ad

ad

She is too young to die -18


Salome amerejewa na fahamu zake baada ya maombi ya muda mrefu na mume wake Gilbert kuwa anampigia kinanda akimwimbia wimbo wa You are the love of my life ambao Salome aliupenda sana. Tukio hili limerejesha furaha katika maisha ya Gilbert ambaye kwa muda mrefu pamoja na utajiri wake amekuwa akihangaika na matatizo mbalimbali ya familia yake kiasi cha kufanya maisha yasiwe na raha.
Lakini mambo yakiwa hivyo, ghafla jambo jingine linatokea, Tecla msichana ambaye ni sekretari wake anamfuata na kumwambia ana ujauzito wake, jambo ambalo Gilbert analikataa kwani hakumbuki kama amewahi kufanya mapenzi na msichana huyo lakini Tecla anamwambia siku moja alipokuwa kwake, alilewa wakafanya tendo la ndoa.
Wakati Gilbert akiendelea kukataa katakata, msichana huyo ameamua kumkomoa kwa kuitisha mikutano na waandishi wa habari, kuwataarifu juu ya kilichotokea ili habari hiyo iandikwe gazetini na kutangazwa kwenye redio na televisheni ili kumuaibisha Gilbert, amejitahidi sana kuizua habari hiyo lakini imeshindikana na sasa imetoka kwenye gazeti la Funua! Asubuhi na mapema akiwa bado yuko kitandani, anasikia redioni habari hiyo ikitangazwa lakini kabla mtangazaji hajaimaliza, Gilbert alizima redio.
Je, nini kinaendelea? SONGA NAYO…

Gilbert alikuwa akitetemeka mwili mzima, hofu kubwa ilikuwa imemwingia, machozi yalikuwa yakimlengalenga kiasi cha kulazimika kukizamisha kichwa chake katikati ya mito ya kulalia! Kichwani alijaribu kupiga picha ya namna ambavyo siku yake ingekuwa, hakuwa na jibu, Watanzania walikuwa wamepata kitu cha kuongelea, hakika jina lake lilikuwa limechafuliwa na hakujua jinsi ya kulisafisha, roho ilimuuma sana kwani mpaka wakati huo aliamini hakuwa na hatia, hata siku moja hakuwahi kukutana na Tecla kimwili, iweje ampe ujauzito? Alijiuliza bila kupata jibu.
“Gilbert! Gilbert! Gilbert!” Salome aliita.
“Naam mke wangu”
“Mbona unalia?”
“Nafikiri jinsi unavyoteseka”
“Hapana, kuna kitu kingine, tabia yako imebadilika sana kwa siku chache zilizopita, kuna kitu kinakusumbua mume wangu, hauhitaji kunificha, mimi ni mkeo tunaweza kupanuana mawazo hata kama tatizo ni kubwa kiasi gani!” Salome aliongea kwa upole lakini hakuweza kumshawishi Gilbert afungue mdomo wake kueleza kilichokuwa kimetangazwa redioni.
“Hakuna tatizo mke wangu, niko sawa”
“Unanidanganya Gilbert, kwanza unalia, tabia yako imebadilika, umezima redio ghafla, kuna nini? Nahitaji kufahamu”
“Hakuna kitu mke wangu”
“Haya, lakini kumbuka huwezi kuficha jambo moyoni mwako, lazima litatokeza nje lenyewe bila juhudi zako!”

