She is too young to die - 23
“Naam Gilbert”
“Hii ni ngumu!”
“Ipi?”
“Hivi unafikiri kumwacha mtu unayempenda sehemu kama hii ni jambo rahisi daktari?”
“Najua sio rahisi!”
“Sasa kwanini unataka nimwache mke wangu hapa, hivi umekwishakuona humo ndani? Hebu chungulia uone watu wanaoishi hapa walivyo, tazama wale wanavyopigana, yaani nimwache hapa Salome? Hapana, roho inaniuma mno, nampenda sana mke wangu daktari siwezi kufanya ukatilii huu!”
“Hufanyi ukatili Gilbert, ni tiba, akiwa hapa mkeo atapata huduma zote muhimu na atasaidiwa kumbukumbu zake zirejee!”
“Eti mama tumwache hapa Salome?”
“Hakuna jinsi mwanangu, hata mimi nampenda mno Salome lakini tumsikilize daktari!”
Machozi yalimtoka Gilbert baadaye alipokubali na kutia saini kwenye fomu, kisha kushuhudia Salome akisukumwa kwa nguvu kuingia ndani, hata yeye mwenyewe alionekana hapendi kuingia sehemu hiyo, aliendelea kupiga kelele akisema “Nipelekeni nyumbani, kwa mume na mtoto wangu” Dk. Hassan alipoyasikia maneno hayo alimhakikishia Gilbert kwamba muda si mrefu kumbukumbu za Salome zingerejea, kwani kitendo cha kufahamu kwamba alikuwa na mume na mtoto ingawa hakuwatambua kama walikuwa eneo hilo ilikuwa ni hatua kubwa.
Ndani ya ngome ya kituo hicho, waliendelea kumsikia Salome akilia na baadaye mtu akipigwa, Gilbert alizidi kuumia na hakutaka kuendelea tena kubaki eneo hilo, akaondoka akifuata na mama yake Salome akiwa amembeba Faith mpaka kwenye gari, daktari akawafuata dakika tano baadaye na kupanda, safari kurejea mjini ikaanza, njia nzima Gilbert alikuwa akiwaza mambo mengi Davis akiwa kwenye usukani. Walinyoosha moja kwa moja hadi nyumbani ambako upungufu wa Salome ulionekana wazi mara tu baada ya Gilbert kuingia ndani, hakuwa na la kufanya zaidi ya kukubaliana na ukweli.
Siku ya kwanza ikapita akiwa mwenye mawazo mengi, hakukumbuka tena habari za Tecla na mtoto wake, akili yake ilikuwa imetekwa na tukio la mkewe kupoteza kumbukumbu! Alijua bado magazeti yangeendelea kuandika lakini hakutaka kusoma wala kusikiliza redio, alikuwa kwenye ulimwengu wa peke yake, kwa mara ya kwanza maishani aliamini kulikuwa na uwezo wa mwanadamu kuishi bila kujua kilichoendelea duniani.
Kila wiki siku ya Jumapili Gilbert na familia yake baada ya kutoka kansiani ilikuwa ni lazima waende kituoni kumwona Salome na Dk. Hassan aliwashauri kila wakienda wampelekee vitu ambavyo vingeweza kumkumbusha mambo ya nyuma, wakawa wanamchukulia picha tangu siku ya harusi, alipokuwa mjamzito, picha ya marehemu baba yake, mama yake na mtoto wake Faith! Bado Salome hakumkumbuka hata mmoja wao, Gilbert alipomsogelea alimpiga na kumfukuza, akimtaka akae mbali yake, hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa mama na hata mtoto wake.
“Uwe unampa anazingalia, inawezekana zikamsaidia kukumbuka alikotoka, lakini mbona ana makovu mengi?”
“Anapigana sana na wenzake!”
“Hamuwezi kumsaidia asipigane?”
“Humu ndani ni pagumu, kuna watu wachokozi sana, ni lazima ajihami!”
“Hakuna jinsi ya kumlinda?”
“Najitahidi sana Gilbert!”
“Haya basi, hizo ndio picha nimemletea leo!”
“Hakuna shida!”
“Sawa sisi tunaondoka lakini tutarudi tena jumapili!”
“Karibuni!”
Wote waliondoka kwa unyonge mpaka kwenye gari, Gilbert alipokaa tu kwenye usukani na kuwasha gari kabla hajaingiza gia akisubiri watu wote wapande, simu yake ililia kuashiria kulikuwa na ujumbe mfupi wa simu umeingia, akaichukua simu yake na kufungua ujumbe uliokuwepo, moyo wake uliruka mapigo kadhaa, jasho na macho yakamtoka aliposoma ujumbe uliokuwepo kwenye kioo cha simu yake.
“Nini tena baba?”
“Hakuna tatizo mama!”
“Huna tatizo? Mbona umeshtuka sana?”
“Mambo ya kawaida tu mzazi” alijibu akiendelea kusoma;
Naitwa Ngowi,
Sijui kama unaweza kunikumbuka,
Nilikuja kwako siku ile mwanao akiwa amepotea,
Nikashauri tuangalie kwenye bwawa la kuogelea,
Tukiwa hospitali ya Dk. Mathew, nilitekwa na watu wasiojulikana,
Hapa nilipo sipafahamu ni wapi lakini ni jijini Dar es Salaam,
Kama utaweza nitafute mpaka unipate, nina ujumbe mzito wa kukupa ambao ndio hasa nilikuja kukueleza siku ile,
Ahsante.
Ngowi.
Ujumbe uliishia hapo, Gilbert alishindwa kuondoa gari kwa muda wa karibu dakika kumi na tano akitafakari juu ya alichokisoma, hakuelewa ni watu gani walimteka Ngowi na kwa sababu ipi na alikuwa amekuja kumweleza kitu gani! Hakuwa na jibu la maswali yote yaliyomwijia kichwani. Mwisho aliamua kuwasha gari na kuondoka hadi nyumbani ambako aliwashusha watu wote aliokuwa nao kwenye gari na kuondoka tena hadi kituo cha polisi kikuu kuonana na mkuu wa upelelezi wa Mkoa, akamwonyesha ujumbe aliokuwa nao kwenye simu yake. Wote wawili wakaanza kuipiga hiyo namba bila mafanikio.
“Tutahitaji maelezo yako, baada ya hapo vijana wataingia kazini kufanya upelelezi tutampata tu! Ni kazi ndogo sana, hawa watu wanaotumia simu za mikononi kutuma ujumbe ni rahisi mno kuwakamata!”
