A JOURNALIST IS BACK (MWANDISHI AMERUDI) - 02
MWANDISHI: NYEMO CHILONGANI
Endelea kulike: www.facebook.com/2jiachie
Tembelea: www.2jiachie.com
“Kwa nini unadhania hivyo?”
“Hebu jifikirie, kwanza habari kuhusu yeye niliiandika miaka miwili iliyopita, halafu kingine, tayari alikwishafariki. Unalikumbuka hilo mkuu?” Dominick alimwambia na kumalizia na swali.
“Mhhhh... Lakini hapa kuna ukweli”
“Sasa swali linalonijia kichwani juu ya mtu aliyehusika na tukio hili” Dominick alimwambia Bwana Idrisa.
Kadri siku zilivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo afya ya Dominick ilivyozidi kushuka. Mwili wake ukapungua kupita kiasi, mawazo juu ya familia yake bado yalikuwa yakimsumbua kila siku. Dominick alijiapia kutaka kulipiza kisasi kwa mtu yeyote mbaye alikuwa amehusika kwa namna moja au nyingine katika kumuumiza.
SONGA NAYO...2JIACHIE NDO MPANGO MZIMA
Katika kipindi hicho hakuwa na nyumba, alikuwa akiishi kwa rafiki yake, Edmund ambaye alikuwa akifanya kazi ya Uandishi pamoja nae. Maisha yake aliyaona yakianza nyuma kabisa katika pointi ya kwanza ambayo alikuwa akiishi kabla ya kuoa.
Kila siku Dominick alikuwa akiuliza kuhusu upelelezi ambao ulikuwa bado ukiendelea kufanyika. Aliona kila kitu kikikwenda taratibu sana. Katika kipindi hicho alihitaji hata tetesi ya nani alikuwa amehusika katika kufanya mauaji yale.
Hakukuwa na tetesi zozote zile alizozisikia kutoka katika kitengo cha polisi cha upelelezi, kila kitu kilionekana kuwa kigumu. Kwa wakati huo, kila gazeti lilikuwa na taarifa zake, waandishi wa habari wakaanza kuingiwa na hofu ya kuandika mambo mengi kuhusiana na wizi ambao ulikuwa ukifanyika katika sekta mbalimbali Serikalini.
Maisha yaliendelea kama kawaida. Baada ya miezi mitatu ya kujipanga upya, Dominick akajiona kuanza kusahau. Akaanza kufanya kazi kama kawaida japokuwa mara kwa mara alikuwa akiikumbuka familia yake hasa kila alipokuwa akiziangalia picha ambazo walipiga pamoja.
“Kuna habari kuhusu nini?” Dominick alimuuliza mwanamke ambaye alimpigia simu.
“Ufisadi. Kuna ufisadi umefanyika katika hili shirika la serikali la nyumba za taifa, NHC. Kuna kamchezo kamefanyika hapa” Sauti ya mwanamke yule ilisikika.
“Kuna ushahidi wowote juu ya habari hiyo?”
“Ushahidi upo. Tuna mikanda baadhi ambayo itakudhihirishia hilo” Sauti ya mwanamke yule ilisikika.
“Sawa. Uko wapi ili nije kuichukua habari hiyo?”
“Njoo hapa New Africa Hoteli”
“Nitakuwa hapo baada ya dakika ishirini” Dominick alisema na kukata simu.
Hakuwa na cha kufanya kwa wakati huo zaidi ya kujiandaa na kisha kuanza safari ya kuelekea katika hoteli ya New Afrika. Dominick alionekana kuwa na hamu kubwa ya kuandika habari ambazo zilikuwa zikihusu wizi ambao ulikuwa ukiendelea kufanyika japokuwa kwa wakati huo tayari ulikuwa umepungua kwa kiasi kikubwa.
Ingawa saa yake ilikwa ikimwambia kuwa ni saa nne usiku lakini hilo hakuonekana kulijali,kitu ambacho alikuwa akikijali ni kufanya kazi yake tu.
