ad

ad

OKWI ATUA DAR KIMYAKIMYA SAMBA SC YATAJWA, AFICHWA DAR


Na Saleh Ally
HUKU kukiwa na taarifa kuwa uongozi wa Yanga umeamua kuachana naye, kiungo mshambuliaji Emmanuel Arnold Okwi, ametua jijini Dar es Salaam kimyakimya.
Okwi ametua kimyakimya kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), hali inayosababisha mkanganyiko wa mambo.

Wakati watu wengi wanaamini Yanga imeamua kuachana naye, kumekuwa na taarifa kuwa watani wao, Simba wako katika harakati za kumrejesha katika kikosi chao.
Okwi alitua nchini juzi saa 5:30 usiku kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (KQ) na kupokewa, halafu akaingia kwenye gari huku akiwa hataki kuzungumza lolote.
Mganda huyo alikuwa amevaa kofia ambayo alijaribu kuiziba asipigwe picha. Baadaye aliingia kwenye gari la kifahari na kuondoka uwanjani hapo. Imeelezwa amejichimbia kwenye moja ya hoteli za kitalii za jijini Dar es Salaam.

Akipokewa na wenyeji wake.
Hofu inazidi kwamba huenda kuna mpango wa kujiunga na Simba, lakini rafiki yake wa karibu ameliambia Championi Jumamosi kuwa, Okwi amekuja kumalizana na Yanga kujua kama wanamhitaji au la kwa kuwa siku zote amekuwa akitaka kuja lakini ikawa inashindikana.
“Okwi ameamua kuja huko kwa nauli yake mwenyewe. Unajua Yanga hawajatoa hata senti, lakini kiustaarabu amewafuata ili wamueleze kama wanamhitaji aendelee au la, basi ajue la kufanya.
“Okwi hataki ugomvi kabisa, nakuambia kuna timu moja ya Misri inamhitaji, lakini amekuwa akikataa kufanya mazungumzo na akawaambia wawasiliane na Yanga. Yeye anafuata taratibu, wao Yanga ndiyo hawataki kumsikiliza,” alisema rafiki huyo na kusisitiza:
“Kama Yanga hawamtaki, wangemuambia ili achukue njia nyingine. Mwenyewe ni mtu anayetaka kuendelea kufanya kazi na hao Yanga, ila hawaelewi.”
Kuhusu hilo, jana mchana Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu, alikiri kuwa na taarifa na ujio wa Okwi.
“Kweli amekuja na hatujamlipia nauli, tunajua Fufa (Shirikisho la Soka Uganda) ndiyo wamemlipia. Hata kwa (Hamis Kiiza) ilikuwa hivyo. Unajua sisi (Yanga) tuliwakatia tiketi za kwenda na kurudi Uganda.
“Likatokea tatizo, Shirika la Ndege la Uganda likafungiwa na tiketi zetu zimefia huko. Sasa Fufa wameamua kutusaidia. Suala la Okwi litashughulikiwa na kamati ya mashindano iliyo chini ya Seif Ahmed ‘Magari’, ambao walikuwa safarini lakini kesho (leo) wanaweza kukutana na kulishughulikia na kupata mwafaka,” alisema Njovu.
Tayari Yanga ina wachezaji wanne wa kimataifa (Haruna Niyonzima, Mbuyu Twite, Jaja na Coutinho), wakati Kiiza na Okwi wanawania nafasi moja iliyobaki. Okwi alibaki Uganda akitaka apewe fedha yake iliyobaki.
Lakini baadaye mchana Championi Jumamosi lilimpata na kuthibitisha haya: “Nisingependa kuzungumza mengi kwa sasa, lakini nimekuja kuzungumza na Yanga. Sikuwahi kukataa kuja, ila kuna mambo lazima yawekwe sawa. Tukimalizana, mtapata taarifa.”
Kama Okwi atashindwana na Yanga, maana yake atajiunga na timu hiyo ya Misri inayomtaka na kwa mzunguko huo, maana yake zile fedha Sh milioni 480 ambazo Simba inaidai Etoile du Sahel ya Tunisia, itakuwa basi.
Kwani inaonekana atakuwa ameuzwa zaidi ya mara moja na fedha hizo ambazo mwenyekiti wa wakati huo, Ismail Aden Rage alishindwa kuzichangamkia, zitakuwa zimepotea

No comments

Powered by Blogger.