Ni mdogo mno kufa - 2
Anachelewa kurudi tofauti na walivyokubaliana, Gilbert akaanza kupiga simu akifuatilia lakini mawasiliano yakawa mabaya! Baadaye akaambiwa kwamba mvua kubwa imenyesha maeneo aliyokuwepo mkewe, madaraja yamevunjika na kuna mafuriko! Hakuna njia ya kutoka. Akitafakari nini cha kufanya ofisini kwake, ghafla anaingia askari kutoka kituo cha polisi cha kati na kumwambia alikuwa na habari za kusikitisha. Je, amekuja kumwambia nini? SONGA NAYO…
Kabla askari hajafungua mdomo kusema ujumbe aliokuwa nao, Gilbert alishajifunza kitu Fulani kutoka kwenye macho yake kwamba kulikuwa na habari ya msiba; pengine mke wake alikuwa ameaga dunia akijaribu kuondoka maeneo yaliyokumbwa na mafuriko ili awahi mjini kwenda kujifungua! Masikio ya Gilbert hayakuwa tayari kwa ujumbe huo, ulikuwa ni ukweli ambao hakutaka kuusikia. Hata hivyo akajitahidi kukaa vizuri kitini kusikiliza habari zilizodaiwa kwamba ni za kusikitisha. Kama mtoto wa kiume alikuwa tayari kwa lolote.
“Habari gani hizo za kusikitisha afande?” alimuuliza.
“Tumepokea polisi meseji leo asubuhi, yaani ujumbe kwa mawasiliano ya mtandao wa polisi kutoka kijijini Bupandwamhela ikitutaka tukutaarifu kwamba mkeo yupo katika hali mbaya, masaa matatu yaliyopita alishikwa na uchungu wa kujifungua katika hali ambayo siyo ya kawaida, akaanza kumwaga damu nyingi kuliko kawaida! Juhudi za kumchukua kumpeleka hospitali zimeshindwa kuzaa matunda kwa sababu barabara zote zilibomolewa na mafuriko, kifupi eneo hilo kwa hivi sasa ni kama kisiwa! Hawajui ni kwa njia gani watafanikiwa kumwondoa angalau kumfikisha hospitali ya Wilaya Sengerema kwenye huduma bora zaidi!”
“Mungu wangu weee!Nitafanya nini mimi? Mke wangu Salome, nilimshauri asiende kwao lakini hakukubali…unaona sasa! Afande naomba unishauri, nifanye nini?”
“Unachoweza kufanya labda ni kukodisha helkopta kama unaweza!”
“Wapi? Sina tatizo na fedha hata kidogo, nazitafuta usiku na mchana ili zinisaidie! Hivyo basi ni lazima niokoe maisha ya mke na mwanangu, iko wapi helkopta ya kukodi?”
“Nenda Coastal Airline, wanazo nyingi tu!”
“Sihitaji kwenda…!” alijibu Gilbert na kupiga namba ya Katibu Mhutasi wake akimtaka atafute kwenye kitabu cha simu namba ya kampuni hiyo ya ndege haraka na kuipiga.
Ndani ya dakika tano simu ya mezani kwa Gilbert iliita, akainyanyua na kuanza kusikiliza, alikuwa ni sekretari wake akimuunganisha na kampuni ya ndege ya Coastal Airline. Ingawa mwili wake haukuwa na nguvu, Gilbert alijitahidi na kuanza kuongea.
“Coastal Airline?”
“Ndio! Nikusaidie?”
“Naweza kupata helkopta ya kukodi?”
“Kwenda wapi?”
“Kahunda, Sengerema mkoani Mwanza!”
“Subiri nikuunganishe na watu wa mauzo…” aliongea msichana mwenye sauti nyororo, baadaye ukimya ukatokea ambao ulifuatiwa na sauti nzito ya mtu aliyejitambulisha kama Mohamed Jabir.
“Nimeambiwa unataka helkopta kwenda Kahunda?”
“Ndio!”
“Kufanya nini?”
“Mke wangu ni mgonjwa sana amekwama huko!”
“Ni shilingi milioni saba kwenda na kurudi!”
“Hakuna shida!”
“Basi njoo ofisini ulipie ili tuondoke!”
“Nakuja!” alijibu Gilbert, akachukua kitabu chake cha benki na kumtaka askari ashuke naye hadi chini.
