She is too young to die - 20
Ingawa hali yake ilikuwa bado dhaifu, Gilbert asingeweza kuishi mbali na mke wake, uamuzi alioufikia ni kuhamia chumbani kwa Salome, akawa amehama Aga Khan kwenda Muhimbili na mama mkwe wake kurejea nyumbani. Salome hakuwa na fahamu, hakuelewa kilichoendelea duniani kwa wakati huo na Gilbert alitamani sana azinduke ili aweze kumweleza ukweli juu ya kilichotokea kati yake na Tecla badala ya kufuata yaliyoandikwa na vyombo vya habari ambayo hatimaye yalimrejesha kwenye hali ya kupoteza fahamu.
Salome hakuzinduka hata wiki moja baadaye, aliendelea kuwa katika hali hiyo hiyo, Gilbert akiwa pembeni mwa kitanda chake, kila siku akimwomba Mungu atende muujiza. Wakati hayo yakiendelea hospitali, Tecla naye aliendelea kufoka kupitia vyombo vya habari akitangaza kwamba mara tu baada ya kujifungua yeye, mtoto na Gilbert ni lazima wangepimwa DNA ili kumthibitisha baba wa mtoto, jambo hili bado liliendelea kumtisha sana Gilbert na hakuwa na uhakika kama angelifanya. Kuna sehemu fulani ndani ya moyo wake iliyomnong’oneza kwamba huenda kweli alifanya tendo hilo na Tecla bila kujitambua na kujikuta akimpa ujauzito.
Hata hivyo hakutaka suala hilo limchukulie sana muda wake, alishafika mahali akakubaliana na kila kitu kilichokuwa kikiendelea mitaani, kama ni jina lake lilishachafuka na hakuwa na jambo lolote la kufanya, cha muhimu kwake kwa wakati huo alikuwa ni mke wake Salome, bado aliamini alikuwa ni mdogo mno kufa, kwa gharama yoyote ile ilikuwa ni lazima ajaribu kuokoa maisha yake ili apone na kumwomba msamaha kwa usumbufu wote aliomsababishia. Hisia zikamrejea tena kwenye kinanda chake, bado aliamini wimbo kipenzi kwa Salome uitwao You are the one of my life, ungeweza kumzindua tena usingizini kama alivyofanya huko nyuma, akakiagiza kinanda chake kikaletwa wodini, siku ya kwanza tu aliyokipiga na kuimba wimbo huo, Salome alitabasamu! Furaha ikamjaa Gilbert moyoni mwake.
Kazi yake ikawa ni hiyo kila siku mara tatu, akimwimbia mke wake wimbo alioupenda na kila alipofanya hivyo, Salome alitabasamu! Madaktari walifurahishwa sana na hatua hiyo na kumruhusu Gilbert kuendelea na utaratibu huo, wakidai pia ulikuwa ni tiba kwa ubongo wake uliofanyiwa upasuaji mara nyingi. Wiki tatu baadaye jioni kabla ya kulala, Gilbert akipiga kinanda chake kando ya kitanda cha Salome, alishangaa kumwona akifumbua macho na kumwangalia kwa muda kama dakika tano bila kusema chochote.
“Salome! Salome!” Gilbert aliita.
“N…di..o”
“Amka mke wangu, amka tuongee, nikueleze ukweli wa kilichotokea!”
“Kitu gani?”
“Yote yaliyotokea na kukufanya upoteze fahamu tena”
“Kwani nini? Niko wapi?”
Gilbert akafunga mdomo wake, hakutaka kusema kitu ambacho pengine kingeweza kuharibu kila kitu, alichofanya ni kubonyeza kengele iliyokuwepo kando ya kitanda kuita wauguzi, ambao dakika mbili tu baadaye waliingia wakiongozana na daktari wa zamu, walishazoea siku zote wakiitwa hali ya mgonjwa ilikuwa mbaya lakini siku hiyo walishangaa kumkuta Salome amefumbua macho akimwangalia mume wake bila kupiga kope kama mtu aliyekuwa akivuta kumbukumbu fulani. Nao wakasimama kando kumshangaa.
“Nime…kumbuka!...nimeku….mbuka mu…me wangu, kwan..ini ulifanyia hivyo? Nilikukosea kitu gani? Au kwa sab…abu nau…mwa ndio uka…chukua ua…muzi wa kwenda ku…zaa na Tecla?” aliongea Salome akibubujikwa na machozi, Gilbert alishindwa kuendelea kukaa hapo akasimama na kuanza kuyalamba machozi hayo kwa ulimi wake huku akimbembeleza mke wake atulie ili apate kumweleza ukweli.
