ad

ad

She is too young to die - 22


Huku  jasho likimtoka, moyo wake ukiwa umejawa na huzuni, Ngowi alitembea hadi nje alikoegesha gari lake dogo aina ya Nissan Dutsan, bodi lake likiwa limechakaa sababu ya kubeba nyasi za Ng’ombe! Hakuna alichokihitaji ili Wokovu wake utimie kama  kupata msamaha wa Gilbert, hakuwa na dhambi nyingine iliyomsumbua isipokuwa hiyo. Alikuwa tayari kwa lolote hata kama ni kupigwa lakini amwambie Gilbert neno “Nisamehe” bila kufanya hivyo Yesu Kristo aliyekuwa ameamua kumpokea hakuwa na maana yoyote.
“WorldCom!” aliwaza neno hilo baada ya kujaribu kwa muda kukumbuka jina la kampuni ya Gilbert.

Tayari alishafika  eneo lililoitwa Sayansi akitokea Kijitonyama, kwa kumbukumbu zake ofisi za WorldCom zilikuwa barabara ya Samora katikati ya jiji, hivyo alikata kulia kuingia barabara ya Ali Hassan Mwinyi, ingawa kasi ya gari lake siku zote  ilikomea sitini, siku hiyo aliendesha mpaka kilometa themaninikwa saa, bahati nzuri hapakuwa na magari mengi barabarani kwa watu walioelekea Mjini, dakika kumi na tano  tu baadaye   tayari aliegesha mbele ya jengo refu ambalo juu yake liliandikwa neno WorldCom,  mlinzi akaja haraka mpaka kwenye gari akiwa ameshikilia bunduki yake.

“Sema mzee!”
“Vipi wamefunga hawa?”
“Huwa wanafunga saa kumi na mbili tu”
“Gilbert?”
“Alishahamisha ofisi hapa”
“Ok! Kwa hiyo watu wanaotaka kumwona?”
“Nyumbani kwake ndiko iko ofisi ndogo,  si unajua tena mkewe mgonjwa?”
“Kwa hiyo nikitaka kumwona mpaka nyumbani kwake?”
“Ndio!”
“Hivi yuko pale pale au  amehama?”
“Pale pale tu  Mikocheni!”

Mlinzi alitoa maelekezo ya kumfikisha Ngowi nyumbani kwa Gilbert bila kuelewa alichokuwa akifanya,  akapewa shukrani ya shilingi elfu moja na Ngowi akawasha gari na kuondoka,  kilichomfanya achelewe kufika Mikocheni  ingawa safari ilikuwa ni sawa na kutoka Sayansi mpaka mjini ni foleni ya magari, hata hivyo ndani ya saa moja na nusu alisimamisha gari lake mbele ya lango la nyumba ya Gilbert na kupiga honi lakini lango halikufunguliwa, akaendelea kufanya hivyo kwa muda ndipo akasikia sauti nyuma ya lango ikiongea kuulizia mahali mlinzi alipokuwa.

“Sijui alipokwenda baba,  tangu  tatizo hili litokee sijamwona!” Ilikuwa ni sauti ya kike.
Sekunde chache baadaye Ngowi alimwona mtu akichungulia kwenye kidirisha kidogo na kumuuliza yeye alikuwa nani, akajitambulisha na kutoa maelezo machache kwamba alikuwa na jambo la kumweleza mwenye nyumba. Lango likafunguliwa na gari lake likaingia hadi ndani ambako alikuta kundi kubwa la watu wamekusanyika, kulikuwa na dalili zote za msiba. Akaegesha gari kando na kushuka.

“Naitwa Gilbert!”
“Naitwa Jamal Ngowi kama nilivyosema!”
“Sura yako sio ngeni,  niliwahi kukuona wapi?”
“Tutaongea ndugu yangu,  kuna tatizo hapa eh?”
“Ndio! Mtoto wangu mdogo amepotea katika mazingira ya kutatanisha!”
“Alikuwa wapi?”
“Alikuwa amekaa na mama yake pale kwenye bwawa la kuogelea!”
“Mungu wangu, mama yake anasemaje?”
“Ni mgonjwa wa akili!”
“Masikini, hawezi kuwa amemdumbukiza kwenye bwawa?”
“Hatujaangalia, lakini angekuwa kwenye bwawa angekuwa ameelea!”
“Mh! Huwezi kujua,  mtu akishaitwa mgonjwa wa akili ndugu yake anaweza kufanya lolote, si jambo la ajabu hata kidogo akili yake kumtuma afunge jiwe na kumzamisha majini!”
“Inawezekana eeh?” Gilbert aliuliza, akasahau hata kutaka kufahamu shida iliyomleta bwana Ngowi nyumbani kwake,  wazo hilo likaonekana ni la maana zaidi, wakitembea kwenda ndani ambako Gilbert alitegemea kupata msaada wa vijana ambao wangezamia simu yake ya mkono ililia, akaipokea.