“Hakuna shida!”
“Acha basi niite kijana wangu mmoja aje achukue maelezo yako!”
“Hakuna shida”
Mkuu wa upelelezi alichukua simu na kupiga namba fulani, muda mfupi tu baadaye akaingia kijana mrefu mwembamba na kupiga saluti mbele yake na baadaye kumsalimia Gilbert ndipo Mkuu wa Upelelezi akampa maelezo kijana huyo juu ya kazi ya kufanya, akaondoka na Gilbert mpaka ofisini kwake na kuanza kumhoji juu ya tukio zima, ilimchukua saa nzima kukamilisha, akaondoka kurejea nyumbani akiwa amewaachia namba ya simu iliyotuma ujumbe ili wao waendelee na kazi ya upelelezi.
***
“Mh! Picha nzuri ya harusi, walipendeza, lakini mbona hii sura inafanana ya kwangu? Ni mimi, huyu ni mume wangu Gilbert” Salome aliwaza akiwa ameshikilia picha mikononi mwake, moyo wake ukajaa furaha, akaiweka picha hiyo chini na kuchukua nyingine.
“Mh! Huyu ni marehemu baba yangu…masikini alikufa kwenye maji akijaribu kwenda kunitafutia daktari wa kunisaidia nilipokuwa mjamzito wa mimba ya mwanangu Faith…”Aliwaza Salome, huzuni kubwa ikamwingia, akaukumbuka usiku huo wa mvua kubwa huku akivuja damu, machozi yakamtoka, kilio kikubwa kikasikika ndani ya kambi, muuguzi akafika akikimbia.
“Salome!”
“Bee”
“Mbona unalia mwanangu?”
“Picha! Zimenikumbusha mbali, zimenikumbusha mume wangu na marehemu baba yangu aliyekufa kwenye maji!”
Muuguzi akacheka, yeye pia furaha ikamiminika moyoni mwake.
Naitwa Ngowi,
Sijui kama unaweza kunikumbuka,
Nilikuja kwako siku ile mwanao akiwa amepotea,
Nikashauri tuangalie kwenye bwawa la kuogelea,
Tukiwa hospitali ya Dk. Mathew, nilitekwa na watu wasiojulikana,
Hapa nilipo sipafahamu ni wapi lakini ni jijini Dar es Salaam,
Kama utaweza nitafute mpaka unipate, nina ujumbe mzito wa kukupa ambao ndio hasa nilikuja kukueleza siku ile,
Ahsante.
Ngowi.
Baada ya hapo alijaribu kuipiga namba hiyo bila mafanikio, ilionekana kuwa imezimwa! Alichokifanya ni kwenda kituo cha polisi cha kati na kutoa taarifa na maelezo yake kuchukuliwa, akaruhusiwa kuondoka polisi wakiwa wameahidi kufuatilia.
Kwenye kituo, Salome anaangalia picha ambazo Gilbert humpelekea kama njia ya kumrejeshea kumbukumbu zake, huo ndio ushauri ambao Dk. Hassan, bingwa wa magonjwa ya akili aliutoa. Ghafla, anaitambua sura ya baba yake mzazi ambaye ni marehemu, picha yote ya siku alipokufa inamwijia, kumbukumbu zinarejea na pia amemkumbuka mpaka mume wake Gilbert, hapo hapo akalia na kupiga kelele, muuguzi akaja akikimbia na kumuuliza ni kitu gani kilikuwa kimetokea ndipo akasimulia kumbukumbu za siku baba yake alipokufa, muuguzi akafurahi!
Je, nini kitaendelea? SONGA NAYO…
Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam alikuwa amekaa nyuma ya meza kubwa ya duara, hakuwa peke yake, idadi ya watu kama sita hivi walikuwa wameizunguka meza hiyo, hao ndio wapelelezi aliowaamini. Kilikuwa ni kikao cha kawaida cha kujadili mambo yaliyojitokeza jijini Dar es Salaam, mengi yalishaongelewa na ilikuwa imefika zamu ya kujadili taarifa ambazo Gilbert alizitoa, faili likafunuliwa na mmoja wa maaskari kuanza kusoma maelezo yaliyotolewa kituoni na Gilbert juu ya ujumbe mfupi wa simu alioupokea.
“Tutafanyaje vijana? Ni lazima huyu mtu apatikane ili tujue ni ujumbe gani alionao na ni watu gani walimteka!” Mkuu wa Upelelezi aliongea.
“Wala sio kazi kubwa Afande!”
“Mtafanyaje?”
“Tukio hili sio la kwanza Afande, kuna watu pia siku hizi wana utaratibu wa kununua laini za simu na kuzitumia kutukana ama kutisha watu kisha kuzitupa, dawa yao tumeshaipata! Wengi hivi sasa tunawakamata”
“Nauliza mtafanyaje?”
“Namba hii ni 0164 122347, hawa ni Tantel, tutakwenda ofisini kwao tukaulizie hii simu ni ya nani na kama itakuwa haitumiki basi tutauliza namba zilizowahi kuingia kwenye simu hiyo au kupigwa na simu hiyo, hawa ndio watakaotuambia huyu mwenye namba hii ni nani tukishampata, atatueleza Ngowi yuko wapi!”
“Excellent! Safi sana, nataka vijana wenye akili kama yako, hivi sasa Jeshi la Polisi linaendeshwa kisomi, endeleeni na kazi nipeni majibu baada ya masaa matano, sawa?”
“Sawa Afande!”
Kikao kikamalizika, vijana wakaondoka na kushuka hadi chini ambako waliandika barua kwenda kampuni ya simu za mikononi ya Tantel kuomba kufahamu mwenye simu alikuwa nani na namba zilizoingia na kutoka kwenye namba hiyo, kazi hiyo ilipokamilika waliingia kwenye gari na kwenda moja kwa moja makao makuu ya kampuni hiyo na kuonana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ambaye baada ya kuipokea barua yao na kuisoma alipiga simu kitengo cha uthibiti wa simu, kijana mmoja akafika na kukabidhiwa jukumu la kutoa chapa namba zote zilizoingia na kutoka kwenye namba iliyotajwa.
