Kumbe Vikiungwa Vitamu - 02
Lakini nilimuomba Mungu usiku na mchana ili aniepushe na mataanio ya wanaume. &&&& Japo nilikuwa na furaha ya kupata kazi kwenye ofisi, lakini bado moyo wangu ulikosa raha kutokana na kuwa na bahati ya kupendwa lakini mkosi wa kuachwa. Lakini nilijipiza moyoni kuwa na msimamo wa kutojirahisi kwa wanaume yoyote.
Baada ya taarifa zile shoga yangu aliondoka na kuniacha nikijipanga kwa ajili ya siku ya pili. Niliapa tena kutomkubalia mwanaume yoyote kimapenzi kutokana na kujijua nina kasoro ambayo sikuifahamu. Mwanzo nilikuwa nikisimama mbele ya kioo na kujiangalia niliona mwanamke mzuri kuliko wote. Hata nilipotipa mbele za watu, watu waliumia shingo kunitazama, wenye pesa waligongana. Nilimchagua niliyempenda lakini mwisho wa siku walinitema kama ganda la mua. Lakini sasa hivi hata kusimama mbele ya kioo naona udhia sikuwa na kipya, sikujua sababu ya mimi kugeuzwa mpira wa kona kila mmoja anataka kufunga na akifunga hana hamu tena na mimi. Nikiwa katika lindi la mawazo mara aliingia Bi Shuu bila hodi kama kawaida yake. Alipofika alisimama mbele yangu kama jini wa kutumwa, kwa sauti ya nyodo alisema. “Hivi Manka utaendelea kuwa tegemezi mpaka lini?” “Mbona sikuelewi Bi Shuu, mbona leo umenishupalia hivyo mtoto wa mwenzio?” Nilijikuta namtolea uvivu maana toka asubuhi amekuwa na mimi huku akizidi kunikosesha raha bila kosa. “Hujui?” Aliniuliza kwa jicho la kukata.
”Kujua nini Bi Shuu?” “Baada ya kukueleza ujitume katika maisha yako unaona nakuonea, badala yake unampigia simu shoga yake. Hujisikii aibu mwenzio ana maisha yake utaendelea kuomba mpaka lini?” Mmh, makubwa nilijikuta nikimshangaa Bi Shuu kwa kunishupalia kwa maneno bila sababu, hata bila kujua Mage alikuja kufanya nini yeye ananibwatukia. Au sababu nipo kwake kanigeuza mtoto wake. “Bi Shuu leo naona umeniamkia.” “Sijakuamkia bali nakupa makavu, chungu lakini dawa.” “Unajua shoga yangu kaniletea nini?” Nilimuuliza huku nikumtazama jicho kali. “Kuna kingine zaidi ya kukuletea ya pesa za kodi, hivi hujiulizi mwenzako anaishi vipi na mumewe muda wote na wewe kwa nini umekuwa kama ubao wa shabaha kila mwanaume akionja arudi una tatizo gani mtoto wewe wa kike?” “Lakini Bi Shuu, shoga yangu hakuleta pesa alikuja na mengine kabisa.” “Mankaaaa weweee, unataka kunidanganya mtu mzima mimi niliyeona jua kabla yako.” “Bi Shuu unanionea, shoga yangu hakuniletea hela.” “Haya nieleze amekuletea nini?” “Taarifa ya kazi.” “Kazi! Wapi?” “Kwenye kampuni ya rafiki ya mumewe.” “Mmh, kazi gani?” “Ya secretary wa bosi.” “Mmh, kama nakuona vile, kama kweli chumba utaendelea kukaa bure sitaki hata senti tano yako. Shida yangu kubwa ujishughulishe si kingine ndiyo maana hata hao wanaume niliwatafuta ili upate chochote na ikiwezekana upate mume miongoni mwao.” “Nashukuru Bi Shuuu, niombee niipate hiyo kazi.” “Si umesema kila kitu tayari?” “Eeh, pamoja na dua zako ni muhimu wewe ni mama yangu.” “Dua zangu zote kwako wala usiihofu utaipata.” Tulijikuta nimekuwa kitu kimoja tena kwa kuondoa tofauti za mwanzo, Bi Shuu alikenua mpaka gego la mwisho lilionekana baada ya taarifa zangu za kupata kazi. “Manka kaoge basi tuje tupate kifungua kinywa.” Nilikwenda kuoga na kuungana na Bi Shuu kupata kifungua kinywa, moyoni nilijiuliza bila kupata taarifa za kazi Bi Shuu angenifanya nini. Lakini nilimshukuru Mungu kwa muujiza