“Ndio…ni Gilbert…hospitali kwa Dk. Mathew?...masikini mwanangu…nakuja!” alisema akibubujikwa na machozi ghafla.
***
 “Mungu wangu mbona mtoto yuko majini?” Mlinzi wa Gilbert alisema baada ya kumwona mtoto akihangaika ndani ya bwawa kutoka kwenye kijumba  cha mliniz alichokuwa ameketi ndani yake

Hapakuwa na muda wa kupoteza  akakimbia moja kwa moja na kudumbukia ndani ya maji akiwa na nguo pamoja na viatu vyake, bahati nzuri alikuwa mtaalam wa kuogelea, akamdaka Faith na kutoka naye hadi nje na  kumlaza chini kisha kuanza kuligandamiza tumbo  lake lililojaa maji,  yakaruka kama bomba! Hakuonekana  kuhema, akili yake ikamrejesha kwenye elimu ya huduma ya kwanza aliyojifunza kwenye chuo cha polisi Moshi, hapo  hapo akapiga magoti chini na kuanza kumpulizia  Faith pumzi mdomoni ili kuyashtua mapafu yake lakini kila aliponyanyua kichwa kumwangalia alikuwa ametulia tu.
“Masikini sijui kafa?” aliwaza akimbeba mtoto na kukimbia naye hadi nje ambako alifikiria ni kwa namna gani angeweza kufika hospitali ya Dk.Mathew iliyokuwa kama mita mia tano kutoka nyumbani kwa Gilbert.

Akiwa barabara mara ilipita  teksi, akanyoosha mkono juu na dereva akasimama,  akajieleza kwamba alihitaji msaada kufika hospitali kama kungekuwa na malipo  yoyote ambayo dereva angehitaji basi wazazi wa mtoto huyo wangekuja kulipa. Dereva teksi alimwonea huruma na kumwambia angempa msaada tu bila malipo,  mlinzi akaingia ndani na gari kuondoka,  dakika tatu tu tayari teksi  iliegesha mbele ya jengo la hospitali ya Dk. Mathew iliyoitwa Good Samaritan Health Center, wauguzi wakafika na kumbeba mtoto kwenda kwenye chumba cha daktari.

“Huyu mtoto ni wa nani?”
“Wa bosi wangu”
“Kafanya nini?”
“Kadumbukia kwenye bwawa la kuogelea”
“Masikini!” Dk. Mathew aliongea kwa sauti ya chini akionyesha masikitiko jambo lililomthibitishia kabisa  mlinzi kwamba tayari Faith alishaaga dunia.
“Umesema baba yake ni nani?”
“Gilbert!”
“Gilbert mfanyabiashara wa  WorldCom?”
“Ndio, mimi ni mlinzi wake”
“Nina namba yake ya simu,  acha nimpigie!”
“Kwani vipi mzee? Amekufa?”
Dk. Mathew alichukua simu yake na kubonyeza namba kadhaa kisha kuanza kusikiliza, iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa, akapiga tena na tena lakini hali iliendelea kuwa hiyo hiyo, akaachana na simu na kumgeukia mtoto aliyelala kitandani,  akaweka mikono yake yote miwili kifuani upande wa moyo na kuanza kugandamiza kwa nguvu, alipoacha alipuliza pumzi mdomoni mwake! Alikuwa akifanya kile ambacho wataalam huita Cardiac Massage   ili kuushtua moyo wa Faith na alipomaliza zoezi hili alimpulizia pumzi mdomoni lakini bado mtoto hakushtuka, akamnyanyua na kumbeba mikononi  kisha kutoka naye nje.
“Nifuateni!”
“Wapi daktari?”
“ICU!” aliongea akizidi kutembea kwa haraka, mlinzi wa Gilbert  na wauguzi wakifuta nyuma.
“ICU ni wapi?” mlinzi aliuliza.
“Chumba cha wagonjwa mahututi”
“Mimi nilifikiri ni chumba cha maiti, kumbe mtoto bado mgonjwa?”
“Ndio, daktari anahangaika kuokoa maisha yake”