Gilbert alibaki kimya, huku kichwani mwake yakizunguka mawazo mengi yasiyokuwa na majibu, alishindwa kuelewa angetoka vipi ndani ya nyumba yake siku hiyo, kwani lazima kila mahali ambako angepita watu wangekuwa wamesoma magazeti na vidole vingekuwa vikimsonta nyuma yake, ilikuwa ni aibu ambayo hakuwa na uwezo wa kuibeba, akapoteza uhakika kama angeendelea kuishi baada ya hapo. Alichokifanya ni kukurupuka kitandani na kwenda moja kwa moja hadi kwenye chumba alichokifanya ofisi yake na kupiga namba ya Tecla, hakukawia kuipokea.
“Nilijua utapiga na bado, safari ndio kwanza imeanza!”
“Unasema?”
“Gazeti umelisoma, mchana tena naongea na Waandishi wa habari, huwezi kunipa mimba halafu ukanitelekeza!”
“Tecla!”
“Jina langu”
“Lakini unajua kabisa sikukupa mimba, ni kwanini unanifanyia hivi?”
“Mimba ni ya kwako Gilbert”
“Mungu anajua, kwanini unataka kumtesa mke wangu? Unataka apoteze fahamu tena baada ya kupata taarifa hizi? Tecla usinilazimishe kulipa kisasi, usinilazimishe kufanya mambo ambayo sikuwahi kuyafikiria katika maisha yangu kwamba naweza kuyafanya, usitake kuufahamu upande wangu wa pili unaweza usiufurahie sana!”
“Usinitishe, mwanaizaya wewe, umeingia mjini tunakuona hapa ukitembea kama bata, leo hii unajifanya eti na wewe mjanja sasa nitakuonyesha mji!”
“Tecla unaelewa unachokisema?”
“Naelewa”
“Haya bwana mshindi wewe” Gilbert alijibu na kukata simu, hasira yake ilikuwa imeongezeka mara mbili akaifananisha kabisa na siku aliposhuhudia mama yake akipigwa kibao na tajiri wa kiarabu, wakati huo alikuwa na umri wa miaka kumi na nne, alichokifanya ni kuchukua jiwe na kumpiga nalo Mwarabu huyo usoni, akachanika na kumwaga damu! Tangu wakati huo hakuwahi kufanya kitendo cha aina hiyo tena, hakupenda ugomvi, siku zote alipenda urafiki na hakuchokoza watu lakini alichokuwa akikifanya Tecla ni uchokozi, alikuwa akikitekenya kituo chake cha hasira.

Gilbert hakuwa amepima madhara ya habari iliyokuwa imechapishwa, muda mfupi tu baada ya kurejea chumbani simu zilianza kumiminika, watu wakimpa pole na wengine walimkejeli kwa kumwambia siku zote alijifanya muaminifu kumbe alikuwa mchafu. Roho ilimuuma sana na simu zilizidi kumiminika utafikiri simu yake ilikuwa ni ya Huduma kwa Wateja katika kampuni ya simu za mkononi ya Tigo.
“Vipi mbona simu yake imekuwa bize sana?”
“Sijui kwanini”
“Hao ni watu tu wanakupigia?”
“Wengine wanabip!”
“Mh! Gilbert hapo lazima kuna jambo na ninavyokuangalia usoni kuna kitu najifunza, mume wangu unanitisha, kuna nini lakini? Tafadhali naomba unieleze”

Gilbert hakuweza kujibu, machozi yakambubujika, ili kuepusha tatizo na maswali mengi alitoka chumbani na kwenda moja kwa moja ofisini ambako alikaa kwenye kiti na kulaza kichwa juu ya meza, simu akazima kabisa. Mawazo yalikuwa mengi, siku zote watu walimheshimu lakini sasa hatima ya heshima yake ilikuwa imewadia kwa kosa ambalo hakulifanya, alitamani dunia yote ielewe hakuwa na hatia kiasi gani lakini hapakuwa na namna ya kulifanya jambo hilo, hata kama angeitisha mkutano na waandishi wa habari bado angeonekana anajitetea.

Katika maisha yake hakuwahi kuonja pombe, lakini siku hiyo alisikia sauti ikimwambia “Katafute pombe unywe Gilbert, utapunguza mawazo” akaitii sauti hiyo na kutoka hadi chumbani, akachukua fedha na kutembea moja kwa moja hadi kwenye gari lake nje ya nyumba ambako aliendesha kuingia mitaani, ilikuwa bado ni asubuhi sana, maduka mengi yakiwa yamefungwa. Kila alikozunguka, alipishana na vijana wauza magazeti wakiwa wamening’iniza gazeti la Funua mbele kabisa, picha ya Gilbert na Tecla ilikuwa ukurasa wa mbele chini ya kichwa cha habari; Mfanyabiashara maarufu ampa mimba mimba sektretari wake.
“Babu habari motomoto! Vipi nikupe hii la Funua? Linauzika kweli leo!” Muuza magazeti alimwambia Gilbert akiwa kwenye foleni maeneo ya Mikocheni kwa Nyerere bila kuelewa alikuwa akiongea na mhusika.
“Ahsante kijana nimeshalisoma”
“Mbona unalia mzee?”
“Nina msiba”

