ad

ad

She is too young to die - 21



Mambo yameharibika tena, majibu yametoka na kuthibitisha kwamba mtoto aliyezaliwa na  Tecla ni wa Gilbert  jambo ambalo Gilbert hakubaliani nalo. Ni bora basi ingeishia hapo, lakini bahati mbaya sana  habari hiyo imemfanya Salome apasuke mshipa kichwani tena na kuhitaji  upasuaji mwingine, jambo ambalo madaktari wa Muhimbili wamesema hawawezi kufanya  kwani alikwishafanyiwa upasuaji kwenye ubongo wake mara mbili, hivyo wameamua asafirishwe kwenda India na Gilbert ameshughulikia kila kitu.

Wakiwa njiani kuelekea uwanja wa ndege, kwenye taa za Tazara,  wanakumbana na  msururu mrefu wa magari na kuambiwa na madereva wengine kwamba msafara wa Rais ulikuwa unapita,  Gilbert akachanganyikiwa kwani isingewezekana kusubiri, ndege ingewaacha. Akamtoa dereva wa gari la wagonjwa kwenye usukani na yeye kulipitisha kando kando karibu na mtaro mpaka mbele  ambako msafara wa Rais ulikuwa ukipita na askari wa usalama barabarani walikuwa wakiruhusu gari za upande mmoja  tu, Gilbert akaamua kuliingiza gari barabarani bila kuogopa kuvunja sheria. Je, nini kitatokea? Atawahi ndege? SONGA NAYO…

Gari lilipoingia barabarani tu, maaskari  watano wenye bunduki walilizunguka wote wakiziweka bunduki zao tayari kwa jambo lolote, kwa kilichoonekana kutaka kutokea haikuwa rahisi hata kidogo kuamini  kwamba gari hilo kweli lilikuwa limebeba mgonjwa. Tayari   mmoja wa maaskari akafungua mlango wa dereva na kukutana uso kwa uso na Gilbert akiwa kwenye usukani, akazima gari na kuchomoa ufunguo huku akihema kwa hasira.
“Wewe huna akili nini? Unaona msafara wa Rais unapita wewe unataka kuingiza gari lako barabarani,  ili usababishe ajali na utie vitumbua vyetu mchanga?”
“Sio hivyo afande, namheshimu sana Rais wangu lakini pia nampenda sana mke wangu ambaye  ni mgonjwa, amelala huko nyuma, nawahi uwanja wa ndege mkuu, nasafiri kwenda India kwa matibabu, ndege inaondoka ndani ya  dakika arobaini zijazo, ungekuwa wewe ungefanya nini afande?”
“Ni kweli lakini…” askari huyo aliongea akiwaangalia wenzake usoni, ni kweli maneno ya Gilbert yalikuwa yamemwingia  kichwani mwake hasa baada ya kumwona akibubujikwa na machozi.
“Aisee itabidi avumilie kidogo, msafara wenyewe umekwisha!” askari mwingine aliongea na Gilbert akainamisha kichwa chake kwenye usukani akifikiria hatma ya maisha ya mke wake aliyempenda sana.

Dakika  mbili baadaye alishtukia akiguswa begani, akanyanyuka na kuangalia,  alikuwa ni askari akimkabidhi ufunguo wake na kumtaka aendelee na safari yake. Akamshukuru Mungu na kuliwasha gari, kisha kuondoka kwa kasi na kuwasili uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere dakika saba baadaye na kuliegesha gari mbele ya jengo la uwanja,  akashuka na kufungua mlango wa nyuma,  machela ambayo Salome alilala juu yake ikateremshwa na kusukumwa hadi  ndani ya uwanja, Gilbert na Davis wakifuata nyuma na kuonyesha vielelezo vyote,  ni kweli walikuwa wamechelewa lakini kwa jinsi hali ya mgonjwa ilivyokuwa, hata wafanyakazi wa shirika la Ndege la Kenya walijikuta wakiwa tayari kumsaidia.

Salome akachukuliwa na kupakiwa moja kwa moja ndani ya ndege ambako alilazwa juu ya kitanda maalum, Gilbert akaketi kwenye kiti na kumshukuru Mungu kwa yote yaliyotokea, mpaka kuwa uwanjani wakati huo aliamini ni muujiza wake. Kila kitu  alichokishuhudia ndani ya ndege hiyo kilimkumbusha safari yake na Faith kwenda India,  ambayo hata hivyo ilikomea kwenye uwanja wa  ndege wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi,  huo ndio  ukawa mwanzo wa matatizo katika maisha yake. Alimwomba Mungu lisitokee tena jambo kama hilo watakapotua kwenye uwanja wa Jomo Kenyatta,  kweli jambo hilo halikutokea,  wakatua kwenye uwanja wa Mumbai saa kumi na moja alfariji saa za  huko na kupokelewa na wafanyakazi wa hospitali ya Kimataifa ya Jaslok waliokuwa uwanjani wakiwasubiri tangu saa tisa na nusu usiku.

Kutoka uwanjani mpaka hospitalini hapakuwa na umbali mkubwa, iliwachukua muda wa kama dakika thelathini na tano kufika, Salome akapokelewa na kupelekwa kwenye chumba maalum kilichoandikwa mlangoni Specialists Boardroom,  ambako walikuta kundi la watu wasiopungua kumi na moja wakiwa wameketi kwenye meza ya duara, mgonjwa akaingizwa na kulazwa kwenye kitanda kilichokuwa pembeni, taa zikawashwa na Gilbert akawakabidhi karatasi zote alizopewa hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“You are welcome to India!” (Unakaribishwa India) alisema mmoja wa madaktari baada ya kujitambulisha.
“Thank you!” (Ahsante) Davis na Gilbert wakaitikia.
“So this is the referral letter?” (Kwa hiyo hii ndio barua ya rufaa sio?) mmoja wa madaktari aliuliza ambaye wakati wa kujitambulisha alijitaja kama Dk. Muneer Kotecha, bingwa wa upasuaji wa ubongo na uti wa mgongo.
“Ndio”
Madaktari hao wakaanza kuisoma barua kisha kumchunguza mgonjwa,  pamoja na kwamba vipimo vyote vilifanyika Dar es Salaam  ilibidi virudiwe tena na kuthibitisha kwamba kilichoonekana Muhimbili ndicho kweli kilichokuwa kikimsumbua mgonjwa, bonge la damu kubwa lilikuwa limekwama ndani ya fuvu lake na kwamba madaktari wa Muhimbili walishindwa kumpasua kwa sababu tayari alikwishafanyiwa upasuaji kwenye ubongo wake mara mbili kabla, hiyo iliwatia hofu kwamba huenda wangeweza kusababisha matatizo mengine makubwa zaidi.
“We can do this! “(Tunaweza kufanya hili)
“Sure?” (Hakika?) Gilbert aliuliza akitabasamu.
“We have done major brain operations, just two weeks ago we separated two Siamese twins” (Tulikwishafanya upasuaji mkubwa wa  ubongo,  wiki mbili tu zilizopita tulitenganisha mapacha walioungana)