“Siw…ezi! Umeni…umza Gilb…ert! Unahitaji kuniomba msamaha mume wangu na uahidi kuto…rudia tena ten…do hilo, kama ungehitaji kufanya hivyo si tungeongea na kukubaliana kama wanandoa? Ni kweli najua mimi siwezi tena na wewe ni binadamu, kwanini hatukushauriana badala yake ukanizunguka?”
“My dear wife, I am Innocent!’ (Sina hatia mke wangu mpendwa)
“Unamdanganya nani? Unafikiri sikuliona gazeti?”
“Ni kweli, najua uliliona lakini nakuhakikishia mke wangu tangu umeugua sijawahi kumjua mwanamke yeyote, huu ni mpango tu wa kunichafulia jina langu!”
“Haiwezekani Gilbert, kama ni hivyo basi unayo kazi ya kuthibitisha, kwanini usifanye kipimo cha DNA? Suala hili linaniumiza mno, kama kweli unanipenda mume wangu na unataka niendelee kuishi, basi kubali kufanya kipimo hicho!”
Gilbert alibaki kimya, mambo yalikuwa yakipita humo humo, moyoni mwake alishakataa kufanya kipimo hicho akihofia pengine ingekuwa kweli akajikuta kwenye aibu kubwa, lakini mke wake alikuwa akishinikiza sasa! Taratibu msimamo wake ukaanza kulegea, nia ya kuthubutu ikaanza kuzama ndani ya moyo wake. Hapo hapo akamwinamia mke wake sikioni mbele ya madaktari na wauguzi na kumbusu kisha kumtamkia maneno yaliyomfurahisha Salome.
“Niko tayari mke wangu, nitapima DNA! Lolote litakalokuwepo mbele tutaliona”
“Ahsante Gilbert!”
“Leo hii hii nitawatangazia waandishi wa habari ili tupate kumaliza ubishi!” Gilbert aliongea akitetemeka, sehemu fulani ndani ya moyo wake bado ilikuwa na wasiwasi juu ya uamuzi huo lakini hakuwa na jinsi kwa sababu ndicho kitu pekee kingeweza kumpa mke wake nafuu.
Siku hiyo hiyo mchana aliitisha mkutano na waandishi wa habari kwenye chumba cha Mikutano cha hospitali ya Muhimbili na kuwaeleza wazi juu ya ukubali wake, habari hiyo ilirushwa kwenye taarifa za habari za televisheni zote na siku iliyofuata iliandikwa na magazeti yote, Tecla akaisoma, kama ilivyokuwa kawaida yake na uzoefu wa kuongea na vyombo vya habari, siku hiyo hiyo mchana naye aliitisha mkutano na waandishi na kuwaeleza kwamba alikuwa tayari kufanya jambo hilo. Wananchi wote wa jiji la Dar es Salaam na Tanzania nzima waliisoma habari hiyo na wengine kuisikia kwenye taarifa, hivyo ndivyo ilivyokuwa hata kwa mzee Toboatobo, kijijini Kimbiji Kigamboni, akaahidi kufuatilia suala hilo kwa karibu.
Miezi tisa ikatimia, Tecla akajifungua mtoto wa kiume ambaye kwa kumwangalia tu sura yake hakufanana kabisa si tu na Gilbert bali hata mama yake, alikuwa ni mtu mwingine kabisa, usingeweza kumhusisha na watu hao wawili. Akiwa na miezi miwili, mapaparazi walimpiga picha na kuitoa kwenye magazeti, watu wote waliomwona walijua hakuwa mtoto wa Gilbert, lakini uthibitisho kamili ulikuwa ni kipimo cha DNA, kilichosubiriwa kwa hamu. Kila kitu kiliripotiwa kwenye vyombo vya habari, suala la Gilbert na Tecla lilikuwa limegeuka kuwa kama la Bill Clinton na Monica.
