ad

ad

She is too young to die - 7


Gilbert anafanikiwa kukodisha helkopta hadi kijijini Kahunda wilayani Sengerema ambako mke wake (Salome) mjamzito anayevuja damu vibaya,  amekwama baada ya mvua kubwa kunyesha na kuvunja madaraja pamoja na kuharibu miundo mbinu yote! Kwa helkopta hiyo anafanikiwa kumfikisha hospitali ya Wilaya ambako Salome anapokelewa na kukimbizwa  chumba cha upasuaji na kufanyiwa operesheni kumwondoa mtoto tumboni, bahati nzuri mtoto alikutwa yuko hai ingawa  dhaifu! Hali ya Salome ndio ilikuwa  mbaya, damu nyingi ziliendelea kumtoka,  juhudi za madaktari wote  zilishindwa kuizuia damu hiyo iliyotishia maisha ya Salome! Uamuzi uliofikiwa ni kuuondoa mfuko wa uzazi katika operesheni ambayo kwa kitaalam inaitwa Hysterectomy!

Gilbert alipoitwa na kupewa taarifa za mtoto wake kuwa hai alifurahi mno lakini baadaye alipoambiwa hali ya mkewe ilikuwa mbaya na kwamba ili kuokoa maisha yake ilikuwa ni lazima mfuko wa  uzazi uondolewe,  alishika kichwa chake kwa  huzuni, hakuwa tayari kuwa na mtoto mmoja tu maishani mwake!

Alipouliza  kama kulikuwa na utaratibu mwingine  Dk. Bisige,  bingwa wa upasuaji wa akinamama alimkatalia kabisa na Gilbert hakutaka kukubali kirahisi, akaomba  apewe msaada wa madaktari, wauguzi ili  kwa helkopta aliyokodi aweze kuwahamishia wagonjwa wake hospitali  kubwa ya Bugando ambako aliamini   kungekuwa na suluhisho jingine tofauti na kuuondoa mfuko wa uzazi wa mke wake,  jambo ambalo hata   yeye angekuwa na fahamu zake aliamini asingekubali.

Madaktari wakamkubalia na kumpa kila msaada alioutaka,  Salome akachukuliwa   huku chupa za damu pamoja na maji zikidondoka taratibu kuingia kwenye mishipa yake, vile vile mtoto wao ambaye aliwekwa ndani ya mashine maalum ya kuokolea maisha,  wote wakapakiwa ndani ya helkopta na Dk. Bisige akawasiliana na  daktari Mkuu wa hospitali ya Bugando na taarifa juu ya wagonjwa waliokuwa wakipelekwa.
Je, nini kitaendelea? SONGA NAYO…

Helkopta iliiacha ardhi ya Sengerema, ndani yake wakiwemo watu  tisa; Gilbert, Mwalimu Mchele, Mama yake Salome,  Salome na mtoto wake, wauguzi wawili pamoja na daktari mmoja.  Angani kazi ya  wauguzi na daktari ilikuwa kuangalia hali za wagonjwa, kuhakikisha damu ilidondoka vizuri na mashine za oksijeni zilifanya kazi  ipasavyo! Pamoja na kuwa mwanaume,  kwamba wanaume siku zote hawakutakiwa kulia,  Gilbert alishindwa,  aliinamisha kichwa chake miguuni kwenye kiti alichokalia na machozi yalikuwa yakidondoka kwenye sakafu ya helkopta taratibu.