Badala ya kusema chochote alijikuta akitabasamu, matumaini ya mke wake kupona yakarejea, hakuna alichokuwa akikifikiria wakati huo ndani ya ubongo wake isipokuwa kupona kwa mke wake,  aibu iliyotapakaa Tanzania kwamba alizaa na sekretari wake wala haikumsumbua, jambo hili angeweza kulishughulikia baadaye. Mtu yeyote aliyeonekana kutaka kumsaidia mke wake,  huyo ndiye alikuwa rafiki wa kweli, maneno yaliyosemwa na daktari yaliuponya moyo wake.
“So what next?” (Kwa hiyo kinafuata nini?)
“Operation!” (Upasuaji)
“When?” (Lini?)
“Now!” (Sasa hivi)
Daktari alipomaliza kusema maneno hayo,  machela ambayo Salome alikuwa amelala juu yake ilichukuliwa na kuanza kusukumwa kuelekea chumba cha upasuaji huku madaktari,  Gilbert  pamoja na Davis wakifuata nyuma. Kichwani mwakeGilbert aliendelea kuitafakari hali ya kujiamini ambayo Muneer aliionyesha, ghafla akajikuta akihisi mke wake angefia chumba cha upasuaji, asingemwona tena, bila kutarajia akaanza kulia.
“Mbona unalia tena?” Davis alimuuliza.
“Mara nyingi watu wanaongea kwa kujiamini kama Dk. Muneer huwa wanafanya makosa mengi maishani mwao, nahisi Salome sitamwona tena!”
“Sio hivyo, Gilbert sikiliza rafiki yangu, kuna wakati unapaswa kumwamini Mungu!”
“Najua!”
“Basi leo fanya hivyo!”
“Sawa! Naacha kila kitu mikononi mwa Mungu”
***
Kwa masaa saba walibaki nje ya chumba cha upasuaji, muda wote huo kama Gilbert alikuwa halii basi alikuwa akisali kumkumbusha Mungu juu ya kumlinda mke wake   kwenye kitanda cha upasuaji, alimtaka yeye Mungu ndiye awe daktari mkuu ili mke wake aweze kufanyiwa upasuaji na kutoka salama. Aliyatamka maneno hayo ndani ya moyo wake kwa imani kubwa na kujikuta akiwa tayari kwa lolote ambalo lingetokea. Machela nyingi zilizobeba wagonjwa zilitoka ndani ya chumba hicho cha upasuaji kikubwa kuliko  vyote alivyowahi kuviona, kila machela iliyopita alinyanyuka kwenda kuiangalia na kukuta hakuwa Salome.

Saa  sita na dakika  thelathini mchana, mlango ulifunguliwa na machela nyingine ikasukumwa, Gilbert akasogea  na kuangalia  juu, hakuamini macho yake  alipokuta mtu aliyelazwa juu yake ni Salome  kichwa chake kikiwa kimefungwa kwa bendeji na kuacha uso peke yake nje.  Hapo hapo akapiga kelele kumwita Davis ambaye alikuja mbio na kushuhudia.

Wote wakafurahi kwamba Salome alikuwa hai. Kwa pamoja wakaisindikiza machela mpaka chumba cha wagonjwa mahututi. Alichokifanya Gilbert ni kupiga simu Dar es Salaam kuwataarifu juu ya maendeleo, angalau alikuwa na kitu cha kuwaeleza, mtu wa kwanza kuongea naye alikuwa ni mama yake Salome ambaye pia alifurahi kusikia taarifa hizo.
“Tunasubiri afumbue macho tu, najua itachukua muda mrefu!”
“Hakuna shida mwanangu ili mradi ni mzima”
“Sawa mama, msalimie Faith!”

Masaa  120 baadaye ikiwa ni katikati ya usiku  bado Gilbert alikuwa hajapitiwa na usingizi hata kidogo,   chumbani alikuwemo yeye peke yake, siku zote walizokaa Mumbai Davis alilazimika kulala hotelini. Macho yake yalikuwa yakimwangalia Salome kitandani, katika kitu kilichoonekana kuwa kama ndoto, alimwona amefumbua macho na kupiga kope!

Hakuamini,  ikabidi akaze macho na kuendelea kuangalia zaidi ili apate kuthibitisha alichokiona, Salome akaendelea  kupiga kope. Gilbert akapiga magoti chini na kuanza kusali akimshukuru Mungu kwa muujiza uliotendeka, alianza kuamini kwamba kweli Mungu hujibu maombi ya watu  wakimhitaji.
“Salome!Salome!” Alimwita lakini hakuitika na kujikuta akichukua simu na kupiga ofisini ndipo wauguzi  na daktari wakaja wakikimbia na kukuta kweli amefumbua macho na alikuwa akitabasamu.
“I thank God!” (Namshukuru Mungu) ndio maneno pekee aliyoweza kuyasema Gilbert akibubujikwa na machozi ya furaha.
Hivyo ndivyo ilivyotokea, baadaye wauguzi wakaondoka na kuwaacha Gilbert na Salome chumbani, muda wote alikuwa akimwita ili wapate kuongea, alitamani sana kusikia sauti yake lakini Salome hakusema chochote. Kwa muda wa siku tatu aliendelea hivyo, fahamu zake zikawa zimerejea lakini hakusema chochote na Gilbert, mwisho katika hali ya kushangaza kabisa alianza kulia na kupiga kelele.
“Gilbert! Gilbert! Njoo unisaidie mume wangu, jambazi ameingia chumbani, anataka kuniua!”   Salome aliongea kwa sauti ya juu,  Gilbert akasogea karibu zaidi akiamini alikuwa amemtambua.
“Tokaaaaa!  Toka jambazi, unataka kuniua kwa sababu mume wangu hayupo?”
“SALOME! MIMI NDIYE GILBERT!”
“Gilbert sio mbaya hivi,  toka jambazi wewe!” alizidi kupiga kelele Salome, wauguzi na daktari wakafika na kuuliza kilichotokea,  Gilbert alipowasimulia waliamua kumchoma Salome sindano ya usingizi, wakidai kulia kungeweza kusababisha mshipa kwenye ubongo wake ipasuke tena, alipozinduka masaa manne baadaye aliendelea kulia akimtaka mwanaume aliyekuwa chumbani mwake aondolewe, ilivyoonekana hakujua hata alipokuwa ni wapi.
Maisha yakawa  ya vidonge vya usingizi na alipozinduka, Salome hakuacha kulia akilalamikia kuwemo kwa mwanaume asiyemfahamu ndani ya chumba alicholala.  Wauguzi na madaktari  walijitahidi kadri ya uwezo wao   kumkumbusha  kwamba Gilbert alikuwa ni nani  kwake lakini  hakuna hata chembe ndogo ya kumbukumbu iliyomwingia kichwani mwake,  aliendelea kulia na kupiga kelele na kudai Gilbert aondolewe.
“Mimi mume wako Salome!”
“Sina mume mwenye sura mbaya kama yako, toka chumbani kwangu, sijawahi kuolewa!”
“Salome umekuwaje?”
“Sijawa kitu, nipishe ukiendelea kung’ang’ania humu ndani ipo siku nitakuua!”
“Ni bora uniue mke wangu, nakupenda Salome,  yote yaliyotokea huko nyuma kati yangu na Tecla ni uongo mtupu, naomba unisamehe, nipo tayari kufa lakini nisitoke humu chumbani!” Gilbert aliongea akiwa amepiga magoti chini, kichwani mwake alifikiri labda Salome alikuwa akimkana kwa sababu ya chuki ya mambo yaliyotokea Dar es Salaam kabla hawajaondoka kwenda India.
“Tecla ndio nani?”
“Si yule aliyedai nimempa mimba!”
“Unaongea kitu gani wewe mwanaume? Ndio maana nasema sikujui, inawezekana umechanganya!”
“Salome!”
“Mimi sio Salome!”
“Wewe ni mama wa mtoto wangu Faith!”
“Faith ndio nani?” Salome alizidi kuuliza maswali yaliyomchanganya akili Gilbert,  akaanza kuhisi kulikuwa na tatizo kubwa, isingewezekana hata kidogo mke wake amemsahau mpaka mwanae wa kuzaa.