Nje ya chumba cha wagonjwa mahututi kilichokuwa mita kama sabini na tano hivi kutoka idara ya wagonjwa wa nje, mlinzi wa Gilbert alizuiliwa kuingia akitakiwa kubaki nje ili awape nafasi ya kufanya kazi,  wauguzi peke yao pamoja na daktari ndio waliendelea hadi ndani ambako Faith alilazwa kwenye kitanda na kufungiwa mdomoni na puani mashine iliyoitwa Respirator ili imsidie kupumua, mashine nyingine ya kutumia umeme ilifungwa kifuani upande wa moyo, ilipowashwa ilitetemesha  kifuani  kwa lengo la kuushtua moyo wa Faith ambao ulikuwa ukipiga kwa kasi ya dakika moja kati ya pigo moja na jingine, haikuwa rahisi kugundua kama ulikuwa ukipiga.
“Atapona?” Muuguzi alimuuliza daktari.
“Angelina hutakiwi kukata tamaa,  wewe ni muuguzi!”
“ Sijakata tamaa daktari, ila nawaonea huruma sana wazazi  wake, ni mzuri mno, lazima wataumia sana!”
“Kama unawaonea huruma basi mtibu vizuri, ili apone!”
“Najitahidi daktari!”
Dk. Mathew hakuondoka chumba cha wagonjwa mahututi mpaka ilipotimu saa mbili na nusu usiku, hali ya Faith ikiwa imetengemaa kidogo, alikutana na  mlinzi nje  na kuanza kumweleza hali ya mgonjwa ilivyokuwa ikiendelea, alimwomba msamaha kwamba walikuwa wamemsahau kabisa na akili zao kuishia kwa Faith peke yake. Mwisho alikumbuka suala la kumpigia simu Gilbert kumweleza juu ya mtoto wake, akachukua simu na kuibonyeza namba yake, safari hii iliita mara moja tu na kupokelewa.
“Hallow ni Gilbert?...hapa ni hospitali kwa Dk. Mathew….ndio…mtoto wako yuko hapa, anaumwa sana aliletwa hapa na mlinzi wako….naomba  kama inawezekana ufike hapa haraka… sawa  nilikuwa naondoka lakini sasa nakusubiri!”  Dk. Alisema na baadaye kukata simu, ingawa  mlinzi hakusikia sauti ya Gilbert upande wa pili alielewa ni kitu gani alichosema kutoka na jinsi  daktari alivyokuwa akiongea.
“Ahsante sana daktari, tajiri yangu atafurahi mno bila shaka anaweza hata kuniongezea mshahara kwa sababu nimeokoa maisha ya mtoto wake, bila mimi Faith angekufa!”
“Kweli kabisa, unaitwa nani?”
“Mcholemchole!”
“Umefanya kazi ya ulinzi kwa muda gani?”
“Miaka thelathini na tano sasa”
“Hongera! Una watoto?”

Waliendelea kuongea mambo mengi wakisubiri Gilbert  afike, mzee Mcholemchole alikuwa na hamu kubwa ya kumwona tajiri yake ili angalau apate nafasi ya kujipendekeza, alimwomba Dk. Mathew amchombezee ili aongezewe mshahara kwa sababu alikuwa amefanya kazi kubwa.

***
Baada ya kupokea simu, Gilbert aliingiwa na furaha ya ajabu,  kufahamu tu kwamba mtoto wake alikuwa  hospitali ilikuwa ni faraja kubwa. Haraka akatembea mpaka kwenye kundi la watu waliokuwa wamekusanyika wakijadiliana na kuwapa taarifa alizozipokea, wote wakafurahi na  alipowaaga kwamba alikuwa anakwenda hospitali, hawakuwa tayari kumwacha aondoke peke yake,  kundi kubwa wakaingia kwenye magari yao,  yeye akiwa amepanda kwenye gari la Ngowi na kuongozana moja kwa moja hadi hospitali ya Dk. Mathew ambako waliegesha na kushuka.
“Chumba cha wagonjwa mahututi ni wapi dada yangu?” Gilbert alimuuliza msichana aliyemkuta mapokezi.
“Hata salamu kaka?”
“Nisamehe ndugu yangu nimechanganyikiwa, mwanangu yuko huko! Hujambo lakini?’
“Sijambo shikamoo! Mwanao nani?
“Faith!”
“Wewe ni Gilbert?”
“Ndio!”
“Nimekuwa nikikusikia muda mrefu, twende nikupeleke nilikuwa huko sasa hivi, Dk. Mathew anakusubiri!”