Hakika alikuwa katika wakati mbaya kuliko mwingine wowote katika historia yake ya maisha,  hakuwa na uhakika kama mke na mtoto wake wangepona jambo ambalo hakutaka kabisa litokee,  kwani utajiri na mafanikio yote aliyokuwa nayo yasingekuwa na maana yoyote bila Salome! Hilo ndilo alilifahamu ndio maana alikuwa tayari kutumia chochote alichokuwa nacho kuhakikisha anapona na si hivyo tu bali pia hapotezi hata sehemu moja ya mwili wake.
Baada ya kuruka kwa dakika kumi, helkopta ilianza kushuka chini na baadaye mji wa Mwanza wenye milima ya mawe ukaonekana, Gilbert akanyanyua kichwa chake na kuchungulia nje,  majengo marefu    ya  hospitali ya Bugando  yalikuwa ya kwanza kuonekana mlimani, mwalimu Mchele aliyekuwa nyuma  yake akamwonyesha na kumwambia ndipo mahali walipokuwa wakienda.
“Ni hapo!”
“Wacha nimwambie rubani!”
“Napafahamu!” rubani alijibu kabla ya kuelezwa na kuendelea kuishusha helkopta chini kwa kasi.
Ilitua moja kwa moja kwenye sehemu ya wazi mbele ya lango kuu la kuingilia kwenye hospitali hiyo,  gari la wagonjwa likasogezwa karibu kabisa na  mlango na wauguzi wakapanda ndani wakiwa na machela, hazikupita hata dakika kumi wakaonekana wakishuka na  mgonjwa kwenye  machela ambaye  nusu ya mashuka aliyokuwa amefunikwa yalilowa damu na baadaye alifuatiwa na   mashine ndogo ambayo ndani yake  alilazwa mtoto mchanga, wote wawili wakapandishwa ndani ya gari la wagonjwa. Gilbert, mama yake Salome, Mwalimu Mchele nao walipanda ndani ya gari hilo hilo na likaendeshwa kwa kasi kuingia ndani ya hospitali kupitia mlango wa magari.
“Mshusheni haraka!” aliamuru mzee mmoja mfupi mnene mwenye kichwa chenye mvi nyingi.
“Sawa daktari!”
“Ndugu zake wako wapi?”
“Niko hapa!” Gilbert alijitambulisha.
“Njoo hapa ofisini wakati wakimshusha mgonjwa!”
Gilbert akamfuata mzee huyo nyuma hadi ofisini kwake ambako  alianza kuulizwa maswali juu ya hali ya mgojwa, naye akaeleza kila kitu alichokifahamu ingawa kwa kifupi. Wakati anamalizia tayari wagonjwa walishaingizwa ofisini,   daktari akanyanyuka kitini na kuamuru  Salome apandishwe kitandani,  akashangazwa na jinsi damu ilivyokuwa ikimwagika baada ya hapo akaomba barua ya rufaa kutoka  hospitali ya Wilaya Sengerema,  daktari waliyesafiri naye kutoka Sengerema akakabidhi.
“Hatuna la kufanya zaidi ya kumpeleka chumba cha upasuaji kumwondolea mfuko!”
“Mungu wangu! Daktari…!”
“Naam kijana!”
“Jambo hilo ndilo nimelikataa Sengerema!”
“Hakuna jinsi,  hapa inabidi uchague kuokoa maisha ya mkeo au…!”
“Hakuna namna nyingine?”
“Hakuna! Ninaomba usichelewe sana kufanya maamuzi, bila shaka unaona namna damu inavyomwagika,  hii ni aina mbaya kabisa ya  ugonjwa  uitwao Abruptio placenta! Ukichelewa sana mke wako atapoteza maisha” daktari alisema na Gilbert akainamishwa kichwa chake kutafakari,  dakika  moja baadaye alishtukia akiguswa begani akageuza kichwa chake kuangalia.
“Baba…” ilikuwa ni sauti ya mama mkwe wake.
“Naam mama!”
“Inabidi ukubali ili tuokoe maisha ya mkeo,  Mungu ndiye anayejua na mtoto mmoja pia anatosha kama hivyo ndivyo Mungu alivyopanga!” mama huyo aliongea kwa upole.
“Nimekubali! Daktari nimekubali!” alimwambia daktari aliyekuwa akiandika  mambo fulani kwenye faili.
“Haya mpelekeni mtoto chumba cha wagonjwa mahututi na  huyu mama mpelekeni moja kwa moja chumba cha upasuaji!”
“Sawa daktari!”
Hivyo ndivyo ilivyofanyika,  Gilbert  akatenganishwa na mtoto wake aliyepelekwa chumba kingine na  yeye, mwalimu Mchele na mama mkwe wake wakaifuata machela ambayo juu yake alilazwa Salome moja kwa moja hadi chumba cha upasuaji ambako Gilbert alipewa fomu ya kukubali  mke wake afanyiwe upasuaji  kuondolewe mfuko wa uzazi, hakuwa na jinsi, ingawa kwa shingo upande alikamata peni na kutia saini yake na  Salome akaingizwa chumba cha ndani zaidi.
 Hawakuondoka nje ya chumba hicho mpaka masaa manne baadaye,  kazi ikiwa moja tu kusali wakimwomba Mungu amsaidie Salome. Mlango ulipofunguliwa baada ya masaa hayo,  machela ilionekana ikisukumwa na juu yake akiwa amelala mgonjwa, wote wakainuka kumwangalia,   macho yao yaliwaambia ukweli kwamba mtu huyo  alikuwa ni Salome,  taratibu wakaanza kuifuata machela hadi chumba cha wagonjwa mahututi ambako walimkuta mtoto wao pia amelazwa kando ya kitanda alicholazwa Salome!
“Tumshukuru Mungu!” mama yake Salome aliongea baada ya wauguzi kuondoka akiwataka mwalimu Mchele na Gilbert wapige magoti chini kumwomba Mungu, wote wakasujudu  wakiwa wamekizunguka kitanda na  kuanza kusali wakimshukuru Mungu, baadaye walihamia kwenye kitanda cha mtoto na kufanya hivyo hivyo.
 Waliendelea kubaki ndani ya chumba hicho mpaka giza likaanza kuingia,  simu ya Gilbert ikaita na  alipoisikiliza ilikuwa ni sauti ya  Rubani akimtaarifu kuwepo kwake uwanja wa ndege wa Mwanza  baada ya kuruka kutoka  hospitali ya Bugando, Gilbert alimtaka aendelee kusubiri mpaka atakapompa maelekezo mengine. Hawakutoka hospitali mpaka saa sita za usiku,  wauguzi walipowaomba watoe nafasi ndipo Gilbert akawabusu Salome na mtoto wake kwenye mapaji ya nyuso zao na  wote wakaondoka hadi nje ya hospitali ambako walikodisha teksi iliyowapeleka moja kwa moja hadi katikati ya jiji la Mwanza na kupanga kwenye hoteli ya  Christmas Tree na kulala hadi asubuhi ya siku iliyofuata waliporejea hospitali na kumkuta Salome amefumbua macho.