Salome aliendelea kulia huku Gilbert akimbembeleza, macho yake yalionyesha woga wa ajabu,  alionekana kuogopa hata kuyafumba kwa fikra kwamba angeweza kuuawa, hilo lilijionyesha waziwazi usoni mwake. Gilbert hakukoma wala kukata tamaa, alikuwa mke wake aliyempenda, hata kama kingetokea kitu gani ilikuwa ni lazima awe pamoja naye,  alifanyiwa mambo yote kwa kuonyeshwa kwamba alikuwa hatakiwi,  likiwemo la kutemewa mate usoni lakini bado aliendelea kukaa kando ya kitanda cha mke wake,  akiamini kilichokuwa kikimsumbua ni ugonjwa ambao baada ya muda ungeondoka na angerejea katika hali ya kawaida.

Haikuwa hivyo, ugomvi uliendelea ndani ya chumba chao  Salome akidai angekuwa na mikono inayofanya kazi lazima angempiga  mwanaume aliyekuwa chumbani mpaka afe,  alishangaa ni kwanini mikono yake ilikuwa hainyanyuki,  yalikuwa ni maneno ya kutisha lakini Gilbert aliyapuuza  na kuendelea kumtunza mkewe! Siku zikazidi kusonga  huku fahamu za Salome zikiwa vile vile, hakumkumbuka kabisa Gilbert  wala maisha yake ya nyuma,  wala hakuwahi kutambua alikuwa na  mtoto aliyemwacha Dar es Salaam, yeye akiwa India kwa  matibabu. 

Kila siku wataalam wa mazoezi walimfuata chumbani kwake na kumfanyia kile ambacho kwa kiingereza kiliitwa Physiotherapy,  wakitumia vifaa vya kawaida na vya umeme kushtua misuli yake  iliyopooza. Kulikuwa na matumaini kwamba siku moja Salome hata kama asingeweza kutembea kabisa,  basi angalau angeweza kuwa na uwezo wa kutumia mikono yake kusukuma  kiti cha matairi manne. Gilbert hakuliamini kabisa jambo hilo,  alishakata tamaa kuhusu mke wake kutembea wala kutumia mikono,  haikumuumiza akili tena, cha muhimu kwake ilikuwa ni Salome kuwa hai.

“Ipo siku atatembea, kama si kutembea   basi atatumia mikono,  hivi sasa anaendelea vizuri, baadhi ya misuli imeashanza kushtuka,  nafikiri tukiendelea kwa miezi sita atakuwa na nafuu sana!” daktari bingwa  wa mazoezi ya viungo aliyekuwa akimtibu Salome alimwambia Gilbert asubuhi moja.

“Kweli? Salome atembee?”
“Kabisa! Hizi mashine si mchezo,  kuna watu walikuwa na hali mbaya kuliko yeye lakini leo hii wanatumia miili yao”
“Nitashukuru Mungu sana  lakini jambo la muhimu kwangu ni yeye kuwa hai na kumbukumbu zake kurejea, inanisikitisha sana ninapomwona mke wangu tuliyependana amenisahau, si jambo rahisi kuamini!”
“Ndivyo  Amnesia ilivyo,  usiwe na shaka ipo siku atakukumbuka tu!”
“Lini?”

“Itafika tu hiyo siku,  kila kitu kitarejea katika hali ya kawaida, itakuwa kama vile anaota ndoto,  jaribu kuwa unamwonyesha vitu mbalimbali vitakavyomkumbusha mambo ya zamani,  kama vile picha au mkirejea nyumbani utakuwa unamtembeza sehemu mbalimbali za maeneo mnayoishi,  anaweza kuona kitu kikazishtua  kumbukumbu zake, lazima kuwe na namna ya kuzishtua!”
“Najitahidi kufanya hivyo lakini hanielewi,  ninamwambia juu ya mtoto wake lakini wala hakumbuki kabisa kwamba ana mtoto!”
“Atakuja kukumbuka tu!”

Miezi mitatu baadaye, tayari Salome alishaanza kuketi kwenye kiti cha matairi manne na wakati mwingine kuyasukuma matairi mwenyewe, mazoezi ya viungo yalikuwa yamefanya  kazi yake. Gilbert alifurahi mno kilichomsikitisha ni  kumbukumbu kutorejea! Bado Salome alimchukukia kupita kiasi, aliomba Mungu jambo hilo pia lipate jibu ili  inapowadia siku  ya kurudi nyumbani Tanzania, kila kitu kiwe kimekaa sawa, furaha iwe mahali pake,  jambo moja tu ndilo  liwe limebaki; kuthibitisha kwamba mtoto wa Tecla hakuwa wa kwake, bado mpaka wakati huo alihisi kuna  jambo lililokuwa limefanyika kutoa majibu ya uongo.

