ad

ad

She is too young to die -19

Hawa ni marafiki zake Amanda na Christine,  wameingia wakiwa na magazeti yaliyaondika habari juu ya Gilbert kumpa mimba sekretari wake, hawajui kwamba jambo hilo ni siri,  wamekwenda kumpa rafiki yao pole.

Je, nini kitatokea wodini alikolazwa Gilbert na nyumbani kwake ambako wageni hawa kuna uwezekano mkubwa wakavujisha siri? SONGA NAYO…


Baada ya Tecla kuondoka, Gilbert alibaki akilia kwa uchungu, tayari mama mkwe wake alishaelewa kilichoendelea,  kwake ilikuwa aibu kubwa! Ni heri angekuwa amelifanya jambo  lililodaiwa, hiyo ingepunguza maumivu zaidi lakini sasa hakuwa na hatia,  moyoni mwake aliamini hakuna hata siku moja amewahi kukutana na Tecla kimwili mpaka kupelekea msichana huyo apate mimba,  angekuwa mwanasiasa angehisi kuna watu wanamchafua lakini haikuwa hivyo, alikuwa ni mtu aliyeishi na kila mtu vizuri hata wale alioshindana nao kibiashara,  iweje leo Tecla ampakazie jambo zito kiasi hicho ambalo lingeweza kuhatarisha hata maisha ya mke wake ambaye siku zote hakutakiwa kusikia habari mbaya? Gilbert alijiuliza moyoni mwake bila kupata majibu. Akawa na hasira nyingi dhidi ya Tecla.
“Pole baba!” mama mkwe wake alimwambia.
“Ndio dunia mama yangu,  msichana huyu amenionea sana, sijawahi kufanya anayoyadai,  sijui ni kwa sababu gani amenishupalia kiasi hiki, wakati mimi bado naumwa, kwa sababu yake nimenusurika  kifo kwanini asiniache peke yangu?”
“Usijali baba,  ukubwa ni jalala! Vumilia mwanangu yote yatapita, hakuna ambalo huja kudumu milele”
“Ahsante mama lakini sitaki kabisa Salome ajue habari hizi,  nisaidie mama,  huko nyumbani unapokaa naye hakikisha hasikilizi redio wala kusoma magazeti, hata marafiki zake wasimtembelee,  wakija waeleze hayupo hasa wawili waitwao Amanda na Christine, ni waongo sana lazima tu watafika kumpelekea umbea, fanya hivyo mama, nakuomba mimi mwanao! Hii itasaidia sana kuokoa ndoa na maisha ya  mke wangu mpendwa Salome, nakuhakikishia  mzazi wangu, sijawahi kukutana na huyu binti kimwili hata siku moja,  hiyo mimba inatoka wapi?” aliongea Gilbert kwa sauti ya juu, wauguzi waliokuwa bado wako chumbani walimwonea huruma,  macho yake yaliwakilisha kilichokuwemo kifuani.
“Nitafanya hivyo baba,  sitaki kukaa sana, acha nikimbie nyumbani maana mgonjwa nimnemwacha peke yake!”
“Ahsante mzazi wangu, nakushukuru sana kwa msaada wako, msalimie sana Salome ila usimwambie nilipata ajali,  atakufa!”
“Sitafanya hivyo, jambo hilo ni siri tumekubaliana na rafiki zako wengine tusimwambie kwa hivi sasa!”