“Gilb…ert!”
“Naam mke wangu!”
“Ume…okoa mai…sha yangu! Samaha…ni kwa usumb…ufu wote”
“Usijali huo ni wajibu wangu!”
“Shikamoo mama!”
“Marahaba hujambo?”
“Sijambo kidogo,  nawashukuruni sana kwa kila kitu!”
“Usijali!”
“Baba yuko wapi?”
 Si mama yake Salome wala Gilbert aliyekuwa na uwezo wa kujibu swali hilo,  ni kweli  Gilbert alifahamu  kilichotokea lakini asingeweza kumwambia mke wala mama mkwe wake! Aliamini  hiyo ingewaweka kwenye hali mbaya.  Salome aliposhinikiza kuelezwa   Gilbert  ingawa alifahamu kabisa kwamba mzee Magoma alifariki  dunia kwa kusombwa na maji ya mvua akiwa njiani kwenda nyumbani kwa Mkunga,  ilibidi adanganye kwamba mzee alibaki nyumbani kulinda mji.
“Kuna kitu kwenye macho yako Gilbert,  mimi nakufahamu huwezi kunidanganya, najua nikipona utanieleza ukweli!”
“Hakuna kitu mke wangu,  nafurahi kwamba umepona na sasa tunaye mtoto mzuri ambaye kwa kweli  kwa mambo yote yaliyojitokeza hatuna  jina jingine ambalo linamfaa zaidi ya kumwita Imani, au unaonaje?”
“Subiri nipone vizuri!”
Ilikuwa ni siku ya  furaha mno kwao, walitumia muda mwingi wakimshukuru Mungu,  Gilbert hakujali  fedha iliyotumika ili mradi alikuwa amefanikiwa kuokoa maisha ya  mtu ampendaye na zaidi ya yote mtoto  aliyekuwa tumboni mwa Salome!  Siku mbili baadaye, mwalimu Mchele aliaga kurudi nyumbani,  kwa kumshukuru kufuatia wema aliomtendea,  Gilbert alimpatia  shilingi milioni moja kama ahsante ndipo wakaagana.
Yeye  pamoja na mama mkwe wake waliendelea kuishi kwenye hoteli ya Christmas Tree kwa  mwezi mzima  wakimuuguza Salome na mtoto, hali ikawa nzuri na  wakaruhusiwa kutoka hospitali  kuungana nao hotelini ambako Gilbert hakuona sababu ya kuendelea kuficha juu ya kilichompata mzee Magoma,  akavunja ukimya na kuwaeleza kwamba mzee alifariki dunia usiku wa siku hiyo hiyo! Salome na mama yake waliangua kilio,  msiba ukaanza upya.
“Lazima nikaone mahali alipolala baba yangu!”
“Salome huoni hali ya hewa ilivyo mbaya?”
“Hapana Gilbert, baba yangu nilimpenda mno na alikufa akijaribu kunisaidia mimi,  lazima nirudi kijijini!”
“Hapana!”
“Nakuambia kweli mume wangu!”
“Hali ni mbaya,  mvua bado inanyesha sana na  barabara ni mbovu kila mahali katika mkoa huu!”
“Siwezi! Nakuambia siwezi,  kodisha tena helkopta!”
“Siwezi kukuruhusu tena urudi kijijini, unakumbuka wakati ule ulilazimisha mambo yakaharibika?”
“Ni kweli nakumbuka lakini ni  lazima nirudi kijijini,  angalau nikalione kaburi la baba!”
“Salome naongea kama mumeo,  haiwezekani!”
“Gilbert usipime heshima yangu kwako,  unanitia majaribuni!”
Kwa masaa mawili waliendelea kuvutana, Salome akimlilia baba yake  kwa uchungu na kudai alitaka kurudi kijijini angalau kuliona kaburi la baba yake mzee Magoma aliyetoa uhai wake kumfia akijaribu  kutafuta mkunga wa kumsaidia usiku wa mateso yake, bahati mbaya akachukuliwa na mafuriko na kufa mtoni! Gilbert alilipinga kabisa jambo hilo, alimpenda mke wake kuliko kitu kingine chochote na zaidi mtoto wao Faith, lakini kwa mahangaiko aliyoyapata akijaribu kumwokoa  hakuwa tayari  kuruhusu Salome arejee tena kijijini kwao. Walibishana mpaka mama akaingilia kati na kumsihi Gilbert alegeze msimamo kidogo.
“Mkeo alikuwa rafiki mkubwa wa baba yake, si rahisi akaacha hata kuliona kaburi lake, nakusihi baba umruhusu aende hiyo itasaidia kumpunguzia maumivu moyoni mwake!”
“Sawa mama lakini…!” Gilbert aliongea na baadaye kusita, dakika kama tatu zikapita bila kusema chochote  kichwa chake kikiwa kimeinamishwa,  alipokinyanyua  sekunde chache baadaye alimwangalia mke wake, wakagonganisha macho! Salome alikuwa amekusanya mikono yake yote miwili akimwomba Gilbert atoe ruhusa.
“Nimekubali, itabidi nipige simu Dar es Salaam ili  helkopta ije tena kwa ajili ya kazi hiyo!”
“Ahsante mume wangu!” Aliongea Salome akinyanyuka kutoka mahali alipokuwa amekaa na kumfuata Gilbert,  akamkumbatia kwa furaha.
Siku mbili baadaye helkopta  ilishawasili kutoka Dar es Salaam na  walikuwa juu ya mji wa Mwanza,  wakiruka kuelekea kijijini Kasheka nyumbani kwao na Salome,  hakuna aliyekuwa na furaha hata mmoja! Salome na mama yake walikuwa bado wakimlilia mzee Magoma,  kazi ya Gilbert ilikuwa ni  kujaribu kuwabembeleza  lakini faraja zake hazikufaa chochote,  kifo cha mzee huyo kiliwaumiza sana. Safari hii hawakutua shuleni  Bupandwamhela kama ilivyotokea mwanzo na kumchukua Mwalimu Mchele,  kilichofanyika walipokaribia kufika ni rubani kuishusha helkopta chini na kuanza kumuulizia Salome kama aliweza kupafahamu nyumbani kwao.
“Ni pale kwenye kile kilima, ile pale ni shule ya msingi Kasheka, naomba tu kama anaweza atue pale halafu tutembee kwa miguu kwenda nyumbani,  sio mbali sana!” alisema Salome na Gilbert akaufikisha ujumbe huo kwa rubani, helkopta ikatua shuleni ambako  dakika chache tu ilizungukwa na watu wakiishangaa,  ilivyoonekana katika maisha yao hawakuwahi kuona kitu cha aina hiyo.