Haikuwa kazi ngumu kama ilivyotarajiwa, ingawa mwisho wa siku hawakumjua mwenye simu alikuwa nani kwani simu haikuwa hewani, walifanikiwa kuzipata namba zilizoingia na kutoka, iliyopigwa na kuingia sana ilikuwa ni namba 0162 172031, siku nne tu kabla ilishaingia kwenye simu hiyo. Huyo ndiye akawa mtu muhimu kwa upelelezi, wakawashukuru wafanyakazi wa Tantel na kuondoka hadi makao makuu ambako waliipiga namba hiyo bila kupoteza wakati.
“Inaita!” mmoja wa maaskari alisema macho yakiwa yamemtoka.
“Kata kwanza!” mwenzake akaongea.
“Hapana, tukikata atashtuka!”
“Sasa utamwambiaje?”
“Wewe subiri utaona!”
Muda mfupi baadaye, sauti ya kike ilisikika kutoka upande wa pili, askari akajitambulisha kama mfanyakazi wa shirika la ndege la Uingereza, tena akiongea kwa kiingereza kilichonyooka kabisa na kumtaarifu aliyepokea simu kwamba alikuwa amejishindia tiketi ya kwenda kwenye jiji la London na kulala kwenye hoteli ya Hilton kwa muda wa siku tatu.
“Mh! Mbona sijawahi kushiriki?”
“Watu waliojishindia si waliowahi kushiriki, tumefanya shindano hili kwa kushirikiana na Tantel, tafadhali fika ofisi za British Airways hapa Hoteli ya Royal Palm, uchukue tiketi yako na upewe taarifa kamili, unaitwa nani?”
“Monica!”
“Umekubali au?”
“Ha! Kuna mtu anaweza kukataa?”
“Basi fika hapa haraka iwezekanavyo, umevaaje ili tukutambue?”
“Nimevaa nguo ya rangi ya pinki!”
“Una kitambulisho chochote, hati ya kusafiria au kitambulisho cha mpiga kura?”
“Nina hati ya kusafiria!”
“Basi njoo nayo, tukupe muda gani?’
“Nusu saa”
Simu ilipokatika tu maaskari walinyanyuka na kushuka ngazi haraka hadi chini ambako walipanda gari lao aina ya Landrover 110 wakaendesha kwa kasi mpaka hoteli ya Royal Palm na kuegesha kwenye maegesho kisha kushuka na kuinga ndani ya hoteli ambako waliketi na kuagiza kahawa jirani kabisa na mlango wa kuingilia kwenye ofisi za Shirika la ndege la Uingereza, haukupita muda mrefu sana, mwanamke mrefu mwembamba akiwa amevaa gauni la rangi ya pinki na miwani mikubwa ya rangi nyeusi, shingoni akiwa na mikufu mikubwa ya dhahabu akaonekana akitembea kwa maringo kuelekea sehemu waliyokuwa wamekaa, mmoja wa maaskari akachukua simu yake na kupiga namba ya mwanamke huyo, wakamwona anapunguza mwendo na kufungua mkoba.
“Ndio yeye!” akasema askari huyo na kukata simu.
“Sasa?”
“Tukae tayari kumkamata!”
Mwanamke huyo alipoukaribia mlango wa ofisi za shirika la ndege la Uingereza, maaskari walisimama na kumzunguka, kisha mmoja wao kutoa kitambulisho na kumpa taarifa kwamba alikuwa chini ya Ulinzi. Alionyesha mshtuko wa ajabu lakini kabla hajafanya chochote alianza kuongozwa kuelekea nje ya hoteli ambako alipakiwa ndani ya gari na moja kwa moja kupelekwa hadi kituo cha polisi cha kati, akapandishwa ofisini kwa Mkuu wa upelelezi.
“Mkuu tumemleta mtu wetu!”
“My God! Kazi nzuri, huyu ndiye…!”
“Ndiye mwenye ile namba inayoingia mara nyingi kwenye ile namba aliyotumia Ngowi!”
“Paaa!” ulikuwa ni mlio wa kibao kiitwacho kelbu, msichana huyo akasikia kizunguzungu na kwenda moja kwa moja hadi chini.
“Mbona mnanipiga?”
“Tueleze hii namba ni ya nani?” Mkuu wa upelelezi akauliza.
“Ipi?”
“Hii!”
“Ni ya mpenzi wangu!”
“Nani?”
“Ayubu Jeremia”
“Yuko wapi?”
“Nyumbani kwake”
“Tunataka tumpate sasa hivi, kwa usalama wako tupeleke!”
“Sina tatizo, wala hapakuwa na sababu yoyote ya kunipiga!”
“Nendeni naye!” Mkuu wa upelelezi aliamuru na Monica akashushwa ngazi na kupakiwa ndani ya gari, moja kwa moja hadi Mwananyamala karibu kabisa na hospitali ambako waliicha gari na kuanza kutembea kwa miguu kuingia ndani kwenye nyumba ambazo hazikuwa kwenye mpangilio mzuri wa kuruhusu gari kupita, wakafika kwenye nyumba moja ndogo iliyoezekwa kwa madebe yenye kutu, wote wakaingia na kukuta watu wengi wakiwa wamelala chini uani, kwa kuwaangalia tu walikuwa ni watumiaji wa dawa za kulevya, Monica akawaongoza hadi ndani ambako walimkuta Ayubu amelala kwenye kochi na kukamatwa kisha kufungwa pingu.
Nyumba ikaanza kupekuliwa, mzigo mkubwa wa dawa za kulevya ulikutwa ndani pia kadi ya simu yenye namba iliyotumiwa na Ngowi ilikutwa juu ya meza! Pilikapilika hizo ziliwafanya mateja waliokuwa wamelala nje watimue mbio, maaskari waliwaacha kwa sababu hawakuwa na uwezo wa kuwadhibiti, wakafuata kilichowapeleka kwa wakati huo. Mwisho wa upekuzi, Ayubu alitakiwa aonyeshe mahali Ngowi alipokuwa, hakuwa na la kufanya zaidi ya kuwachukua kutoka hapo kwenda ndani zaidi kwenye jumba ambalo lilikuwa halijamalizika kujengwa na kuwaingiza ndani, Ngowi alikuwa kwenye moja vya vyumba akiwa amefungwa kamba mikono na miguu, maaskari wakamfungua.
“Utatueleza ni kwanini mlimteka!”
“Sio mimi Afande, nilitumwa tu nikafanya kazi hii sababu ya njaa!”
“Ulitumwa na nani?”
“Kuna demu mmoja simfahamu jina ila namba yake ninayo, aliniambia huyu jamaa kuna siri anaifahamu ambayo hataki ijulikane!”
