TAMBWE ABAKI SIMBA ACHOTA MILIONI 40
Mshambuliaji wa Simba, Amisi Tambwe.
STRAIKA wa Simba, Amissi Tambwe, ameingia kwenye orodha ya wachezaji wanaolipwa mishahara mikubwa zaidi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya Wekundu wa Msimbazi kuamua kumuongezea mshahara.
Simba imeamua kumuongezea mshahara Tambwe kutokana na kufanya vizuri kwenye ligi hiyo msimu uliopita. Alifunga mabao 19 na kuwa kinara wa mabao Tanzania.
Lakini taarifa nyingine zinadai kuwa, Simba imeamua kumuongezea mshahara kutokana na hofu ya kusaini timu nyingine, kwa kuwa alipotua hapa nchini wiki iliyopita na kuondoka jana Jumapili, inadaiwa alifanya mazungumzo na moja ya klabu za Tanzania.
Awali, Tambwe alikuwa akilipwa kiasi cha dola 800 ambazo ni sawa na Sh milioni 1.3 kwa mwezi, lakini sasa atakuwa akipata dola 2,000 (Sh milioni 3.4) ambazo ukizipigia mahesabu, utabaini kuwa kwa mwaka atakuwa akichota zaidi ya Sh milioni 40.
“Tumeamua kumuongezea mshahara Tambwe. Kikubwa ni kwamba tuliridhishwa na mchango wake kwetu msimu uliopita na yeye mwenyewe alidai nyongeza.
“Tumeona ni sawa tukimpa mshahara wa dola 2,000 kwa mwezi kwa kuwa anastahili kupata kiasi hicho,” kilisema chanzo cha habari cha kuaminika kutoka ndani ya Simba.
Nyongeza hiyo, inamfanya Tambwe awe mchezaji wa nane, sawa na Joseph Owino, miongoni mwa wachezaji wanaolipwa mshahara mkubwa zaidi nchini.
Anayeongoza ni Emmanuel Okwi wa Yanga ambaye analipwa dola 4,000 kwa mwezi, ambazo ni sawa na Sh milioni 6.7.
Wanaomfuatia Okwi ni mastaa wa Azam, Kipre Tchetche, Kipre Balou, Brian Umony, John Bocco na Aggrey Morris ambao wanapata Sh milioni nne kwa mwezi kila mmoja.
Beki kisiki wa Yanga, Mbuyu Twite, yeye anapata Sh milioni 3.6 kwa mwezi, wakati Owino anapata dola 2,000 sawa na Tambwe.
Wachezaji wengine wanaolipwa mishahara mikubwa kwenye Ligi Kuu Bara ni Frank Domayo ambaye Azam wanamlipa Sh milioni 3 kwa mwezi, Mrisho Ngassa wa Yanga (Sh milioni 2.5 kwa mwezi), Hamis Kiiza (Yanga-Sh milioni 2 kwa mwezi) na Amri Kiemba (Simba-Sh milioni 2 kwa mwezi).
Beki Gilbert Kaze wa Simba, mwenyewe anapata Sh milioni 1.2 kwa mwezi.
VIA CHAMPIONI
Post a Comment