Hatimaye siku ya siku ikafika, watu wakafurika hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako kipimo cha DNA kilitakiwa kufanyika, waandishi wa habari wa vyombo vyote walikuwepo, wakipiga picha kila tukio, kuanzia kuwasili kwa Tecla na mtoto wake, vivyo hivyo kwa Gilbert akifuatana na rafiki yake Davis, moyo ulikuwa ukimdunda, hakuwa na uhakika sana kama majibu yangekuwa upande wake. Saa nne kamili waliitwa tayari kwa kuingia maabara kwa ajili ya kuchukua kipimo wote wakanyanyuka kwenye viti na kuanza kutembea kuelekea ndani, ghafla walisikia kelele katikati ya watu, wote wakageuka kumwangalia, alikuwa ni mzee mweusi, mwenye kibaragashia kichwani akiwa amevaa kanzu iliyochafuka, Tecla alipomwona mzee huyo nguvu zilimwishia mwilini.
“Na wewe?” akauliza.
“Nataka kupimwa!”
“Jamani muondoeni huyu mwehu!”
“Nani mwehu? Nataka kupimwa, nione kama huyu mtoto sio wangu” ilikuwa ni sauti ya mzee Toboatobo. Maneno hayo yaliwafanya watu waanze kuhisi kweli mzee huyo alikwua amechanganyikiwa, isingewezekana hata kidogo awe amewahi kufanya tendo la ndoa na mwanamke mrembo kama Tecla.Baada ya kugoma kwa muda mrefu kufanyiwa kipimo cha DNA ili kuthibitisha kama mtoto wa Tecla alikuwa wake au la! Hatimaye Gilbert amekubali kufuatia shinikizo la mke wake ambaye hivi sasa amerejewa na fahamu, ingawa hana uhakika kama majibu yatakuwa upande wake au la, Gilbert yuko hospitali ya Taifa Muhimbili ambako yeye, Tecla na mtoto wake wamenyanyuka kuingia chumba cha Maabara ili kuchukuliwa vipimo hivyo.
Wakipiga hatua kuufuata mlango wa maabara, ghafla zilisikika kelele kutoka kwa mzee mmoja ambaye Tecla alipogeuka kumwangalia alimtambua, alikuwa mweusi, mfupi aliyevaa kibaragashia kichwani mwake! Kumbukumbu zikamwijia na kumwonyesha kwamba macho yake yalikuwa yamemwona mzee Toboatobo, mganga wa Kienyeji ambaye alikwenda kwake miezi mingi kabla kutafuta dawa ya mapenzi kumfanya Gilbert amwache mkewe Salome na kumwoa yeye.
Mganga huyu ndiye aliyempeleka Tecla njia panda usiku na kumvua nguo zote, kisha kumlaza chali ardhini na yeye mwenyewe kuvua, akapaka dawa nyeusi kwenye uume wake na kumwambia Tecla kwamba hiyo ndiyo ilikuwa njia ya kuingiza dawa mwilini mwake ili siku Gilbert atakapomwingilia asimwache tena! Tecla alipomwona, aliikumbuka siku hiyo na kujua aibu imewadia.
Je, nini kitaendelea? Kipimo hiki kitachukuliwa? SONGA NAYO…
“Na wewe?” Tecla akauliza mwili wake ukitetemeka huku macho yake yakiangaza huku na kule na kujaribu kumwonyesha mzee Tobaotobo ishara kwamba aondoke eneo hili lakini alitingisha kichwa kukataa.
“Nataka kupimwa!” akaongea kwa kujiamini, maneno hayo yaliwafikia watu wote ikiwa ni pamoja na Gilbert ambaye aligeuza kichwa chake kumwangalia mzee huyo bila kuelewa ni jambo gani lilikuwa likiendelea.
“Jamani muondoeni huyu mwehu!” Tecla akapaza sauti yake juu.
“Nani mwehu? Nataka kupimwa, nione kama huyu mtoto sio wangu” ilikuwa ni sauti ya mzee Toboatobo.
Tecla alijaribu kuongea kwa sauti akijaribu kuwashawishi watu waliokuwepo maabara waamini kwamba mzee huyo alikuwa mwendawazimu lakini sauti yake ilikutana katikati na ya Toboatobo akipinga kabisa kile ambacho alikuwa akikisema na kupayuka kwamba mtoto wa Tecla alikuwa ni wake kwa sababu aliwahi kufanya naye tendo la ndoa, watu wote akiwemo Gilbert walishika midomo yao wakiwa katika hali ya kutokuamini jambo lililokuwa likisikika, haikuwa rahisi hata kidogo kwa msichana mrembo kama Tecla kukubali kufanya tendo la ndoa na mzee mchafu kiasi hicho.
