ad

ad

She is too young to die -8


Ni tatizo juu ya tatizo,  balaa baada ya balaa! Pamoja na utajiri wote alionao Gilbert,  mke mwema na mrembo, maisha yanaonekana  kumwelemea. Baada ya kumwokoa mke wake aliyekwama kijijini sababu ya mafuriko huku akiwa  mjamzito,  mtoto aliyezaliwa anaanza kusumbua! Analia usiku na mchana,  kiasi cha kuwafanya Gilbert na mke wake washindwe kabisa  kulala usingizi. Wamekwishazunguka kwenye hospitali nyingi wakitibiwa lakini mtoto wao hapati nafuu pamoja na kuchomwa sindano zisizo na idadi mpaka kufikia hatua ya ngozi yake kuanza kubabuka!  Hatimaye wameamua kuzikataa sindano,  wakitaka kuelezwa ni kitu gani kinachomsumbua mtoto wao. Madaktari waliposhinikiza achome ndipo wakafikia uamuzi wa kuondoka naye kurejea nyumbani ambako mama yao anawaambia  kwamba tatizo la mtoto analifahamu,  ni la kijadi! Wote wanaanza kumdadisi ili awaeleze tatizo hilo ni nini? Je, nini kinaendelea leo? SONGA NAYO…

“Huyu mtoto wenu analilia jina!” Mama  yake Salome aliitikia.
“Analilia jina? Unamaanisha nini mzazi wangu?”
“Wakati mwingine watoto huzaliwa wakililia majina ya babu  au bibi zao walio hai au walikufa! Bila kuwapa  moja ya majina ya watu hao,  mtoto huendelea kulia kila siku na wakati mwingine anaweza hata kupoteza maisha yake,  haya ni mambo ya jadi lakini yana ukweli ndani yake,  mimi nimeshuhudia tangu utotoni ingawa huwa siyaamini sana, kweli mimi ni Mkristo lakini wakati mwingine huwa si vibaya kurejea kwenye mila zetu, kazi na dawa watoto wangu! Hatuhitaji kutupa kila kitu tulichokuwa nacho kabla wazungu hawajaleta Ukristo!” aliongea mama yake Salome akimpokea  mtoto Faith kutoka mikononi mwa mama yake.
Gilbert na mke wake wakaangaliana kwa mshangao,  maneno yote yaliyotoka mdomoni mwa mama yao hayakuonekana hata kidogo kuupenya bongo zao,  hayakuwa na ukweli wowote kila waliporejea katika mambo waliyojifunza shuleni na hata katika elimu ya dini! Waliona kilichosemwa ni kama uchawi na  hawakuwa sehemu ya jambo hilo.  Hata hivyo sehemu fulani akilini  mwa Salome, zilianza kuingia hisia  kwamba pengine kulikuwa na ukweli fulani katika kilichosemwa,  ukizingatia aliyekitamka ni mama yake  mzazi,  aliyemlea na kumkuza kwa taratibu hizo hizo.
“Mmenisikia?” mama Salome aliuliza.
“Ndio mama lakini mwenye uamuzi ni baba wa mtoto!”
“Baba unasemaje? Mtoto anateseka huyu!”
“Nimekusikia mama lakini mimi siamini sana katika mambo hayo, mama naomba usione kama nimekukatalia, la hasha! Nakuheshimu sana kama mzazi wangu lakini  naomba tu uache kwanza tujaribu tiba za hospitali na maombi kanisani,  tukishindwa basi tutaangalia unachokisema!” Gilbert alijibu akitumia busara zake zote kuhakikisha kwamba jibu lake halimuudhi mama mkwe wake.
“Sawa baba!” Mama Salome aliitikia ingawa kwa shingo upande.
Kilichofuata baada ya hapo ni kilio cha mtoto,  hawakulala usingizi! Faith alisumbua mpaka majirani wakamsikia,  wazazi wake walikesha wakipokezana,  hakuna hata mmoja kati yao aliyelala! Mtoto akihangaika kuhema na wakati mwingine kuzimia. Hawakuwa tayari kumrejesha tena hospitali kuendelea na sindano ambazo walizikataa lakini pia hawakuwa tayari kujikabidhi katika mila na desturi kisha kusafiri na mtoto  hadi  kijijini kwao Salome ambako sherehe ya kijadi ingefanyika kumpa Faith jina la mizimu! Gilbert  bado alimwamini Mungu ingawa mke wake alishaanza kutetereka kiimani.
“Kesho twende kanisani mtoto wetu akaombewe!” Gilbert alishauri.