Mara baada ya kufika Jangwani, akaongeza kasi ya gari lake mpaka alipofika maktaba ya Taifa ambapo akakata kona kulia na kuanza kuelekea Posta. Wala hakuchukua sekunde nyingi, akaaingia katika eneo la hoteli ya New Afrika.
Huku akiwa hajateremka, ghafla akashtuka baada ya kuwaona vijana watatu wakielekea kule alipokuwa garini. Hata kabla hajajiuliza juu ya watu wale, akashtukia wakiingia ndani ya gari lake.
“Mbona mnai.....” Dominick aliuliza lakini hata kabla hajaalizia swali lake, akajikuta akiwekwa chini ya ulinzi na mwanaume mmoja ambaye alishika bunduki.
“Fuata maelekezo yetu kuanzia sasa. Kama utakuwa mkaidi, utaifuata familia yako” Mwanaume yule alimwambia Dominick.
Hakuwa na la kufanya kwa wakati huo, mdomo wa bunduki ambao alikuwa ameelekezewa ulionekana kumuogopesha kupita kiasi. Akawasha gari lake na kuanza kuelekea kule ambako alitakiwa kwenda kwa wakati huo.
“Lakini nimefanya nini jamani?” Dominick aliuliza huku akionekana kuogopa.
“Kwani wewe umekuja hotelini kufanya nini?” Mwanaume mmoja kati ya wale watatu alimuuliza.
“Nilipigiwa simu ya kikazi. Kama mnataka kuchukua gari, tafadharini, lichukueni ila niachieni niendelee na kazi yangu” Dominick alijitetea.
“Hakuna. Hakuna kitu kama hicho. Kama magari, tunayo mengi na ya kutosha. Kwa sasa hatuhitaji gari, tunachohitaji ni roho yako tu” Mwanaume yule alisema maneno ambayo yalimshtua Dominick.
“Unasemaje?” Dominick aliuliza huku aisimamisha gari.
“Najua umenisikia. Topa, shikiria usukani” Mwanaume yule aliyejiita Kibra alimwambia mwenzake na Dominick kuchukuliwa na kuwekwa katika viti vya nyuma.
“Jamani. Nimefanya nini, nimefanya nini jamani. Mmeiua familia yangu, hamjalidhika tu mpaka mnataka kuniua na mimi?” Dominick aliuliza huku akianza kutokwa na machozi.
Hakuwa na tumaini lolote kwa wakati huo, tayari alijiona kuwa kama mfu ambaye alikuwa akitembea, aliuangalia mdomo wa bunduki ile, bado ulionekana kumtisha. Tayari akaanza kuhesabu dakika za yeye kuvuta pumzi ya dunia hii, hakuwa na uhakika kama angeweza kunusurika katika mikono ya watu hao.
“Lakini ni nani ananifanyia hivi? Kwa nini lakini” Dominick aliuliza.
“Hata sisi hatumfahamu na wala hatufahamu ni kwa nini anafanya hivi. Sisi tunachokitaka ni utekelezaji tu” Kibra alimwambia Dominic.
Njia nzima Dominick alikuwa akilia huku akiwaomba watu wale wamuachie. Hakukuwa na mtu yeyote ambaye alionekana kuelewa chochote kile, kitu ambacho walikuwa wakikitaka kukifanya kwa wakati huo kilikuwa ni utekelezaji wa kile walichotumwa tu.
Gari likafungwa breki katika msitu wa Nyakipande, Dominick akateremshwa. Giza lilikuwa kubwa wakati huo, moja kwa moja akaanza kuingizwa ndani ya msitu huku akiwa amefungwa kitambaa usoni. Muda wote Dominick alikuwa akilia tu huku akiomba msamaha japokuwa hakuwa amelifahamu kosa lake.
Dominick akapelekwa mpaka katika sehemu ambayo ilikuwa na nyasi ndefu na kulazwa chini. Kibra akachomoa bunduki yake na kuanza kuisafisha kwa mbwembwe zote. Bado Dominick alikuwa akilia ingawa hakukuwa na mtu yeyote ambaye alionekana kumjali.
