VITILIVYOGO (PAPA NA MUHOGO) - 06
MTUNZI: DK. AMBE
Endelea kulike ==>www.facebook.com/2jiachie
“Ha, Jay! Vipi mwana?” alimuuliza baada ya kukuta ni mwanafunzi anayemfahamu.
“Nina ujumbe wako.”
“Ujumbe! Upi?” Shaka alishtuka.
“Kutoka kwa Stella.”
“Stella! Yupi?”
“Unayesoma naye.”
“Ooh! Anasemaje?”
“Amenipa bahasha hii.”
Shaka aliipokea na kuiweka kwenye begi la shule na kuelekea kwenye daladala na kuwahi zake nyumbani. Alipofika nyumbani hakukaa sana, alibadili nguo na kwenda kwa mpenzi wake, Betty.
Alipomuona alijawa na furaha.
“Jamani mpenzi wangu za shule?”
“Nzuri mamito.”
“Mmh! Makubwa kumbe nawe mwingi wa habari. Haya patito wangu umesoma kweli au ndo unaniwaza mimi muda wote?”
“Walaa, sasa hivi ndo nasoma ile mbaya ili nipasue niweze kukumiliki.”
“Mmh! Jitahidi.”
Kama kawaida waliingia ndani na kujifungia chumbani na kuweka mkanda wa blue print, ukawafanya wapandwe na mzuka na kujikuta katikati ya mnazi wakishindana kuangusha madafu.
Kwa vile walikuwa wamezoeana walifanya ya hamu na siyo ya shibe tena huku wakijua siku ya kuchimbika bila jembe ilikuwa mwisho wa wiki ambayo Shaka haendi shule.
Baada ya kupeana raha na Shaka kurudi nyumbani kwao majira ya usiku akiwa chumbani kwake alikumbuka kwamba alipewa ujumbe kutoka kwa Stella na kuuweka kwenye mfuko wa shule. Alikwenda anapoweka mfuko wake na kutoa bahasha kisha akarudi kitandani na kujilaza kwenye kitanda chake cha sita kwa sita alichonunuliwa na Betty.
Aliichukua na kuifungua ndani na kukuta kuna noti nyekundu kumi. Alitabasamu na kusoma kipande cha barua kilichokuwemo kwenye bahasha ile kilichokuwa na ujumbe huu:
Mpenzi Shaka najua utashtuka kupokea waraka wa mapenzi kutoka kwangu. Najua atajiuliza vitu vingi, naomba yaliyopita yawe yamepita. Inawezekana wakati ukinitaka nilikuwa na mambo mengi kichwani.
Lakini naomba kukueleza ukweli Shaka nakupenda toka zamani na huu ndiyo wakati wangu wa kudhihirisha penzi langu kwako. Naomba unipe nafasi hii.
Shaka nipe nafasi nikuoneshe mapenzi, naomba nikumiliki peke yangu, nitakulinda kwa gharama yoyote, nakupenda Shaka mpaka bhaaaasi.
Shaka alijikuta akifurahi na kujirusha kitandani huku akisema:
“Uhuuuu!!”
Katika wasichana waliokuwa wakiutesa moyo wake basi alikuwa Stella, mtoto wa kigogo mwenye fedha kama mchanga nchini. Moyoni aliapa kumshikisha adabu baada ya kumdharau kipindi cha nyuma.
Shaka alilala akitamani kesho ifike upesi ili akarudishe jibu la kukubali kumiliki malkia wa nyuki wa shule aliyekuwa akiamini kwake kumpata ni kama ndoto.
***
Siku ya pili Shaka alipokwenda shule alijifanya hajui lolote japokuwa Stella aliteseka kutaka kusikia jibu la ombi lake la jana yake, hata akili ya kushika masomo hakuwa nayo siku hiyo.
