Yanga, Al Ahly hakuna mashabiki
MABINGWA wa Tanzania Bara, Yanga, watacheza mechi
yao ya marudiano na Al Ahly bila ya kuwa na mashabiki watakaoingia
kutazama mechi hiyo.

Mechi
hiyo itakayopigwa Machi Mosi jijini Cairo haitakuwa na mashabiki
isipokuwa wachache tu watakaopata kibali kutoka kwa Shirikisho la Soka
la Misri (EFA).
Mwaka juzi zilizuka vurugu kubwa baada ya timu ya Al Masry kuwachapa
vigogo Al Ahly kwa mabao 3-1, hali iliyosababisha watu 74 kupoteza
maisha na wengine 1,000 kujeruhiwa wakiwemo wengine waliojeruhiwa vibaya
sana. Baada ya hapo, mechi zinachezwa nchini humo, mashabiki wamekuwa
hawaruhusiwi.
Mmoja wa maofisa wa EFA aliyejitambulisha kwa jina la Amir Mohammed
aliliambia Championi Ijumaa juzi kuwa, hakuna mashabiki watakaoruhusiwa
kuingia uwanjani wakati wa mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika
kutokana na sababu za kiusalama.
“Kawaida hata katika mechi za ligi watu wachache wenye kibali maalum
wamekuwa wakiingia uwanjani, hakuna atakayeruhusiwa kuingia. Hivyo kama
itakuwa ni Ahly na timu ya Tanzania, hakutakuwa na mashabiki.
“Labda wachache sana ambao tutawapa kibali, lakini kawaida ni
viongozi na waandishi wa habari pekee. Zaidi ya hapo hatuwezi kuruhusu
watu, waambie Yanga wanapaswa kulijua hilo,” alisema.
Ili kupata
uhakika, gazeti hili liliamua kuwasiliana na baadhi ya Watanzania
wanaoishi katika Jiji la Cairo na mmoja wao aitwaye Mohamed Mdoe alisema
kawaida mashabiki katika jiji hilo wamekuwa wakiangalia mechi za ligi
kuu kupitia runinga.
“Hakuna anayekwenda uwanjani, unajua baada ya zile vurugu za
mashabiki hadi watu wakafariki dunia, walifungiwa na tumeishazoea. Mechi
tunaziangalia kupitia runinga tu hapa,” alisema Mdoe.
Kawaida
mashabiki husafiri na timu zinapokwenda kucheza na wengi wa Yanga
wangependa kwenda na timu yao jambo ambalo sasa linaonekana litakuwa
gumu kutokana na adhabu hiyo wanayoitumikia Misri kutokana na vurugu
hizo zilizosababisha hadi watu kupoteza maisha.
CHANZO NI CHAMPIONI
Post a Comment