“Tutakuua kifo kilichojaa maumivu, ili utakapokuwa ukiumia, basi ujute kwa nini ulikuwa ukipenda kuandika mambo ya watu gazetini” Kibra alimwambia Dominick huku akimwuelekezea bunduki.
“Paaaaaa....” Mlio wa risasi ulisikika, Dominick alikuwa akiugulia kwa maumivu huku akiushika mguu wake.
Damu zilikuwa zikimtoka mguuni, risasi ilikuwa imepenya katika mguu wake. Kilio kikubwa ndicho ambacho kilikuwa kikisikika kutoka kwa Dominick. Kibra na wenzake wakabaki wakicheka, walionekana kuyafurahia maumivu ya Dominick.
“Tutaendelea hivi hivi mpaka pale utakapoanza safari ya kuifuata familia yako” Kibra alimwambia Dominick huku akiwa amemuelekezea tena bunduki.
“Paaaaaaa.....” Mlio wa risasi ulisikika kwa mara ya pili.
“Paaaa... paaaa....paaaa...paaaaa...” Milio mingine ya risasi ikasikika katika eneo hilo, damu zikatapakaa katika eneo hilo, ukimya ukatawala, hakukuwa na sauti yoyote ambayo ilisikika katika kipindi hicho hata ile sauti ya kilio cha Dominick haikusikika tena.
************
Siku ziliendelea kukatika, wafanyakazi wa kampuni ya magazeti ya Hold on Publishers wakaonekana kuchanganyikiwa. Siku nyingi zilikuwa zimekatika pasipo Dominick kuonekana. Wasiwasi ukazidi kuogezeka zaidi hasa mara baada ya Edmund kusema kwamba hakuwa amelala kwake karibu siku tano.
Taarifa zikatolewa katika vituo mbalimbali vya polisi na kazi ya kumtafuta Dominick kuanza. Dominick alitafutwa katika sehemu nyingi lakini wala hakupatikana. Taarifa zikatolewa gazetini, kila mtu ambaye aliiona taarifa ile ya kupotea kwa mwandishi ambaye alikuwa akiandika mambo mengi kuhusiana na viongozi wezi alibaki na mshangao.
Maswali mengi yalikuwa yakimiminika vichwani mwa Watanzania, upotevu wa Dominick ukaonekana kumtia wasiwasi kila mmoja. Tetesi za Dominick kuuawa zikaanza kutapakaa katika kila kona ya jiji la Dar es Salaam. Kila mtu aliamini kuwa Dominick aliuawa na watu ambao walikuwa wameiteketeza familia yake.
Baada ya miezi mitatu, mazishi yakaanza kufanyika. Watu wengi walishiriki katika mazishi ya Dominick, picha yake kubwa ilikuwa mbele ya jeneza lake. Watu ambao walikuwa na upendo mkubwa kwa Dominick, walilia mpaka wengine kupoteza fahamu.
Nchi ya Tanzania ikaonekana kumpoteza mtu shujaa, mtu ambaye alikuwa akitaka Watanzania waishi katika maisha mazuri kupitia uandishi kwa kuwataja viongozi ambao walikuwa wakiiba fedha za wananchi. Jeneza likafukiwa katika makaburi ya Kinondoni, hakukuwa na mtu aliyeamini kama Dominick waliyekuwa wakimpenda alikuwa ameuawa.
“Acha akapumzike na familia yake” Kijana mmoja aliwaambia wenzake huku macho yake yakiwa mekundu.
Kampuni ya kutengeneza magazeti ya Hold On Publisher ikatoa siku thelethini za kuomboleza. Wafanyakazi wa kampuni hiyo walipunguziwa masaa mawili ya kufanya kazi ndani ya mwezi huo. Siku ziliendelea kukatika mpaka mwaka kuisha, Dominick akasahaulika vichwani mwa watu.
“Mwaka jana tulikuwa na mwandishi mzuri sana. Aliandika wizi ambao ulikuwa ukifanyika katika sekta mbalimbali, namkumbuka mtu huyu, familia yake iliuawa kabla ya yeye mwenyewe kuuawa na maiti yake kutoonekana mpaka leo” Mwandshi mmoja alimwambia mwenzake mara baada ya kuhitimu masomo yake katika chuo kikubwa cha DSJ (Dar es Salaam School of Journalism).