Wakahisi kulikuwa na jambo na kuamua kumvuta mzee Toboatobo kando ili kumdadisi, shughuli ya kuingia chumba cha maabara ilisitishwa kwa muda, Davis aliendesha mahojiano na mzee huyo huku Tecla akiendelea kulia na kupinga kila kitu alichokisema akidai mzee huyo hakuwa na akili timamu hivyo maneno yake yote yabezwe na waendelee na mpango uliokuwepo.
“Mwendawazimu nani?” Mzee Toboatobo aliuliza.
“Wewe”
“Kuna mwendawazimu wa aina hii, vijana sikilizeni mimi si mwendawazimu hata kidogo, huyu binti alikuja nyumbani kwangu Kigamboni, tukafanya naye tendo la ndoa kabisa, mimi si mwehu kutamka maneno hayo, kwa muda mrefu sana nimekuwa nikimfuatilia anavyolumbana na Gilbert, nimekuja hapa ili nihakikishe kama kweli siku ile tulipokutana naye kimwili hakupata ujauzito!” mzee Toboatobo aliendelea kujenga hoja zilizomwingia Gilbert sawasawa kichwani mwake na kujikuta yeye mwenyewe akikubaliana na wote wanne kupimwa, likashabikiwa na Davis lakini Tecla akaendelea kulipinga.
“Huyu mzee anatoku sensi!” mmoja wa vijana waliokuwa jirani alishabikia akimaanisha jambo ambalo mzee Toboatobo alikuwa akiliongea lilikuwa na ukweli ndani yake hivyo ni lazima wote wapimwe.
“Sensi gani? Hakuna sensi yoyote, sipo tayari, kama mnataka tupime huyu mzee aondoke” Tecla aliongea kwa hasira.
“Kwanini?” Gilbert akauliza.
“Hatuwezi kupoteza muda na mtu wa aina hii, hivi kweli wewe Gilbert unafikiri mimi naweza kutoka na mzee wa aina hii?”
“Sijasema mimi, yeye ndiye ametamka maneno hayo na nionavyo, hakuna ubaya kama sote tukipimwa ili kuonyesha kwamba huyu mzee ni muongo!”
“Siwezi!” Tecla alikataa.
Kelele nyingi zilizokuwa zikipigwa nje ya chumba cha maabara zilifanya idadi kubwa ya watu wakusanyike, wote wakitaka kufahamu ni jambo gani lililokuwa likitokea, haikuwa kawaida kwa vurugu kama zile kutokea hospitali. Hii ilifanya walinzi wa hospitali wafike na kujaribu kutuliza lakini hawakuweza, Tecla alikuwa amegeuka mbogo na kumlaza mtoto wake chini, kisha kuanza kupambana na mzee Toboatobo akimsukuma kuondoka hospitali, walinzi walipofika walimkamata na kumtaka atulie. Hayo yalitokea bila watu kujua kwamba mmoja wa watu waliokuwepo alipiga namba polisi 111 na gari la polisi lililojaza askari likafika hospitali ya Muhimbili mpaka chumba cha maabara.
“Kuna nini tena?” mmoja wa maaskari aliuliza.
“Si huyu mzee mwehu anataka kuingilia mambo ya watu!”
“Nani mwehu? Unataka kunidhulumu mtoto wangu?”
“Kwani kimetokea nini?” askari akauliza tena na Gilbert akachukua muda wa kama dakika kumi kumweleza kilichotokea, akawa ameifahamu historia ya suala zima na namna ambavyo vyombo vya habari vilimwandika vibaya sababu ya ujauzito wa Tecla, habari ambazo ni Tecla mwenyewe aliyezipeleka kwenye magazeti ili ziandikwe na kumchafua, bila kutarajia askari walijikuta wakimwonea huruma Gilbert kwa sababu alichokuwa ameamua kifanyike kilikuwa kitu sahihi ili kuondoa ubishi.
“Mimi sioni kama kuna tatizo, pimeni tu!” Mmoja wa maaskari alisema.
“Sikubali, aitwe mwanasheria wangu!”
“Ni nani?”
“Jonathan Ndunguru!”
“Tupatie namba yake!”