Gilbert na watu wote aliokuwa nao waliongozana hadi chumba cha wagonjwa mahututi,  wakawakuta Dk.Mathew na mlinzi  wameketi nje kwenye benchi wakiwasubiri, wa kwanza kusimama alipowaona alikuwa mlinzi, akatembea haraka mpaka mbele ya Gilbert huku akitabasamu.
“Nimejitahidi sana bosi, bila mimi mambo yangekuwa mengine…heeee!Heeee! sasa hivi Faith anaendelea vizuri, nisemehe niliacha lindo”  Mlinzi aliongea mfululizo lakini Gilbert alionekana kabisa kutoyajali mazungumzo yake,  akamwacha na kusogea mbele ambako alishikana mkono na Dk. Mathew wakisalimiana.
“Usiwe na wasiwasi tena, tumefanikiwa kuokoa maisha ya mtoto ila una kila sababu ya kumshukuru bwana Mcholemchole!” Dk. Mathew aliongea.
“Hakuna tatizo, ahsante sana Mcholemchole!”
“Hakuna shida bosi, mimi na wewe ndugu, si unajua naipenda sana familia yako? Kama ambavyo wewe unanipenda mimi? Heeee!Heeeee! najua utaniangalia angalia kidogo miwsho wa mwezi angalau mzee wako nipendeze”
“ Daktari naweza kumwona Faith?” Gilbert alimwamba daktari kama vile hakusikia kilichosema na mlinzi wake.
“Hakuna tatizo, lakini wataruhusiwa kuingia watu wawili tu!”

Gilbert akamchukua rafiki yake Davis na kuingia naye ndani,  hakuamini macho yake alipomwona Faith amelala kitandani mdomoni amewekewa mashine ya kupumulia, kwenye mkono akiwa na dripu! Bado hakuwa na uwezo wa kufumbua macho wala kuongea, Gilbert akapiga magoti kando ya kitanda  na kuanza kusali huku  akibubujikwa na machozi,  kwenye maombi yake alimshukuru Mungu kwa  yote yaliyokuwa yakimtokea akiamini kwamba yote ilikuwa ni mitihani na baada ya kuishinda maisha yake yangebarikiwa kama alivyobarikiwa Ayubu.

Baada ya sala yake alinyanyuka na kumbusu mwanae usoni, kisha kumgeukia daktari na kuanza kumshukuru kwa  wema aliomtendea, wote wakaanza kuongozana kwenda nje ambako walikuta watu walioongozana nao wakiongea kwa sauti ya juu kama vile kulikuwa na tatizo lililojitokeza, Gilbert akasogea karibu yao na kuwauliza ni kwanini walikuwa wakiongea kwa sauti ya juu  hivyo wakati walikuwa ndani ya mazingira ya hospitali.
“Kuna watu wawili wamekuja hapa wakamuulizia Ngowi, akajitokeza yule bwana uliyekuwa naye na wakaomba kuongea naye lakini walipokwenda pale pembeni,  tulimwona mmoja kama amechomoa bastola mkononi na kumwekea shingoni kisha kuanza kuondoka naye, sasa tunajiuliza wale ni maaskari au?”
“Wako wapi?”
“Wameondoka hapa sasa hivi tu, hata dakika tano hazijapita!”
“Kuelekea wapi?”
“Huko nje!”
“Mh! Sijui bwana, huyo Ngowi mwenyewe nimekutana naye leo tu,  wala simfahamu!” Gilbert aliongea  akimfuata daktari aliyemtaka waongozane kwenda ofisini kwake kwa maongezi zaidi.
“Mh! Sijui bwana, huyo Ngowi mwenyewe nimekutana naye leo tu,  wala simfahamu!” Gilbert aliongea  akimfuata daktari aliyemtaka waongozane kwenda ofisini kwake kwa maongezi zaidi.
“Kweli?”
“Ndio”
“Sisi tulifikiri labda ni ndugu yetu!”
“Huwezi kuamini  alifika nyumbani muda mfupi tu kabla simu ya Dk. Mathew haijaingia, simjui!”