“Namkumbuka sana. Si yule Dominick aliyekuwa akiitwa shujaa. Namkumbuka sana, katika maisha yangu sitoweza kumsahau mtu kama yule” Mwandishi mwingine alisema.
“Mungu Amlaze Pahali Pema Peponi”
“Amen”
*************
Mzee Mrisho alikuwa mtu maarufu sana katika sehemu yote ya Mbezi. Kila mtu ambaye alikuwa akiishi Mbezi alikuwa akimfahamu mzee huyu kutokana na biashara yake aliyokuwa akiifanya ya kuuza nyama katika moja ya bucha lake lililokuwa Mbezi kwa Yusufu.
Nyama mbalimbali zilikuwa zikipatikana buchani kwake hali ambayo iliwafanya watu wengi kumiminika buchani hapo kununua nyama kwa ajili ya mboga. Nyama nyingi zilikuwa zikipatikana buchani hapo, swala, nyati, mbuzi na ng’ombe zilikuwa ni moja ya nyama ambazo zilikuwa zikipatikana kwa wingi.
Mzee Mrisho alizaliwa miaka hamsini iliyopita mkoani Shinyanga. Alizaliwa katika familia ya mwindaji, baada ya miaka kadhaa nae akaanza kuelekea kuwinda pamoja na baba yake. Mpaka anakuja kufikisha miaka kumi na nane, Mrisho alikuwa mwindaji mzuri.
Alipofikisha miaka ishirini, baba yake alifariki dunia, kazi ya uindaji ikabakia kwake, kila siku alikuwa akielekea porini kuwinda. Kila mtu aliyekuwa akiishi Shinyanga alikuwa akimfahamu Mrisho ambaye maisha yake yalikuwa yakiendeshwa na biashara hiyo.
Kila siku jina la Dar es Salaam lilikuwa kichwani mwake, jiji hilo ambalo alikuwa akilisikia masikioni mwake kutoka kwa watu mbalimbali lilionekana kumvutia. Mrisho akajikuta akitamani kufika jijini Dar es Salaam na kuanza maisha huko.
Alichokifanya Mrisho ni kuanza kuzihifadhi fedha alizokuwa nazo. Baada ya miaka miwili alikuwa na fedha za kutosha ambazo zilimfanya kusafiri kuelekea Dar es Salaam. Mrisho alionekana kuwa mshamba kwa kila kitu ambacho alikuwa akikiona, majengo mazuri pamoja na mpangilio wa nyumba vilikuwa vitu ambavyo vilimvutia kupita kiasi.
Mrisho hakutaka kukaa tu nyumbani, akaanza kutafuta kazi. Kazi hazikuwa rahisi kupatikana, alitembea umbali mrefu kutafuta kazi lakini hakukuwa na mafankio yoyote yale. Miaka ilizidi kukatika, Mrisho akaamua kuanza biashara ya kuuza genge.
Mara baada ya kusikia juu ya wanyama waliokuwa wakipatikana katika msitu wa Nyakipande, Mrisho akavutiwa, akaamua kuhamia Mbezi. Huko ndiko ambako akaanza kazi kama ile ambayo alikuwa akiifanya Shinyanga.
Kila siku alikuwa akitoka asubuhi kuelekea katika msitu wa Nyakipande ambako alikuwa akiwinda na kurudi jioni huku akiwa na vitoweo vya kutosha. Biashara ya kuuza nyama ikaonekana kuchanganya, akaamua kuanzisha bucha ambalo alikuwa akiuza nyama mbalimbali.
Watu walikuwa wakimiminika. Kila baada ya siku mbili alikuwa akiingia porini kuwinda. Mrisho akaonekana kuuzoea msitu wa Nyakipande, kila kona za msitu huo alikuwa akizifahamu vilivyo. Mrisho hakuwa akipata kazi kutokana na makazi mengi ya wanyama kuyafahamu.