“Ni 0700182018”
Bila kupoteza hata sekunde chache, askari huyo alibonyeza namba alizotajiwa kwenye simu yake na kuanza kusikiliza, ilipopokelewa simu alijitambulisha na kumtaka wakili Ndunguru afike hospitali ya Muhimbili idara ya maabara ambako mteja wake Tecla alikuwa kwenye matatizo, akaahidi kufika ndani ya dakika ishirini na hivyo ndivyo ilivyotokea. Akasimuliwa suala zima, kama alivyokuwa ameshauri askari, ndivyo pia mwanasheria wa Tecla alivyoshauri, hakuwa na ubishi tena, akanyanyuka kwa shingo upande kuingia ndani, mzee Toboatobo akiwa amejawa na tabasamu usoni, wote wakaketi vitini na kuchukuliwa kipande cha nyama chini ya ulimi kwa ajili ya kuchunguzwa.
“Nendeni nyumbani mje kesho!”
Wote wakatoka nje na kuwataarifu watu waliokuwepo, pia mama yake Salome alikuwa bado amesimama pembeni akisubiri nini kingefuata. Hakuwa na mahali pa kwenda Gilbert zaidi ya kurejea wodini kwa mke wake, akamsimulia kila kitu kilichoendelea na uso wake ukakunjuka. Ilikuwa ni siku njema sana kwa Gilbert, ujio wa mzee Toboatobo ulikuwa umefungua njia ya kuufahamu ukweli, siku nzima aliendelea kumsimulia Salome namna ambavyo hakuwa na hatia, alimhakikishia kabisa kwamba hakuwahi kufanya tendo la ndoa na Tecla bali kilichotokea kilikuwa ni njama za kutaka kumchafulia jina lake na hatimaye biashara zote alizokuwa nazo.
“Naelewa mume wangu, nakupenda sana Gilbert na si wewe tu bali pia mtoto wetu Faith, tena leo naomba mmlete jioni nimwone mtoto wangu pekee na kama alichokisema huyo mzee ni kweli basi leo ni siku ya furaha sana katika maisha yangu, natamani kusimama nitembee lakini sina uwezo, ahsante sana mume wangu kwa kuwa mwaminifu!”
“Hakuna tatizo Salome, kamwe siwezi kukusaliti, najua ulinichukia sana baada ya kusoma gazeti sasa angalau umeufahamu ukweli!”
“Ni kweli, niliumia, moyoni nilihisi umenitenda hivyo kwa sababu nimepooza, nilikuona mbaya mno!”
“Pole mke wangu!”
“Ahsante, kesho majibu ni saa ngapi?”
“Saa nne asubuhi ila nitakwenda mapema zaidi, uzuri niko hapa hapa hospitali!”
Jioni ya siku hiyo Faith aliletwa na mama yake Salome, furaha yao ikaongezeka, ikawa kama vile hawakuwa hospitali na hakurejea nyumbani na bibi yake bali alibaki wodini na kulala kitanda kimoja na baba yake mpaka asubuhi ya siku iliyofuata. Gilbert ndiye alikuwa mtu wa kwanza kuamka, akasali akimshukuru Mungu kwa ulinzi wa usiku mzima, kisha kuingia bafuni kujiandaa. Saa mbili kamili mama mkwe alikwishafika na kifungua kinywa, Gilbert akamsaidia mke wake kupiga mswaki, baadaye kuanza kumlisha, Faith akiwa usingizini na hawakutaka kumwamsha.
Saa tatu na nusu baada ya kifungua kinywa kumalizika, Gilbert aliaga na kutembea taratibu hadi chumba cha maabara, alimkuta mzee Toboatobo amekwishafika, rafiki yake Davis pia aliwasili kama dakika kumi na tano baadaye akifuatiwa na Tecla pamoja na mwanasheria wake. Baadaye makundi ya watu mbalimbali yalianza kufika, wengi walikuwa wameona taarifa kwenye vyombo vya habari na walitaka kujua nini kingetokea siku hiyo, kama watu mia tatu hivi walikuwepo chumba cha maabara, saa nne kamili mlango ulifunguliwa, akatokea mfanyakazi wa maabara yuleyule aliyekuwepo jana yake na kuwakabidhi majibu yao.
Walichokishuhudia watu ni Tecla akiruka juu na kushangilia huku akikimbia huku na kule na mtoto wake mgongoni, lakini Gilbert akaangua kilio akiwa na karatasi yake mkononi, Davis akatembea haraka kumfuata lakini kabla hajamfikia alianguka chini na kuzimia, damu zikaanza kumtoka puani! Watu wote wakamzunguka kutaka kujua ni nini kilikuwa kimetokea, tayari Davis alishakichukua cheti na kuanza kukisoma, kilionyesha mtoto alikuwa wa kwake.