“Niko tayari kwa lolote,  kwa hali aliyonayo mwanangu ukizingatia huyu ndiye mtoto pekee nitakayekuwa naye maishani, Gilbert,  sikufichi niko tayari kufanya lolote ili mradi Faith apone! Nitaishije mimi? Bila kuwa na mtoto? Gilbert niko tayari kwenda kumpeleka mbele ya Mchungaji na kuombewa, sijui ni wapi?”
“Kuna Mchungaji Buguruni  anaitwa Saru, Mungu anamtumia sana, watu wengi wanakwenda pale na matatizo yao yanakwisha!”
“Twende sasa hivi!”
“Hivi sasa ni saa tisa na nusu mke wangu,  lazima atakua amelala!”
“Tutamuamsha, tuna shida Gilbert, atatuelewa yule ni mtumishi wa Mungu, bila shaka yupo tayari kupokea watu wenye matatizo wakati wowote!”
“Sawa! Twende!”
“Mbebe mtoto!” Salome alimwambia Gilbert.
Wakaondoka chumbani na kufunga mlango nyuma yao, kwenye chumba alicholala mama yake Salome waligonga na alipofungua walimuaga kwamba wanampeleka mtoto kuombewa, kama alivyosema Gilbert, yeye pia aliwashauri waende asubuhi yeye  pia aliwashauri waende asubuhi lakini Salome alikataa katakata! Ikabidi mama aamue kuwasindikiza, wakatoka hadi nje na kuondoka ndani ya gari mpaka Buguruni Malapa kama walivyowahi kusikia kwamba hapo ndipo huduma ya mchungaji Saru ilipopatikana.
“Habari yako ndugu?” Gilbert alimsalimia Mmasai aliyeonekana kuwa mlinzi wa duka kando ya barabara.
“Msuri!”
“Tunaulizia nyumbani kwa mchungaji Saru!”
“Kwa ile msee inaombea watu napona?”
“Ndio!”
“Pita ile njia, kwenda moja kwa moja takuta mabanda ya bati! Hapo hapo ndio nakaa!”
“Ahsante, chukua hii!” Gilbert alisema akimkabidhi Mmasai huyo noti ya shilingi elfu tano, fedha kwake katika kipindi hicho ilionekana kutokuwa na thamani tena, mtu yeyote aliyempa msaada ndiye alistahili kula fedha yake.
“Ahsante msee!”
Wakati Mmasai huyo akishukuru wala Gilbert hakusikia, tayari alishaingia barabarani bila kuangalia kulia wala kushoto,  alichokisikia ni tairi za gari zikijivuta kwenye lami! Akakanyaga moto haraka na kuvuka kwenda upande wa pili akiliacha gari basi lililotaka kumgonga likielekea kwenye mtaro,  wala hakusimama ama kupunguza mwendo! Alizidi kukanyaga mafuta bila kuangalia nyuma akijua kusimama kwake kungefanya acheleweshe kumpeleka mtoto wake kwenye huduma. Mbele kama mita mia moja hivi, aliyakuta mabanda aliyoelekezwa na kuegesha gari  lake kando palipoonekana kuwa na  uwazi, haraka akashuka kwenda upande wa pili ambako alimchukua mtoto kutoka mikononi mwa Salome na kuwaomba wote washuke.
Watu walisikika wakiimba  nyimbo za kumsifu Mungu katika moja ya mabanda hayo, Gilbert akaongoza msafara kulisogelea banda hilo, mlango ulikuwa wazi hivyo hawakuhitaji kubisha hodi, wakazama moja kwa moja hadi ndani na kuketi kwenye benchi ndipo sekunde chache baadaye mwanamke mmoja wa makamo aliwafuata na kuwauliza shida yao.
“Tuna mtoto mgonjwa, tunahitaji kumwona mchungaji Saru ili amwombee!” Gilbert aliitikia, Salome hakuwa na uwezo wa kuongea,  muda wote alikuwa akilia huku moyoni mwake akijisikia  ni mtu mwenye bahati mbaya pengine kuliko wote waliopo duniani.
“Poleni sana, ni lazima yeye?”
“Tutajisikia vizuri zaidi tukimpata yeye!”
“Kijana wake je? Yeye pia ana uwezo mkubwa!”
“Sawa, subiri nikamuamshe!”
Mama huyo aliondoka kuelekea  gizani,  aliporejea aliongozana na mzee wa makamo aliyevaa nguo nyeupe,  walipomwona tu walifahamu huyo ndiye hasa waliyekuwa wakimtafuta! Salome akanyanyuka na kuanguka miguuni kwake huku akilia na kumwomba amsaidie kuokoa maisha ya mtoto wake pekee. Mzee huyo akamwinua Salome na kumsimamisha wima.