Salome na mama yake walipoonekana, msiba ulianza upya, ndugu, jamaa na marafiki waliokuja kuona helkopta walibadilisha mtazamo,  wakaanza kulia kwa uchungu! Katika maisha yake Gilbert hakuwahi kuona watu wakilia kiasi hicho kwenye msiba,  ilibidi  mtoto amchukue yeye mwenyewe na wakaanza kutembea moja kwa moja kuelekea nyumbani kwao na Salome, kilometa kama moja hivi kutoka mahali helkopta  ilipotua!

 Huko ndiko mambo yalikuwa makubwa zaidi,  makumi ya watu waliokuwa wameshaanza kusahau juu ya msiba wa mzee Magoma,  walikusanyika  nyumbani kwake kuanza kuomboleza! Salome alilala kwenye kaburi la baba yake na kuendelea kulia kwa uchungu, juhudi za Gilbert akiwa amembeba mtoto  kumwomba anyanyuke haikuzaa matunda.
“Niache! Niache Gilbert,  acha nimlilie baba yangu, sitamwona tena!”
“Najua, lakini jaribu kujikaza kumbuka afya yako bado haijawa madhubuti!” Gilbert alisema maneno hayo lakini  hakuwa na uhakika kama Salome aliyasikia,  kwani  sekunde mbili baadaye aligundua alikuwa amezimia akaanza kuwaita  watu waje kumsaidia, akabebwa kupelekwa ndani ambako alimwagiwa maji na kuzinduka.

Kwa siku tatu  mfululizo walizokaa kijijini hapo wakipigwa na baridi,  Salome alizimia mara kwa mara na kumwagiwa maji. Jambo  lililomfanya  Gilbert aone  ilikuwa imetosha  kuomboleza na kumshauri waondoke kurejea Dar es Salaam ambako angechunguzwa afya yake vizuri na pia ya mtoto ambaye kila siku usiku alilia mfululizo, Gilbert akawa anahisi yawezekana alikuwa amepatwa na kichomi sababu ya baridi! Salome hakuwa na kipingamizi tena lakini akaomba aondoke na mama yake kwenda kuishi naye Dar es Salaam kwani hakuwa na mtu mwingine wa kumsaidia.

Kilichofanyika ni kulijengea vizuri kaburi la mzee Magoma kazi iliyochukua siku mbili zaidi, wakawaaga wanakijiji na   kuruka  hadi Mwanza ambako   rubani aliongeza mafuta na baadaye kuruka hadi  Kilimanjaro,  huko pia wakaongezea mafuta na kuruka tena  moja kwa moja hadi Dar es Salaam,   uwanja wa ndege walipokelewa na idadi kubwa ya wafanyakazi wa kampuni ya WorldCom pamoja na  marafiki,  waliowachukua katika magari hadi nyumbani kwao ambako Wachungaji wa  kanisa lao walijumuika na waumini wengine kwa maombi ya kumshukuru Mungu, Gilbert alipotoa ushuhuda wa mambo yaliyompata,  kwa wengi haikuwa rahisi kuamini! Siku mbili baadaye ilikuwa ni siku ya Jumapili, familia nzima ilikuwepo kanisani kutoa sadaka ya shukrani,  kila mtu aliyemwona Faith alimfurahia.
“Anafanana sana na baba yake ingawa ni mtoto wa kike!”
“Mbona bado mdogo mmejuaje? Hawezi kufanana na Gilbert, lazima afanane na mimi mama yake!”Aliongea Salome kwa  utani.
***
   Maisha yaliendelea vizuri baada ya hapo, Salome akijaribu kusahau  yaliyotokea,  fikra za kwamba asingezaa mtoto mwingine tena maishani mwake zilimwijia mara kwa mara lakini hakuruhusu zimuumize! Tatizo lililomsumbua ni mapigo yake kuwa yanashuka mara kwa mara na kusababisha azimie,  madaktari wa hospitali ya Regency alipotibiwa walishauri apumzike nyumbani na asithubutu kusafiri umbali mrefu wala kupanda ndege, kwani hiyo ingeweza kuhatarisha maisha yake. Wote wawili walikubali ushauri wa daktari na kumshukuru Mungu aliyewawezesha kusafiri kwa helkopta kutoka Mwanza hadi Dar es Salaam bila Salome kupata shida wakati tatizo lilianzia kijijini kwao wakati wa maombolezo ya baba  yake,  hii ilifanya  hata arobaini  ya mzee Magoma washindwe kusafiri kwenda kijijini zaidi ya kufanya ibada  na kutoa sadaka ya shukrani jijini Dar es Salaam.