Kijana huyo akamwangalia Gilbert kisha kuangalia kwenye ukurasa wa gazeti, akamwambia neno moja tu “Pole” na kutembea taratibu kusimama pembeni. Foleni ilipoanza kutembea, Gilbert alizidi kusonga mbele mpaka maeneo ya Shoppers Plaza, bado hakuona duka lolote la pombe lililofunguliwa lakini akaona duka dogo la dawa likiwa wazi, akakata kona na kuegesha gari yake pembeni kisha kutembea mpaka kwenye duka hilo.
“Hujambo binti?”
“Sijambo!”
“Huwa nina matatizo ya shinikizo la damu, limepanda sana, hapa nilipo sina cheti cha kukuonyesha lakini naomba unisaidie dawa ambazo natumia kupumzika!”
“Dawa gani?”
“Valium!”
“Bila cheti?”
“Naomba msaada wako, siwezi kukudanganya”
“Kaka unanitia matatizoni!”
“Nisaidie kwa mvua, nitakusaidia kwa jua”
“Haya kidonge shilingi ishirini!”
“Chukua elfu tano hii, nipe vidonge kumi pamoja na dawa ya kikohozi inayoitwa Kofylini, chenji inayobaki utakunywa chai!”
“Ahsante kaka!” Msichana huyo aliitikia na kumkabidhi Gilbert dawa alizozihitaji ndani ya muda wa dakika tano, akaondoka bila hata kuaga mpaka kwenye gari lake akirejea nyumbani.
Njiani kama mita mita tano kutoka dukani alisimamisha gari lake kando ya barabara na kuvichukua vidonge vyote kumi alivyopewa, kwa kutumia chupa ya dawa ya Kofylini akaanza kuvisaga mpaka vikawa unga ndipo akaumwaga unga huo ndani ya dawa ya kikohozi na kuitikisa mpaka aliporidhika kwamba ilikuwa imetosha ndio akaanza kuinywa, kwa sababu ya utamu wa dawa ya kikohozi, alibugia mara mbili tu chupa nzima ikawa imekwisha, akawasha gari na kuanza kuendesha kwenda nyumbani.
Hakwenda mbali sana, dakika kumi tu baadaye macho yake yalianza kuwa mazito lakini hakutaka kuegesha gari lake pembeni akazidi kuendesha kwa kasi akitaka afike nyumbani kabla hajazidiwa, hakufanikiwa kulifanya jambo hilo kwani mita chache tu mbele, mlio wa ajabu ulisikika, watu wakashika mikono kichwani.
“Kuuuuu!” vumbi likatimka.
***
Nusu saa baadaye, simu ya mezani nyumbani kwa Gilbert ililia, mama yake Salome akaipokea na kutaka kujua ni nani alikuwa amepiga, haikuwa kawaida kwa simu hiyo kutumika mara nyingi simu za mkononi za Gilbert na Salome ndio zilifanya kazi sana.
“Hapo ni nyumbani kwa Gilbert?” sauti iliuliza baada ya salamu.
“Ndio!”
“Naweza kuongea na mke wake?”
“Anaumwa, niambie tu mimi nitampa ujumbe!:
“Nina habari mbaya za kuwapa…!”
Lilikuwa ni gari la mchanga likija kwa kasi kutokea maeneo ya Mbezi, dereva wake akiwa amewasha taa kuonyesha lilikuwa linakata kulia kuingia barabara ya Rose Garden, gari la Gilbert ndilo lilikuwa mbele likitokea maeneo ya Shoppers Plaza, mwendo ulikuwa wa taratibu sababu Gilbert alikuwa usingizini, dereva wa lori akafikiri mwendo ulikuwa umepunguzwa kumruhusu yeye apite, akakata kona ghafla lakini badala ya gari Gilbert aina ya Toyota RAV 4 New Model kusimama kuruhusu lori lipite, lilizidi kuserereka kwenda mbele yakakutana uso kwa uso!