“Hivi kwanini wewe hutaki kutoka chumbani kwangu?”
“Wewe ni mke wangu Salome,  siwezi kukuacha!”
“Mkeo nani? Hivi kwanini hunielewi?”
“Sio rahisi kukuelewa, ni ugonjwa tu unaokusumbua!”
“Ugonjwa gani? Nani anaumwa? Ndio maana naona marafiki zako wanakuja hapa kila siku kunichezea mwili wangu, aliyekuambia naumwa nani? Ngoja sasa, nitakufundisha somo ili hapa chumbani usikae kabisa!”

Gilbert aliyapuuza maneno hayo kama ilivyotokea siku zote na kwa sababu ilikuwa ni saa sita usiku, haukupita muda mrefu sana sababu ya uchovu  akajikuta amepitiwa na usingizi na kuanza kukoroma  akimwacha Salome macho!  Kilichomzindua  usingizini ni  maumivu makali sikioni,  ilikuwa ni kama ndoto ya jinamizi lakini alipofumbua macho yake haraka na kuanza kupiga kelele akiomba msaada,  alimwona Salome,  mdomo wake ukiwa sikioni,  alikuwa amemng’ata.

Wauguzi wa zamu ya usiku walipofika walimkuta Salome  amefunika mdomo wake  kwenye sikio la mkono wa kuume wa Gilbert huku  damu nyingi zikitiririka pembeni na kumfanya awe mwekundu maeneo yote yaliyozunguka mdomo na pua,  wakajua hiyo ilikuwa ni hatari, kwa pamoja wakaanza kumsihi amwachie lakini hakufanya hivyo,  maneno aliyoyaongea hayakusikika kwa sababu  meno yake yalikuwa yamezama kwenye nyama! Gilbert alikuwa akilia na kuwaomba wauguzi wamtoe.
“Mtoeni jamani! Jamani mtoeni!” alipiga kelele Gilbert.

Wauguzi wakamkamta Salome na kujaribu kumvuta  kwa nguvu  lakini kichwa kikawa kinamfuata   huku  Gilbert  akizidi kulia  na damu  kububujika, wakaamua kumwachia na kuanza kumbembeleza  aachie kwa hiari yake lakini hakufanya hivyo,  alizidi kusaga meno na ilivyoonekana  sehemu ndogo sana ilikuwa imebaki ili sikio litoke.
Haikuwa rahisi kulinusuru sikio la Gilbert kwani walipofanikiwa kumtenganisha Salome, alikuwa nalo mdomoni, akiwa ametapakaa damu kuanzia puani mpaka kwenye kidevu. Kila mtu aliamini akili yake ilikuwa haijakaa sawa, wakamlaza chini na kumbana taya zake huku mdomo wakiupanua,  wakafanikiwa kukitoa kipande cha sikio! Bila kupoteza wakati Gilbert alianza kukimbizwa kwenda chumba cha upasuaji huku akilia kwa maumivu makali aliyokuwa nayo, mkono alioufunika sikioni haukuweza kuizuia damu kutoka. Salome akachomwa sindano ya usingizi na kulala.

Kazi iliyofanyika chumba cha upasuaji ni kulishona tena sikio la Gilbert mahali pake akiwa amepewa dawa  ya nusu kaputi,  kazi hiyo iliwezekana kwa sababu ulikuwa haujapita muda mrefu sana tangu sikio likatike. Iliwachukua madaktari muda wa saa moja na nusu tu kuikamilisha kazi hiyo, Gilbert  akarejeshwa wodini lakini si kwenye chumba cha Salome. Alibaki katika hali hiyo mpaka masaa matatu baadaye ndipo fahamu zake zikarejea na kukuta upande mmoja wa kichwa ukiwa umefunikwa na bendeji,  akakumbuka kila kitu kilichotokea lakini akawa tayari kumsamehe mke wake.
“Litapona?”
“Ndio usiwe na wasiwasi”
“Kweli?”
“Litaota?”
“Hiyo ni uhakika!”
“Hivi mke wangu amekuwaje? Amepatwa na tatizo gani?”
“Ana Amnesia, tatizo la kupoteza kumbukumbu, sio kwamba anakutania, hakukumbuki kabisa Gilbert!”
“Inawezekana kweli?”
“Hiyo ni hali ya kawaida tu”
“Itakuja kuondoka?”
“Lazima,  lakini itachukua muda, kama tulivyokwishakueleza, ikitokea ukarejea nyumbani Tanzania jaribu kuwa unamfanyia mambo ambayo zamani alikuwa akiyafanya au kumpeleka kwenye maeneo aliyozoea kutembelea, ipo siku kumbukumbu zake zitafufuka upya!”
“Nitamshukuru Mungu sana kama ikitokea Salome akarejea katika hali ya kawaida, nimejitahidi sana kadri ya uwezo wangu kuhakikisha anakuwa salama,  ni miaka mingi sijaingia kazini na ninamshukuru Mungu kwamba ninaye mtu anayeweza kusimamia kazi zangu vizuri, vinginevyo ningeweza kufilisika!”

Hakuweza kukaa mbali na mke wake,  pamoja na ajali ya kung’atwa sikio iliyojitokeza, alimpenda Salome na alisikitishwa na  yote yaliyotokea.  Jioni ya siku hiyo alikuwepo chumbani kwa Salome, alimkuta yu usingizini sababu ya dawa alizokuwa akipewa. Alikaa hapo kwa masaa mawili, Salome akazinduka na kumkuta ameketi  kando ya kitanda chake.  Macho yake yakabadilika sekunde chache tu baada ya kumwona, hasira ikapanda upya, hapo hapo akaanza kushuka kitandani tayari kwa mapambano,  kuona hivyo Gilbert alimfuata haraka na kumkamata kifuani, tukio ambalo wauguzi waliliona kutokea wodini.
“Vipi?”
“Muondoeni huyu jambazi hapa chumbani, kwanini ananifuatafuata?”
“Mimi si jambazi Salome, ni mumeo baba wa mtoto wako Faith!” aliongea akijaribu kumshawishi lakini Salome hakuwa tayari.
“Sitaki!Sitaki! sikujui, sijawahi kuzaa mtoto!”