Miezi sita baadaye,  Faith akiendelea kukua vizuri ghafla alianza kusumbua, akawa na tabia ya kulia mara kwa mara hasa nyakati za usiku na kuhema kwa shida. Walipompeleka hospitali ya watoto iliyoitwa Child Care Clinic iliyoko  maeneo ya Upanga jijini Dar es Salaam,  daktari alisema Faith alikuwa na kichomi kilichosababishwa na baridi kali iliyoharibi mapafu yake,  wote wakarejea baridi iliyompiga akiwa mtoto mdogo kijijini wakati  wa maombolezo.
“Inawezekana!” Daktari alisema baada ya kusikia historia hiyo.
“Kabisa!”
“Kama si hivyo basi yawezekana wakati wa kujifungua, mtoto alivuta maji maji yakaingia mapafuni!”
“Lakini alizaliwa kwa operesheni!”
“Yawezekana kuna tatizo lilitokea, akavuta maji!”
“Sasa tufanye nini daktari?”
“Ahaa! Hili ni tatizo dogo, tutampa dawa za kichomi lakini ni za sindano, atachomwa kwa muda wa siku tano baada ya hapo ataendelea na vidonge,  atakuwa safi kabisa!”
“Hakuna shida!”

Wakalipia matibabu na kuendelea na sindano kwa siku tano, shughuli za Gilbert zikawa zimesimama tena,  asingeweza kwenda ofisini wakati mtoto wake akiugua! Yeye na mke wake walihangaika pamoja. Siku tano zikakatika lakini Faith akiendelea kulia na kuhema kwa shida,  wakamrejesha tena kwa daktari ambaye aliamua kubadilisha dawa na kumpa dawa ya kuua wadudu mwilini ambayo ni kali zaidi ya ile ya mwanzo.
“Wacha nimpe Powercef, hii ni kali kuliko ya mwanzo lakini atapona tu!”
“Ahsante daktari nakusikiliza wewe!”
“Niaminini mimi, lakini itabidi alazwe!”
“Hakuna shida daktari, ninachotaka ni uzima wa mtoto wangu!” Gilbert aliongea kwa huzuni,  maisha yalikuwa yamembadilikia.