“Binti usinisujudie, yakupasa umsujudie aishie ndani yangu kwani huyo ndiye atakayempa mwanao uponyaji,  si mimi! Ukiwa na imani hakika utauona utukufu wa Mungu!”
“Ameni!” Wote waliitikia.
“Mtoto wenu anaumwa nini?”
“Analia tu!”
“Wala hana homa?”
“Ndio, yeye analia muda wote!”
Palepale mzee huyo aliweka mikono yake  yote miwili juu ya Faith na kuanza kumwomba Mungu atende muujiza,  katika hali ya kushangaza kabisa, Faith ambaye muda wote alikuwa akilia alinyamaza pale pale! Wote wakapigwa na butwaa,  mzee Saru akawaeleza wazi kwamba muujiza ulikuwa umetendeka,  pepo mbaya alikuwa ametoka hivyo walichotakiwa kufanya ni kuendelea kumwamini Mungu na kuomba, baada ya hapo aliwaruhusu warejee nyumbani kwani uponyaji ulikwishatokea.
Hakuna aliyekuwa tayari kuamini, mpaka wanafika nyumbani Faith alikuwa hajalia hata kidogo,  wakalala mpaka asubuhi bila kusikia kilio cha mtoto! Akinyonya kama mtoto mwingine wa kawaida,  haikuwa rahisi kumwambia  mtu kwamba  alikuwa mgonjwa na akakubali. Maisha yaliendelea hivyo kwa wiki mbili nzima, Gilbert akarejea kazini kwake ambako aliendelea kuwasimulia watu ushuhuda juu ya mambo ambayo Mungu aliwatendea.
Mwanzo wa wiki ya tatu,  wote wakiwa usingizini walizinduliwa na kilio cha mtoto wao,awali walifikiri ni hali ya  kawaida lakini alipolia mpaka asubuhi ya siku iliyofuata walielewa tayari tatizo limerejea,  wakahisi mmoja wao alikuwa amepungukiwa na Imani! Asubuhi hiyo walirejea kwa mchungaji na kumweleza shida waliyokuwa nayo,  akawaombea tena lakini safari hii Faith hakunyamaza,  aliendelea kulia ingawa kwa siku nzima walishinda kwa mchungaji Saru wakiombewa. Saa mbili na nusu ya usiku ndipo walirejea nyumbani ambako kilio kiliendelea mpaka asubuhi, mtoto akiwa hataki hata kunyonya na rangi ya ngozi yake hasa ndani ya midomo na macho ilikuwa ikibadilika kuwa  ya bluu.
“Tufanyeje mke wangu?”
“Nashauri twende hospitali!”
“Sawa, niko tayari!”
“Sasa twende hospitali gani?”
“Twende Sinza kwa  daktari mmoja wa watoto, anasifika sana!”
“Anaitwa?”
“Dk. Msomekela!”
Wote walikubaliana na kuondoka hadi Sinza Palestina ilipokuwa hospitali ya daktari huyo wakimwacha  mama mkwe nyumbani, wakaegesha gari  mbele ya jengo lililoandikwa  EMEN Hospital na kushuka  kisha  kutembea haraka hadi mapokezi ambako walipokelewa na msichana aliyevaa nguo nyeupe,  wakauliza kama walikuwa wamemkuta daktari waliyekuwa wakimtafuta.
“Ndio kaingia sasa hivi!”
“Tunaomba tumwone!”
“Subirini!” Alijibu msichana huyo na kuondoka.
“Gilbert”
“Ndio mke wangu!”
“Akisema kumchoma sindano tu tuondoke!”
“Sawa!”
Dakika mbili baadaye msichana alirejea na kuwakaribisha chumbani kwa daktari,  Gilbert akambeba mtoto mkononi na kuanza kumfuata msichana huyo,  nyuma yake akiwepo Salome. Walipoingia, macho yao yalikutana na mzee  mwenye uso ulijaa tabasamu,  aliyeongea kwa sauti ya upole ambaye aliwakaribisha vitini.
“Vipi?”
“Daktari mtoto anaumwa,  katusumbua sana!”
“Alianza lini?”
“Muda mrefu sasa!”
“Tatizo ni kitu gani? Hebu mlazeni hapa”
“Analia tu na  anahema kwa shida mno,  hataki kunyonya na anapoteza uzito halafu leo tunaona huku mdomoni na ndani ya macho yanakuwa na rangi ya bluu!”