“Mwingizeni huku!” Ilikuwa ni sauti ya daktari aliyekuwa Idara ya wagonjwa wa nje.
Gilbert alibebwa juu juu baada ya kuanguka nje ya chumba cha uchunguzi wa DNA baada ya kusoma karatasi ya majibu na kugundua kwamba mtoto wa Tecla alikuwa ni wake! Kwake hilo lilikuwa ni jambo lisilowezekana, hakuwa na kumbukumbu kabisa hata kidogo za kukutana kimwili na mwanamke huyo, iweje mtoto yule awe wake? Alijiuliza bila kupata majibu na hapo hapo akaanguka chini na kupoteza fahamu, akipiga pua yake kwenye jiwe lililokuwa kando na damu nyingi kumtoka.
“Amekuwaje?”
“Ameanguka”
“Sababu?”
“Tulikuwa kwenye chumba cha kupimia DNA, nafikiri majibu yaliyotoka hakuyatarajia!”
“Huyu si ni Gilbert?”
“Ndio”
“Sakata lake na yule mwanamke bado tu?”
“Daktari tunaomba umpime mgonjwa!” Davis aliongea na daktari akachukua kipimo cha shinikizo la damu na kumfunga Gilbert mkononi kisha kuanza kusikiliza.
“Shinikizo lake limepanda sana, huwa ana tatizo la presha?”
“Kwa kweli hatujui!”
“Apelekwe wodini tumuanzishie matibabu ya kushusha shinikizo lake, liko juu mno siwezi kumwacha hivi hivi!”
“Yuko hapa hapa wodini, mke wake amelazwa chumba cha wagonjwa mahututi na yeye anaishi naye hapo hapo wodini!”
“Basi apelekwe huko huko!”
Wauguzi walimweka Gilbert juu ya machela na ikasukumwa kwa haraka mpaka wodini na kuingizwa, Salome alikuwa macho wakati anaingizwa, moyo wake ukashtuka na kujikuta akitaka kufahamu ni jambo gani lilikuwa limempata mume wake, Davis akamsimulia juu juu bila kugusa suala la majibu, akielewa wazi kwamba kumweleza Salome ukweli juu ya mtoto wa Tecla kungezua jambo jingine, lazima angepoteza fahamu zake kama ambavyo siku zote alifanya.
“Shemeji nieleze basi, mume wangu kawaje?” Aliuliza Salome, Gilbert akilazwa juu ya kitanda kilichokuwa jirani.
“Presha imepanda shemeji!”
“Kwanini?”
“Salome, elewa kwamba presha imepanda basi, mumeo amekuwa na matatizo mfululizo sana!” Mama yake Salome aliingia kati, hakutaka kabisa mtoto wake asikie taarifa za majibu.
“Mama kuna kitu mnanificha, ni bora kuniambia sasa hivi kuliko nifahamu baadaye!”
“Hakuna kitu, tulia mtoto wangu, mumeo anatibiwa atapona, kama kuna kitu cha kuongea basi mtaongea ninyi wenyewe wawili, sisi hatuna cha kukueleza!”
“Mamaa!”
“Ndio”
“Naomba mniambie”
“Hakuna cha kukuambia Salome, mumeo amenguka ghafla tukiwa maabara!”
“Haya!” Salome aliitikia kwa shingo upande, akatamani kunyanyuka kutoka kitandani kwake na kwenda alipolazwa Gilbert lakini hakuwa na uwezo huo, bado mwili wake ulikuwa umepooza kuanzia shingoni hadi miguuni, sehemu pekee iliyofanya kazi ilikuwa ni kichwa.
Madaktari walianza kuhangaika na Gilbert, wakishusha shinikizo la damu kwa dawa za sindano na dripu, mpaka saa kumi jioni ndipo Gilbert alizinduka na kuangaza macho yake huku na kule, kwanza hakuelewa ni wapi alikokuwa, lakini aliendelea kuongea maneno bila kuelewa kwamba alisikika, Davis aliyekuwa jirani alimwonyesha ishara asiendelee lakini hakuelewa.
“Jamani huo ni uongo tena mkubwa, mtoto huyu si wangu, nahisi majibu yamechezewa, Tecla anaweza kufanya lolote ili nionekani nina hatia, jamani nisaidieni majibu haya si ya ukwe..!” Gilbert aliendelea kuongea kwa sauti na kunyamaza Davis alipoufunika mdomo kwa kiganja chake.