Kwa siku kumi na nne mfululizo Faith alilazwa hospitali,  siku tano za mwanzo alitundikiwa dripu  na tisa za mwisho akazimalizia kwa sindano za kuchomwa matakoni lakini bado hali ya mtoto  iliendelea kuwa dhaifu,  akilia usiku na mchana hata kunyonya hakutaka tena! Jambo lililofanya afya yake izidi kudhoofika na kupoteza uzito mkubwa zaidi kiasi cha kubaki na ngozi na mifupa! Gilbert hakutaka kupoteza muda zaidi katika hospitali hiyo, akaamua kumwondoa mtoto wake hadi hospitali ya Taifa Muhimbili ambako baada ya vipimo kufanyika bado mtoto alionekana kuwa na matatizo kifuani.
“What is the problem?” (Tatizo ni nini?) Daktari mmoja alimuuliza mwenzake.
“The child has history of  irritability!” (Mtoto ana historia ya kulia mara kwa mara)
“Investigations?” (Vipimo?)
“Normal  full blood picture, normal ESR, no Malaria Parasites,  but some  chest crepitations!” (Damu yake iko sawa, muda inaochukua kujichuja uko sawa, hakuna malaria lakini kifuani ana kelele kidogo!)
“What are you thinking about?” (Unafikiri nini?)
“Probably Pulmonary Pneumonia!” (Labda kichomi cha kifuani!)
“What is the past medical history?” (Historia yake ya huko nyuma ikoje?”
“Born by Caesarian  section,   has been  on various antibiotics like Powercef  but no improvement…” (  Alizaliwa kwa  upasuaji,  amekuwa kwenye dawa nyingi za kuua wadudu kama Powercef  lakini hakuna maendeleo…) alimaliza kuongea Dk. Malick,  bingwa wa  watoto katika hospitali ya Muhimbili.
“So?” ( Kwahiyo?) daktari mwenzake aliuliza.
“I will  have to retry Powercef ,  see the outcome!” (Nitajiribu tena Powercef nione matokeo yake!)
“No doctor,  you are not putting my kid on an injection again!” (Hapana daktari,  sitakuruhusu umweke mwanangu kwenye sindano tena!) Salome aliongea kwa uchungu akiwa amembeba mtoto mikononi.
“Ha! Sasa unataka tufanye nini?”
“Keshachoma sindano sana,  mpaka ngozi yake imeanza kubabuka, sitaki tena tafadhali niambieni kitu gani kinamsumbua mwanangu!”
“Hakuna kitu kingine cha kufanya!”
“Sindano tu?”
“Ndio!”
“Ahsante!” alijibu Salome na kunyanyuka akiwa amembeba mwanae mikononi,  akaanza kutoka  nje Gilbert akimfuata nyuma,   alipomfikia alimshika begani.
“Mbona unaondoka?”
“Nimekwishasema mwanangu hachomwi sindano tena!”
“Salome…!”
“Nimekwishasema,  alizochoma zinatosha!”
“Utamuua mtoto wetu, tuwasikilize madaktari!”
“Haiwezekani Gilbert,  mwanangu amebaki ngozi tupu,  nimechoka kuona machozi yake! Kumbuka huyu ni mtoto wangu pekee, sitapata mwingine tena!”
“Kama unalifahamu hilo, basi turudi hospitali!”
“Nimekwishasema sitaki, mume wangu kwanini hutaki kunielewa? Twende nyumbani!”
Gilbert hakutaka kumbishia tena,  alichokifanya ni kunyoosha moja kwa moja hadi kwenye gari,  wote wakapanda  huku Faith akiendelea kulia na kwenda moja kwa moja hadi nyumbani ambako mama yake Salome aliwapokea na kutaka kujua kilichotokea hospitali siku hiyo.
“Vipi?”
“Wanataka kumchoma sindano tena!”
“Sasa sikilizeni watoto,  kwa muda mrefu nimeaacha mhangaike lakini mimi nalifahamu tatizo la mjukuu wangu, si la kutibiwa hospitali haya ni mambo ya  kijadi!”
“Kijadi? Unamaanisha nini mama?” Gilbert aliuliza.
“Huyu mtoto wenu analilia jina!” Mama  yake Salome aliitikia.
“Analilia jina? Unamaanisha nini mzazi wangu?”
“Wakati mwingine watoto huzaliwa wakililia majina ya babu  au bibi zao walio hai au walikufa! Bila kuwapa  moja ya majina ya watu hao,  mtoto huendelea kulia kila siku na wakati mwingine anaweza hata kupoteza maisha yake,  haya ni mambo ya jadi lakini yana ukweli ndani yake,  mimi nimeshuhudia tangu utotoni ingawa huwa siyaamini sana, kweli mimi ni Mkristo lakini wakati mwingine huwa si vibaya kurejea kwenye mila zetu, kazi na dawa watoto wangu! Hatuhitaji kutupa kila kitu tulichokuwa nacho kabla wazungu hawajaleta Ukristo!” aliongea mama yake Salome akimpokea  mtoto Faith kutoka mikononi mwa mama yake.
Gilbert na mke wake wakaangaliana kwa mshangao,  maneno yote yaliyotoka mdomoni mwa mama yao hayakuonekana hata kidogo kuupenya bongo zao,  hayakuwa na ukweli wowote kila waliporejea katika mambo waliyojifunza shuleni na hata katika elimu ya dini! Waliona kilichosemwa ni kama uchawi na  hawakuwa sehemu ya jambo hilo.  Hata hivyo sehemu fulani akilini  mwa Salome, zilianza kuingia hisia  kwamba pengine kulikuwa na ukweli fulani katika kilichosemwa,  ukizingatia aliyekitamka ni mama yake  mzazi,  aliyemlea na kumkuza kwa taratibu hizo hizo.