Miaka iliendelea kwenda mbele hadi alipokuja kuoa na kupata watoto. Serikali ikakataza uwindaji ambao ulikuwa ukifanyika katika msitu wa Nyakipande, ulinzi mkali ukawekwa. Maisha yalionekana kuwa tofauti kwake lakini baada ya muda, maisha yakaanza kurudi katika hali ya kawaida kama zamani.
Akaanza kuwinda usiku na kurudi nyumbani asubuhi. Hayo ndio yalikuwa maisha yake, aliingia msituni usiku na kurudi asubuhi. Nyama ambazo alikuwa akizipata porini ndizo ambazo alikuwa akiziuza buchani ambako mtoto wake, Selemani ndiye alikuwa msimamizi wa bucha hilo.
“Twendeni kule” Sauti ilisikika msituni.
Mzee Mrisho aliisikia sauti ile vizuri, akachukua gobole lake na kujificha. Tayari akili yake ilikwishamwambia kuwa watu hao ambao walikuwa wakiongea walikuwa mapolisi ambao kazi yao ilikuwa ni kuhakikisha ulinzi msituni mule.
Sauti za watu wale ziliendelea kusikika. Mzee Mrisho alitaka kupiga hatua kurudi lakini akajikuta akishindwa kufanya hivyo. Alijikuta akivutiwa zaidi kuwafuatilia watu hao ambao alikuwa na uhakika kuwa hawakuwa walinzi.
“Hawa sio walinzi, ulinzi gani usiku namna hii?” Mzee Mrisho alijiuliza.
Akaanza kupiga hatua kuelekea kule ambako watu hao walisikika wakielekea. Mgobole wake ulikuwa makini mkononi mwake, alionekana kutaka kujitetea na hatari yoyote ambao ingeweza kutokea mahali hapo.
Aliendelea kuwafuatilia watu hao huku akijifichajificha. Safari ya watu wale ikashia katika sehemu ambayo ilikuwa na uwazi mkubwa. Ingawa kulikuwa na giza lakini mzee Mrisho alikuwa akiona kila kitu ambacho kilikuwa kinaendelea.
Mtu mmoja aliwekwa chini, sauti ya mtu yule haikuwa ikisikika vizuri hali ambayo aliigundua kwamba alikuwa amezibwa mdomo kwa kutumia kitambaa. Mwanaume mmoja akaonekana akichomoa bunduki na kisha kumuelekezea mtu yule ambaye alikuwa chini.
“Tutakuua kifo kilichojaa maumivu, ili utakapokuwa ukiumia, basi ujute kwa nini ulikuwa ukipenda kuandika mambo ya watu gazetini” Sauti ya mwanaume mmoja ilisikika.
Mlio wa risasi ukasikika, mwanaume yule aliyekuwa chini alisikika akipiga kelele za maumivu. Tayari mzee Mrisho aliona hakukuwa na amani mahali pale, alijiona kuwa na nafasi ya kufanya chochote ili aokoe maisha ya mwanaume yule.
Wanaume wale watatu walibaki wakicheka hali iliyoonyesha kwamba walikuwa wakiyafurahia maumivu ya mwanaume yule aliyekuwa akilia. Mwanaume yule ambaye alimpiga risasi mwanaume yule aliyekuwa chini, akamuelekezea tena bunduki tayari kwa kumpiga risasi nyingine.
Mzee Mrisho akajikuta akichukua mgobole wake na kumwelekezea mwanaume yule aliyekuwa ameshika bunduki. Hakutaka kuchelewa, hapo hapo akamfyatulia risasi ya kichwa, mwanaume yule akaanguka chini kama mzigo wa viazi.
Hata kabla wale wenzake hawakujua wafanye nini, wakashtukia wakipigwa risasi za vifuani, damu zikatapakaa mahali pale. Wote wakaanguka chini ambako wakaanza kurusha mikono na miguu yao, baada ya muda, wakatulia hali iliyoonyesha tayari walikuwa wamekufa.