“Nyamaza Gilbert, utaharibu kila kitu!” alinong’ona lakini alichokifanya hakikusaidia, tayari Salome alishasikia, masikio yake yalikuwa na uwezo mkubwa mno kufanya kazi ni kama nguvu zote za miguu zilihamia kwenye masikio.
“Davis unajisumbua, nimekwishasikia, kumbe mume wangu alizimia baada ya majibu kutoka yakionyesha mtoto wa Tecla ni wa kwake? Imeniuma…imeniuma…imeniuma…imeniu…!” hakumalizia neno la mwisho akatulia, kama ilivyotokea huko nyuma povu likamtoka.
Madaktari waliitwa na kuja haraka kumwangalia, wote walithibitisha tatizo lake lilikuwa limejirudia, Gilbert ambaye sasa alikuwa na nguvu kama kawaida baada ya shinikizo lake la damu kushuka, alinyanyuka kwenye kitanda chake na kusogea karibu, akijilaumu kwa kutamka maneno yaliyoleta matatizo. Akaanza kuwauliza madaktari kama kulikuwa na jambo lolote ambalo wangeweza kufanya ili kuokoa maisha yake maana tayari alikuwa akikakamaa mwili wote.
“Sidhani, ubongo wake umekwishafanyiwa upasuaji mwingi mno, hapa kwetu hatuwezi kumpasua tena!”
“Please doctor do something, she is too young to die!” (Tafadhali daktari fanya kitu fulani, ni mdogo mno kufa)
“At this juncture there is nothing I can do as a Tanzanian Surgeon!” (Kwa hapa tulipo, hakuna ninachoweza kufanya kama daktari bingwa wa upasuaji hapa Tanzania)
“Pleeeease! Do something doctor, save my beloved wife’s life, she is everything I have got” (Tafaaadhali! Fanya kitu fulani daktari, okoa maisha ya mke wangu, yeye ni kila kitu nilichonacho!)
“Tumejitahidi sana, tatizo ni kwamba kabla hajapona vizuri ninyi mnampasua mshipa kwa kumpa habari mbaya, mnarudisha kazi ya madaktari nyuma, hakuna tunachoweza kufanya kwa hivi sasa, huo ndio ukweli vinginevyo hata sehemu ndogo ya ubongo iliyobaki hai nayo itakufa, hivyo kuyakomesha kabisa maisha yake, sitaki kufanya hivyo! Huo ndio ukweli Gilbert!”
“Daktari naomba unisaidie, mke wangu ni mdogo mno kufa!” alisema Gilbert akiwa amepiga magoti chini, kwake suala la mtoto wa Tecla halikuwa na umuhimu tena wakati huo, vyovyote ambavyo dunia ingesema ilikuwa sawa lakini cha muhimu mke wake apone, daktari aliendelea kuweka msimamo.
“Labda ujaribu nchi nyingine!”
“Wapi?”
“India au Uingereza”
“Unaweza kunifanyia mawasiliano?”
“Acha niwasiliane na India, wenzetu wana vifaa bora zaidi, pengine wanaweza kusema umpeleke!”
Gilbert, Davis na mama yake Salome walibaki chumbani wakiwaangalia wauguzi waliokuwa wakihangaika kumsaidia Salome, hali ya Gilbert kwa wakati huo ilikuwa nzuri mno, halikuwa jambo rahisi hata kidogo kuamini kwamba mtu huyo huyo ndiye aliyeanguka nje ya chumba cha DNA na kubebwa juu juu hadi chumba cha wagonjwa mahututi, shinikizo lake la damu lilikuwa katika hali ya kawaida kabisa. Saa nzima baadaye, daktari alirejea na kuwapa taarifa kwamba daktari bingwa wa upasuaji wa Ubongo kwenye hospitali ya Jaslok, jijini Mumbai alikuwa amekubali kumpokea Salome na kujaribu kumfanyia upasuaji kwa njia iliyoitwa Laser. Gilbert alifurahi kupita kiasi.
“Kila kitu kikiwa sawa, itabidi msafiri kesho saa kumi kwenda India, sisi leo mpaka kesho tunamwandaa tu hapa kwa ajili ya safari hiyo!”