Baada ya kuagana mama yake Salome alitoka hadi nje ambako aliingia ndani ya gari la  kampuni ya WorldCom na kupelekwa moja kwa moja hadi nyumbani, akashuka na kutembea  haraka kuingia ndani, mlangoni aliona jozi mbili za viatu ambazo hakuzifahamu,  hiyo ilimaanisha kwamba kulikuwa na wageni ndani ya nyumba. Alipowakosa sebuleni wasiwasi ulimwingia akaamua kumfuata msichana wa kazi jikoni.
“Viatu vilivyoko nje ni vya akina nani binti?”
“Rafiki zake na mama”
“Nani na nani?”
“Amanda na Chrstine”
Majina hayo mawili yakawasha taa nyekundu kichwani mwake, alikuwa ameyasikia muda mfupi tu kutoka kwa  Gilbert  wodini, mfanyakazi wa ndani akaenda mbele zaidi kwa kumwambia kwamba wageni hao walikuwepo chumbani wakiongea na mama. Taa nyekundu ikazidi kuwaka, hakutaka kupoteza muda hata kidogo,  mama akatembea haraka kuelekea chumbani na kusukuma mlango.
“Si mumeo kamp…!”  ndio maneno aliyoyasikia aliposimama chumbani,  Amanda ndiye aliyekuwa akiongea, lakini alipomuona alisita kuendelea.
“Hamjambo binti zangu?”
“Hatujambo shikamoo mama, tumefurahi kukuona, tumekuwa tukikusikia tu!”
“Sijafurahi kuwaona, utaratibu gani huu wa kupitiliza chumbani kwa mtu? Nani kawapa kibali?”
“Mama waache,  hawa ni marafiki zangu!”
“Hawa si ni Amanda na Christine?”
“Ndio mama,  kumbe unatufahamu hata majina?”
“Nasema hivi ondokeni chumbani mkakae sebuleni,  hiyo ndiyo sehemu  wageni wote wanatakiwa kukaa,  chumbani  ni kwa wenyeji!”
“Mama waache!”
“Mwanangu Salome, ninafahamu ninachokifanya,  haya ondokeni!” mama alifoka  na bila ubishi Amanda na Christine wakanyanyuka na kuanza kutembea kuelekea sebuleni mama akiwasindikiza,  kilichotokea huko kilikuwa ni kugombezwa, akawaambia kabisa tabia mbaya waliyokuwa nayo ya kuingia hadi chumbani kwa mtu ikome na ikiwezekana wasifike kabisa hapo nyumbani tena hata kama  Salome alikuwa akiwakaribisha, wakanyanyuka na kutoka hadi nje ambako walivaa viatu na kutembea harakaharaka! Walikuwa wameiabika.
“Shosti mama noma!”
“Kweli kabisa, mimi nafikiri wanamficha Salome kinachoendelea!”
“Inawezakan!”
“Ah! Nimesahau!”
“Nini?”
“Gazeti langu la Funua!”
“Achana nalo utanunua jingine mbele,  ukirudi humo ndani utasababisha ugomvi!” Christine alimwambia Amana wakivuka  lango kubwa.

****
Baada ya kuwachachafya Amanda na Christine, mama yake Salome alirejea chumbani akihema, bado alikuwa na hasira nyingi moyoni mwake, kitendo cha kuingia mpaka chumbani kilikuwa kimemkera kupita kiasi. Alitaka kumwomba mwanae msamaha  kwa yote yaliyotokea pia amweleweshe sababu kubwa ya kuchukua hatua hiyo dhidi ya rafiki zake, lakini alipoingia tu chumbani na kutupa macho kitandani kitu cha kushtusha kilionekana,  macho ya Salome yalikuwa yameangalia juu, mapovu ya kimtoka mdomoni na alikuwa akihangaika kuhema.
“Mungu wangu! Salome!Salome!” aliita bila kuitikiwa.