Waliongozana na Dk. Mathew mpaka ofisini kwake ambako walianza kumwongelea Faith, hali aliyokuwa nayo na matarajio yalivyokuwa, daktari akamhakikishia  mtoto angepona,  maneno hayo   yalirejesha furaha ya Gilbert  kwani hakuna kitu kilichomuumiza akili yake kama kufiwa na mwanae pekee, aliporejea kwa wenzake aliwapa taarifa hizo nao wakafurahi pia na  saa nzima baadaye waliondoka pamoja na mlinzi  kurejea nyumbani wakimwacha Gilbert peke yake, akakaa nje ya chumba cha wagonjwa mahututi mpaka asubuhi ndipo akaruhusiwa kuingia ndani na kumkuta Faith amefumbua macho akitabasamu, machozi ya furaha yalimtoka Gilbert.
“Ahsante Mungu!” ndio maneno pekee aliyoyatoa akimpiga mtoto wake busu usoni.

Kwa siku tatu walibaki hospitali Faith akitibiwa kichomi kilichojitokeza sababu ya  kuvuta maji kwenye mapafu ndipo hali yake  ikawa nzuri na kuruhusiwa kurejea nyumbani ambako  ilibidi  sherehe ndogo ya kumshukuru Mungu ifanyike na marafiki kualikwa nyumbani, Salome alikuwepo, wala hakuelewa ni  kitu gani kilikuwa kikiendelea, kumbukumbu zake zilikuwa hazijakaa sawa, muda wote alikuwa kimya kwenye kiti chake cha matairi manne. Wote waliomtazama walishikwa na  huzuni, haikuwa rahisi kuamini mwanamke mrembo kama yeye, hatimaye alikuwa ametulia kwenye kiti.

Hivyo ndivyo alivyoishi, alikuwa mkimya na  alipoamua kuongea ilikuwa ni kufoka, alishikwa na hasira sana na mara zote alitishia kuua mtu akitaka arejeshwe alikotoka, akidai hapo alipokuwa hapakuwa nyumbani kwao na watu waliomzunguka walikuwa majambazi,   madaktari  walimweleza Gilbert kwamba hiyo haikuwa dalili nzuri, kulikuwa na uwezekano mkubwa  siku moja Salome angeweza kumdhuru mtu na kitu cha hatari! Gilbert alipuuza akihakikisha kabisa  Faith haingii mikononi mwa mama yake kwa sababu ndio alikuwa mtu pekee katika hatari ya kufa.
“Nitamwangalia vizuri, sitamwacha peke yake!” Dk. Hassan, bingwa wa magonjwa ya akili kutoka hospitali ya Muhimbili alimshauri Gilbert alipokwenda kumtembelea nyumbani kwake.
“Sawa lakini kwa ushauri wangu ni bora angepelekwa kwenye kituo cha kulea watu wenye magonjwa ya akili, tunacho kimoja kule Vingunguti!”
“Mke wangu? Apelekwe kwenye kituo cha watu wenye magonjwa ya akili? Siwezi!”
“Naelewa Gilbert,   kila mtu huwa hayuko tayari kulifanya jambo hili lakini kuna wakati unalazimika, najua unampenda sana Salome,  hupo tayari kutenganishwa naye lakini nakushauri kitaalam kwamba mwache aende kwenye kituo!”
“Siwezi daktari!”
“Sawa, itabidi sasa uwe unakaa naye karibu, maana asipomzuru mtu anaweza kujizuru mwenyewe!”
“Hakuna shida, nitakuwepo  kumwangalia!”

Wiki moja baadaye,  Gilbert akiwa  bafuni kusaidia kumwosha Faith, mama akiwa jikoni kutayarisha chakula cha mchana,  wote walisikia kelele kutoka sebuleni ambako Salome alikuwa amekaa, wakakimbia na kumkuta ameshika waya wa umeme uliokuwa wazi kwenye ukuta,  ukimtetemesha mwili mzima! Gilbert akakimbia mpaka bafuni na kuchukua mwiko ambao alikuja kuutumia kumtenganisha na umeme, akaanza kumpa huduma ya kwanza kuushtua moyo wake, alifanya hivyo kwa muda mfupi akamwona amefumbua macho.
“Mama  acha nimpeleke hospitali!”  Gilbert alisema.
“Sawa baba, tujulishe hali itakavyokuwa!”
“Ahsante mwangalie Faith!”