Alitamani apate jibu la Shaka ili ajue kama amepata au amekosa. Siku zote katika maisha yake aliwashangaa wasichana wanaowatongoza wanaume. Kutokana na kujiamini yeye ni mzuri tena mtoto wa tajiri, alikuwa na nyodo na kumchagua mwanaume anayemtaka yeye katika watakaomtongoza basi awe na vigezo anavyovitaka.
Katika nyodo zake ukimtongoza hukuangalia chini mpaka juu, akikuheshimu anaondoka bila kukusemesha, lakini akikudharau hukutemea mate na kuondoka.
Katika watu waliowahi kukutana na dharau ile pale shuleni mmoja wapo alikuwa ni Shaka kutokana na muonekano wake wa kimaskini. Lakini baada ya kugundua uzuri wa Shaka alikuwa yupo radhi kulamba matapishi yake kumtongoza mwanaume.
Aliamini kama atachelewa kusema asubiri kutongozwa basi kuna wasichana vipanga kama shoga yake Diana aliyemshuhudia kwa macho na masikio yake mwenyewe akijitongozesha kwa Shaka ingekula kwake.
Akiwa darasani muda mwingi aliibia kumwangalia Shaka kwenye dawati lake, kila alipotabasamu moyo ulimpasuka na kutamani tabasamu lile lingekuwa lake. Muda ulikatika bila kuona dalili zozote za kupata jibu.
Shaka naye muda mwingi alijipanga kurudisha jibu, lakini mazingira yalikuwa hayaruhusu hivyo alitulia kutafuta nafasi. Diana shoga ya Stella alitoka kwenda msalani, Shaka aliitumia nafasi ile kutoka ili akampe ujumbe wa shoga yake.
Alipotoka alisubiri muda kidogo naye alijifanya kwenda msalani na kikaratasi cha ujumbe wa Stella mkononi. Alitembea taratibu ili kuvuta muda akutane na Diana njiani.
Alipokaribia msalani alimuona Diana akitoka msalani, alijua watakutana njiani. Walipokutana Shaka alinyoosha mkono kama anataka kumsalimia:
“Mambo Dia.”
“Poa Sweet.”
“Diana acha hizo, naomba karatasi hii mpe Stella.”
“Poa, lakini pamoja kuwa mpenzi wa Stella nitahakikisha unakuwa mpenzi wangu hata kwa day worker (deiwaka).”
“Bidii yako tu.”
Shaka alimjibu na kuelekea msalani ili kutimiza alichotaka kukifanya. Alipogeuka nyuma alishangaa kumuona Diana akisoma kile kikaratasi alichompa ampe shoga yake.
Alimshangaa kusoma ujumbe wa shoga yake, lakini haikumsumbua alijua wanajuana wenyewe. Diana baada ya kupewa kikaratasi na Shaka moyo wake ulimsukasuka sana na kutaka kujua kimeandikwa nini ndani ya ujumbe ule.
Ujumbe alioukuta ulimshtua na kuona kumbe shoga yake alimdanganya. Ujumbe ulisomeka hivi;
Kuhusiana na ombi lako la jana jioni, nimekubali ila ukileta za kuleta nakupiga chini.
“Mmh! Mbona Stella alisema Shaka ni mpenzi wake wiki sasa kumbe ombi lenyewe ni la jana jioni. Mmh! Nikimzodoa lazima atajua nimesoma ujumbe wake, sina budi kukaa kimya ili asijue nimemgundua. Lakini lazima mla mbuzi alipe ngombe,” Diana aliwaza baada ya kuona ule ujumbe.
Aliukunja na kuurudisha kama alivyopewa na kumpelekea shoga yake aliyekuwa kama mgonjwa siku ile. Alipofika karibu na dawati lake alimkuta amezama kwenye lindi la mawazo, macho yake yakiwa yametazama mlangoni.
“Stella,” alimwita huku akimwinamia.
“Ee..ee..ee,” Stella alishtuka kama anatoka usingizini.
“Vipi shoga leo sikuelewi una nini?”
“Nipo sawa, kwani nipo vipi?”
“Kama huumwi basi kuna kitu kinakuchanganya au bado Mose anakuchanganya?”