alionifanyia wakati nilikuwa nimeisha kata tamaa. ******* Usiku kabla ya kulala nilitafuta nguo nzuri yenye heshima itakayofaa mbele ya macho ya watu. Kuhusu umbile na sura Mungu alinipendelea lakini sijui alininyima nini mwilini kiasi cha kuonekana Big G za Kichina ukitafuna kidogo utamu umekwisha. Baada ya kuchagua suti rangi ya bluu, niliinyoosha vizuri na viatu vyangu ambavyo nilivipiga kiwi tangu mchana niliviweka vizuri na kupanda kitandani. Saa kumi na mbili nilikuwa tayari nipo bafuni naoga, baada ya kuoga wakati najipamba mlango uligongwa. Nilijua shemeji amefika, kumbe alikuwa Bi Shuu nilipomuona nilitabasamu na kumkaribisha. “Bi Shuu karibu, mbona asubuhi?” “Hakuna cha ajabu, umeamkaje?” “Mmh, salama shikamoo.” “Marahaba, umeisha jipamba?” “Ndiyo Bi Shuu.” “Njoo mara moja.” Nilitoka hadi chumbani kwake, nilipofika nilikutana na kitezo kilichokuwa kikifuka moshi uliokuwa na harufu nzuri. Nilijiuliza vitu vile alivifanya wakati gani na alimfanyia nani au mimi. Nikiwa nimesimama nisijue alichoniitia aliniambia. “Manka chutama kwenye kitezo hicho,” mmh, makubwa madogo yana nafuu, nilifanya kama alivyoniagiza. Baada ya kuchutaka alitoa udi kwenye karatasi na kuuongeza kwenye makaa ya moto, baada ya kuuweka ulianza kutoa moshi wenye manukato mazuri. Alinipa shuka nijifushe, niliuinamia ule moshi ulionifanya ninukie kila kona ya mwili. Baada ya kujifusha alinieleza niufunike ule moshi na sketi kwa kuchutama moshi wote uliingia chini. Mtoto wa kike nilinukia kama malkia wa Kihindi, baada ya kuhakikisha nanukia kila kona alinipa pafyumu ambayo sikuwahi kuiona na kunipulizuia kidogo na mwisho alinipa wanjaa mwembamba kwa kunisaidia kunipaka. Kwa kweli nilipendeza mtoto wa kike. “Manka leo mwanangu umependeza,” Bi Shuu alinisifia. “Asante.” Wakati huo shemeji alikuwa amefika kwa kupiga hoi, kabla ya kuondoka Bi Shuu alinipa usia. “Manka Mungu kakujalia kila kitu alichotakiwa kuwa nacho mtoto wa kike, kama ningekuwa mtoto wa kiume ningekupata kwa gharama yoyote. Sasa usiwe macho juu. Hii inaweza kuwa nafasi ya pekee kupata bwana aliye bora ambaye atakuwa mumeo. Itumie nafasi yako vizuri, kazi njema.” “Asante, pia nimekusikia Bi Shuu yote nitayafanyia kazi.” “Basi kazi njema mmmwa.” Kwa mara ya kwanza Bi shuu alinibusu kuonesha furaha ya ajabu moyoni mwake. Baada ya kuachana na Bi Shuu alikwenda chumbani kwangu kupitia mkoba wangu kisha niliifuata gari aliyokuja nayo shemeji. Shemeji aliponiona tu alitanguliza sifa. “Hakika mke wangu umependeza.” “Asante mume wangu.” “Kwa mtindo huu nisije ibiwa tu.” “Ni wewe tu mume wangu, haya ni mapambo lakini upendo wangu kwako upo moyoni.” Nilijibu shemeji huku nikiingia ndani ya gari. Gari liliondoka huku utuli niliojinyunyizia ukitalawa ndani ya gari, baada ya kujuliana hali na shemeji aliniuliza maswali mawili matatu. “Mmh, shemu ulikuwa unaishije bila kazi maana mwenzio aliniambia siku hizi huchukui huduma?” “Bi Shuu kwa kweli alinilea kama mtoto wake.” “Sasa ungekaa kumtegemea mpaka lini?” “Ndiyo hivyo kazi zenyewe kila mtu anakutaka kimapenzi ukiwanyima inakuwa kero, nitawakubali wangapi?” “Ooh, pole.” “Sasa ni hivi kampuni ni ya rafiki yangu kipenzi hivyo nakuomba ujiheshimu ili kunilindia heshima yangu.” “Nakuahidi shemeji kujiheshimu.” “Itakuwa vizuri.” Tulipofika kwenye kampuni ya rafiki ya shemu tulitelemka na kuingia ndani, tulipofika