Mzee Mrisho akachomoka kutoka kichakani na kumfuata mwanaume yule aliyekuwa akilia kwa maumivu makali, akambeba na kuanza kuondoka nae pasipo kuongea nae kitu chochote kile. Safari ya kurudi nyumbani ikaanza, ilikuwa safari ndefu huku mwanaume yule akiwa mgongoni mwake.
Alitumia masaa mawili, akawa amekwishafika nyumbani huku ikiwa saa tisa usiku. Mkewe akamfungulia mlango, mshangao mkubwa ukampata, hakuelewa ni kitu gani ambacho kilikuwa kinaendelea mpaka mumewe kurudi na mtu ambaye alionekana kuwa kama maiti.
“Kuna nini tena mume wangu?” Bi Sikujua aliuliza.
“Bandika maji jikoni kwanza” Mzee Mrisho alimwambia mkewe.
Pasipo kuuliza kitu chochote kile, Bi Sikujua akaelekea jikoni ambako akabandika sufuria iliyokuwa na maji na kisha kurudi sebuleni ambako mzee Mrisho akaanza kumuelezea kila kitu kilichotokea.
“Kwa hiyo haumfahamu kabisa?”
“Ndio. Niliamua kumsaidia, niliona akiwa katika hali ya hatari” Mzee Mrisho alimwambia mkewe.
Maji yalipochemka, yakaletwa na mzee Mrisho kuanza kufanya kazi ya kuiondoa risasi katika mguu wa mwanaume yule. Kilio kikubwa kilisikika lakini mzee Mrisho hakuonekana kujali, aliendelea na kazi ile mpaka risasi ilipotoka na kisha kumfunga bandeji.
“Asubuhi ikifika, tutaelekea hospitalini kumnunulia dawa” Mzee Mrisho alimwambia mkewe, Bi Sikujua.
“Kwa nini tusimpeleke hospitalini tu?”
“Hapana. Maisha yake bado nayaona kuwa katika hatari” Mzee Mrisho alimwambia mkewe.
************
Maisha yaliendelea mbele, Dominick hakuruhusiwa kutoka nje, kila siku maisha yake yalikuwa ndani ya nyumba ya mzee Mrisho. Kila kitu alikuwa akikipata ndani ya nyumba ya mzee Mrisho, maisha yake hayauonekana kuwa na amani nje ya nyumba hiyo.
Kitu alichokuwa akikifahamu ni kwamba kila siku angekuwa akitafutwa kwa lengo moja tu la kuuawa. Hakuamini kama watu ambao waliwatuma vijana wale wangeridhika kama wangepeta taarifa kuwa mtu ambaye alitakiwa kuuawa hakuuawa kama ilivyotakiwa iwe.
Dominick akajiona kuingia katika vita, vita ambayo alitakiwa kuimaliza kwa mikono yake mwenyewe. Kila siku maombi yake yalikuwa juu ya kumfahamu mtu au watu ambao walikuwa nyuma ya mpango wa kuuawa kwake.
Kila siku Dominick alikuwa akiyafikiria maneno yale ya BoT ambayo yalikuwa yameandikwa nje ya geti lake katika siku ambayo nyumba yake ilichomwa moto na familia yake yote kuangamia. Maneno yale yalieleweka vizuri na hata makao makuu ya idara ile alipafahamu vilivyo.
Kitu alichokijua ni kwamba hakukuwa na mtu yeyote kutoka katika idara ile ambaye alihusika kutokana na yule mtu aliyefanya ufisadi kuuawa kwa kulegezewa breki ya gari lake alipokuwa akielekea Dodoma. Bado Dominick alionekana kuchanganyikiwa, hakuelewa kabisa mtu ambaye alikuwa nyuma ya tukio hilo.
Kila siku alitamani kuwasiliana na marafiki zake ili kuwapa taarifa juu ya uwepo wake katika nyumba ya mzee Mrisho lakini kila alipotaka kufanya hivyo, alisita kwa kuogopa kujulikana kuwa yuko hai.
Kila siku alikuwa mtu wa kulala ndani, hakutakiwa kutoka nje wala hakutakiwa mtu yeyote kufahamu kuwa yuko ndani ya nyumba ile.