“Mose hanijui siku zake zinahesabika,” Stella alisema huku amekunja uso.
“Mmh! Pole nina ujumbe wako.”
“Kutoka kwa Joel, kwa nini kile kivulana hakisikii, kiambie mimi siyo hadhi yake awafuate wanuka mikojo wenzie. Unajua kuna wanaume hawajui wanawake wa saizi yao mimi na Joel wapi na wapi.”
“Mbona kwa Shaka ulisema hivyohivyo leo hii anakuchanganya?”
“Shaka alikuwa kama nyoka alijificha kwenye gamba sasa hivi katoka mwenyewe live, Shaka bonge la ‘handsome’.”
“Kwa hiyo ujumbe niliokuletea nisikupe?”
“Kama unatoka kwa Joel naomba uuchane tu.”
“Siyo kwa Joel.”
“Kwa nani?”
“Shaka.”
“Shakaaa! Muongo!” Stella alishtuka na kutoa macho kama kaona ng’ombe akitoa maziwa.
“Kweli, nimekutana naye msalani amenipa kikaratasi hiki nikupe.”
“Mungu wangu sijui kaandika nini?” Stella alishika mikono kifuani kuteremsha presha.
“Vipi shoga?” Diana alimshangaa shoga yake.
“Mmh! Wee acha tu.”
“Au nisikupe leo nikupe kesho naona haupo vizuri.”
“Hapana we nipe hata ukiwa mbaya nipe sina jinsi, upo wapi?”
Diana alimpa shoga yake kwa chati na kisha aliondoka kurudi kwenye dawati lake haraka na kujifanya yupo bize lakini jicho lake lilikuwa kwa shoga yake amuone ataupokeaje ujumbe ule.
Stella baada ya kutulia alikifungua kikaratasi huku mikono ikimtetemeka kama ana malaria kali. Alipofungua alianzia chini na kukutana na neno lililoandikwa nakupiga chini. Mapigo ya moyo yalimwenda mbio na kijasho chembamba kilimtoka.
Kabla ya kupandisha juu kusoma aliishusha pumzi ili kujipa ujasiri na kuanza kusoma akiwa anamini kabisa Shaka lazima atalipa kisasi cha kumtoa nishai siku za nyuma.
Swali lililomuumiza akili lilikuwa kama Shaka amemtolea nje atauweka wapi uso wake kwa shoga yake Diana aliyejitangaza kwake kuwa Shaka ni mpenzi wake.
Alipeleka macho juu na kukutana na neno Kuhusiana na ombi lako la jana jioni, nimekubali ila ukileta za kuleta nakupiga chini.
Stella alijikuta akijisahau kama yupo darasani, akapiga yowe la furaha.
“Come ooon, sasa watanikoma wavimba macho na hapa hapigwi mtu chini.”
Kauli hiyo iliwashangaza baadhi ya wanafunzi na kujiuliza wavimba macho gani na nani hapigwi chini? Alikaa chini na kurudia kukisoma kile kikaratasi na kukikumbatia kifuani kisha alikibusu na kukiweka kwenye mfuko wa sketi.
Kwake ilikuwa furaha lakini kwa shoga yake yalikuwa maumivu makali moyoni mwake kwa kuamini shoga yake alimfanyia umafia mkubwa wa kumchukulia mpenzi wake kwa hila za uongo.
Lakini aliapa kula naye sahani moja kama hakula nyama basi lazima aambulie hata mchuzi. Shaka alipotoka msalani alirudi kwenye dawati lake na kutulia kama hajui kilichokuwa kikiendelea darasani.
***
Stella baada ya kupata jibu alilokuwa akilisubiri kwa hamu aliona muda ukichelewa, hamu yake ilikuwa kuzungumza na Shaka ili kupanga penzi lao litakavyokuwa baada ya kukubaliwa.