tulipokelewa. Muda ule Mkurugenzi alikuwa hajafika tulikaribishwa kwenye makochi. Baada ya dakika kumi aliingia alipomuona shemeji walisalimiana kwa kukumbatiana. “Ooh, Aloys karibu sana.” “Asante Mr Shaka .” “Samahanini kwa kuchelewa.” “Bila samahani hatujafika muda mrefu.” “Basi karibuni ofisini.” Tuliongozana naye hadi ofisini kwake, mmh lilikuwa bonge la ofisi ambalo sikuwahi kuwaza kuingia katika ofisi kama ile. Nilibakia nang’aa macho mtoto wa kike kwa ushamba. Lakini niliuficha ushamba wangu, baada ya kutulia tuli kitini mwenyeji wetu ambaye nilimfahamu jina kwa kumsikia akiitwa na shemu Mr Shaka alikuwa akipitia vitu muhimu mezani kabla ya kutugeukia. “Mhu, Mista lete habari?” “Habari nzuri, huyu ndiye shemeji yangu,” alisema huku akinigeukia. “Ooh, mrembo kwanza nilisahau kukusalinia, za asubuhi?” “Nzuri tu.” “Pia hongera umependeza” ‘Asante.” “Basi kama ulivyoelezwa kazi ipo na unatakiwa kuianza mara moja, wala usihofu ugeni ila nitakuwa nawe pamoja muda wote.” “Nitashukuru kwa hilo.” Baada ya kupokelewa kazini shemeji aliaga na kuniacha kwenye kazi yangu mpya, baada ya kuondoka nilibaki nimeinama chini kama mwanamwali. Pamoja na ukali wa Bi Shuu bado alinipa mafunzo kwa mtoto wa kike kuinamisha macho mbele ya mwanaume. “samahani mrembo unaitwa nani” “Manka” “Manka nani Kileo” “Jina zuri” “Asante.” Mr Mateja alinyanyuka na kunishika mkono huku akisema. “Hebu njoo uanze kazi mama.” Alinipeleka katika computer iliyokuwa nje ya ofisi yake ilikuwa imekaa vizuri sana. “Basi hapa kuanzia leo ndio ofisi kwako.” “Nashukuru sana” Alinionesha kazi za kufanya siku ile, kabla ya kuanza nilijitetea. “Lakini bosi ni muda mrefu sijafanya kazi hivyo lazima nitakuwa mzito.” “Usihofu kwa hilo fanya kwa uwezo wako,” pia alinielekeza kutumia simu nikiwa nana shida ame nimelaliza kazi bila kumfuata ofisini kwake. “Asante bosi,” nilishukuru kwa upole na ukarimu wa bosi “Niite Mr Mateja” “Sawa Mr Mateja” “Nakutakia kazi njema.” “Nawewe pia” Baada ya kuondoka niiliingia kwenye kazi ya kuchapa kazi zilizokuwa wenye meza yangu. Hazikuwa kazi ngumu sana nilizifanya kwa muda mfupi sikuwa nimepoteza kasi ya mikono kihivyoo. Baada ya kuchapa kazi niliyopewa, niliziprinti kwenye karatasi na kuzipiga pini kisha nilimpelekea ofini. Nilimkuta bosi macho yapo kwenye monitor ya computer, nilimuona alinyanyua macho kunitazama. Aliponiona aliachia tabasamu pana, nakiri kuwa bosi wangu Mr Shaka alikuwa mwanaume mtanashati tena mwenye umbile la mvuto kwa mwanamke yoyote. Kule kutabasamu kwake kuliniweka katika wakati mgumu sana kwa kumuomba Mungu aniepushe na shetani wa upendo. Niliamini kama akinitaka kimapenzi jibu la sitaki litakosekana mdomoni mwangu, lakini nilipiga moyo konde kufuata kilichonipeleka ofisini kwa bosi. “Manka karibu.” “Asante bosi, kazi iliyokuwa na haraka nayo tayari.” “Ooh, vizuri sana sikutegemea ungeifanya kwa muda mfupi hivi.” “Najitahidi japo nilikuwa na muda mrefu sijagusa computer,” nilimjibu huku nikimkabidhi kalatasi, nami nikiachia tabasamu pana ambayo huogopa kuitoa kwa wanaume ili kuepusha ungongano wa mawazo. Ilikuwa ugonjwa wa wanaume kila ninapotabasamu mashavu huweka visima ‘dimples’ wanaume wengi ulikuwa uchawi mkubwa kwao. Kila mwanaume niliyekutana naye alipenda kunifurahisha ili aone madhari mantashau ya mashavu yangu.
ITAENDELEA SIKU YA JUMAMOSI

Post a Comment