Gilbert hakuwa na la kufanya, wauguzi wakamshauri aondoke kwenda chumbani kwake ambako alijifungia na kuanza kulia kwa uchungu,  akishindwa kabisa kuelewa nini lingekuwa suluhisho la matatizo aliyokuwa nayo. Akachukua simu yake ya mkononi na kumpigia Davis hotelini ambaye alifika wodini muda mfupi tu baadaye na kumkuta analia na sikioni akiwa na bendeji.
“Vipi tena? Umekuwaje sikio?”
“Salome! Alining’ata mpaka sikio likakatika!”
“Kwanini?”
“Kama unavyojua hanikumbuki, anadai mimi ni jambazi hataki nikae chumbani kwake,  sijui nitafanya nini nimekuita rafiki yangu unishauri!”
“Aisee! Hali hii imefikia pabaya!”
“Kabisa!”
“Madaktari wanasemaje?”
“Kama wanavyodai siku zote, kwamba tutakapofika nyumbani baada ya muda usiojulikana fahamu zake zinaweza kurejea!”
“Basi tuvumilie,  huna jinsi rafiki yangu!”
“Nipo tayari lakini inaiuma sana!”

Davis hakuondoka chumbani, alilazimika kulala wodini akimfariji rafiki yake na asubuhi ya siku iliyofuata wote waliondoka kwenda chumbani kwa Salome ambako aliwafukuza kabla hawajaingia. Kwenye korido wakakutana na daktari aliyekuwa akimtibu Salome, akawaita ofisini kwake kwa ajili ya mazungumzo. Alichokiongea kiliwapa faraja kwamba Salome alikuwa akiendelea vizuri na kwa jinsi upasuaji ulivyofanyika kwa mafanikio,  hapakuwa na sababu ya kuwa na wasiwasi tena,  mwisho wa siku angepona na kumbukumbu zake zote zingerejea kama kawaida.
“Kwa hiyo nawashauri  kama kuna uwezekano mrejee nyumbani ambako kumbukumbu zake zitaendelea kurejea taratibu, tatizo hili litachukua muda mrefu kidogo, mnaweza kukaa hapa India kwa muda hata wa miaka miwili mpaka mitatu bila kumbukumbu kukaa sawa,  kwa maoni yangu mrejee Tanzania!”
“Hakuna tatizo daktari, tuko tayari  kufanya hivyo wasiwasi wetu ni  tutamsafirishaje mtu  asiyetukumbuka?”
“Hilo ni jambo dogo,  tutachukua kibali cha kusafirisha mgonjwa na tutawapa muuguzi mtakayesafiri naye mpaka Tanzania, lakini kabla ya kupanda kwenye ndege atachomwa sindano ya usingizi”
“Itakuwa vyema mkifanya hivyo!” alijibu Davis akimwangalia Gilbert usoni, wote walionekana kufurahia uamuzi huo.

Siku hiyo hiyo walipotoka ofisini kwa daktari taratibu za safari zilianza, pia wakawasiliana na  ndugu zao Tanzania  na kuwajulisha juu ya ruhusa yao kurudi  nyumbani,  kila mtu alifurahi kusikia hivyo, wakakaa mkao wa kusubiri. Tiketi za safari zilikuwa tayari asubuhi siku iliyofuata, uongozi wa hospitali nao ulikuwa umeshughulikia vibali vyote vya kuruhusiwa kumpandisha mgonjwa ndani ya ndege akiwa usingizini.  Hakuna kitu ambacho Gilbert alikitamani kwa wakati huo kama kufika nyumbani ambako angeuchangia mzigo wa maumivu aliokuwa nao na  watu wengine  ni kweli  sikio lake lilikuwa likiuma  sana lakini aliamini lingepona akiwa Tanzania ambako  kwa Salome kukutana na mtoto wake lazima kumbukumbu zake zingerejea.

Saa sita usiku  walipanda ndege ya shirika la ndege la Kenya na kuruka moja kwa moja hadi Nairobi ambako walifika  asubuhi siku iliyofuata, Salome akiwa bado yu usingizini na dawa ikiongezwa  na muuguzi  kila ilipopungua, wakiwa hapo  Gilbert na Davis walipiga simu  Dar es Salaam na kuwataarifu  kwamba wangekuwa Dar es Salaam ndani ya masaa mawili,  taarifa zikasambaa na watu wote kuanzia ofisini WorldCom,  mitaani ambako Gilbert na  Salome walikuwa maarufu mpaka nyumbani kwa Gilbert, waliondoka na kuelekea Uwanja wa ndege kusubiri, baadhi wakiwa na maua kwa ajili ya kuwakaribisha mashujaa nyumbani.

Kama walivyokuwa wameongea, ndani ya muda huo huo ndege ilitua kwenye uwanja wa J.K Nyerere, Salome akashushwa akiwa juu ya machela na taratibu zote zilipokamilika alitolewa hadi nje ya uwanja ambako makundi ya watu walikuwepo kusubiri,  Gilbert alilia machozi baada ya kuuona wingi wa watu, alipomwona mwanae Faith na mama mkwe wake ndio machozi yalizidi kumtoka. Ikabidi achukuliwe na kupelekwa moja kwa moja ndani ya gari, hapo ndipo safari kuelekea  nyumbani ikaanza ambako Salome aliendelea kuwa usingizini huku watu wengi wakiwa wamefurika wakisubiri kumsalimia.

Baada ya kusubiri kwa takribani masaa matatu, dawa za usingizi ikiwa imesitishwa, hatimaye Salome akafumbua macho yake na kujikuta amelala chumbani, kando akiwepo mwanamke mzee ambaye hakumfahamu, mkononi akiwa amembeba mtoto mdogo, akakodoa macho  yake kuwaangalia kama vile alikuwa haamini alichokuwa akikiona.
“Mwanangu Salome, namshukuru Mungu umerudi, kweli Mungu ana nguvu!’
“Mwanao nani? Wewe bibi umechanganyikiwa? Ninyi ndio wale wale majambazi ninaowang’ata masikio, hebu ondoka hapa na hicho kimsukule chako mkononi, nitawapiga mimi, muulizeni mwenzenu nimemng’ata sikio! Au hamtaki kutoka?” aliuliza mama yake akiwa haamini alichokuwa akikisika.

Sekunde chache baadaye Gilbert  ambaye wakati  yote hayo yakitokea alikuwa sebuleni akiongea na muuguzi juu ya safari yake kurudi India,  alisikia kelele za mama mkwe wake pamoja na Faith wakilia chumbani na kuomba msaada akanyanyuka haraka na kuanza kukimbia kwenda chumbani muuguzi, Davis na marafiki wengine kadhaa wakimfuata nyuma.
Walipoingia chumbani walimkuta mama mkwe akinyang’anyana mtoto na Salome ambaye uso wake ulikuwa umekunjwa na kuvimba kwa sababu ya hasira,  Gilbert akaruka na kumkamata Salome mikono yake  yote miwili akaibana ndipo  Davis akamtoa mtoto mikononi,  wote wakaanza kuuliza ni kitu gani kilikuwa kimetokea na mama mkwe akawasimulia namna Salome alivyomchukua mtoto na kuanza kumfunika  puan na na mto wa kulalia  ili ashindwe kupumua na kufa,  wote wakashtuka.