Muda wa kutoka shule ulipofika, alijitahidi kujisogeza kwa Shaka ili kumpa ujumbe aliokuwa ameuandika kwenye karatasi. Alipomfikia karibu alimshikisha kikaratasi mkononi kwa haraka, baada ya kumkabidhi alichepua mwendo kuwahi eneo la tukio na kuwacha Shaka aliyekuwa akizungumza na rafiki yake Issa ambaye hakujua kilichokuwa kikiendelea.
Kitendo kile kilikuwa kikifuatiliwa na Diana ambaye alikuwa nyuma. Alishangaa kuona shoga yake siku ile anaondoka bila kumuaga baada ya kumsogelea Shaka bila kufanya kitu na kuondoka bila kugeuka na kutoka nje ya geti la shule.
Naye aliona ile ndiyo nafasi yake ya kutia neno lake kabla hajatoka nje ya shule kwa vile hakujua shoga yake yupo wapi. Alichepua mwendo hadi kwa Shaka aliyekuwa akitembea taratibu.
“Shaka,” alimwita.
Shaka aligeuka bila kuitika na kukutana na Diana.
“Sema Dia.”
“Poa Sweet naomba tuzungumze kidogo.”
“Poa,” Shaka alisema huku akimfuata alipokuwa amesogea pembeni.
“Vipi?”
“Poa,” Diana alisema akiwa ameangalia chini kwa aibu.
“Lete stori umetumwa na Stella?” alimuuliza akiwa amemkazia macho.
“Walaa.”
“Ulikuwa unasemaje?”
“Shaka kwa nini umenifanyia hivyo?” Diana alianza kulalamika.
“Kukufanyia nini tena Stella?” Shaka alishtuka.
“Yaani mimi nikuwahi, mapenzi umpe Stella ni haki kweli?”
“Mbona sikuelewi unamaanisha nini?”
“Shaka unajua, lakini ulichonifanyia si kitu kizuri,” Stella alizungumza kwa sauti ya kilio ikifuatiwa na machozi.
“Diana usilie nimekuelewa.”
“Kwa hiyo?”
“Si tupo pamoja tutayamaliza.”
“Hapana Shaka nipe jibu langu leo.”
“Itakuwaje ikiwa tayari nipo na shoga yako?”
“Kama kuanza nimeanza mimi yeye kadandia, kama vipi kila mtu ale kwa wakati wake.”
“Mmh! Nimekuelewa, je, Stella akijua?”
“Hawezi kujua penzi letu halitakuwa la matangazo kama lake.”
“Poa nimekuelewa basi mengine tutapanga tukiwa pamoja?”
“Lini sasa?”
“Punguza presha, kwa vile tupo pamoja kila kitu kitakwenda sawa.”
“Nashukuru sana Shaka.”
“Poa.”
Shaka aliachana na Diana na kurudi kwa Issa aliyekuwa amesimama pembeni akimsubiri.
“Issa twende zetu.”
“Shaka vipi unaangusha mnyama nini?”
“Kwa nini?”
“Yule demu anajifanya matawi sana.”
“Kivipi?”
“Si anachukuliwa na mtoto wa waziri basi nyodo kibao kila mwanaume shuleni anamuona hafai.”
“Umeishatia timu?”
“Mara kibao kuna siku nilimtangazia mzigo lakini akanitolea nje.”
“Na shoga yake Stella?” Shaka alimdodosa Issa bila kujua.
“Yule si ndiyo anajifanya malkia wa shule, kweli Stella mzuri pia kwao wana umatemate lakini amezidisha mashauzi anaringa sana na kutuona wanafunzi wenzie kama kinyesi.”
“Unataka kuniambia Stella hana mwanaume hapa shuleni?”
“Hana, naye anachukuliwa na mtoto wa mzee Songwe tajiri mwenye fedha kufuru. Nasikia alimnunulia gari baba yake akakataa.”
“Duh! Nani Mose?”
“Huyohuyo.”
“Nasikia jamaa kwa mademu koma.”
“Hata shoga yake Diana nasikia jamaa kaangusha.”
“Wachaa.”