“Hii kwa kitaalam inaitwa Cynosis,   yaani  hewa ya oksijeni inapopungua kwenye damu huwa kunajitokeza rangi ya bluu kwenye ngozi!” aliongea daktari akikisikiliza kifua cha Faith kwa kutumia kipimo ambacho kilichogusa kifuani huku akisikiliza masikioni, hakuchukua hata dakika tatu akanyanyuka na kukiondoa kipimo masikioni.
“Poleni sana!”
“Ahsante daktari!”
“Mtoto wenu anaumwa!”
“Nini?”
“Ana ugonjwa  unaoitwa PDA!”
“Ni nini daktari?” wote waliuliza macho yakiwa yamewatoka, hawakuwa na uhakika kama kweli  walikuwa tayari kulipokea jibu.

Gilbert na mke wake walikuwa wakitetemeka,  hofu kubwa ilikuwa imewapata, katika maisha yao hakuna hata mmoja kati yao aliyewahi kusikia neno hilo! Lilikuwa geni,   picha iliyowajia kichwani ni  kwamba huo ulikuwa ni ugonjwa mkubwa tena mpya kama ilivyokuwa kwa  magonjwa kama Homa ya Bonde la Ufa au Ebola. Waliendelea kumshuhudia daktari akimpima Faith kitandani, aliponyanyuka kuwaangalia kwa mara ya pili swali lao lilikuwa ni lile lile,  PDA ulikuwa ni ugonjwa gani.
“Ni maelezo marefu kidogo, kaeni kwenye kiti ili niwafahamishe!”
“Una tiba?” Gilbert aliuliza, hakuna kitu alichotaka kukifahamu  zaidi ya kupona kwa mtoto wake.
“Tulia Gilbert niwaelezeni, usiwe na haraka, tutafika tu huko!”

Wote wawili wakaketi kwenye viti vya mbao maarufu kama ‘office chair’ vilivyokuwa mbele ya  meza ya Dk. Msomekela ambaye usoni kwake wala hakuonyesha wasiwasi wowote,  tabasamu lilikuwa vile vile na sauti yake ya upole iliendelea kumtoka taratibu akiwaondolea wasiwasi. Ilikuwa ni kawaida ya madaktari kutoonyesha mshtuko hata kama mgonjwa alikuwa na hali mbaya kiasi gani, lakini kwa uzoefu wake Gilbert macho ya Dk. Msomekela yalimwonyesha wazi kwamba tatizo la mtoto wao lilikuwa kubwa.
“Tumetulia daktari tueleze sasa!”
“Kabla mtoto hajazaliwa, akiwa tumboni mwa mama yake huwa ana mfumo wake wa damu ambao hauchanganyiki kabisa na mfumo wa mama! Damu huwa inakutana kwenye kondo la nyuma tu ambako damu ya mtoto huja kuchukua hewa safi, chakula na kuacha hapo uchafu ili utolewe nje na mama! Hii inamaanisha kwamba kwa sababu hewa safi hutoka kwenye damu ya mama, mapafu ya mtoto huwa hayafanyi kazi…mnanisikia?”
“Ndio daktari tunakusikia!” Gilbert  aliitikia akimsikiliza daktari kwa makini,  Salome  wala hakusema chochote, machozi yalikuwa yakimbubujika na kulowanisha nguo zake! Alijisikia  miongoni mwa binadamu wenye bahati mbaya, tayari alishapoteza mfuko wake wa uzazi,  alishapoteza baba yake na sasa mtoto pekee ambaye angekuwa naye maishani ndiye  huyo aliyekuwa katika hali mbaya bila matumaini ya kupona.
“Salome!” Daktari aliita.
“Bee daktari!”
“Unanisikia?”
“Nakusikia daktari, lakini  napenda kufahamu kama mwanangu atapona!”
“Sikiliza kwanza, nataka mnielewe vizuri…!”
“Sawa!”  Salome aliitikia akijifuta machozi, muda huo huo Faith alianza kulia tena kwa sauti ya juu, akanyanyuka kwenda kumchukua kutoka kwenye kitanda alipomlaza na kuketi naye mikononi akijaribu kumpa titi ili anyonye lakini hakuwa tayari.
“Moyo una vyumba vinne,  viwili juu vinavyoitwa Atriums  na vya chini vinaitwa Ventricles, katika mwili wa binadamu mkubwa vyumba vya juu  husukuma damu kwenda kwenye vyumba vya chini kupitia kwenye valvu ziitwazo Bicuspid na Tricuspid, damu ikiwa  kwenye  chumba cha chini upande wa  kushoto husukumwa kuingia kwenye mshipa uitwao Pulmonary Vein kwenda kwenye mapafu kuchukua hewa safi na   iliyopo  kwenye chumba cha  chini kulia  ambayo huwa imetoka kwenye mapafu kuchukua hewa husukumwa kuingia kwenye mshipa uitwao Aorta kwenda sehemu mbalimbali za mwili! Mmenielewa?”