“Salome kwanini unataka kufanya hivyo? Umesahau kwamba huyo ni mtoto wako?”
“Muondoeni huyo nyau na ninyi sitaki kuwaona hapa chumbani!” Alizidi kufoka.
“Gilbert bado Salome hajawa na kumbukumbu vizuri, ni lazima muwe mnakaa karibu na msijaribu kumwacha na mtoto, anaweza kumuua!”
“Hatutafanya hivyo tena!”

Salome aliendelea kulia, akidai  watu wote waondoke chumbani,  hakuwa akitania ni kweli hakuwa na kumbukumbu hata kidogo kichwani mwake,  wala hakujitambua yeye ni nani. Alichokifanya muuguzi ni kumdunga sindano nyingine ya usingizi,  dakika chache baadaye akalala ili apumzike na akili yake itulie. Hayo ndiyo yakawa maisha yake kila siku kwa muda wa wiki nzima,  sindano, usingizi,  sindano! Akilishwa chakula kupitia mpira wa puani.

Wiki moja  baadaye muuguzi aliamua kusimamisha sindano  za usingizi  ili apate kuangalia  kama Salome angeendelea na hali ya ukorofi,  kulikuwa na mabadiliko makubwa sana,  alikuwa ametulia kuliko siku nyingine zote na wakati mwingine alionyesha tabasamu lakini hakuongea maneno mengi.  Kila mmoja akaanza kuamini hatimaye sasa alikuwa ameanza kurejea katika hali ya kawaida, kwa Gilbert na familia nzima hili  ni lilikuwa jambo la kufurahia mno. Muuguzi akawashauri waanze kuwa wanamfanyia vitu ambavyo tangu zamani alikuwa akivifanya, hivyo ndivyo vingezishtua kumbukumbu zake.
Gilbert akaanzisha utaratibu wa kuwa anambeba kwenye gari na kutembea naye mjini akimwonyesha sehemu mbalimbali, bado hakukumbuka na mara nyingi aliuliza swali la hapa ni wapi? Hata katika sehemu ambazo alizoea kwenda na migahawa ambayo waliingia na kula pamoja. Hakuna sehemu  aliyopenda kula chakula cha usiku kama kwenye mgahawa wa Kihindi wa Anghit uliopo maeneo ya  Victoria,  Gilbert aliamua kumpeleka hapo kuona kama angekumbuka,  pia haikufanya kazi,  wafanyakazi wa mgahawa huo siku zote walimzoea na hata kutaniania naye lakini siku hiyo walishangaa kuona amekuwa mkimya  kupita kiasi, hata wao hakuwakumbuka na mgahawa hakuutambua.
“Wewe, hapa ni India? Mbona wahindi wengi namna hii?” alimuuliza Gilbert, siku zote hivyo ndivyo alivyomwita, hakulikumbuka jina lake kabisa.
“Hapana ni Dar es Salaam”
“Dar es Salaam ndio wapi?”
“Nyumbani kwetu”
“Wewe unaishi Dar es Salaam?”
“Ndio! Unaitwa nani?”
“Gilbert!”
Gilbert! Gilbert! Gilbert!  Jina  hilo lilirudia mara nyingi kichwani mwa Salome akijaribu kulikumbuka kama aliwahi kukutana na mtu yeyote mwenye jina hilo, kumbukumbu zikawa zinakuja na kupotea,  ni kweli alimfahamu mtu aliyeitwa hivyo lakini wapi na alikuwa na nani yake haikumwingia. Mpaka wanaondoka mgahawani alikuwa bado akizungusha akili yake kulifikiria jina hilo. Walipofika nyumbani walioga na baadaye kuingia kitandani kulala, bado aliendelea kufikiria bila kupata jibu. Asubuhi  ya siku iliyofuata alimgusa Gilbert  begani.
“Uliniambia unaitwa nani kweli?”
“Gilbert!”
“Mimi?”
“Salome!”
“Mh!” akaguna.
Salome! Salome! Salome!   Akalitamka jina hilo kimoyo moyo huku akifikiria kama hilo lilikuwa jina lake kweli,  hakupata jibu na alipojaribu kukumbuka jina lake alilolifahamu, pia   halikumwijia kichwani, akaamua kuachana nalo. Alipotupa macho yake  kwenye kitanda kilichokuwa pembeni akamwona mtoto amelala juu yake.
“Na yule?”
“Mtoto”
“Wa nani?”
“Wa kwako, Salome hukumbuki?”
“Sina mtoto!”
“Humkumbuki Faith?”
“Ndio nani?”
“Mtoto wetu”
“Mtoto wenu na nani?”

Halikuwa  jambo rahisi kuliamini, kwa mtu asiyekuwa na elimu ya mambo ya afya ilikuwa ni rahisi sana kuhisi kwamba Salome alikuwa akijifanyisha. Lakini huo ndio ulikuwa ukweli, kumbukumbu zote zilikuwa zimefutika,  kila kitu ilikuwa ni lazima kiingie upya, hali hiyo ilimsikitisha sana Gilbert.