“Namba yake iko wapi?”
“Ni 0162 282940!”
Mmoja wa maaskari akaipiga na kuanza kuongea na mtu wa upande wa pili, akatumia ujanja wote wa kipelelezi na kugundua alikuwa ni mwanamke aitwaye Tecla, wakatumia njia ile ile waliyoitumia kumnasa Monica na kumtaka afike ofisi za Shirika la ndege la Uingereza baada ya saa moja muda ambao wao wangekuwa tayari wameshawafikisha Ayubu na Monica kituoni.
Ndani ya saa moja na nusu, tayari Tecla alikuwa kituoni akihojiwa kwa kumteka Ngowi, hakuwa na la kusema zaidi ya kulia! Muda huo maaskari waliona ulifaa kumpigia simu Gilbert, hilo likafanyika na ndani ya dakika ishirini akawa amekwishafika na kuwakuta Tecla, Ayubu, Monica na Ngowi kituoni, akamkumbatia Ngowi kwa furaha lakini hakumfurahia Tecla hata kidogo na hakuelewa ni kwanini alikuwa pale mpaka maaskari walipomsimulia mkasa mzima, hakuamini!
“Naweza kuongea na Ngowi pembeni?”
“Hakuna shida, mchukue tu!”
Akamsaidia kutembea wakaenda kwenye korido ambako Ngowi alimsimulia sababu ya kwenda nyumbani kwake siku aliyotekwa, Gilbert hakuamini alipogundua kwamba alikuwa ni mfanyakazi wa maabara na alikuwa amekwenda kumweleza ukweli juu ya majibu ya DNA baada ya kutoka nyumbani kwa Tecla.
“Nisamehe ndugu yangu, nilitoa majibu ya uongo kwa sababu ya tamaa ya fedha, hivi sasa nimeokoka na nilikuja nyumbani kwako kuomba msamaha!” Ngowi aliongea akilia.
“Mungu wangu unasema kweli?” Gilbert aliuliza kwa mshangao akiwa haamini kabisa maneno yaliyokuwa yamepenya kwenye ngoma za masikio yake, majibu ya DNA yalikuwa ni ya uongo? Alijiuliza bila ya kupata jibu, wimbi la furaha likajaa moyoni mwake, akajikuta akitamani kuona mke wake Salome anarejewa na fahamu zake kisha nae kugundua kwamba kumbe kashfa ya mume wake ilikuwa ni ya kutunga yenye lengo la kumchafulia jina.
“Ni kweli ndugu yangu, mimi nimempokea Kristo siwezi kusema uongo tena, ndio maana nilikuja kwako siku ile kuomba msamaha!”
“Umempokea Kristo tangu lini?”
“Wiki moja na nusu sasa, siku ile nilipokuja kwako ndiyo nilikuwa nimetokea viwanja vya Jangwani kwenye mahubiri, nikaenda kwanza nyumbani kwa Tecla na kumweleza msimamo wangu, nikamrudishia kiasi cha pesa alichowahi kunipa ili nikusaliti wewe, naomba unisamehe, kwa mara nyingine tena nakuomba, usinichukie nimejuta kiasi cha kutosha, watu hawa ni wabaya waliniteka na kunipeleka mahali ambako kwa kweli wamenitesa sana, nawashukuru polisi!”
“Nimekusamehe, utahitaji kuongea maneno haya mbele ya mke wangu kama ikitokea siku moja akapata nafuu!”
“Bado tatizo la kupotewa na kumbukumbu linamsumbua?”
“Hivi sasa hali ni mbaya zaidi, tumeshamwondoa nyumbani na kumpeleka kwenye kituo cha kulea watu wenye ugonjwa wa akili, alibadilika na kuwa hatari kwa kila mtu!”
“Pole sana, mtoto je?”
“Alipona, hivi sasa anaendelea vizuri!”
Hawakuongea tena zaidi ya hapo, wakakumbatiana kama ishara ya kupeana msamaha na muda huo huo mlango ukafunguliwa, askari akatokea nje na kuwapata taarifa kwamba mkuu wa upelelezi wa mkoa alikuwa akiwahitaji waingie ndani ili kazi iendelee. Gilbert akamsaidia Ngowi kutembea tena hadi ndani ya ofisi ambamo waliketi viti vya jirani, Gilbert akigonganisha macho yake mara kwa mara na Tecla ambaye muda wote alikuwa akilia huku akitoa maelezo.
“Siwezi kupinga, ni kweli mimi ndiye niliyewatuma wamteke Ngowi!”
“Kwanini?”
“Kwa sababu sikutaka siri itoke nje!”
“Siri gani?”
“Ya majibu ya mtoto wangu!”
“Ilikuwaje mpaka ukakutana na Ayub Jeremiah?”
“Baada ya Ngowi kuondoka nyumbani kwangu akiwa amedhamiria kwenda kumwambia Gilbert ukweli, niliwasha gari nikaenda mpaka Mwananyamala sehemu zenye giza ambako watu huwa wanakabwa sana, ndipo Ayub na wenzake walinifuata lakini nikawaambiaa wasinidhuru sababu nilikuwa na kazi ya kuwapa ambayo ingewapatia kipato kikubwa zaidi kuliko kunikaba mimi!”
“Walikubali?”
“Ndiyo!”
“Kikafuata nini?”
“Nikawasha gari na kuondoka nao kwa kasi hadi nje ya nyumba ya Gilbert, nilijua lazima Ngowi alikuwa hajafika na ndivyo ilivyokuwa, kwani muda mfupi baadae nae alifika na kufunguliwa lango akaingia ndani, tukasubiri ili atoke tufanye kazi yetu lakini alipotoka baadae alikuwa kwenye gari tena akiwa na Gilbert, kasi yao ilitufanya tuhisi kuna jambo ikabidi tufuatilie nyuma mpaka hospitali ya Dk. Mathew, wakashuka na kuingia ndani, Ayub na wenzake wakawafuatilia mpaka kwenye chumba cha wagonjwa mahututi ambako walimteka Ngowi kwa bastola ya bandia na kumleta mpaka kwenye gari tukaondoka nae kwenda kumficha ili baadae auawe jambo ambalo halikufanyika!” Tecla alizidi kuongea akibubujikwa na machozi, hakuona sababu ya kukanusha jambo lolote kwani kila kitu kilikuwa wazi.