“Ndio daktari!”
“Sasa   hiyo ni kwa mtu mzima kama mimi na ninyi lakini  kwa mtoto mdogo mapafu huwa hayafanyi kazi, hivyo damu inayosukumwa kutoka kwenye chumba cha chini kushoto badala ya kwenda kwenye mapafu huingia kwenye mshipa wa Aorta, kupitia kwenye tundu liitwalo Ductus arteriosus na kupelekwa sehemu mbalimbali za mwili wa mtoto! Tundu hili hutakiwa kuziba muda mchache tu baada ya mtoto kuzaliwa na kulia ambapo mapafu huanza kufanya kazi, hivyo damu kuanza kupita kwenye mshipa wa Pulmonary Vein kwenda kwenye mapafu kuchukua hewa ya oksijeni, kwa bahati mbaya kwa baadhi ya watoto tundu hili huwa linagoma kuziba, ndipo PDA hujitokeza, PDA ni kifupi cha neno PATENT DUCTUS ARTERIOSUS, nikimaanisha tundu lililogoma kuziba, mmenielewa?”
“Ndio,  kwa hiyo mtoto wetu ana tundu lililogoma kuziba?”
“Dalili zote zinaonyesha hivyo,  hata hivyo itabidi nifanye kipimo kiitwacho ECG ili niweze kuona namna moyo unavyofanya kazi!”
“Ugonjwa huo una tiba?”
“Ni mpaka upasuaji!”
“Hapa nyumbani inawezekana?”
“Sio rahisi, lazima msafiri kwenda India tena haraka iwezekanavyo!”
“Mungu wangu!” Salome alijishika kichwani.
Daktari aliandika kwenye faili na kuagiza mtoto alazwe kwenye  chumba cha wagonjwa mahututi wakati vipimo vikifanyika, huko aliwekewa hewa ya oksijeni na mpira wa kula chakula kupitia puani huku akipewa dawa za kuuongeza moyo wake nguvu ya kufanya kazi! Masaa ishirini na nne  baadaye, Gilbert akiwa bado yuko nje ya wodi, majibu ya vipimo vyote yalitoka na kuonyesha alichokisema daktari kilikuwa sahihi, Salome aliposikia hivyo moyo wake ulianza kwenda mbio, akamtaarifu mume wake ambaye bila kuchelewa alimwambia daktari, akapimwa mapigo na kuonyesha yalikuwa yameshuka mpaka kufikia tisini chini ya sitini!
“Una presha ya kushuka?”
“Ndio!”
“Ngoja tukupe kitanda upumzike wakati mimi na mumeo tukiendelea na taratibu nyingine, hapa hakuna tunachoweza kufanya zaidi ya ninyi kusafiri haraka sana kwenda India vinginevyo tunaweza kupoteza mtoto,  tatizo lake limekomaa sana, alitakiwa kuwa amegundulika mapema lakini bahati mbaya madaktari mliopita mikononi mwao hawakugundua tatizo lake wakaendelea kumpa dawa ambazo hazikuwa sahihi!” alisema Dk. Msomekela na  alipokwishakutoa maagizo ya Salome kupewa kitanda pamoja na dawa za kumsaidia kupandisha mapigo yake,  yeye na Gilbert waliondoka kwenda moja kwa moja  Wizara ya afya kufanya mpango wa mgonjwa kusafirishwa kwenda India, waliporejea   dakika arobaini na tano baadaye walimkuta  Salome akiwa na hali nzuri kidogo.
“Vipi imekuwaje huko?”
“Hali ni mbaya, kuna wagonjwa  elfu moja wanaosubiri kusafirishwa! Hivyo kama sisi tunataka mtoto wetu aende kutibiwa ni lazima tukae kwenye foleni,   Faith awe wa elfu moja na moja! Sijui lini atapelekwa”
“Gilbert, tumia akili yako tuokoe maisha ya mtoto wetu, hatuwezi kuwa na mtoto mwingine tena!”
“Sawa, lakini nitafanyaje sasa? Acha nifikirie!”
Je, nini kitatokea? Watafanikiwa kuokoa maisha ya mtoto wao? Ni kweli,  She is too young to die!

No comments

Powered by Blogger.