ad

ad

NDOA YA FLORA MBASHA CHALI

 Flora Mbasha akiwa na mumewe Emmanuel Mbasha.
BAADA ya kudumu kwa zaidi ya miaka 10, imebainika kuwa ndoa ya mwanamuziki mahiri wa muziki wa Injili Bongo, Flora na mumewe Emmanuel Mbasha ipo chali kwa maana ya kuanguka huku ikidaiwa kuwa, kusimama imara tena inawezekana lakini ni kazi kubwa.
Hilo limejitokeza wiki moja baada ya madai ya mwanaume huyo kudaiwa kumbaka
shemeji yake na kesi ipo polisi.
 
Imeelezwa Flora na mumewe ambao walifunga ndoa Agosti 22, 2002 wamepita
katika migogoro mizito lakini wawili hao walikuwa wakiyamaliza kifamilia hadi
kufikia hili la hivi karibuni ndilo lililoziba mataumaini ya wawili hao kuishi kama mume na mke.
Chanzo kilicho karibu na wawili hao kimeeleza kuwa, mzizi wa wawili hao kugombana
ulichochewa na mwanamke mmoja (jina tunalo) ambaye alikuwa akikinzana na ushauri wa
Mbasha mara kwa mara.
“Kuna vitu Mbasha alikuwa akimshauri huyo mama lakini walikuwa wakipishana Kiswahili 
na hapo ndipo tatizo lilipokua hadi kufikia hatua ya kumwagana,” kilisema chanzo.
Flora na mumewe Emmanuel Mbasha wakiwa kwenye pozi.
TUJIUNGE NA MBASHA
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Emmanuel alizungumza na mwandishi wetu ambapo alikiri
 ndoa yake haina uhai tena na si rahisi kurejea katika hali ya kawaida licha ya kudai kuwa bado anampenda mkewe.
“Tulikuwa tunagombana sana na Flora lakini tulikuwa tukipatana ila mama… (anamtaja jina) alichangia ugomvi,
Flora naye alikuwa na nyendo zake mbaya, kuna wakati alikuwa anatoka kwenda
gym (sehemu ya mazoezi) anachelewa kurudi ikafika wakati na nguvu ya ndugu wa
mke ikawa kubwa kiasi cha kunizidi mimi na hapo ndipo mambo yalipofikia pabaya kabisa.”
FLORA ATIMKA NYUMBANI
Mbasha anaendelea: “Ugomvi ulizidi, ilifika wakati tulipishana kiasi cha yeye kuondoka
nyumbani na kwenda kuishi katika nyumba ya wageni kwa miezi kadhaa wakati huo.
“Ndani ya ugomvi huo nilisikia mengi, baadhi ya watu wananiambia mke wangu anaonekana na Prado na mwanaume mwingine mwenye pesa, iliniuma sana ingawa sijawahi kumuona moja kwa moja,” alisema Emmanuel.
Kuhusu ugomvi huo, hivi karibuni Flora alikaririwa katika vyombo vya habari akisema hana
 tatizo na mumewe na ameshasamehe na kusahau yote yaliyopita hivyo ajitokeze tu ili akajibu mashitaka ya kudaiwa kubaka binti wa miaka 17 yaliyofunguliwa.
“Mimi sina tatizo kabisa na mume wangu, nimeshasamehe yote yaliyopita, kuhusu
mashitaka ningeweza kuyafuta kama ningekuwa mimi ndiye niliyemshitaki,” alisema Flora.
FLORA ADAIWA KUHAMIA KWA GWAJIMA
Wakati gazeti hili likiendelea kusaka undani juu ya sakata hili, kuna chanzo kingine
kilipenyeza data kuwa baada ya ugomvi kuwa mzito, Flora alihamia kwa Mchungaji wa
Kanisa la Ufufuo na Uzima Dar, Josephat Gwajima ambako ndiko alikuwa akisali kila
Jumapili.
“Kwani nyinyi Global hamna habari? Flora amehamia kwa Gwajima Jumapili iliyopita,
 kwanza alihudhuria ibada jioni akaenda kuishi maana Gwajima ni mchungaji wake kwa sasa,” kilisema chanzo.
GWAJIMA ACHOMOA
Ili kupata mizani ya madai hayo, juzi Amani lilimpigia simu Mchungaji Gwajima na
kumuuliza kama kweli Flora amehamia kwake kufuatia ugomvi kati yake na mumewe
ambapo alikataa katakata.
“Flora hayupo hapa…mnataka niwaambiwe yuko hapa  halafu vyombo vya habari muanze
kuandika vibaya? Hakuna kitu kama hicho,” alisema Gwajima.
KWA NINI CHALI?
Ndoa kuwa chali ni ile ambayo imeanguka lakini inaweza kusimama tena tofauti na ndoa
kuvunjika. Global iliwahi kuandika NDOA YA THEA CHALI baadaye ikasimama tena.
Thea ni msanii wa filamu alifunga ndoa na Michael Sangu ‘Mike’ ambaye pia ni mwigizaji.
Flora na mumewe Emmanuel Mbasha wakilishana keki.
Wakati Emmanuel akizungumza na mwandishi wetu, alikiri kuwa Flora ameshamgeuka
na nguvu kubwa imemuingia ndani ya moyo wake hivyo kuna ugumu sana wa kurudiana.
“Flora ambaye nilitegemea awe msaada katika hili lakini amefikia steji ya kuacha
kunisikiliza, anasema haniamini, kwamba ninaweza kumfanyia lolote, sasa si bora kama
anataka tuachane kwa heri kuliko kuniundia zengwe ambalo linataka kunipeleka mimi jela?”
alihoji Mbasha.
Kutokana na mvutano huo pamoja na kesi hiyo ya kudaiwa kubaka inayomwandana Mbasha ni dhahiri kwamba kila mmoja hana imani na mwenzake tena hivyo suala la wawili hao kuishi kama zamani linakuwa gumu kuliko ngamia kupenya kwenye  tundu la sindano.
Emmanuel Mbasha alishitakiwa katika Kituo cha Polisi cha Tabata Shule, Mei 30, mwaka huu kwa madai ya kumbaka shemejie.Uchunguzi juu ya tukio hilo unaendelea hadi sasa shitaka ambalo mwenyewe amelikanusha.
CHANZO NI GPL

1 comment:

  1. may GOD help both of you...macho yenu yamefungwa....lait mngepata kuona mngelitambua ukweli.Flora chukua muda utafakari.bdo hujatambua yanayokuzunguka

    ReplyDelete

Powered by Blogger.