Akaendelea kwa muda lakini hali ilikuwa hiyo hiyo,  hapakuwa na lolote angeweza kufanya zaidi ya kupiga simu ofisini,   dakika kumi na tano baadaye alisikia ving’ora nje ya nyumba,  alipochungulia kupitia dirishani aliona gari la wagonjwa lililoandikwa ubavuni  neno Tanzania Health Insurance, Ambulance. Watu   wanne walishuka wakiwa wamebeba machela mikononi na kuanza kukimbia kuingia ndani,  mbele yao alikuwepo Davis,  rafiki wa Gilbert na Meneja wa WorldCom, akashuka mbio ili akutane nao sebuleni.
“Vipi mama?”
“Hali yake imebadilika ghafla!”
“Yuko wapi?”
“Chumbani,  njooni huku, pandisheni ngazi,  nifuateni!” mama aliongea maneno mengi akitaka wamwelewe kwa haraka.
Davis alikuwa nyuma yake wakati akipandisha ngazi,  akifuatiwa na watu wanne waliobeba machela wakiwa kwenye mavazi meupe, wote wakapanda mpaka ghorofani na kuonyeshwa chumba alicholala Salome, hapakuwa na muda wa kuangalia uzuri wa chumba ingawa  wafanyakazi wa shirika la  bima ya afya Tanzania walishaona. Salome akabebwa na kulazwa juu ya machela na kushushwa hadi  chini ambako alipakiwa ndani ya gari la wagonjwa na safari ikaanza, mama yake Salome  na Davis wakiwa ndani ya gari moja, hakutaka kumchukua Faith.
Moja kwa moja walinyoosha hadi hospitali ya Muhimbili ambako Salome alishushwa na kukimbizwa chumba cha wagonjwa mahututi, vipimo vikafanyika haraka na kugundua kwamba mshipa ulikuwa umepasuka kichwani na damu ilikuwa ikivuja chini ya fuvu, tiba pekee ilikuwa ni upasuaji. Hii ilimaanisha Salome alikuwa akifanyiwa upasuaji kwa mara ya tatu kwenye kichwa kimoja,  hapakuwa na nafasi ya kubisha wala kujadili,  mama yake akatia saini fomu za kukubali na mgonjwa akakimbizwa chumba cha upasuaji ambako kazi iifanyika kwa masaa manne  mpaka kukamilika, ndipo Salome akatolewa na kwenda kulazwa wodini.
“Atapona?” mama alimuuliza daktari.
“Hakuna shida tatizo lake tumeshaliondoa, wala usihangaika sana mama kukaa hapa, kila kitu kitafanywa na wauguzi wewe unaweza tu kwenda nyumbani sasa, naona umechoka!”
Ulikuwa ni ushauri wa daktari lakini mama yake Salome hakuufanyia kazi, aliendelea kubaki nje ya wodi mpaka saa  tatu za usiku ndipo akaondoka kurejea nyumbani, Faith alikuwa amekwisha lala wakati anaingia na hakutaka kumwamsha,  aliongea na mfanyakazi wa ndani tu kuhusu maendeleo yake na kuingia chumbani ambako alijitupa kitandani bila kuoga wala kuvua nguo, usingizi ukamchukua.
Kuwika kwa jogoo ndiko kulikomwamsha usingizini saa kumi na mbili kamili za asubuhi, akanyanyuka na kushangaa alikuwa kama alivyoingia usiku, bila kupoteza wakati akaanza maandalizi kwenda hospitali. Saa moja kamili ndipo  gari lilifika na kumchukua moja kwa moja hadi Muhimbili, akamkuta Salome  hajarejewa na fahamu zake jambo ambalo hata madaktari alipoongea nao walimwambia lilikuwa likiwashangaza.
“Zitarejea?”
“Zitarejea tu!”
“Kweli?”
“Usiwe na wasiwasi mama yangu!”
 Hakukaa sana Muhimbili sababu alikuwa na wagonjwa wawili,  akaamua kuondoka moja kwa moja hadi hospitali ya Aga Khan, huko alimkuta Gilbert akiendelea vizuri ingawa bado alikuwa akilalamikia maumivu ya mbavu, mashine ya oksijeni ilishaondolewa,  alikuwa akihema kwa pafu lake moja. Alifurahi kumwona mama mkwe wake lakini kitu cha kwanza alichotaka kufahamu ilikuwa ni hali ya mke wake.
“Anaendeleaje mke wangu?”
“Sio mbaya!”
“Umemwambia niko wapi mama?”
“Hapana!”
“Faith?”
“Pia hajambo!”
Tayari mama yake Salome alikuwa na siri mbili za kuficha kifuani mwake.
Mama yake Salome aliendelea kutengeneza pembe tatu ya nyumbani, Aga Khan, Muhimbili kwa muda wa  karibu mwezi mzima bila kufungua mdomo wake kumweleza Gilbert kilichoendelea. Bado Salome alikuwa hajarejewa na fahamu zake, madaktari walifanikiwa kumfanyia upasuaji kuondoa damu iliyoganda lakini kukajitokeza kitu kingine  ambacho awali hakikuwepo, akawa anapatwa na degedege mara kwa mara! Jambo lililosababisha madaktari wampe dawa ya kupambana na hali hiyo,  ambazo kwa kawaida ziliambatana na usingizi mnene,  walipozisimamisha tu,  degedege ilianza tena hivyo zikafanywa kuwa sehemu ya maisha yake mpaka sehemu ya ubongo iliyokuwa imeamua ipone.

Gilbert hakukoma kumuulizia mke wake, jibu alilopewa ni anaendelea vizuri, mtoto wake Faith ndiye alipelekwa hospitali mara kwa mara kumwona lakini hakuwa na uwezo wa kueleza kilichotokea nyumbani. Wafanyakazi wa WorldCom pia waliombwa na mama yake Salome kutoitoa siri hiyo mpaka yeye mwenyewe atakapoona inafaa. 