Gilbert alikuwa haamini alichokuwa akisikia, hakuwahi hata mara moja katika maisha yake kufikiri Tecla angekuwa msichana katili kiasi hicho, alishindwa kuelewa ni wapi hasa alikojifunzia tabia za kijambazi ambazo hazikufanana kabisa na sura yake! Maelezo yake yalipokabilika, Ngowi aliitwa na kujieleza kwa karibu dakika arobaini na tano nzima, ikawa vivyo hivyo kwa Ayub Jeremiah na huyo ndiye alikuwa wa mwisho kwani tayari Gilbert alishatoa maelezo yake. Wote wakachukuliwa na kutupwa mahabusu isipokuwa Ngowi.
“Ahsante sana afande, kwa kweli leo ni siku ya furaha mno kwangu!” Gilbert alimwambia Mkuu wa Upelelezi
“Kwanini?”
“ Nafikiri unaifahamu aibu ambayo imewahi kunipata!”
“Ile ya kuzaa na Tecla?”
“Kumbe na wewe unaifahamu!”
“Kuna asiyelifahamu jambo hilo kweli Gilbert?”
“Basi jina langu litasafishika, Ngowi amesaidia sana, itabidi turudie tena kufanya DN..!” Hakumalizia sentensi yake, simu ya mkononi ikalia, mwanzoni alifikiri labda ni ya mtu mwingine ndani ya ofisi akidhani ya kwake aliiacha garini, alipotulia vizuri alisikia ikilia ndani ya mfuko wake, akaichukua na kuanza kusikiliza.
“Haloo… nani?.... ndiyo…. Kuna nini?...kawaje?... aaaah!...basi nakuja, niko kituo cha polisi nitakuwa hapo baada ya muda mfupi… muangalie sana… kweli kabisa?...” Aliuliza Gilbert, hakuna mtu aliyeelewa alikuwa akiongea na nani juu ya nini lakini macho yake yalionyesha furaha ya ajabu.
“Nini zaidi?”
“Today is my day!” (Leo ni siku yangu!)
“Why?” (Kwanini!)
“My wife’s memory is back on track!” (Kumbukumbu za mke wangu zimerejea)
“Kweli?” Mkuu wa upelelezi aliuliza.
“Ndiyo maana wananipigia simu, wanataka niende nikashuhudie kwa macho yangu, lazima nipitie nyumbani kumchukua mwanangu na mama mkwe, anamlilia mtoto wake, yaani siwezi kuamini, hii lazima itakuwa ni ndoto tu!”
“Inawezekana, basi we nenda tutawasiliana baadae, acha sisi tumpeleke Ngowi hospitali ili kama itawezekana hawa watu wafikishwe mahakamani kesho, hakuna kesi hapa hawa watafungwa tu!”
“Basi ahsanteni!” Gilbert alijibu na kuondoka akikimbia hadi nje, watu waliokutana nao njiani walimshangaa lakini hakujali, akaingia ndani ya gari lake na kuendesha kwa kasi hadi nyumbani kwake na kumsimulia mama mkwe juu ya simu aliyopigiwa, hata yeye alionekana kutokuamini, wakambeba Faith na kukimbia nae hadi kwenye gari ndipo Gilbert akaanza kuendesha kuelekea Vingunguti kwenye kituo cha kulea watu wenye magonjwa ya akili yaliyoshindikana.
Nusu saa tu walishafika na kuegesha gari mbele ya kituo, Gilbert akambeba Faith na wote kuanza kukimbia kuingia ndani, mwangalizi wa wagonjwa akawapokea na kuwasainisha kitabu kisha kuwaingiza ndani mpaka mahali alipokuwa ameketi Salome kwenye baskeli yake ya matairi manne, alipowaona tu alianza kutabasamu na hapo hapo akaanza kuisukuma baiskeli yake kwenda mbele akiwafuata.
“Jamani Darling! Ulikuwa wapi siku zote hizi, mwanangu Faith nimekukumbuka kupita kiasi, mamaaa! Nakupenda mzazi wangu, muda mfupi uliopita nilikuwa naangalia picha ya baba, nimelia sana! Nani amewaleta?”
Wote walikuwa kimya, wakiwa hawaamini kilichokuwa kikitokea, Gilbert alishindwa kuyazuia machozi akashtukia mashavu yake yakiloa, haikuwa rahisi kukubali kwamba alikuwa akiongea mbele yake na Salome, mwili wake ukiwa umejaa majeraha! Akamkabidhi mtoto wake na kupiga magoti mbele yake akisali kumshukuru Mungu, Salome alionekana kutokumbuka kwamba aliwahi kumtupia mtoto wake kwenye bwawa la maji ili afe.
Tecla na Ayubu wamekamatwa na polisi na kufikishwa kituoni ambako wanahojiwa na kukiri kwa pamoja kufanya mpango wa kumteka Ngowi kwa lengo la kumuua ili kuzuia siri ya majibu ya DNA ambayo yalibadilishwa na kuonyesha kwamba mtoto wa Tecla alikuwa ni mtoto wa Gilbert jambo ambalo halikuwa kweli lakini baada ya kuokoka Ngowi aliamua kueleza ukweli wa kilichotokea, jambo ambalo Tecla hakutaka litokee, akamkodisha Ayubu na vijana wengine kwenda kumteka na baadaye kumficha maeneo ya Mwananyamala kabla ya kumuua.
Baada ya kuokolewa na polisi Ngowi anapelekwa hospitali ya Ilala ambako amelazwa kupewa matibabu, hali yake si nzuri sana. Gilbert naye ameitwa kwenye kituo cha kulea wagonjwa wa akili kilichopo vingunguti, huko ndiko mke wake Salome alipo baada ya kushindwa kuishi naye nyumbani pale alipoanza kusababisha hatari. Muuguzi wa kituo hicho amemtaarifu Gilbert kwamba mkewe amerejewa na fahamu zake, jambo ambalo Gilbert hakuliamini mpaka alipofika kituoni na kumkuta Salome amemkumbuka.
Siku iliyofuata Gilbert akiwa ameongozana na rafiki zake walimchukua Salome kurudi nyumbani akiwa na fahamu zake kamili, amemkumbuka hata mama yake na mwanae Faith ambaye alimtupa kwenye bwawa la kuogelea ili afe bila kufahamu jambo alilokuwa akifanya. Walipofika nyumbani na kuingia ndani, Salome aliiona ofisi ya Gilbert, akamkumbuka Tecla, hapo hapo picha yote ya yaliyotokea juu ya mwanamke huyo kudai alikuwa amezaa na mume wake ikijijenga kichwani, Salome akabadilika na kumuuliza Gilbert juu ya jambo hilo, yeye alimtuliza na kumwambia baada ya muda si mrefu angempa jibu.