“Mungu wangu, ajali! Ajali! Ajali!” ndio maneno yaliyosikika kutoka midomoni mwa watu waliokuwepo kando ya barabara mara baada ya kuona magari hayo hakigongana, wote wakaanza kukimbia kuelekea eneo la tukio huku wakipiga kelele.

Gilbert alikuwa ndani ya gari akiwa amebanwa na sehemu ya mbele pamoja na usukani kifuani, ilikuwa picha mbaya mno, alionekana kabisa amekufa kwa jinsi alivyokuwa ametulia! Wala hakuwa na habari ya kilichotokea sababu ya kiasi kikubwa cha dawa alichokuwa amekunywa. Tayari wapiga picha wa televisheni za ITV, TBC, Channel Ten walishafika na kuanza kulirekodi tukio zima kwa ajili ya kurusha hewani, wengi walisikitika kugundua aliyepatwa na ajali hiyo ni Gilbert, baadhi ya watu walikuwa na gazeti la Funua mkononi wakalihusisha tukio hilo na habari iliyochapishwa.
“Haya magazeti bwana, amechanganyikiwa na habari hii mpaka akaendesha gari kwa mawazo na kupata ajali!” mmoja wa watu alisikika akisema.

Dereva wa lori hakuumia ingawa gari lake lilibondeka kidogo kwa mbele, akashauriwa aingie tena ndani ya gari na kurudisha gari kinyumenyume, ndipo juhudi za kumtoa Gilbert garini zikaanza, haikuwa kazi rahisi, alikuwa amebanwa kiasi cha kutosha! Dakika kumi na tano baadaye alikuwa bado amekwama ndani ya gari, uamuzi uliotolewa ni kutafutwa kwa mashine ya kukatia chuma ili bodi la gari likatwe, watu wengine wakashauri gari livutwe akiwa ndani yake mpaka hospitali ya TMD, iliyokuwa jirani na eneo la tukio, mabishano kidogo yalitokea juu ya nini cha kufanya lakini baadaye uamuzi ulifikiwa kwamba bodi likatwe na Gilbert atolewe.

Mashine ya kukatia chuma ikaazimwa kutoka kituo cha Mafuta cha BP kilichokuwa mita chache tu kutoka eneo hilo na waya mrefu wa umeme ukaunganishwa mpaka kufika mahali magari yalipokuwa na bodi likaanza kukatwa, kazi hiyo iliwachukua dakika arobaini na tano, Gilbert akiwa bado ametulia tuli, ndipo wakafanikiwa kumtoa na kumlaza chini, walipomgusa kifuani moyo wake ulikuwa umetulia, wote wakaamini amekwishakufa.
“Masikini huyu tayari, mwisho wa Gilbert!”
“Inasikitisha sana”
Haraka akabebwa na kupakiwa ndani ya gari jingine hadi hospitali ya TMD ambako alipokelewa na wauguzi, haraka akaingizwa chumba cha daktari ambaye bila kuuliza barua ya polisi namba tatu alianza kumpima, akagundua moyo wake ulikuwa bado ukipiga kwa mbali lakini alihitaji haraka sana kupelekwa chumba cha wagonjwa mahututi ili aunganishiwe mashine ya hewa ya oksijeni wakati mipango mingine ikiendelea, hilo likafanyika na madaktari wakakutana kwenye chumba hicho kujadili juu ya hatua za kuchukua.
“Urgent chest X-ray, abdominal Ultrasound and head CT-Scan, ok?” (Haraka sana apigwe picha ya kifua, tumbo na kichwa, sawa?) Dk. Nilesh Kumar, bingwa wa masuala ya mifupa aliongea baada ya kumwona mgonjwa na kumpima, hakuwa ameumia sehemu yoyote ya miguu lakini tumbo lake lilikuwa limevimba kuashiria kwamba damu ilikuwa ikivuja ndani.
“There are signs and symptoms of Internal bleeding!” (Kuna dalili za damu kuvujia ndani)
“While we are doing everything we can to save life, start a normal Saline drip, 30 drops per minute, run it as fast as possible, raise the lower parts of the bed so that more blood can go to the brain, ok?” (Wakati tunafanya kila kinachoweza kuokoa maisha, anzisheni dripu ya maji ya chumvi, pelekeni matone 30 kwa dakika, ikimbizeni kadri mnavyoweza, pia nyanyueni miguu ya kitanda ili damu nyingi zaidi iende kichwani, sawa?)
“Yes doctor, but we have a problem!” (Ndio daktari, lakini tuna tatizo?)
“What is it?” (Nini?)
“The oxygen machine!” (Mashine ya hewa ya oksijeni)
“What it the matter?” (Nini tatizo?)
“It is not working!” (Haifanyi kazi)
“Oh! My God, what a bad luck! I just used it yesterday” (Mungu wangu! Hii ni bahati mbaya kiasi gani, niliitumia jana tu)
“That is the truth, we have tried it so many times in vain!” ( Huo ndio ukweli, tumejaribu kuitumia lakini hakuna mafanikio!)
“What can we do?” (Tufanye nini?)
“As far as I know, there is nothing we can do here, because we have only one oxygen machine and the patient is in need of oxygen if we want to save his life, he is turning blue!” (Kwa ninavyofahamu hakuna tunachoweza kufanya hapa, kwa sababu tuna mashine moja tu ya oksijeni na mgonjwa anahitaji hewa hiyo haraka kama tunataka kuokoa maisha yake, tazama anabadilika kuwa wa rangi ya bluu!)
Ni kweli hali ya Gilbert ilikuwa imezidi kuwa mbaya, bila hewa hiyo kupatikana haraka iwezekanavyo, maisha yake yalikuwa hatarini! Tayari alishaanza kubadilika rangi na kuwa na ile ambayo madaktari huuita Cynosis, dalili kwamba mwili haukuwa na oksijeni kabisa hivyo kama isingepatikana lazima Gilbert angekufa.