Asubuhi  hiyo hiyo wakati wa kifungua kinywa  muuguzi kutoka India Anita Bhanji, alimtaarifu Gilbert kwamba kwa sababu hali ya mgonjwa ilikuwa ikiendelea vizuri,  ilikuwa ni bora yeye  arudi India siku hiyo hiyo kwani familia yake ilikuwa ikimhitaji, Gilbert hakuwa na sababu yoyote ya kumzuia ili mradi kumbukumbu za Salome zilikuwa zimeanza kurejea, akamkubalia na wote wawili ilipofika saa tatu na nusu wakaondoka nyumbani kwenda kufuatilia tiketi.
“Tutakukumbuka!”
“Hata mimi, niliwazoea sana”
“Ahsante kwa kila kitu, umekuwa mwema sana Anita! Nitakupa dola elfu tano kama shukrani”
“Hiyo sio rushwa?”
“Hapana! Hata mimi rushwa huwa sitoi”
“Huwa sipendi kupokea fedha kutoka kwa ndugu wa mgonjwa hata kama ingeitwa shukrani, huo ndio utaratibu niliojiwekea!” Anita aliongea.
Gilbert hakuongea kitu, alichofanya baada ya kuwa amepata tiketi ni kuingia kwenye duka la sonara na kununua hereni, mikufu pamoja na pete za dhahabu hizo ndio akamkabidhi Anita kama zawadi,  hakuwa na tatizo kwenye kupokea vitu hivyo ili mradi hazikuwa fedha taslimu. Wakarejea nyumbani ambako maandalizi ya safari yaliendelea,  Anita aliumia moyoni kwamba alikuwa akimwacha mgonjwa wake lakini hakuwa na jinsi,  Salome wala hakujali kwani hakuuona umuhimu wake. Saa tisa alasiri,  Salome akiwa ameketi kando ya bwawa la kuogelea, mkononi akiwa amembeba Faith, zoezi ambalo muuguzi alisisitiza wawe wanalifanya wakiamini pengine lingesaidia kurejesha kumbukumbu zake, alimsogelea na kumuaga kisha kumbusu usoni tayari kwa safari ya kwenda uwanja wa ndege.
“Mama acha nimsindikize! Nitarejea baada ya saa moja na nusu” Gilbert aliongea na mama mkwe akamruhusu.
Alichokifanya Gilbert ni kusogea karibu na mtoto wake na kumbusu usoni,  akafanya hivyo pia kwa Salome ambaye alionyesha uso wake siku hiyo ulikuwa tofauti na siku nyingine zote, hata hivyo akamuaga na kuondoka mpaka kwenye gari, saa yake ya mkononi ilisomeka saa tisa na dakika tano, alitegemea kuwa amerejea nyumbani saa kumi na dakika thelathini na tano, akaiwasha gari na akaondoka kwa kasi mpaka uwanja wa ndege na kumshusha Anita ambaye aliingia ndani ya uwanja kwa kufanya taratibu za safari, ndege ilitegemewa kuruka saa kumi na mbili kamili kuelekea Nairobi na baadaye Mumbai, India.
***
“Hili toto sijui la nani? Silipendi, wao wananilazimisha kulibeba, macho yake kama paka! Ngoja nije nilitupie ndani ya  maji life” aliwaza Salome mama yake akiwa amekaa kando,  muda huo huo simu ikasikika ikilia chumbani,  mama akanyanyuka na kuanza kukimbia kwenda kuichukua, ilikuwa ni tabia ya Gilbert kupiga simu akiwa njiani kurejea nyumbani kuulizia mahitaji yaliyohitajika,  alipopokea alikuwa ni Gilbert.
“Mama tuna mayai ya kutosha?”
“Hapana baba!”
“Nini kingine hakipo?”
“Acha niangalie kwenye friji!” alijibu na kuzama jikoni.
“Dubwiii!” huo ndio mlio uliosikika kwenye bwawa la kuogelea na maji yakaruka, Salome akaanza kuchekelea namna mtoto alivyohangaika majini.
Dakika tano baadaye, mama yake Salome alisikia kicheko cha ajabu kutoka nje akiwa jikoni. Hakukitilia maanani sana sababu mara nyingi  Salome alicheka peke yake kama mtu aliyechanganyikiwa, akaendelea na kazi ya kuangalia mahitaji ndani ya friji huku akiwasiliana Gilbert aliyekuwa dukani na kumtajia kila kitu kilichopungua ndani ya nyumba, alipomaliza simu ilikatika na akaanza kutembea haraka kwenda nje, akijilaumu moyoni mwake ni kwanini alikuwa amemwacha Salome na mtoto kipindi kirefu namna ile.
“Mh!” aliguna baada ya kumkuta Salome peke yake bila mtoto mkononi huku akicheka kwa sauti ya juu.
“Vipi Salome?”
“Haaa!Haaa! Haaaa!” badala ya kujibu  Salome aliendelea kucheka.
“Mtoto yuko wapi?”
“Haaa!Haaa!Haaa!”

Mshtuko uliompata mama yake haukuwa na maelezo, akaanza kukimbia huku na kule bustanini akimtafuta mtoto bila mafanikio,  kila baada ya muda mfupi alirudi tena kwa Salome na kumuuliza mahali Faith alipokuwa, hapakuwa na jibu zaidi ya kicheko! Wazo la kuangalia kwenye bwawa la kuogelea hakuwa nalo,   akakimbia  hadi ndani ambako  alianza kupekua vyumba vyote, chini ya makochi,  ndani ya kabati  akimtafuta mtoto bila mafanikio, aliposikia gari likiunguruma nje ya nyumba alitoka mbio akiamini  huyo alikuwa ni Gilbert, hivyo ndivyo ilivyokuwa, alimkuta akishusha mizigo garini.
“Vipi mama mbona  unatoka jasho sana?”
“Mtoto!”
“Kawaje?”
“Simwoni”
“Humwoni?”
“Ndio”
“Kwani alikuwa wapi?”
“Nilimwacha na Salome ulipopiga simu lakini niliporudi nilimkuta hayupo!”
“Mungu wangu, ulimwacha na Salome? Mama ulisahau kabisa kwamba Salome ni mgonjwa?”
“Nisamehe mwanangu, niliposikia simu inaita nilichanganyikiwa kabisa nikajikuta nimepitiwa!”
“Sasa mtoto yuko wapi?”
“Kusema kweli mwanangu nimemwangalia kila mahali bila mafanikio, sielewi kilichotokea na haiwezekani kwamba mtu ameingia humu ndani ya ngome akamchukua!”
“Dah! Sasa tufanyeje?”Aliuliza Gilbert na kuiacha kazi ya kushusha mizigo kwenye gari, yeye na mama mkwe wake wakaanza kuzunguka huku na kule ndani ya nyumba na baadaye kuhamia nje wakipekua kila kona  bustanini lakini hawakumwona, Salome alikuwa bado akicheka kwa sauti ya juu.
“Sasa atakuwa wapi?” Gilbert aliuliza.
“Hata mimi sielewi!”
“Acha nipige simu polisi, angalau waje watusaidie kumtafuta” alisema Gilbert akichukua simu yake ya mkononi na kupiga namba 911, polisi walipopokea aliwataarifu na kuwaelekeza mahali nyumba yake ilipokuwa, ndani ya muda wa dakika ishirini tayari gari la polisi lilipiga honi kwenye lango kuu la kuingilia, Gilbert akatulia kusubiri mlinzi awafungulie mlango lakini hakujitokeza, ikabidi yeye mwenyewe ndiye akimbie hadi langoni na kufungua akisonya  kwa hasira kwa sababu mlinzi alikuwa haonekani.
“Mmempata?” Kiongozi wa msafara wa maaskari aliuliza.
“Hapana!”
“Ilikuwaje?”