Wiki moja baadaye Gilbert alitembea hospitali ya Ilala kwenda kumwona Ngowi, ili aendelee kujenga ushahidi wake kabla hajamwambia Salome kilichotokea juu ya Tecla, hakuwa na wasiwasi wowote kwa sababu alikuwa na cha kusema. Hospitalini alimkuta Muuguzi, alipomuuliza habari za Ngowi muuguzi huyo akashangaa kama kweli alikuwa ni ndugu yake ni kwanini alikuwa hajui kilichotokea na alionyesha wasiwasi mwingi.
Je, nini kinaendelea? SONGA NAYO…
“Kama angekuwa ndugu yako lazima ungekuwa na taarifa!” muuguzi aliongea akionyesha wasiwasi huku akiwa amemtolea macho Gilbert na kumfanya ahisi kulikuwa na jambo baya lililotokea.
“Taarifa gani dada? Amefariki?” Gilbert aliuliza akiwa ameshika mikono kichwani.
“Hapana hajafariki!”
“Fyuuuu!” Gilbert alishusha pumzi, Ngowi alikuwa mtu muhimu sana kwake.
“Mbona umeshusha pumzi?”
“Nilikuwa nimeshtuka mno, yuko wapi hivi sasa?”
“Huyu bwana alikuwa amelazwa hapa wodi namba mbili, wakaja watu wakiwa wamevaa makoti meupe kama madaktari mpaka kwenye kitanda chake, hakuna aliyewashtukia lakini baadaye muuguzi aliingia ghafla na kuwakuta, alipowauliza maswali walionekana kushtuka na alikuwa hawafahamu, hivyo akapiga kelele watu hao wakakamatwa na kupelekwa polisi ambako walihojiwa na kukiri hawakuwa madaktari ila walikuwa wametumwa kwenda kwenye hicho kitanda kumuua mgonjwa!”
“Mungu wangu! Hivi Tecla ana mtandao kiasi hiki?”
“Tecla ni nani?” muuguzi aliuliza.
“Tuyaache hayo mzazi wangu, kwa hiyo yuko wapi hivi sasa?”
“Yupo hospitali ya Jeshi Lugalo akitibiwa chini ya ulinzi mkali, inadaiwa ni shahidi kwenye kesi muhimu!”
“Mama ahsante sana, chukua hii na wewe utakunywa soda!”
“Mh, baba!”
“Sio rushwa mama ni shukrani!”
“Haya ahsante mwanangu!”
Gilbert alitoka akikimbia mpaka kwenye gari lake, watu waliomwona walimshangaa, alichokifanya ni kuingia ndani ya gari na kuwasha kisha kuondoka kwa kasi mpaka hospitali ya Jeshi Lugalo akiwa amepitia barabara za Uhuru, Kawawa mpaka Morocco na barabara ya Ali Hassan Mwinyi. Aliegesha gari yake mbele ya hospitali na kushuka kisha kutembea mpaka mapokezi ambako alimuulizia mgonjwa wake.
“Yupo”
“Naweza kumwona?”
“Ni nani yako?”
“Rafiki yangu!”
“Jina lako?”
“Naitwa Gilbert Mushi!”
“Subiri!” Muuguzi alijibu na kugeukia pembeni ambako alichukua mkono wa simu na kuanza kubonyeza namba kadhaa, baadaye akaanza kuongea na mtu akimuuliza kama alimfahamu Gilbert Mushi, Gilbert akaelewa alikuwa akiongea na Ngowi, simu ilipokatwa muuguzi alimwelekeza kwenye wodi ya wanaume ambako aliingia ndani na kumkuta Ngowi amelala kitandani kando akiwepo askari mwenye nguo za JWTZ ambaye alimpekua Gilbert kabla ya kumsogelea mgonjwa.
“Vipi rafiki yangu?”
“Walitaka kuniua tena”
“Pole sana!”
“Ahsante”
“Lakini hivi sasa unaendeleaje?”
“Mungu amenisimamia, nasali sana, yuko upande wangu hakuna adui atakayeshinda!”
“Ameni!”
“Ahsante”
“Yule mwanamke na wenzake wanaendeleaje?”
“Wako mahabusu, wamekiri kosa!”
“Watafungwa, mke wako je?”
“Sijawahi kuwa na furaha kama kipindi hiki maishani mwangu!”
“Kwanini?”
“Mke wangu anaendelea vizuri, kumbukumbu zimerejea na nimekuja kuongea na wewe ili nijue msimamo wako, kwa sababu mke wangu ameniulizia tena suala la Tecla, sijamwambia chochote kuhusu DNA wala kukakamatwa kwake kwa kukuteka na kutaka kukuua wewe ili usiseme ukweli, nataka niyaseme haya nitakapokuwa na uhakika, kuna mabadiliko yoyote?”
“Hakuna, nitasimama popote kutoa ushahidi, mimi nimeokoka Gilbert na nimeokoka kweli kweli sio utani!”
“Ahsante!”
Waliongea mengi kwa karibu saa nzima ndipo Gilbert akaondoka akiwa amemwachia Ngowi shilingi laki tatu za matumizi, hakuwa na sehemu nyingine yoyote ya kupita isipokuwa kunyoosha moja kwa moja kuelekea nyumbani kwake, njiani alimpigia mkuu wa Polisi na kumuuliza ni lini kesi ya Tecla na wenzake ingefikishwa mahakamani.
“Jumatatu!”
“Nitakuwepo!”
“Karibu sana, hawana ujanja wale, wakienda miaka kidogo sana jela ni thelathini!”
“Ni sawa tu!”
Alipofika nyumbani Gilbert hakuwa na jambo jingine la kumwambia mkewe baada ya salamu zaidi ya kumsimulia kila kitu kilichotokea, majibu ya DNA yalivyopindishwa, mpango wa kumteka Ngowi kwa lengo la kumuua ili ukweli usijulikane. Salome alipigwa na butwaa, masikio yake yalionekana kutoamini kabisa alichokuwa akikisikia, akatamani kufika mahakamani na hospitali ili ajionee mwenyewe kama kweli Tecla alikuwa amekamatwa na Ngowi alikuwa hospitali.
“Mpaka nione!”