Dakika tano tu baadaye wakati wakitafakari juu ya nini cha kufanya watu wa vipimo ambavyo daktari aliagiza vichukuliwe walifika na kuvichukua mara moja na majibu kutolewa haraka, kila kitu walichokuwa wamekiwaza madaktari kilikuwa hivyo hivyo, ni kama walikuwa wameona ndani ya mwili wa Gilbert kwa macho yao, mbavu zilikuwa zimevunjika na moja kulichoma pafu la kushoto, likasinyaa! Kiungo kiitwacho Dayaframu ambayo huwa kama kitenganisho cha tumbo na kifua na husaidia katika kupumua kilikuwa kimepasuka na kufanya sehemu ya utumbo mwembamba uhame kutoka tumboni na kuingia kifuani pia damu nyingi ilikiwa imemwagikia ndani ya tumbo, bahati nzuri hakuumia kichwani kabisa, ubongo wake ulikuwa salama.
“Lets shift this patient!” (Tumhamisheni huyu mgonjwa) Dk. Lupembe, mmoja wa madaktari katika hospitali hiyo alishauri.
“To?” (kumpeleka wapi?)
“Aga Khan, or else he will die before our eyes!” ( Aga Khan, vinginevyo atakufa mbele ya macho yetu)
Wote wakakubaliana juu ya jambo hilo, kwani picha iliyokuwemo ndani ya mwili wa Gilbert iliwatisha, alihitaji kukimbizwa chumba cha upasuaji haraka iwezekanavyo lakini chochote kisingeweza kufanyika bila kuwepo mashine ya oksijeni, uamuzi huo ulipokubaliwa gari la wagonjwa lilisogezwa karibu na Gilbert akiwa bado hajitambui akapakiwa king’ora kikaanza kulia na gari kuondoka kwa kasi kubwa. Hakuna aliyekuwa na uhakika kama Gilbert angepona.