Hayo yakiendelea Tecla hakukoma, bado alivitumia vyombo vya habari kumchafua Gilbert na kwa sababu habari zake ziliuza, karibu kila siku Gilbert aliandikwa. Alichokifanya ni kuwaomba wauguzi  waiondoe televisheni iliyokuwemo chumbani, redio na pia wasimletee magazeti,  akawaagiza waandike karatasi ndogo yenye maandishi “Ukiingia humu usiongee habari za magazeti” na kuibandika kwenye mlango wa kuingilia.

Alitaka ajitenge kabisa na dunia, asiwe na mawasiliano na kilichoendelea na alifanikiwa kulifanya jambo hilo vizuri, akaishi kwa amani ingawa alijua kabisa lazima alikuwa amechafuka. Katikati ya mwezi wa pili akiwa hospitali, Gilbert alianza kuwaomba madaktari wamruhusu kurejea nyumbani ambako angepona taratibu, hali yake iliridhisha, isitoshe alikuwa amemkumbuka sana mke wake hilo aliliweka wazi mbele ya madaktari akiamini  pia lazima habari za Tecla zilikuwa zimemfikia hivyo alikuwa na wajibu wa kumfariji na kumwambia ukweli wa kilichotokea,  maneno kutoka kwake yangesaidia zaidi kuiponya roho yake, hakuwa na taarifa kabisa kwamba Salome alikuwa hospitali ya Muhimbili kwa muda sawasawa na wake ambao yeye alikaa hospitali.
“Gilbert leo utakwenda nyumbani!” wiki moja baada ya kuanza kuomba ruhusu hatimaye daktari alimtamkia maneno hayo wakati akipita raundi.
“Kweli daktari?”
“Kabisa, Mungu amekusaidia lakini unapaswa kuwa makini sana na  kazi ngumu, kumbuka sasa una pafu moja!”
“Nafahamu”
“Basi mimi nimekwishakuruhusu, wakati wowote ukitaka kuondoka unaweza kufanya hivyo!”
“Sawa daktari, ahsante sana kwa kila kitu,  naishukuru sana hospitali ya Aga Khan,  imeokoa maisha yangu!”
“Hakuna shida, huo sisi ni wajibu wetu! Tutaendelea kuwasiliana lakini kila baada ya wiki mbili ni lazima urejee hospitalini kwa ajili ya uchunguzi, sawa?”
“Nitafanya hivyo bila kukosa!”
“Ahsante!”