Mapokezi alimtaarifu Katibu Mhutasi wake juu ya jambo lililojitokeza na kumtaka awataarifu wafanyakazi wengine juu ya safari aliyotegemea kuwa nayo siku hiyo, hakutoa maelezo zaidi ya hayo na kuanza kukimbia hadi kwenye lifti, wote wawili wakashushwa hadi chini ambako waliagana na Gilbert kuingia ndani ya gari lake aina ya Vogue na kuendesha kwa kasi hadi ofisi za Coastal Airline mtaa wa Che-mundugwao karibu na benki ya Posta, kabla gari haijasimama vizuri alishashuka na kuanza kukimbia kuelekea ofisini, .watu wote waliomwona wakifahamu kwamba yeye alikuwa ni nani walishangazwa kwa vitendo alivyofanya.
“Naitwa Gilbert kutoka WorldCom, muda mfupi uliopita nimeongea na mtu aitwaye Mohamed Jabir, nipo hapa kumwona yeye kwa ajili ya malipo ya Helkopta!”
“Taarifa zako tunazo lakini malipo hayafanyiki kwa Mohamed, nenda kwenye dirisha lile pale!” msichana wa mapokezi alimwonyesha Gilbert, akaondoka akikimbia ingawa kulikuwa na umbali wa kama mita kumi na tano tu hivi.
“Hatupokei hundi!”
“Nini?”
“Nasema hivi kaka hatupokei hundi, malipo yote ni taslimu, tulishapokea hundi nyingi mwisho wa siku zikaonekana akaunti hazina fedha! Kwa hiyo uongozi ulishaamua malipo yote ni taslimu”
“Dada hivi unafahamu unafanya kazi kwenye shirika la ndege?”
“Hata kama! Huo ndio utaratibu.”
“Mh! Naomba kuonana na bosi!”
“Hatakusaidia!”
“NAOMBA KUONANA NA BOSIIIIII!” Gilbert alifoka akipiga meza, watu wote waliokuwa jirani waligeuza shingo.
“Vipi kaka?” bwana mmoja wa Kiarabu alimuuliza Gilbert.
“Mke wangu anaumwa na nimekuja hapa kukodisha helkopta nimfuate halafu naambiwa mambo ya taslimu, nani anatembea na fedha mfukoni siku hizi? Mpigieni meneja wa benki yenu mmuulize kama akaunti yangu ina fedha au la!”
“Wewe ni Gilbert?”
“Ndio! Ukipenda unaweza kuniita WorldCom”
“Mimi naitwa Mohamed, Aisha pokea tu hundi yake huyu mzee haina matatizo…hawa ndio wazee wenyewe bwana!” aliongea mwanaume huyo akimwelekeza msichana wa kwenye ofisi ya malipo.
Akiwa amechanganyikiwa kabisa, Gilbert aliandika kiasi cha fedha kilichohitajika na kukabidhi hundi. Akachukuliwa moja kwa moja hadi uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere ambako yeye na rubani mwingine mmoja waliruka kwa helkopta, akifikiria kitu kimoja tu kichwani mwake; Salome! Masaa mawili na nusu baadaye, helkopta ilitua Mwanza kujaza mafuta, kutoka hapo ndipo wakaruka moja kwa moja kuelekea jimbo la Buchosa, kata ya Kahunda tarafa ya Nyehunge! Wakiwa juu waliweza kushuhudia namna ambavyo miundo mbinu ilikuwa imeharibiwa na mvua, madaraja mengi yalikuwa yamebomolewa na mafuriko yametambaa kila upande, hata sehemu ambayo watu walivuka kwa miguu kulikuwa na mtumbwi! Gilbert akapoteza kabisa matumaini ya kumpata mke wake. Saa nzima na nusu baadaye, rubani alimweleza kwamba tayari walishafika walikokuwa wakienda, Gilbert akatupa macho chini, hakuona dalili ya uhai, kila sehemu kulikuwa na maji. Machozi yakamtoka.
“Ningejua nisingemruhusu mke wangu aje huku!” aliwaza huku akilia, kwake fedha hazikuwa na maana wakati huo, alichohitaji ni mke wake.
Je, nini kitaendelea sku ya kesho...
:: SHARE nyingi na COMMENT bila kusahau LIKE ndizo zinafanya Chombezo hili kuwa likitoka kila siku na kwa muda muafaka
hapa www.facebook.com/2jiachie pekee.
Hakika si ya kukosa hii.
Wanaotakiwa kusoma chombezo hili ni kuanzia +18 tu!
Hairuhusiwi kunakili. Au kutoa hata neno kuhamishia kwenye kitabu,tamthiliya ama wall ya facebook,twitter,whatsapp na sehemu
nyingine pasipo idhini ya 2JIAHIE bu,tamthiliya ama wall ya facebook,twitter,whatsapp na sehemu nyingine pasipo idhini ya 2JIAHIE

Post a Comment