Muuguzi mmoja wa hospitali ya TMD aliyemfahamu baada ya gari kuondoka alichukua kitabu cha simu na kuanza kutafuta namba ya kampuni ya WorldCom, alifahamu ni ya Gilbert, alipoipata alipiga na kuwapa taarifa kisha kuomba namba ya nyumbani kwake, pia akafanya hivyo na simu kupokelewa na mama mkwe wa Gilbert ambaye hakutaka kumwambia Salome kitu chochote akihofia kumwingiza kwenye matatizo, alichokifanya ni kupiga simu ofisini ambako alikuta tayari taarifa zilikwishafika, akawaomba wakamchukue ili aende hospitali kumwona mkwe wake, gari lilikuwa mbele ya nyumba dakika kumi na tano baadaye.
“Salome!”
“Naam mama”
“Naweza kukuacha kidogo?”
“Unakwenda wapi?”
“Nanyoosha miguu huko nje, nimekaa ndani kwa muda mrefu!”
“Hakuna shida mama, naondoka na Faith!”
“Kwanini usimwache tu na dada?”
“Hapana, acha nizunguke naye kidogo”
“Sawa mama lakini usichelewe sana”
“Nitajitahidi kuwahi!”
Baada ya kuaga mama huyo alimbeba Faith na kutoka hadi nje ambako alipanda kwenye gari la kampuni na safari kwenda hospitali ya Aga Khan ikaanza na ndani ya dakika ishirini nyingine, watu wote ndani ya gari wakiwa kimya huku baadhi wakilia, lilikata kona kuingia kwenye uzio wa hospitali ambako liliegeshwa na wote kushuka na kuanza kuulizia mahali alipokuwa mgonjwa, kwa umaarufu aliokuwa nao Gilbert ilikuwa ni rahisi mno kuonyeshwa chumba cha wagonjwa mahututi ambako hawakumkuta zaidi ya wafanyakazi wa WorldCom ambao walitangulia, wote walikuwa wakilia! Mama mkwe akajua jambo baya limetokea.
Mama huyo hakuweza kuyazuia machozi, fikra za mkwewe kufariki hazikuwa rahisi kuzibeba, alishindwa kuelewa angewezaje kumtunza mwanae Salome ambaye alikuwa hoi kitandani. Akiendelea kulia alifuatwa na Davis, mmoja wa mameneja wa kampuni ya WorldCom ambaye pia alikuwa rafiki mkubwa wa Gilbert, akanyanyuliwa na kwenda kukalishwa kwenye kiti. Uso wa Davis haukuonyesha huzuni sana, hiyo ilimpa matumaini.
“Pole mama!”
“Sijapoa, mpaka nifahamu ukweli juu ya Gilbert na msinifiche kitu, niambieni tu kama mkwe wangu amefariki!”
“Hajafariki mama, ila hali yake sio nzuri, tumwombe Mungu”
“Ameumia kiasi gani?”
“Kwa walivyoniambia madaktari, amepasuka viungo muhimu mwilini likiwemo pafu lake moja!”
“Yuko wapi?”
“Amekimbizwa chumba cha upasuaji dakika kumi na tano zilizopita, madaktari wanajaribu kumsaidia!”
“Mungu amsaidie mkwe wangu, ni mtu mwema sana!”
“Ndio dunia mama”

Chumba cha upasuaji cha hospitali ya Aga Khan kilikuwa na shughuli nyingi sana siku za nyuma lakini siku hiyo hali ilikuwa tofauti, madaktari na wauguzi walikuwa wakikimbia huko na kule kujaribu kuokoa maisha ya Gilbert aliyekuwa katika hali mbaya, pafu lake moja likiwa limepasuka, vile vile diyaframu hivyo kufanya kuhema kwake kuwe kwa shida, mwili wote ulikuwa umebadilika rangi na kuwa rangi ya bluu, bahati nzuri katika hospitali ya Aga Khan mashine ya oksijeni ilikuwa nzima, akawekewa puani na mdomoni hivyo kuendelea kuhema na muda mfupi baadaye ngozi yake ikakaa sawasawa! Wakati hayo yote yakiendelea, damu ilikuwa ikiingia kwenye mishipa yake kwa kasi, chumba nyingine ya maji nayo ilikuwa ikidondoka taratibu kuingia kwenye mkono mwingine huku madaktari wakiwa wamelifungua tumbo la Gilbert pamoja na kifua chake, wakihangaika kurekebisha.
“Give me an artery forceps quickly” (Nipatie mkasi wa kubania mshipa wa ateri haraka!) Dk. Mazula, bingwa wa upasuaji katika hospitali ya Aga Khan aliamuru na muuguzi aliyekuwa jirani akampatia chombo alichohitaji, akataka nyingine na nyingine na nyingine mpaka alipohakikisha kwamba mishipa yote iliyokuwa ikivuja damu imezibwa.
“Now give me scissors and sutures immediately, check all the vital signs and control fluid input and output, understand?” (Sasa nipatieni mikasi na nyuzi za kushonea haraka, pimeni mapigo yake ya moyo, kuhema na joto la mwili, pia hakikisheni mnadhibiti maji yanayoingia na kutoka mwilini mwake, mmenielewa?)
“Yes doctor!” (Ndio daktari)
“Mr. Msangi, are you sure of the anaesthesia you have administered?” (Bwana Msangi una uhakika na nusu kaputi uliyompa?)
“Yes doctor!” (Ndio daktari)
“Everything under control?” (Kila kitu kimedhibitiwa?)
“Yes doctor!” (ndio daktari)