“Sawa daktari! Maisha yangu yamekwishahamia hospitali, nipo tayari kusafiri tena kwenda India ingawa mwili wangu bado haujakaa vizuri”
Davis alichukua hati za kusafiria za Salome, Davis na yake mwenyewe kwani walikubaliana kusafiri watatu ili wasaidiane na kwenda nazo ubalozi wa India siku iliyofuata asubuhi kushughulikia viza ya kuingia nchini humo kwa matibabu,wakati huo huo aliwasiliana na shirika la ndege la Kenya kwa ajili ya tiketi tatu, mtu mmoja akiwa mgonjwa hivyo alihitaji sehemu maalum kulazwa.
Mpaka saa nane mchana kila kitu kilikuwa tayari, daktari alishawasiliana na watu wa India juu ya kuwasili kwa mgonjwa nao wakaahidi kuwepo uwanja wa ndege Alfariji ya siku iliyofuata, safari hiyo ilimkumbusha Gilbert safari yake na Faith kwenda India kwa matibabu ya moyo, ambayo ilikomea uwanja wa ndege wa Kenyatta Jijini Nairobi.
Saa nane na nusu juu ya alama, gari la wagonjwa la hospitali ya Muhimbili liliondoka likiwa na mgonjwa Salome, Gilbert na Davis ndani yake kuelekea uwanja wa ndege wa Dar es Salaam, ilikuwa imebaki saa nzima na nusu tu kabla ndege haijaruka. Wakapita barabara ya Msimbazi mpaka Kamata ambako waliingia barabara ya Nyerere na kunyoosha hadi kwenye taa za Tazara, walisimama umbali kama mita kutoka kwenye mataa, gari nyingi zikiwepo mbele yao, halikuwa jambo la kawaida kabisa! Dereva wa gari la wagonjwa alipiga king’ora chake lakini hakikusaidia, hapakuwa na sehemu yoyote ya magari kupisha gari la wagonjwa lipite.
“Kuna nini?” dereva alimuuliza kijana aliyekuwa akiuza maji.
“Rais anapita akitokea Wizara ya Kilimo na Chakula!”
“Dah! Sasa tutapita wapi sijui?”
“Tuvumilie kidogo labda Rais atapita, mstari ulegeze kidogo ndipo tupite huku pembeni!”
“Sawa!” Gilbert aliitikia lakini hakuwa na uhakika kama maneno ya dereva huyo yalimwingia, alichotaka yeye ni kufika uwanja wa ndege haraka iwezekanavyo kabla ndege haijaruka, asingekubali aendelee kubaki na mgonjwa jijini Dar es Salaam.
Mpaka dakika kumi na tano baadaye msururu wa magari ulikuwa bado haujatingishika, magari ya upande mmoja tu ndio yalikuwa yakipita, Gilbert akazidi kuchanganyikiwa. Alichokifanya ni kufungua mlango na kuruka nje, kisha kukimbia mpaka mbele alikokuwa askari wa usalama barabarani akiruhusu magari ya upande mmoja tu.
“Afande habari yako?” alimsalimia.
“Aisee niko kazini, Rais anapita naomba uniache!”
“Mimi pia nina mgonjwa, nawahi ndege, hali yake si nzuri hata kidogo wewe unaruhusu gari za upande mmoja tu kwanini?”
“Rais anatokea upande huu, siwezi kuruhusu gari za huku zipite!”
“Kwa hiyo mke wangu afe?”
“Swali gumu kaka!”
“Haya subiri sasa!” Gilbert aliongea na kurudi mbio mpaka kwenye gari, akamwamuru dereva wa gari la wagonjwa akae kando lakini hakukubali, akapanda na kumsogeza pembeni kwa nguvu kisha yeye mwenyewe kuliwasha gari, juhudi za Davis kumzuia hazikuzaa matunda, gari likaparamia tuta kando ya barabara na kuanza kutembea kama vile lilitaka kuanguka, hakuna aliyetegemea lingevuka sehemu hiyo na kupanda juu ya tuta hata dereva wa gari la wagonjwa alibaki akishangaa, likapitishwa kando kando mpaka mbele kabisa ambako msururu wa magari bado ulipita kutoka upande mmoja, king’ora cha gari la wagonjwa kikilia kwa nguvu.
“Gilbert msafara wa Rais huo?”
“Achana nao, mke wangu ni muhimu, litakalokuwa na liwe!”
“Utasababisha ajali!”
“Msafara utasimama tu!” aliongea akiliingiza gari barabarani.
ITAENDELEA KESHOOOOOOOOOOOOO

Post a Comment