“Mmenisikia?” mama Salome aliuliza.
“Ndio mama lakini mwenye uamuzi ni baba wa mtoto!”
“Baba unasemaje? Mtoto anateseka huyu!”
“Nimekusikia mama lakini mimi siamini sana katika mambo hayo, mama naomba usione kama nimekukatalia, la hasha! Nakuheshimu sana kama mzazi wangu lakini  naomba tu uache kwanza tujaribu tiba za hospitali na maombi kanisani,  tukishindwa basi tutaangalia unachokisema!” Gilbert alijibu akitumia busara zake zote kuhakikisha kwamba jibu lake halimuudhi mama mkwe wake.
“Sawa baba!” Mama Salome aliitikia ingawa kwa shingo upande.
Kilichofuata baada ya hapo ni kilio cha mtoto,  hawakulala usingizi! Faith alisumbua mpaka majirani wakamsikia,  wazazi wake walikesha wakipokezana,  hakuna hata mmoja kati yao aliyelala! Mtoto akihangaika kuhema na wakati mwingine kuzimia. Hawakuwa tayari kumrejesha tena hospitali kuendelea na sindano ambazo walizikataa lakini pia hawakuwa tayari kujikabidhi katika mila na desturi kisha kusafiri na mtoto  hadi  kijijini kwao Salome ambako sherehe ya kijadi ingefanyika kumpa Faith jina la mizimu! Gilbert  bado alimwamini Mungu ingawa mke wake alishaanza kutetereka kiimani.
“Kesho twende kanisani mtoto wetu akaombewe!” Gilbert alishauri.
“Niko tayari kwa lolote,  kwa hali aliyonayo mwanangu ukizingatia huyu ndiye mtoto pekee nitakayekuwa naye maishani, Gilbert,  sikufichi niko tayari kufanya lolote ili mradi Faith apone! Nitaishije mimi? Bila kuwa na mtoto? Gilbert niko tayari kwenda kumpeleka mbele ya Mchungaji na kuombewa, sijui ni wapi?”
“Kuna Mchungaji Buguruni  anaitwa Saru, Mungu anamtumia sana, watu wengi wanakwenda pale na matatizo yao yanakwisha!”
“Twende sasa hivi!”
“Hivi sasa ni saa tisa na nusu mke wangu,  lazima atakua amelala!”
“Tutamuamsha, tuna shida Gilbert, atatuelewa yule ni mtumishi wa Mungu, bila shaka yupo tayari kupokea watu wenye matatizo wakati wowote!”
“Sawa! Twende!”
“Mbebe mtoto!” Salome alimwambia Gilbert.
Wakaondoka chumbani na kufunga mlango nyuma yao, kwenye chumba alicholala mama yake Salome waligonga na alipofungua walimuaga kwamba wanampeleka mtoto kuombewa, kama alivyosema Gilbert, yeye pia aliwashauri waende asubuhi yeye  pia aliwashauri waende asubuhi lakini Salome alikataa katakata! Ikabidi mama aamue kuwasindikiza, wakatoka hadi nje na kuondoka ndani ya gari mpaka Buguruni Malapa kama walivyowahi kusikia kwamba hapo ndipo huduma ya mchungaji Saru ilipopatikana.
“Habari yako ndugu?” Gilbert alimsalimia Mmasai aliyeonekana kuwa mlinzi wa duka kando ya barabara.
“Msuri!”
“Tunaulizia nyumbani kwa mchungaji Saru!”
“Kwa ile msee inaombea watu napona?”
“Ndio!”
“Pita ile njia, kwenda moja kwa moja takuta mabanda ya bati! Hapo hapo ndio nakaa!”
“Ahsante, chukua hii!” Gilbert alisema akimkabidhi Mmasai huyo noti ya shilingi elfu tano, fedha kwake katika kipindi hicho ilionekana kutokuwa na thamani tena, mtu yeyote aliyempa msaada ndiye alistahili kula fedha yake.
“Ahsante msee!”
Wakati Mmasai huyo akishukuru wala Gilbert hakusikia, tayari alishaingia barabarani bila kuangalia kulia wala kushoto,  alichokisikia ni tairi za gari zikijivuta kwenye lami! Akakanyaga moto haraka na kuvuka kwenda upande wa pili akiliacha gari basi lililotaka kumgonga likielekea kwenye mtaro,  wala hakusimama ama kupunguza mwendo! Alizidi kukanyaga mafuta bila kuangalia nyuma akijua kusimama kwake kungefanya acheleweshe kumpeleka mtoto wake kwenye huduma. Mbele kama mita mia moja hivi, aliyakuta mabanda aliyoelekezwa na kuegesha gari  lake kando palipoonekana kuwa na  uwazi, haraka akashuka kwenda upande wa pili ambako alimchukua mtoto kutoka mikononi mwa Salome na kuwaomba wote washuke.
Watu walisikika wakiimba  nyimbo za kumsifu Mungu katika moja ya mabanda hayo, Gilbert akaongoza msafara kulisogelea banda hilo, mlango ulikuwa wazi hivyo hawakuhitaji kubisha hodi, wakazama moja kwa moja hadi ndani na kuketi kwenye benchi ndipo sekunde chache baadaye mwanamke mmoja wa makamo aliwafuata na kuwauliza shida yao.
“Tuna mtoto mgonjwa, tunahitaji kumwona mchungaji Saru ili amwombee!” Gilbert aliitikia, Salome hakuwa na uwezo wa kuongea,  muda wote alikuwa akilia huku moyoni mwake akijisikia  ni mtu mwenye bahati mbaya pengine kuliko wote waliopo duniani.