Kila kitu ndani ya chumba cha upasuaji kilienda kama kilivyopangwa, hakuna aliyekuwa na uhakika kama Gilbert angetoka chumba cha upasuaji salama lakini Dk. Mazula alikuwa ameamua kujaribu kumsaidia kwa ujuzi wote aliokuwa nao, alikuwa ni daktari mzoefu ambaye kwa miaka karibu mitano alifanya kazi katika hospitali ya Tumbi Kibaha ambayo karibu majeruhi wote waliopatwa na ajali katika barabara ya Morogoro waliletwa kwa matibabu, alishakutana na wagonjwa wenye hali mbaya lakini si kama alivyokuwa Gilbert, utumbo kuhamia kifuani? Hiyo hata kwake ilikuwa mpya lakini hakutaka imkatishe tamaa wala kuonyesha wasiwasi.
Kwa masaa sita kamili Dk. Mazula, Dk. Msangi pamoja na wauguzi wote waliokuwepo chumba cha upasuaji walikuwa wima wakihangaika kuokoa maisha ya Gilbert, miguu ilikuwa imechoka kusimama lakini hawakuwa na jinsi, kilichowafurahisha na kuwatia nguvu ya kuendelea ni hali ya Gilbert, ilikuwa ikiendelea vizuri.

Damu ililkuwa imeacha kutoka na mapigo yake ya moyo yalikuwa yamekaa vizuri, kila mtu ndani ya chumba cha upasuaji alikuwa na furaha, Dk. Mazula alijisikia ushindi na akaamini uliotokea uliuwa muujiza. Mwisho wa saa ya saba, Gilbert alitolewa chumba cha upasuaji, Davis na wafanyakazi wengine walikuwa bado wakisubiri, mama yake Salome hakuwepo aliondoka mapema kumuwahi mgonwja nyumbani pia kumpeleka Faith kupumzika.
“Poleni sana kwa kusubiri muda mrefu!” Dk. Mazula aliwaeleza Davis na wenzake alipowakuta nje ya chumba cha wagonjwa mahututi.
“Ahsante, anaendeleaje mgonjwa wetu?”
“Huyu? Kapona! Nendeni mkaandae Mbuzi tu wa sherehe, Mungu amemsaidia”
“Amina, tunakushukuru sana daktari!” wote waliitikia na kubaki nje ya chumba hicho bila kuruhusiwa kuingia ndani mpaka saa tisa za usiku ndipo wakaamua kuondoka kwenda nyumbani ili warejee asubuhi kujua jinsi alivyoendelea, hata wao walikuwa na amani mioyoni mwao, Davis alimpigia mama yake Salome simu na kumpa taarifa juu ya kilichokuwa kikiendelea, yeye pia akafurahi.