Baada ya daktari kuondoka, ikiwa tayari ni saa sita,  muda wa kuona wagonjwa ukiwa haujafika, Gilbert hakuona sababu ya kumsumbua mama mkwe wake,  akapiga simu ofisini na kumtaka Davis afike na gari ili ambebe kwenda nyumbani. Hicho ndicho kilichotokea,   dakika kumi na tano tu baada ya kupiga simu, Davis aliwasili akiwa na kijana mwingine mmoja,  wakasaidiana kuibeba mizigo yote iliyokuwa chumbani kwa Gilbert na kuishusha mpaka kwenye gari, walipomaliza wakamsaidia kutembea mpaka kwenye lifti ambako walishuka mpaka ghorofa ya chini  lilikokuwa gari, safari ya kwenda nyumbani ikaanza,  Gilbert akiongea mambo mengi juu ya mke wake.
“Davis niambie ukweli, unafikiri mama Faith hajasikia habari za Tecla?”
“Aaaa!Sijui, lakini nafikiri bado!”
“Kweli?”
“Kabisa!”
“Anaendeleaje lakini ulipomwona mara ya mwisho?”
“Anaendelea vizuri!”
“Ulikuwepo lini?”
“Mh!...hivi hii nyumba ni ya Mkapa?”  Davis aliongea wakipita mtaa wa SeaView yaliko makazi ya Rais mstaafu wa awamu ya tatu, alifanya hivyo kupoteza lengo,  hakutaka maswali zaidi juu ya Salome na baada ya hapo aliendelea kubadilisha maongezi mpaka wakafika nyumbani kwa Gilbert, gari likaegeshwa na Gilbert akasaidiwa kushuka kisha kuingizwa ndani ambako hakutaka hata  kukaa sebuleni,  akanyoosha moja kwa moja hadi chumbani akifuatwa nyuma na mtoto wake,  kitanda kilikuwa kitupu.
“MAMAAAA! YUKO WAPI MKE WANGU?” alipiga kelele akimwita mama mkwe.
Gilbert aliendelea kupiga kelele akimwita mama mkwe wake mpaka Davis akashindwa kuwa mvumilivu na kuamua kutembea kuingia chumbani,  jambo ambalo hakutaka kulifanya kwa sababu ya heshima iliyokuwepo kati yao. Alimkuta Gilbert ameketi chini akilia na kutaka aonyeshwe  haraka mahali mke wake alipokuwa  na kama alikuwa amekufa basi aambiwe ukweli. Davis alitabasamu.
“Davis yaani mimi naongea vitu vya maana wewe unacheka?”
“Hapana sio hivyo bosi, nauelewa ukweli wa jambo hili,  shemeji hajafa na angekuwa amekufa tungeshakuambia!”
“Yuko wapi?”
“Yuko hospitali!”
“Hospitali?”
“Ndio!”
“Aliingia lini?”
“Wiki hiyo hiyo ambayo wewe ulipata ajali!”
“Nini kilitokea?”
“Kuna watu walimpelekea gazeti nyumbani,  lililoandika juu ya wewe kumpa mimba Tecla, mama alikuwa hospitali,  tunaamini aliliona gazeti hilo,  akapandisha presha na mshipa ukapasuka kichwani, ikabidi tumkimbize hospitali ya Muhimbili ambako amelazwa mpaka leo akiwa hana fahamu!”
“Kwanini hamjaniambia?”
“Mama alikataa, alisema tusikueleze kwanza ukweli mpaka utakapopona!”
“Mngeniambia tu,  hivi sasa anaendeleaje mke wangu Salome?”
“Hali yake sio mbaya, amekwishafanyiwa upasuaji,  bonge la damu lililoganda kichwani likaondolewa!”
“Operesheni ya tatu hiyo,  masikini mke wangu! Bila Tecla kuniharibia maisha asingerejeshwa kwenye chumba cha upasuaji, najuta kumfahamu msichana huyu, Davis…!”
“Naam”
“Huwezi kuamini,  sijawahi kukutana na Tecla kimwili, labda kama nilikuwa usingizini!”
“Usijali bosi, hivyo ndivyo dunia ilivyo, wakati mwingine huwa tunachafuliwa na matope ambayo hatukuyagusa!”
“Mama yuko wapi?”
“Nafikiri atakuwa hospitali!”
“Davis siwezi kukaa hapa bila mke wangu, ingawa naumwa naomba unipeleke Muhimbili nikamwone Salome wangu!”
“Sina tatizo twende”

Wakaingia ndani ya gari pamoja mtoto Faith na  Davis kuendesha kwa kasi mpaka hospitali ya Muhimbili wakipita barabara za Ali Hassan Mwinyi na Umoja wa Mataifa. Mbele ya jengo lililoitwa ‘Private wards’ gari liliegeshwa, Davis akashuka na kuzunguka upande wa pili ambako alimfungulia Gilbert mlango na kumsaidia kuteremka,  akambeba Faith na wakaanza kutembea kuelekea wodini. Walimkuta mama mkwe amesimama nje ya chumba alicholazwa Salome,  macho mekundu akionekana kabisa alikuwa akilia muda mfupi kabla hawajafika.
“Nisamehe baba!” alisema baada ya kuitikia salamu ya Gilbert.
“Kwanini mama?”
“Kwa kutokukuambia ukweli kuhusu mkeo!”
“Usijali mama, ninaelewa, anaendeleaje?” Gilbert akauliza, badala ya mama yake Salome kujibu akaangua kilio na hakutaka kuzungumza tena, hapo ndipo Gilbert akaona haikuwepo sababu ya kusubiri,  akamuuliza Davis kama mlango uliokuwa mbele yao ni wa chumba alicholazwa Salome,  akatingisha kichwa kuashiria kukubali,  Gilbert akausukuma na kuingia ndani, kulikuwa na kitanda kimoja kilichozungushiwa mapazia ya rangi ya kijani, nyuma yake kukiwa na watu waliokuwa wakiongea.