“Utaweza kwenda mahakamani jumatatu?”
“Naweza”
“Basi itabidi twende wote, maana inaonakana ninayokueleza huyaamini!”
“Niko tayari!”
Ilikuwa ni siku ya jumamosi, mbele yao kulikuwa na Jumapili kabla ya Jumatatu kufika. Gilbert akavuta subira kwa masaa thelathini hatimaye asubuhi ikawadia, akamwandaa mkewe kwa safari ya mahakamani. Moja na nusu walikuwa nje ya mahakama ya Kisutu, watu walikuwa wamefurika kufuatilia kesi hiyo, taarifa hazikukawia kusambaa kwamba Salome alikuwepo mahakamani, waandishi wa habari wakamtafuta mpaka kumpata ndani ya gari aina ya Hiace walilokwenda nalo akiwa ameketi kwenye kiti cha matairi manne na kumpiga picha nyingi akitabasamu, hakuna aliyeamini kwamba hali yake ilikuwa imeendelea vizuri kiasi hicho.
Saa mbili kamili wote waliingia ndani ya ukumbi wa mahakama, Gilbert na mke wake wakaketi mbele kabisa kulipokuwa na nafasi ya kuweka kiti cha matairi, baadaye washtakiwa wakaanza kuingizwa mmoja baada ya mwingine na kuketishwa kizimbani, Salome alipomwona Tecla, hasira yake ilipanda, machozi yakaanza kumtoka! Haukupita muda mrefu wakagonganisha macho yao, Tecla hakuamini alichokuwa akikiona, akasimama wima na kunyanyua mikono yake juu.
“Salome!Salome! Naomba unisamehe, nimekukosea sana nimekwishamwomba mume wako msamaha bado wewe, hata kama nitafungwa lakini naomba ninyi mnisamehe kwanza!” Alipaza sauti ndani ya mahakama wakati Jaji akiingia na kuketi kitini, hakukoma, akaendelea kufanya hivyo na maaskari wakawahi kizimbani na kumketisha chini.
“Hautakiwi kupiga kelele mahakamani, nitakupeka jela sasa hivi!” Jaji alifoka.
“Niko tayari! Lakini hawa watu wanisamehe!” Tecla aliongea akiwa na mtoto wake mdogo mgongoni.
Walinda Usalama Mahakamani walimsaidia Tecla kuketi kitini kama ilivyokuwa kwa washtakiwa wenzake, alikuwa akilia kwa uchungu, kila kitu katika maisha yake kilikuwa kimebadilika na kuwa giza na kilichokuwa mbele yake hakikuwa kingine isipokuwa kifungo. Tamaa ya kumpata Gilbert kwa gharama yoyote ilikuwa imemponza, akamwangalia mtoto wake aliyekuwepo miguuni, bila ubishi alikuwa mtoto wa mzee Toboatobo, akaikumbuka siku aliyolazwa njia panda usiku wa manane na mzee huyo kumwingilia bila ridhaa yake kwa kisingizio cha kumwekea dawa ya mapenzi ndani ya uke wake akitumia uume ili siku Gilbert akifanya naye tendo la ndoa asimwache tena, hakujua kama siku hiyo ndiyo mimba ilikuwa ikiingia. Machozi yakazidi kumtoka.
“Kesi Jinai namba 223 ya mwaka huu, washtakiwa ni Tecla Kimambo, Ayubu Jeremia, Ponsian John, Ibrahim Haji na Elias Kipande! Washtakiwa wote wapo mahakamani?” Jaji Agness Mutayoba aliuliza.
“Ndio Mheshimiwa!” Mwendesha mashtaka alisema kwa sauti ya juu.
“Naomba wasimame!”
Tecla na wenzake wakatii amri hiyo na kusimama wima kizimbani, ndipo Jaji akaanza kuwauliza mmoja baada ya mwingine akiwataja majina na namba, Tecla alikuwa mshtakiwa namba moja, kama walikuwa wakikana au kukiri shtaka hilo. Badala ya kujibu Tecla aliangua kilio na kusababisha kelele kubwa mahakamani, Jaji akaamua anyamazishwe ili mahakama iendelee, maaskari wawili wa kike wakamsogelea na kuanza kumtuliza, muda wote alikuwa akiwaomba msamaha Salome na Gilbert. Alipotulia, Jaji alimwita.
“Tecla!”
“Ndio Mheshimiwa!”
“Unakiri au kukubali kosa la kumteka bwana Ngowi na kumpeleka mahali kwa lengo la kumuua?”
“Siwezi kukataa Mheshimiwa Jaji, ni kweli, ila naomba kusamehewa!” aliongea akizidi kulia, watu aliokuwa nao kizimbani wote waligeuka na kumwangalia kwa jicho la chuki, ilivyoonekana hakuna aliyekuwa ametegemea jibu kama hilo.
Jaji alipomaliza kuandika maelezo mafupi ya Tecla aliwageukia washtakiwa wengine, wote wakakanusha makosa yao, wakidai hawakuwa na uhusiano wowote na Tecla na kuyakana maelezo yote waliyoyatoa polisi, kwamba waliteswa ndipo wakajikuta wakikiri, Tecla aligeuka na kuwaangalia kwa mshangao. Kesi hiyo ikaahirishwa mpaka wiki mbili baadaye, wote wakatolewa kizimbani na kwenda kufungiwa mahabusu, muda wote huo Salome na Gilbert walikuwa wakimwangalia Tecla na kumwonea huruma, waliamini alikuwa amejifunza kiasi cha kutosha, pengine alihitaji msamaha lakini hilo halikuwa mikononi mwao tena.
Waliotaka kumuua Ngowi wodini wakiwa wamevaa mavazi ya kidaktari, walikuwa ni washirika wa Ayubu, walitaka kupoteza ushahidi. Nao walikuwa miongoni mwa washtakiwa, wakiwa mahabusu walijadili sana juu ya nini cha kufanya lakini hawakuwa na jibu la swali hilo, kila kona ilikuwa imewafunga kwani kama ni kukamatwa walikamatwa kweli wakiwa na mavazi ya kidaktari, wakaanza kukata tamaa ya kupata ushindi.
