasa sijafahamu. Ila kuna kitu nataka kukifanya na ningependa msaada wako” Dominick alimwambia Edmund.
“Kitu gani?”
“Subiri”
Dominick akaingiza mkono mfukoni na kisha kuitoa simu yake. Akaiwasha na moja kwa moja kwenda katika sehemu ambayo ilikuwa na kumbukumbu juu ya simu zote zilizoingia.
“Kuna namba hii nataka uende ukaiulizie” Dominick alimwambia Edmund huku akimpa simu.
“Namba ya nani hii?”
“Ya mwanamke yule aliyenipigia siku ile”
“Sasa nitamjua vipi?”
“Nenda katika kampuni hii ya simu, ukifika waambie uongo wowote hadi wakwambie namba hii ni ya nani na anakaa wapi. Tukimpata huyu mwanamke, kila kitu kitakuwa rahisi” Dominick alimwambia Edmund.
“Sawa”
**********
Pius akakifuata kitanda kile na kulifunua shuka. Kila mtu alikuwa na uhakika kwamba Dominick ndiye ambaye alikuwa amejifunika kitandani pale. Pius akalifunua shuka, ni mito tu ndio ambayo ilikuwa kitandani pale, ilikuwa imepangwa vizuri.
INAENDELEA NDANI YA WEBSITE YETU HII

Post a Comment