ad

ad

Kila Mtanzania sasa anadaiwa Sh600,000



Dodoma. Wakati Serikali ikibanwa na wabunge kwa kushindwa kutekeleza Bajeti ya
mwaka 2013/14 kutokana na kutegemea fedha za wahisani, Kamati ya Bunge ya Uchumi,
Viwanda na Biashara imesema deni la taifa limeongezeka kwa Sh8.2 trilioni kwa kipindi
cha miezi saba tu.
Ilisema jana kuwa hadi Juni, mwaka jana deni hilo lilikuwa Sh21.2 trilioni lakini hadi
Januari mwaka huu, deni hilo lilipaa hadi Sh29.4 trilioni na fedha hizo zimekopwa kwa
ajili ya kuendeshea warsha, semina, safari, mafunzo na matengenezo ya magari.
Akiwasilisha taarifa ya kambi ya Upinzani, Waziri Kivuli wa Fedha, James Mbatia alisema ukiligawanya deni hilo kwa idadi ya Watanzania milioni 45, kila mwananchi atakuwa
anadaiwa Sh600,000.
Kati ya Sh5.8trilioni za bajeti ya Wizara ya Fedha mwaka 2014/15, Sh4.3trilioni
 zimetengwa kwa ajili ya kulipa Deni la Taifa
Akiwasilisha taarifa ya Kamati, Mwenyekiti wake, Luhaga Mpina alisema Sh24.18trilioni
 ni deni la Serikali, Sh3.75trilioni ni deni la sekta binafsi na Sh1.15trilioni ni deni la
Benki Kuu Tanzania (BoT).
“Ongezeko hili la deni haliendi sambamba na kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo
na ujenzi wa miundombinu ya uchumi. Hali hii inajenga hofu kuwa huenda deni hili
limekuwa ni uchochoro wa ubadhilifu wa fedha za umma,” alisema Mpina.
Alisema licha ya Serikali mara kadhaa kueleza kuwa deni hilo ni himilivu, kuna viashiria vinavyoonyesha kuelemewa kwa taifa na mzigo mkubwa wa madeni.
“Mfano ni mapato ya ndani yamezidiwa na matumizi ya kawaida hivyo kuifanya
Serikali kukopa hata kwa ajili ya warsha, semina, safari, mafunzo na matengenezo ya magari,” alisema Mpina.
“Deni la Taifa sasa limefikia asilimia 47 ya Pato la Taifa na kwa kipimo cha bei ya sasa
deni la taifa limefikia asilimia 24, huku deni la nje pekee likiwa ni asilimia 19” alisema
 Mpina na kuongeza:
“Licha ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kuahidi kwa muda mrefu
kufanya ukaguzi maalumu wa deni la taifa, hadi sasa taarifa yake haijawasilishwa. Ni lini
taarifa hiyo itawasilishwa bungeni ili kuwawezesha wananchi kufahamu undani wa jambo hili?” alihoji.
Kamati hiyo pia iliilipua Serikali kwa kuuza mashine za elekroniki (EFD), kati ya
Sh600,000 hadi 700,000 kwa maelezo kuwa kiwango hicho ni kikubwa kwa mzunguko
 wa biashara ya mtaji wa Sh14 milioni kwa sababu mtaji wake hauzidi Sh5milioni.
Mpina alisema mashine hizo zinatakiwa kugawiwa bure kwa wafanyabiashara wenye
kipato chini ya Sh40milioni na kufafanua kuwa chombo hicho chenye taarifa muhimu za mapato ya Serik

Mpina alibainisha kuwa utafiti uliofanywa na Mtandao wa Kimataifa wa Global Financial Integrity (GFI), umebaini kuwa Tanzania inapoteza Sh3trilioni kila mwaka kutokana na mzunguko wa fedha haramu.
“Kamati inataka taarifa ya mabilioni ya fedha zilizofichwa katika Benki za Uswisi iwasilishwe mapema kabla Bunge halijaisha ili kuwawezesha wabunge na wananchi kujua ukweli wa jambo hili,” alisema.
Waziri Kivuli
Akizungumzia mikopo Mbatia alisema: “Dhamira kubwa ya kuruhusu Serikali kukopa ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo, lakini hakuna taarifa za kuridhisha kuhusu namna ambavyo fedha zinazokopwa zinatumika katika uwekezaji wa maendeleo.”
Alisema Wizara ya Fedha imeshindwa kusimamia viwango vya riba vinavyotozwa na mabenki kwa maelezo kuwa vinapanda wakati mfumuko wa bei umeshuka kutoka asilimia 19 mwaka 2011 hadi asilimia sita Machi, mwaka huu.
“Deni la Taifa limeongezeka kutoka Sh9.3trilioni hadi Sh22.2 trilioni Aprili, mwaka huu. Takwimu zinaonyesha kuwa deni lote la taifa la ndani na nje limefikia Sh28trilioni.”
Awali, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya aliwasilisha Bajeti ya wizara hiyo ambayo ni Sh5.8trilioni, kati ya hizo, Sh66bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh29.8 kwa ajili ya matumizi ya miradi ya maendeleo.
Alisema Hazina imetengewa Sh1trilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh47bilioni kwa ajili ya matumizi ya miradi.
“Sh4trilioni zimetengwa kwa ajili ya kulipia deni la taifa, Mhasibu Mkuu wa Serikali ametengewa Sh82bilioni kwa matumizi ya kawaida Sh7.9bilioni kwa ajili ya matumizi ya miradi ya maendeleo,” alisema.
Alisema Tume ya Pamoja ya Fedha imetengewa Sh2.3bilioni, Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu kimetengewa Sh2bilioni kwa matumizi ya kawaida na Sh195bilioni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Alisema Ofisi ya Msajili Hazina imepewa Sh88bilioni kwa matumizi ya kawaida na Sh1.9bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Wabunge waiponda Bajeti

Wakichangia bajeti hiyo, Mbunge wa Igunga (CCM), Dk Peter Kafumu alisema shida kubwa iliyopo ni kwamba fedha hazitoki Hazina. “Mwisho wa mwaka tunakuwa na fedha zimetoka asilimia 20, 40, sasa tutaweza kuendesha kweli miradi namna hii?
Mbunge wa Nkenge (CCM), Asumpta Mshama alisema tatizo kubwa la fedha zinazoidhinishwa na Bunge kutokwenda kwa wakati linatokana na bajeti ya Serikali kuzingatia fedha taslimu.
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Christina Mungway alisema hali ya kutopeleka bajeti kwa wakati inasababishwa na mambo mengi ikiwamo kutokuwapo kwa vyanzo vya mapato vya kutosha.
Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila alisema kuna changamoto kubwa kwa Serikali kushindwa kukusanya mapato yake... “Ifike wakati tuwe na mkakati mkubwa wa kuhakikisha kuwa maeneo yote ambayo hayakusanywi kodi yanakusanya.”
Alitoa mfano wa Mgodi wa Mwadui ambao tangu nchi ipate uhuru mwaka 1961 wanasema hauapati faida lakini wanaendelea kuwepo nchini.
SOURC Ewww.mwananchi.co.tz 

No comments

Powered by Blogger.