Mwezi mmoja baadaye kesi ilirejea tena mahakamani na kuanza kusikilizwa, ushahidi uliotolewa na Ngowi mahakamani uliwagandamiza wote, Ayubu na washirika wake wakajikuta hawana mahali pa kutokea! Hata hivyo kesi ikaahirishwa tena na wote wakarejeshwa mahabusu. Kesi hiyo iliendelea kwa muda wa miezi mitatu, ikiwa imetawala vyombo vyote vya habari, mwisho ikaja kutolewa hukumu, Tecla na wenzake wakahukumiwa kwenda Jela miaka kumi na tano kila mmoja pamoja na kazi ngumu.
Akitoka mahakamani siku hiyo, Gilbert huku akisukuma kiti cha matairi ambacho juu yake aliketi mke wake, alishtuka alipoguswa bega, akageuka na macho yake yakakutana ana kwa ana na mzee Toboatobo, akamwamkia na baadaye mzee huyo akaomba kuongeana Gilbert pembeni. Uso wake ulionyesha huzuni kubwa, wakasogea kando na kukaa kwenye mabenchi.
“Huyu ni mke wangu anaitwa Salome…Salome huyu ni mzee Toboatobo!” Gilbert aliwatambulisha.
“Nafurahi kukufahamu mwanangu!”
“Ahsante baba”
“Sasa Gilbert…eeh…!”
“Ndio baba”
“Kesi ndio imekwisha, mimi namtaka mtoto wangu, naamini yule mtoto ni mali yangu kabisa, si unaona tulivyofanana?”
“Ni kweli, kwa muda mrefu sana nilifikiria kukutafuta sababu baadaye nilikuja kugundua kilichotokea kwenye kipimo tulichofanya, majibu yalibadilishwa!”
“Nimekwishasikia hapa mahakamani, siku zote nilikuwa nakuja lakini sikutaka tu kukusemesha!”
“Kwa hiyo ndiyo hivyo, nilikuwa nakutafuta ili turudie vipimo!”
“Itakuwa vizuri sana ili usafishe jina lako, limechafuka sana na mimi nipate haki yangu, ni kweli kabisa yule mtoto ni wa kwangu nilifanya ngono na Tecla alipokuja kwangu kutafuta dawa ya mapenzi na sisi huwa tunabahatika watoto wazuri kwa mtindo huo huo…heeh! heeh!” aliongea mzee huyo akitabasamu, haukuwa uongo kwa hadhi aliyokuwa nayo, hakika halikuwa jambo rahisi kumpata msichana mzuri kama Tecla na kufanya naye ngono.
“Ilikuwaje mpaka ukafanya naye tendo la ndoa?” Salome aliuliza akicheka.
“Si unajua tena wajinga ndio waliwao, nilimwambia tu nataka kumwingizia dawa sehemu za…kwa kutumia…ah! Ninyi ni watu wazima mmekwishaelewa!”
“Basi sawa mzee, una simu?”
“Hapana, chukua hii hapa kadi yangu utanipigia mwisho wa wiki, nitakuwa nimeshaongea na wakili wangu ili aande utaratibu wa kurudia vipimo!”
“Nitafurahi sana!”
Hukumu ya Tecla na wenzake ilikuwa kwenye vyombo vyote vya habari, kidogo ilikuwa imeanza kumsafisha Gilbert, lakini hiyo haikumtosha bado alitaka suluhisho kwenye suala la mtoto wa Tecla. Hilo lilikuwa ni jambo baya ambalo kwa kweli lilimharibia sana sifa yake aliyojijengea katika jamii. Nyumbani yeye na mke wake Salome hapakuwa na tatizo lolote, furaha ilikuwa imeanza kutawala, majeraha ya nyuma yalikuwa yameanza kufutika ndoa yao ilianza kuimarika tena, mwisho wa wiki alimpigia mzee Toboatobo baada ya kuwa amekwishaongea na wakili wake na kukubaliana kwamba suala hilo wangelishughulikia kisheria, Gilbert hakutaka kufanya mambo kimya kimya, ikabidi amwite mzee Toboatobo ili wafanye mkutano na Waandishi wa Habari.
Jambo hilo lilifanyika kwenye Idara ya Habari Maelezo ambako waandishi walifurika wakati Gilbert akitangaza nia yake kurudia kipimo cha DNA ili kuthibitisha kwamba mtoto wa Tecla hakuwa wa kwake, akamtambulisha pia mzee Toboatobo ambaye maswali ya waandishi ya habari yalimbana mpaka kufikia hatua ya kueleza kila kitu kilichotokea kati yake na Tecla. Habari hiyo ndiyo ilitawala vyombo vya habari kwa wiki nzima na kuvutia idadi kubwa ya wasomaji waliokuwa wakifuatilia habari za Gilbert na familia yake.
Siku iliyofuata wakili wa Gilbert, Johnson Tenga alifanya taratibu zote za kisheria akapata kibali kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani cha kuomba Tecla na mtoto wake wakachukuliwe vipimo vyao huko huko gerezani Segerea, jambo hilo likafanyika. Mchana wa siku hiyo hiyo tayari vipimo vyao wote vilishachukuliwa, lakini majibu hayakutoka mpaka siku iliyofuata asubuhi.
Hakuna aliyekuwa tayari kuamini baada ya majibu kuthibitisha kwamba mtoto alikuwa ni wa mzee Toboatobo, alikimbia kando akishangilia kama vile ambavyo wacheza mpira hufanya, akiwa amevua shati lake na kubaki kifua wazi. Alipata furaha ya ajabu, waandishi walimpiga picha ambazo zilitumika kwenye magazeti ya siku hiyo na siku iliyofuata chini ya kichwa cha habari; Furaha ya kumpata mwana, habari hiyo ilikuwa gumzo nchi nzima ya Tanzania, kwa Gilbert ulikuwa ushindi mkubwa, heshima yake ilikuwa imerejea.
Wiki mbili baadaye Mzee Toboatobo alimwomba Wakili wa Gilbert amsaidie kumpata mtoto wake kutoka gerezani ili aweze kuishi nyumbani sababu alikuwa akiteseka bila sababu yoyote ya msingi, hakuwa na kosa lolote lililomfanya akae kifungoni. Kwa maelekezo ya Gilbert, wakili huyo aliifanya kazi kwa uaminifu mkubwa mpaka akafanikisha zoezi la mtoto kukabidhiwa mikononi mwa Mzee Toboatobo kisheria, ambaye hata hivyo aliomba msaada kwa Gilbert ili aweze kumlea mtoto huyo vizuri.
“Hakuna shida mzee, tutasaidiana!”
TUKUTANE SIKU YA KESHOOOOOOOOOOOO

Post a Comment