Mpaka taarifa za kifo chake zilipokuwa zinatangazwa, yeye mwenyewe alikuwa akiangalia katika televisheni. Dominick alibaki akifurahia kwani alijua kuanzia kipindi hicho asingeweza kupata usumbufu wowote ule.
Siku ziliendelea kukatika mpaka mwezi mmoja kupita, bado Dominick alikuwa akishinda ndani. Hakutakiwa kutoka kabisa nje ya nyumba hiyo, na kama alitaka kutoka, basi kitendo hicho kilitakiwa kufanyika usiku, muda ambao hakukuwa na watu wengi mtaani.
Hayo ndio maisha ambayo Dominick alikuwa akiishi. Kila kitu ambacho kilikuwa kinaendelea, alikuwa akipata taarifa kupitia televisheni na magazeti ambayo mzee Mrisho alikuwa akiyaleta.
“Kila mtu anajua kuwa uliuawa, hakuna mtu ambaye anajua kama uko hai” Mzee Mrisho alimwambia Dominick.
“Kwa hiyo wanachofahamu kuwa kwa sasa nipo kaburini?”
“Ndio. Tena umeoza kabisa” Mzee Mrisho alimwambia Dominick.
Dominick hakutaka kuendelea kukaa sebuleni hapo, moja kwa moja akainuka na kuaelekea chumbani. Mzee Mrisho alibaki sebuleni pale akiangalia televisheni. Dakika ziliendelea kukatika, mzee Mrisho hakutaka kwenda chumbani mpaka muda wa taarifa ya habari utimie, aliendelea kusubiri zaidi na zaidi.
Huku akiendelea kuwa sebuleni hapo, mara umeme ukakatika na giza kutawala mahali hapo. Mzee Mrisho akaonekana kukasirika, akainuka kutoka pale alipokaa na kuelekea kule ilipokuwa soketi ya umeme na kuizima.
Hata kabla hajapiga hatua kuelekea chumbani, mara akasikia mlango ukigongwa. Mzee Mrisho hakuonekana kuwa na wasiwasi, akaanza kupiga hatua kuufuata mlango na kuufungua.
Mzee Mrisho akashtuka kupita kawaida, mdomo wa bunduki ulikuwa umeelekezewa usoni mwake na mtu ambaye hakuweza kumhamu kutokana na giza lililokuwa mahali pale. Hata kabla mzee Mrisho hajaamua ni kitu gani alitakiwa kufanya, akaamriwa kuingia ndani.
“Jamani, kuna nini tena?” Mzee Mrisho aliuliza huku akionekana kuwa na hofu.
“Tutakachohitaji, tutataka kupatiwa. Na kama hatutopatiwa, milio ya risasi itakwenda kusikika mahali hapa” Mwanaume yule alimwambia mzee Mrisho huku wenzake wawili wakiwa wamekwishaingia ndani ya nyumba ile.
“Mnataka nini? Mnataka nini jamani?” Mzee Mrisho aliuliza huku hofu ikizidi kuongezeka.
Hata kabla mwanaume yule hajajibu chochote juu ya kile walichokuwa wakikitaka, Bi Sikujua akatokea sebueni pale. Akaamriwa anyamaze kimya, sauti yoyote kutoka kwake isisikike. Mwanaume mmoja alimsogelea na kumvuta katika upande aliokuwa mzee Mrisho.
“Tunamuhitaji mtu wetu” Mwanaume yule alimwambia mzee Mrisho
“Mtu gani jamani? Mbona mnanichanganya” Mzee Mrisho aliuliza.
“Unakumbuka nilichokuambia? Unakumbuka nilikwambia nini nilipoingia hapa?” Mwanaume yule aliuliza huku sauti yake ikisikika kama mtu aliyekasirika.
“Ndio. Ninakumbuka”
“Basi tunamuhitaji mtu wetu, hatuna muda mwingi wa kukaa mahali hapa” Mwanaume yule alimwambia mzee Mrisho.
ITAENDELEA SIKU YA KESHO.

Post a Comment