Ilikuwa ni tatizo juu ya tatizo, bandika bandua! Hospitali Salome alipimwa na kugundulika kwamba alikuwa amepata mshtuko wa umeme lakini hali  yake haikuwa mbaya sana, akapumzishwa kwa masaa mawili na  baadaye akaruhusiwa, kabla  hawajaondoka Dk. Hassan alifika wodini kuongea na Gilbert,  akamkumbusha  Gilbert tena juu ya kumpeleka  mke wake kwenye kituo cha watu wenye matatizo ya akili ambako angekaa na wataalam ambao wangemwangalia  vizuri asijizuru yeye wala kumzuru mtu mwingine.
“Sina jinsi daktari, ingawa sipendi kutenganishwa na mke wangu, nampenda mno!”
“Naelewa, hata mimi nampenda sana mke wangu, sipendi kutenganishwa naye lakini kuna wakati inabidi, maana uking’ang’ania sana unaweza kusababisha maisha yake kupotea!”
“Sawa daktari, tumpeleke!”
“Acha basi nifanye maandalizi!”
“Sawa, subiri nipige simu ofisini WorldCom, wakamchukue mama pamoja na mwanangu waje waagane naye!”
“Fanya hivyo basi wakati mimi nakamilisha taratibu nyingine, nakushukuru kwa uamuzi wako wa busara!”

Salome alikuwa akicheka peke yake wakati Gilbert akiongea kwenye simu na watu wa  ofisini kwake, si kwamba alielewa kilichoendelea, kumbukumbu hazikuwa sawa, alikuwa kama mwendawazimu. Saa nzima baadaye, mama yake Salome na Faith waliingia wodini na kuwakuta Salome, Gilbert, Dk. Hassan  na Davis wakisubiri, maandalizi yote yalikuwa tayari, wakapewa taarifa ya uamuzi uliokuwa  umefikiwa, mama hakuwa na kipingamizi kwani hali ya mtoto aliifahamu. Akamsogelea mwanae kumuaga kwa kumbusu usoni,  alishangaa kibao kilipotua usoni kwake.
“Wewe bibi mwanga nini? Unanibusu mimi unanijua? Nilishawaambieni ninyi lazima niwaue, nirudishe nilikotoka!”
“Wapi mwanangu? India” Mama  yake aliuliza akijipapasa usoni.
“Kwani kwetu mimi India? Nirudisheni kwa mume wangu, nataka nikwamwone mwanangu!”
“Kumbukumbu zake zimeanza kurejea, ipo siku atatambua kwamba wewe ndiye mume wake!” Dk. Hassan aliongea.
“Mimi ndio mumeo!”
“Toka hapa,  mume wangu awe na sura mbaya kama  kiatu kilichokwisha soli?” Salome aliuliza na wote wakacheka.
“Mnacheka nini?”
Ilibidi familia nzima imsindikize hadi Vingunguti karibu na kiwanda cha Pepsi ilipokuwa kambi wa wazee na wagonjwa wa akili waliohitaji matunzo, walipofika waliegesha magari yao na kushuka, Dk. Hassan akiwaongoza mpaka mapokezi ambako mwanamke mwenye umri kati ya miaka arobaini na tano hadi hamsini, aliyejitambulisha kama muuguzi  Rehema Ramadhan aliwakaribisha kwenye viti na baadaye kuwapa fomu za kujaza Dk. Hassan alipoonyesha karatasi ya mgonjwa. Muda wote hayo yakiendelea, Gilbert alikuwa akichungulia ndani ya  kambi, watu wengi  wachafu wakitembea utupu walionekana kupita katikati ya uwanja,  miili yao ikiwa imejaa ukurutu! Wengi walikuwa wazee, kichwani mwake akajiuliza  “Kwanini  nakuja kumtesa mke wangu hapa?”.
“Haya nipeni mgonjwa wangu, ninyi muondoke!” Muuguzi aliwaambia.
“Daktari!” Gilbert akaita.
“Naam Gilbert”
“Hii ni ngumu!”
“Ipi?”
“Hivi unafikiri kumwacha mtu unayempenda sehemu kama hii ni jambo rahisi daktari?”
“Najua sio rahisi!”
“Sasa kwanini unataka nimwache mke wangu hapa,  hivi umekwishakuona humo ndani? Hebu chungulia uone watu wanaoishi hapa walivyo,  tazama wale wanavyopigana, yaani nimwache hapa Salome? Hapana, roho inaniuma mno, nampenda sana mke wangu daktari siwezi kufanya ukatilii huu!”
“Hufanyi  ukatili Gilbert, ni tiba, akiwa hapa mkeo atapata huduma zote muhimu na atasaidiwa kumbukumbu zake zirejee!”
“Eti mama tumwache hapa Salome?”
“Hakuna jinsi mwanangu,  hata mimi nampenda mno Salome lakini tumsikilize daktari!”