Gilbert hakuhitaji mtu wa kumwambia ni kitu gani kilikuwa kimetokea na  ni jambo gani lilikuwa likiendelea,  taa ikawa kichwani ikimweleza kwamba “Mke wako amekufa na wauguzi wanasafisha maiti” uvumilivu ukamwishia na kujikuta akilivuta pazia, kweli macho yake yakagongana na wanawake waliovaa nguo nyeupe, mikononi wakiwa na mipira, moyo ukamuuma, hakuwa tayari kukubaliana na ukweli kwamba  hatimaye Salome alikuwa amefariki dunia baada ya kuteseka kwa muda mrefu.
“No!No!She is too young to die!” (Hapana!Hapana, ni mdogo mno kufa) alipiga kelele akilia,  tayari muuguzi alishafika na kumshika mkono akimvuta taratibu kwenda nje.
“Please lets go out!” (Tafadhali twende nje)
“I want to see my wife!” (Nataka kumwona mke wangu)
“You will, not now though!” (Utamwona, ingawa sio sasa) Muuguzi alisema akimwongoza Gilbert kwenda nje, hakuwa tayari,  hatua kama mbili kabla hajaufikia mlango alishika nondo ya dirisha na kuanza kulia akiwa amegoma kabisa kwenda nje akitaka angalau aone maiti ya mke wake kwa mara ya mwisho.
“No!I am not going, let me kiss my wife for the last time!” (Hapana! Siendi,  acheni nimbusu mke wangu kwa mara ya mwisho!)  Gilbert aliongea akibubujikwa na machozi.

Davis aliyekuwa nje akimfariji mama yake Salome nje ya wodi, alisikia  mabishano  hayo kati ya Gilbert na Muuguzi, akaingia ndani haraka  na kuanza kumbembeleza Gilbert akubali kutoka nje lakini hakuwa tayari,  aliendelea kushinikiza aonyeshwe maiti ya mke wake lakini muuguzi hakuwa tayari kufanya hivyo.
“Dada hebu nieleze, nini kinaendelea hapa? Mgonjwa amefariki?” Davis aliuliza.
Muuguzi naye alishikwa na kigugumizi akionekana kutokuwa na jibu la kuwapa.
***
“Alinipa ujauzito, kisha amenitekeleza hivi sasa nateseka, kwa kweli nahitaji msaada wa kisheria ili niweze kupata haki yangu!”
“Naitwa John Baltazar, kutoka gazeti la Mtafiti, napenda kujua kama una uhakika mimba  kweli ni ya Gilbert?”
“Hilo sio swali, wewe mwandishi vipi,  ninyi ndio waandishi Makanjanja, yaani mimi ni mtu wa kusingizia nimepewa mimba na mtu asiyehusika? Mimba ni ya Gilbert”
“Uko tayari kufanya DNA mtoto akizaliwa?”
“Kabisa,  sioni sababu ya kuogopa lakini ninavyojua Gilbert lazima atakataa!”
“Akikubali?”
“Wakati wowote akikubali mimi nipo tayari,  tusubiri mtoto azaliwe!”

Yalikuwa ni majibishano ya maswali na majibu kati ya Tecla na waandishi wa habari kwenye  chumba cha Idara ya Habari Maelezo, hiyo ndiyo ilikuwa silaha yake, kuueleza umma juu ya ubaya aliofanyiwa na mwajiri wake na baadaye kutelekezwa. Wengi walimuunga mkono hasa vyama vya kutetea masuala ya Jinsia,  shirika la kutetea haki za wanawake kisheria lililoitwa Women Legal Assistance  liliamua kujitolea mawakili kuhakikisha kwamba Tecla anapata haki yake kama kweli  Gilbert alikuwa amempa mimba na baadaye kumtelekeza.

Kila kitu kiliandikwa kwenye magazeti, habari  juu ya Gilbert zilikuwa zimegeuka  Lulu, kila mtu akitaka kufahamu kilichokuwa kikiendelea, hakuna siku hata moja iliyopita bila jina la Gilbert kuwemo gazetini, alichafuka kupita kiasi, mtu ambaye siku zote watu walimwona muungwana, tayari alikuwa akionekana dhulumati, asiye na huruma kwa binadamu mwenzake.