Gilbert akasimulia alivyoondoka nyumbani kwenda uwanja wa ndege akimwacha mama mkwe wake pamoja na mkewe mgonjwa akiwa amembeba mtoto miguuni, akaeleza pia alivyompigia simu mama mkwe, kisha alivyofika nyumbani na kukuta mtoto haonekani ndipo akaamua kuwapigia simu polisi. Maaskari wote waligeuza macho yao kumwangalia mama mkwe aliyeonekana kuwa na wasiwasi mwingi.
“Mama mtoto yuko wapi?”
“Watoto wangu mimi sijui, niliingia ndani nikamwacha hapa na mama yake, niliporudi nje sikumkuta, mama yake peke yake ndiye alikuwa hapa akicheka kama anavyocheka hivi sasa, sijui yuko wapi mjukuu wangu!” alijieleza mama yake Salome na maaskari wakamwacha na kumsogelea Salome.
“Yuko wapi mtoto?”
“Haaa!Haaa!Haaa!” alicheka kwa sauti ya chini akisonta kidole kwenye bwawa la maji, wote wakageuka kuangalia huko, hakuna kilichoonekana juu ya maji. Salome akazidi kucheka kama vile alikuwa akiwaona wote ni wajinga.

****
Maelfu ya watu walikuwa wamekusanyika kwenye uwanja wa Jangwani wakimsikiliza Mhubiri wa Kimataifa kutoka visiwa vya Caribean,  mchungaji mwanamke Mary Raphael. Mahubiri yake yalikuwa yakiwagusa watu wengi kuliko wahubiri wengine waliowahi kuhubiri kwenye viwanja hivyo, viwete walitembea,  vipofu waliona, viziwi walisikia!

Hata wagonjwa wa  Ukimwi walinyanyuka na kukimbia katika jina la Yesu. Sifa hizi zilisambaa jiji zima la Dar es Salaam, kiasi kwamba maelfu ya watu wakawa wanamiminika kwenda kwenye viwanja hivi kila jioni na kuyatoa maisha yao kwa Yesu Kristo, wakiwa wamekubali kuzaliwa mara ya pili,  hata watu ambao walikuwa wabishi kila lilipokuja suala la Ukristo walibadili njia zao sababu ya mahubiri ya mwanamke huyo,  alikuwa na nguvu za ajabu ambazo Tanzania haikuwahi kukutana nazo.
“Wangapi wako tayari kuyatoa maisha yao kwa Kristo?” Hilo ndilo lilikuwa swali lake kila alipomaliza kuhubiri jioni na mikono ya watu ilinyanyuka juu, wote wakatakiwa kutembea kuelekea jukwaani ambako wangefanyiwa  maombi maalum,  wakati wakitembea wimbo  wa kugusa roho ulisikika;
Narudi nyumbani,
Kutoka mbali,
Bwana unihurumie,
Sasa narudi,
Narudiiiii!
Wimbo huo uliendelea kuimbwa huku makundi ya watu wakitembea kwenda mbele wakiwa wameamua kuyatoa maisha yao kwa Kristo na kuacha dhambi zao zote, mtu mmoja  aliyekuwa amesimama nyuma kabisa alikuwa njia panda ya mawazo, akijiuliza aende au asiende! Moyoni mwake alikuwa akiona aibu sababu alikuwa mtu anayejulikana na watu wengi jijini Dar es Salaam, akawa ameamua kubaki hapo hapo ili  kama wakati wa kuombewa ukifika anyanyue mkono wake juu badala ya kujitokeza na kupigwa picha  za video.
“Najua yupo mtu kati yenu anasitasita, anaogopa kuja mbele kwa kuona aibu, popote ulipo tafadhali chukua hatua hii ndio nafasi yako!” mchungaji Mary alitamka kutoka  jukwaani.

Maneno  hayo yakafika moja kwa moja masikioni mwa mzee Jamal Ngowi na kujikuta akitembea moja kwa moja kuelekea mbele bila  kuona aibu tena, akajichanganya katika kundi la watu waliomtangulia, wakaongozwa sala ya toba na baadaye kuombwa waendelee kwenda kanisani,  maombi maalum yakafanyika kwa ajili yao na kuruhusiwa kurudi sehemu walizokuwa, muda wote machozi yalikuwa yakimtoka Ngowi,  alijutia sana maisha yake ya nyuma,  alikuwa amefanya vitendo vingi viovu ambavyo hakika havikumfurahisha Mungu.

***
Tecla alikuwa amekaa ndani ya nyumba yake akiwa amembeba mtoto wake mikononi, macho yake  yote yameangalia kwenye luninga, kilikuwa ni kipindi cha taarifa ya habari ya ITV, mtangazaji Godwin Gondwe akisoma habari juu ya  Akaunti ya madeni ya nje (EPA), kwa muda mrefu alikuwa amesikia juu ya neno hilo EPA  lakini hata siku moja hakuwa amelitilia maanani, akaketi vizuri ili apate kujifunza. Hakuweza hata kusikia mambo mengi mlango wa  mbele ya nyumba yake ukagongwa, akanyanyuka kwenda kuufungua.
“Shikamoo dada” Ilikuwa ni sauti ya mlinzi wake.
“Marahaba vipi?”
“Kuna mtu hapo nje anaitwa Ngowi, nimruhusu?”
“Ngowi gani?”
“Anasema yeye ni mfanyakazi wa maabara hospitali ya Muhimbili!”
“Ahaaaa! Namfahamu, mwambie aingie!”
“Sawa dada!” Mlinzi akaitikia na kutembea hadi mlangoni ambako alimfungulia Ngowi,  akaingia na kunyoosha moja kwa moja kwenye mlango mkubwa wa nyumba na kukaribishwa ndani.
“Bwana Yesu asifiwe dada?”
“Amen, ninyi  nao kwa kukejeli dini za wengine? Umeokoka lini Ngowi?”
“Leo!”
“Acha utani bwana,  sema shida yako Ngowi, una shida na fedha?”
“Hapana, nimekuletea fedha yako!’
“Ipi? Mbona mimi sikudai?”
“Sio kwamba unanidai, nimeamua kurudi milioni mbili ulizonipa wakati ule ili nidanganye kwenye majibu ya DNA, nimempokea Kristo,  sitaki kuwa na dhambi na ni lazima nimtafute Gilbert hata kama ni nyumbani kwake nimwombe msamaha kwa jambo nililomtendea, nilimfedhesha sana!”
“Ngowi! Umechanganyikiwa?”
“Sijachanganyikiwa hata kidogo, nakueleza ukweli!”Ngowi alisema maneno hayo na kunyanyuka kumkabidhi Tecla fedha zake, hakuwa tayari kuzipokea, ikabidi Ngowi aziweke juu ya meza na kuaga.
Je, nini kitatokea? Fuatilia Siku ya keshoooooooooooo

No comments

Powered by Blogger.