Machozi yalimtoka Gilbert baadaye alipokubali na kutia saini kwenye fomu, kisha kushuhudia Salome akisukumwa kwa nguvu kuingia ndani,  hata yeye mwenyewe  alionekana hapendi kuingia sehemu hiyo, aliendelea kupiga kelele akisema “Nipelekeni nyumbani,   kwa mume na mtoto wangu”  Dk. Hassan alipoyasikia maneno  hayo alimhakikishia Gilbert kwamba muda si mrefu kumbukumbu za Salome zingerejea,  kwani  kitendo cha kufahamu kwamba alikuwa na mume na mtoto ingawa hakuwatambua kama walikuwa eneo hilo ilikuwa ni hatua  kubwa.

Ndani ya ngome ya kituo hicho,  waliendelea kumsikia Salome akilia na baadaye mtu akipigwa, Gilbert alizidi kuumia na hakutaka kuendelea tena kubaki eneo hilo, akaondoka akifuata na mama yake Salome akiwa amembeba Faith mpaka kwenye gari, daktari akawafuata dakika tano baadaye na kupanda, safari kurejea mjini ikaanza,  njia nzima Gilbert alikuwa akiwaza mambo mengi Davis akiwa kwenye usukani. Walinyoosha moja kwa moja hadi nyumbani ambako upungufu wa Salome ulionekana wazi mara tu baada ya Gilbert kuingia ndani, hakuwa na la kufanya zaidi ya kukubaliana na ukweli.

Siku ya kwanza ikapita akiwa mwenye mawazo mengi, hakukumbuka tena habari za Tecla na mtoto wake, akili yake ilikuwa imetekwa na tukio la mkewe kupoteza kumbukumbu! Alijua bado magazeti yangeendelea kuandika lakini hakutaka kusoma wala kusikiliza redio, alikuwa kwenye ulimwengu wa peke yake, kwa mara  ya kwanza maishani aliamini kulikuwa na uwezo wa mwanadamu kuishi bila kujua kilichoendelea duniani.

Kila wiki siku ya Jumapili  Gilbert na familia yake baada ya kutoka kansiani  ilikuwa ni lazima  waende kituoni kumwona Salome na  Dk. Hassan aliwashauri kila wakienda wampelekee vitu ambavyo vingeweza kumkumbusha mambo ya nyuma, wakawa wanamchukulia picha tangu siku ya harusi, alipokuwa mjamzito,  picha ya marehemu baba yake,  mama yake na  mtoto wake Faith!  Bado Salome hakumkumbuka hata mmoja wao, Gilbert alipomsogelea alimpiga na kumfukuza, akimtaka akae mbali yake, hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa mama na hata mtoto wake.

“Uwe unampa anazingalia, inawezekana zikamsaidia kukumbuka alikotoka, lakini mbona ana makovu mengi?”
“Anapigana sana na wenzake!”
“Hamuwezi kumsaidia asipigane?”
“Humu ndani ni pagumu, kuna watu wachokozi sana, ni lazima ajihami!”
“Hakuna jinsi ya kumlinda?”
“Najitahidi sana Gilbert!”
“Haya basi, hizo ndio picha nimemletea leo!”
“Hakuna shida!”
“Sawa sisi tunaondoka lakini tutarudi tena jumapili!”
“Karibuni!”