“Kweli, wale mademu si wanajifanya wa matawi.”
“Shaka,” msichana mmoja wa kidato cha tatu alimwita.
“Ooh! Sofia, unasemaje?”
“Stella anasema vipi mbona kimya?”
Kauli ile ilimfanya Shaka akifungue kikaratasi alichopewa na Stella na kukisoma na kukutana na ujumbe:
“Shaka mpenzi nakusubiri Queen Soft Drink.”
“My God, Issa tutaonana baadaye kuna sehemu nilielezwa niende nikitoka shule.”
“Poa basi tumoro.”
Shaka aliachana na Issa na kufuatana na Sofia aliyetumwa na Stella. Walikwenda hadi Queen Soft Drink kwenye vyumba vya ndani na kumkuta Stella amejaa tele.
“Karibu Shaka.”
“Asante.”
“Sofia Shaka umemkuta na nani?” Stella alijifanya kulia wivu.
“Nimemkuta na Issa Sharobaro.”
“Mmh! Bahati yako, ungekuwa na mwanamke pangechimbika. Shaka mimi ndiye mkeo shuleni na nyumbani.”
“Sawa mpenzi.”
“Eti Sofia, Shaka anafaa?”
“Mmh! Sasa Shaka ndiyo habari ya shuleni, yaani anakimbiza. Kila msichana anamzungumzia yeye.”
“Basi Sofia waambie wenzako sasa hivi ana mwenyewe.”
“Stella mi niwaache wapendao,” Sofia aliaga.
“Nashukuru kwa msaada wako,” alisema huku akimpa asante ya shilingi elfu tano.
Baada ya kuondoka Sofia walibakia Shaka na Stella aliyeonekana kupagawa kuwepo kwa Shaka pale.
“Niambie Shaka.”
“Nakusikiliza wewe.”
“Unatumia kinywaji gani?”
“Utakachonichagulia.”
Alimwita mhudumu na kuagiza juisi mchanganyiko na pizza. Alipotaka kuagiza nyingine Shaka alisema:
“Unajua nini mpenzi?”
“Hata sijui Shaka.”
“Sisi ni wapenzi haipendezi kila mtu ale yake, tutakula pizza moja, glasi moja ya juisi na mrija mmoja au hunipendi?” Shaka alitikisa kiberiti.
“Aah! Shaka usinifanye nikalia, basi nisamehe nakupenda sana mpenzi wangu,” Stella alipiga magoti kuomba msamaha bila aibu na kumfanya mhudumu kushangaa huku Shaka akiamini mtoto wa kike kaimeza ndoano yote.
“Aaah! Baby nyanyuka,” Shaka alimnyanyua huku akiwa haamini binti mwenye nyodo kama Stella kumpigia magoti.
“Hapana baby bado hujanisamehe.”
“Nimekusamehe mpenzi wangu japo kwangu sioni kosa lako.”
“Asante mpenzi wangu.”
VITILIVYOGO (PAPA NA MUHOGO) SEHEMU YA 1- 5
MTUNZI: DK. AMBE SI YA KUKOSA HII
Endelea kulike ==>www.facebook.com/2jiachie
1. www.2jiachie.com/2014/08/vitilivyogo-papa-na-muhogo-01.html
2. www.2jiachie.com/2014/08/vitilivyogo-papa-na-muhogo-01.html
3. www.2jiachie.com/2014/08/vitilivyogo-papa-na-muhogo-03.html
4. www.2jiachie.com/2014/08/vitilivyogo-papa-na-muhogo-04.html
5. www.2jiachie.com/2014/08/vitilivyogo-papa-na-muhogo-05.html
ANGALIZO: ITAENDELEAMPAKA MWISHO HAPA KAMA SHARE ZITAFIKA 3,000 NA COMMENT 2,000 VINGINEVYO MTAMALIZIA KATIKA KITABU #SHARE HAZIJAFIKA ZINAISHIA 60 TU TUENDELEE KUSHARE

Post a Comment