Siku hiyo jioni baada ya  taarifa ya habari, mahojiano hayo yalirushwa moja kwa moja na redio Ujirani mwema iliyosikika karibu katika kila kona ya jiji la Dar es Salaam mpaka kwenye kibanda cha mzee Toboatobo huko Kimbiji kilometa arobaini kutoka Kigamboni,  mzee huyu alitokea kuvutiwa sana na suala hilo kwani alimfahamu  vizuri Tecla, sio jina lake tu,  bali  hata maumbile yake, ndiye mganga wa kienyeji aliyemwingizia dawa mwilini mwake kwa kutumia uume, lengo lake likiwa ni kufanya naye tendo la ndoa kitapeli, hiyo ndiyo njia aliyoitumia kuwapata wanawake wazuri ambao katika hali ya kawaida wasingekubali kuwa na uhusiano naye.
“Hivi DNA ni nini?” Alijiuliza mzee Toboatobo, hakufahamu maana yake.

Siku iliyofuata kazi aliyofanya ni kwenda kwenye zahanati yao ambako alimuuliza  daktari kama alielewa maana ya neno hilo, daktari akamfananulia vizuri kwamba kilikuwa ni kipimo kuthibitisha wazazi wa mtoto,  lakini hufanyika baada ya mtoto kuzaliwa. Akarejea nyumbani na kuendelea kufuatilia habari kwenye magazeti, akisubiri kwa hamu mtoto azaliwe.
“Nahisi mtoto yule anaweza kuwa wangu, si mimi pia nilikutana naye kimwili?” alijiuliza akiwa amejilaza kwenye jamvi ndani ya banda lake.
***
Muuguzi alishusha pumzi kwa nguvu kisha kuwaangalia Davis na Gilbert usoni, akatabasamu huku akiwapigapiga mabegani,  bado Gilbert hakutulia, alitaka kufahamu ukweli wa kilichokuwa kikiendelea nyuma ya pazia.
“Tatizo lenu ninyi wasiwasi ni mwingi!”
“Hata ungekuwa wewe sista, lazima ungekuwa na wasiwasi, haya tuambie basi yu hai au amekufa?” Gilbert aliongea.
“Salome yuko hai!”
“Unadanganya sista”
“Sitakiwi kudanganya!”
“Nyuma ya pazia mnafanya nini?”
“Tunamwosha,  shughuli inayoitwa Bed bath,  yaani kumuoshea mgonjwa kitandani  ndiyo inayofanyika,  bahati mbaya amepata vidonda sehemu zenye mifupa sababu ya kulala sana, hivyo ni lazima tumwekee poda, hilo ndilo limetuchelewesha, vinginevyo tungekuwa tumeshamaliza! Subirini kidogo tumalizie, tutawaruhusu muingie”
“Kweli sista? Unaonea ukweli?”
“Mkeo yupo hai, ingawa kweli hana fahamu bado,  Gilbert punguza wasiwasi,  madaktari wanajitahidi sana!”
“Ahsanteni kwa kila kitu,  mke wangu ni mdogo mno kufa, nitajitahidi kadri ya uwezo wangu wote kuona kwamba anapona!” Gilbert aliongea wakitoka nje kupisha wauguzi waendelee na kazi.
“Hakuna shida!”

Walipofika nje walishangaa  kumkuta Tecla  amesimama  kando ya mama yake Salome akiwa na gazeti mkononi, hakutaka hata kumsalimia Gilbert wala kujua hali ya mgonjwa, wote waliduwaa alijua vipi kama Gilbert alikuwa hapo. Alichokifanya ni kumtupia gazeti la Funua na kuondoka zake akisonya, Gilbert hakutaka kusema chochote wala hakutaka kulisoma gazeti hilo lakini  macho yake hayakuweza kukikwepa kichwa cha habari, kilikuwa wazi.
Tecla asubiri kujifungua ili mtoto apimwe DNA.
Gilbert akashusha pumzi, upande mmoja wa akili yake ulimwambia afanye kipimo hicho lakini upande mwingine ulimwambia asidiriki  kwani kama kweli alifanya tendo la ndoa na Tecla akiwa katika hali ya kutojitambua na hatimaye kumpa mimba,  lazima kipimo hicho kingethibitisha madai ya Tecla na aibu ingekuwa kubwa zaidi.
“Sipo tayari kupimwa,  labda akamtafute Gilbert mwingine” aliwaza kichwani mwake.

No comments

Powered by Blogger.