Wote waliondoka kwa unyonge mpaka kwenye gari, Gilbert alipokaa tu kwenye usukani na kuwasha gari kabla hajaingiza gia akisubiri watu wote wapande,  simu yake ililia kuashiria kulikuwa na ujumbe mfupi wa simu umeingia, akaichukua simu yake na kufungua ujumbe uliokuwepo, moyo wake uliruka mapigo kadhaa, jasho  na macho yakamtoka aliposoma ujumbe uliokuwepo kwenye kioo cha simu yake.
“Nini tena baba?”
“Hakuna tatizo mama!”
“Huna tatizo? Mbona umeshtuka sana?”
“Mambo ya kawaida tu mzazi” alijibu akiendelea kusoma;
Naitwa Ngowi,
Sijui kama unaweza kunikumbuka,
Nilikuja kwako siku ile mwanao akiwa amepotea,
Nikashauri tuangalie kwenye bwawa la kuogelea,
Tukiwa hospitali ya Dk. Mathew, nilitekwa na watu wasiojulikana,
Hapa nilipo sipafahamu ni wapi lakini ni jijini Dar es Salaam,
Kama utaweza nitafute mpaka unipate, nina ujumbe mzito wa kukupa ambao ndio hasa nilikuja kukueleza siku ile,
Ahsante.
Ngowi.

Ujumbe uliishia hapo, Gilbert alishindwa kuondoa gari kwa muda wa karibu dakika kumi na tano akitafakari juu ya alichokisoma, hakuelewa ni watu gani walimteka Ngowi na kwa sababu ipi na alikuwa amekuja kumweleza kitu gani! Hakuwa na jibu la maswali yote yaliyomwijia kichwani. Mwisho aliamua kuwasha gari na kuondoka hadi nyumbani ambako aliwashusha watu wote aliokuwa nao kwenye gari na kuondoka tena hadi kituo cha polisi kikuu kuonana na mkuu wa upelelezi wa Mkoa, akamwonyesha ujumbe aliokuwa nao kwenye simu yake. Wote wawili wakaanza kuipiga hiyo namba bila mafanikio.
“Tutahitaji maelezo yako, baada ya hapo vijana wataingia kazini kufanya upelelezi tutampata tu! Ni kazi ndogo sana, hawa watu wanaotumia simu za mikononi kutuma ujumbe ni rahisi mno  kuwakamata!”
“Hakuna shida!”
“Acha basi niite kijana wangu mmoja aje achukue maelezo yako!”
“Hakuna shida”
Mkuu wa upelelezi alichukua simu na kupiga namba fulani, muda mfupi tu baadaye akaingia kijana mrefu mwembamba na kupiga saluti mbele yake na  baadaye kumsalimia Gilbert ndipo Mkuu wa Upelelezi akampa maelezo kijana huyo juu ya kazi ya kufanya, akaondoka na Gilbert mpaka ofisini kwake na kuanza kumhoji juu ya tukio zima, ilimchukua saa nzima kukamilisha, akaondoka kurejea nyumbani akiwa amewaachia namba ya simu  iliyotuma ujumbe ili wao waendelee na kazi ya upelelezi.

***
“Mh! Picha nzuri ya harusi, walipendeza, lakini mbona hii sura inafanana ya kwangu? Ni mimi, huyu ni mume wangu Gilbert” Salome aliwaza akiwa ameshikilia picha mikononi mwake,  moyo wake ukajaa furaha, akaiweka picha hiyo chini na kuchukua nyingine.
“Mh! Huyu ni marehemu baba yangu…masikini alikufa kwenye maji akijaribu kwenda kunitafutia daktari wa kunisaidia nilipokuwa mjamzito wa mimba ya mwanangu Faith…”Aliwaza Salome,  huzuni kubwa ikamwingia, akaukumbuka usiku huo wa mvua kubwa huku akivuja damu, machozi yakamtoka, kilio kikubwa kikasikika ndani ya kambi, muuguzi akafika akikimbia.
“Salome!”
“Bee”
“Mbona unalia mwanangu?”
“Picha! Zimenikumbusha mbali, zimenikumbusha mume wangu na marehemu baba yangu aliyekufa  kwenye maji!”
Muuguzi akacheka, yeye pia furaha  ikamiminika moyoni mwake.
ITAENDELEA SIKU YA KESHOOOOOOOOOOOOOO...
Je, nini kitaendelea? Fuatilia

No comments

Powered by Blogger.