“Poleni sana, ni lazima yeye?”
“Tutajisikia vizuri zaidi tukimpata yeye!”
“Kijana wake je? Yeye pia ana uwezo mkubwa!”
“Sawa, subiri nikamuamshe!”
Mama huyo aliondoka kuelekea  gizani,  aliporejea aliongozana na mzee wa makamo aliyevaa nguo nyeupe,  walipomwona tu walifahamu huyo ndiye hasa waliyekuwa wakimtafuta! Salome akanyanyuka na kuanguka miguuni kwake huku akilia na kumwomba amsaidie kuokoa maisha ya mtoto wake pekee. Mzee huyo akamwinua Salome na kumsimamisha wima.
“Binti usinisujudie, yakupasa umsujudie aishie ndani yangu kwani huyo ndiye atakayempa mwanao uponyaji,  si mimi! Ukiwa na imani hakika utauona utukufu wa Mungu!”
“Ameni!” Wote waliitikia.
“Mtoto wenu anaumwa nini?”
“Analia tu!”
“Wala hana homa?”
“Ndio, yeye analia muda wote!”
Palepale mzee huyo aliweka mikono yake  yote miwili juu ya Faith na kuanza kumwomba Mungu atende muujiza,  katika hali ya kushangaza kabisa, Faith ambaye muda wote alikuwa akilia alinyamaza pale pale! Wote wakapigwa na butwaa,  mzee Saru akawaeleza wazi kwamba muujiza ulikuwa umetendeka,  pepo mbaya alikuwa ametoka hivyo walichotakiwa kufanya ni kuendelea kumwamini Mungu na kuomba, baada ya hapo aliwaruhusu warejee nyumbani kwani uponyaji ulikwishatokea.
Hakuna aliyekuwa tayari kuamini, mpaka wanafika nyumbani Faith alikuwa hajalia hata kidogo,  wakalala mpaka asubuhi bila kusikia kilio cha mtoto! Akinyonya kama mtoto mwingine wa kawaida,  haikuwa rahisi kumwambia  mtu kwamba  alikuwa mgonjwa na akakubali. Maisha yaliendelea hivyo kwa wiki mbili nzima, Gilbert akarejea kazini kwake ambako aliendelea kuwasimulia watu ushuhuda juu ya mambo ambayo Mungu aliwatendea.
Mwanzo wa wiki ya tatu,  wote wakiwa usingizini walizinduliwa na kilio cha mtoto wao,awali walifikiri ni hali ya  kawaida lakini alipolia mpaka asubuhi ya siku iliyofuata walielewa tayari tatizo limerejea,  wakahisi mmoja wao alikuwa amepungukiwa na Imani! Asubuhi hiyo walirejea kwa mchungaji na kumweleza shida waliyokuwa nayo,  akawaombea tena lakini safari hii Faith hakunyamaza,  aliendelea kulia ingawa kwa siku nzima walishinda kwa mchungaji Saru wakiombewa. Saa mbili na nusu ya usiku ndipo walirejea nyumbani ambako kilio kiliendelea mpaka asubuhi, mtoto akiwa hataki hata kunyonya na rangi ya ngozi yake hasa ndani ya midomo na macho ilikuwa ikibadilika kuwa  ya bluu.
“Tufanyeje mke wangu?”
“Nashauri twende hospitali!”
“Sawa, niko tayari!”
“Sasa twende hospitali gani?”
“Twende Sinza kwa  daktari mmoja wa watoto, anasifika sana!”
“Anaitwa?”
“Dk. Msomekela!”
Wote walikubaliana na kuondoka hadi Sinza Palestina ilipokuwa hospitali ya daktari huyo wakimwacha  mama mkwe nyumbani, wakaegesha gari  mbele ya jengo lililoandikwa  EMEN Hospital na kushuka  kisha  kutembea haraka hadi mapokezi ambako walipokelewa na msichana aliyevaa nguo nyeupe,  wakauliza kama walikuwa wamemkuta daktari waliyekuwa wakimtafuta.
“Ndio kaingia sasa hivi!”
“Tunaomba tumwone!”
“Subirini!” Alijibu msichana huyo na kuondoka.
“Gilbert”
“Ndio mke wangu!”
“Akisema kumchoma sindano tu tuondoke!”
“Sawa!”
Dakika mbili baadaye msichana alirejea na kuwakaribisha chumbani kwa daktari,  Gilbert akambeba mtoto mkononi na kuanza kumfuata msichana huyo,  nyuma yake akiwepo Salome. Walipoingia, macho yao yalikutana na mzee  mwenye uso ulijaa tabasamu,  aliyeongea kwa sauti ya upole ambaye aliwakaribisha vitini.
“Vipi?”
“Daktari mtoto anaumwa,  katusumbua sana!”
“Alianza lini?”
“Muda mrefu sasa!”
“Tatizo ni kitu gani? Hebu mlazeni hapa”
“Analia tu na  anahema kwa shida mno,  hataki kunyonya na anapoteza uzito halafu leo tunaona huku mdomoni na ndani ya macho yanakuwa na rangi ya bluu!”
“Hii kwa kitaalam inaitwa Cynosis,   yaani  hewa ya oksijeni inapopungua kwenye damu huwa kunajitokeza rangi ya bluu kwenye ngozi!” aliongea daktari akikisikiliza kifua cha Faith kwa kutumia kipimo ambacho kilichogusa kifuani huku akisikiliza masikioni, hakuchukua hata dakika tatu akanyanyuka na kukiondoa kipimo masikioni.
“Poleni sana!”
“Ahsante daktari!”
“Mtoto wenu anaumwa!”
“Nini?”
“Ana ugonjwa  unaoitwa PDA!”
“Ni nini daktari?” wote waliuliza macho yakiwa yamewatoka, hawakuwa na uhakika kama kweli  walikuwa tayari kulipokea jibu.
Je, nini kitaendelea? Siku ya keshohapa.

No comments

Powered by Blogger.