****

“Mama!” Salome aliita.
“Naam mwanangu”
“Yuko wapi Gilbert?”
“Gilbert?”
“Ndio”
“Ofisini kwao waliniambia amepata dharura, alikuwa amesafiri kwenda Morogoro, mimi nikashindwa kukupa taarifa!”
“Kweli?”
“Ndio”
“Lakini nahisi kuna tatizo, kuna kitu nafichwa, tangu juzi ulipoondoka umebadilika sana mama, macho yako yananionyesha kabisa kwamba kuna siri unayo moyoni, ni bora uniambie kabla sijaambiwa na watu wengine!”
“Hakuna siri yoyote mwanangu!”
“Haya mama”

Hivyo ndivyo hali ilivyokuwa imetengenezwa na mama yake, hakutaka kabisa Salome aelewe kilichoendelea, redio na televisheni zote zilikuwa zimezimwa ili kumkatia mawasiliano maana vyombo vyote vya habari nchini Tanzania vilikuwa vikiongelea ajali ya Gilbert, uhusiano wake na Tecla na mimba aliyompachika, lilikuwa gumzo kila kona ya nchi, magazeti yalinunuliwa na kuja kutupwa nje ya lango nyumbani kwa Gilbert, mama mkwe wake akayatokota na kuyaficha, hakutaka kabisa Salome akutane na habari zilizoenea.

Siku iliyofuata mchana alipiga simu ofisini na kuomba gari impitie ili aende hospitali kumwona mgonjwa, alikuwa na hamu kubwa ya kuona hali aliyokuwa nayo mkwe wake. Saa nane kamili gari ilikuwa mlangoni, honi ikapigwa na mama akaaga kwamba alikuwa anakwenda ofisini kwa Gilbert kuulizia mahali alipokuwa, Salome hakuwa na kipingamizi, yeye mwenyewe alitaka sana kufahamu ukweli juu ya mume wake. Hospitalini kabla hajaingia chumbani, alikutana na Tecla naye akiwa amekuja kumwona mgonjwa, kwa pamoja wakaingia na kumkuta Gilbert ana nusu saa tangu arejewe na fahamu zake.
“Tecla!”
“Ndio”
“Umekuja kufanya nini?”
“Kukusalimia”
“Sitaki kukuona, umeniharibia maisha yangu kiasi cha kutosha, sasa naomba usinifuatilie, najua lengo lako ni kuniua lakini imeshindikana!”
“Sio hivyo Gilbert, nimekuja kukuona lakini pia kukuambia suala la mimba hii ni lazima tulishughulikie, huwezi kuniruka wakati mimba ni yako!” Tecla aliongea bila aibu mbele ya mama mkwe wake Gilbert.
“Shikamoo mama!”
“Marahaba hujambo mwanangu?”
“Sijambo mama, mke wangu anaendeleaje?”
“Hajambo!”
“Pole sana”
“Ahsante mama, naomba uyapuuze maneno yaliyosemwa na huyu binti, ni uongo mtupu!”
“Uongo gani?” alisema Tecla kwa sauti ya juu ambayo ilifika moja kwa moja hadi ofisini kwa wauguzi, wakaja mbio na kumkuta amesimama huku akifoka na kudai mimba aliyokuwa nayo ni ya Gilbert.
“Sawa hata kama ni mimba ya Gilbert mwache basi apone kwanza, mwenzako ndio ametoka chumba cha upasuaji masaa machache tu yaliyopita, kwanini unamsumbua? Au tukuitie polisi?”
“Hapana!”
“Basi ondoka!”
Tecla akaondoka bila kuangalia nyuma, mwili ukiwa umemvimba kwa hasira.

***
Saa nzima na nusu baada ya mama yake Salome kuondoka Amanda na Christiane, marafiki wakubwa wa Salome waliokuwa safiri Afrika Kusini kwa muda mrefu walifika, kila mmoja akiwa na gazeti lake mkononi. Aliyewapokea mlangoni alikuwa mlinzi, kwa sababu aliwafahamu hakuwazuia akawakaribisha mpaka ndani ambako walinyoosha moja kwa moja hadi chumbani kwa Salome wakiongozwa na mtumishi wa ndani, alipowaona alifurahi mno.
“Pole shosti”
“Ahsante”
“Pole mbili ya kuugua, na hii ya kwenye gazeti!”
“Ya kwenye gazeti ipi tena?”
“Hujasoma?”
“Kwani kuna nini?”
“Si mumeo kamp…!” Amanda akasita.
Je, nini kitaendelea? Fuatilia siku ya

ENDELEA KUTEMBELEA NA KULIKE >>www.facebook.com/2jiachie

No comments

Powered by Blogger.