ad

ad

Pluijm awapa mtihani wa kwanza Yanga

KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van Der Pluijm, raia wa Uholanzi, ameupa mtihani wa kwanza uongozi wa klabu hiyo baada ya kusema anahitaji benchi lake la ufundi liboreshwe.
Hans ameanza kukinoa kikosi cha Yanga hivi karibuni baada ya kukifuata kikosi hicho nchini Uturuki akibeba mikoba ya Mholanzi mwenzake Ernie Brandts aliyetupiwa virago. Hans amesaini mkataba wa miezi sita.
Akizungumza  Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Abadallah Bin Kleb, alisema kocha amefurahishwa na kikosi alichokiona lakini amehitaji marekebisho kadhaa katika benchi lake hilo la ufundi.
“Kwa mujibu wa taarifa tulizozipata kutoka Uturuki, hali ya kikosi inaendelea vizuri na kocha amefurahia viwango vya wachezaji tofauti na alivyofikiria ambapo amefanya tathmini ya mchezaji mmojammoja.
“Ila amehitaji kuongezewa nguvu katika benchi la ufundi, vitu vingine anavyohitaji viboreshwe ni vidogovidogo ili kukiimarisha zaidi kikosi.
“Timu inatarajia kurudi nchini tarehe 23 (Alhamisi ijayo) mara baada ya kumaliza kambi yao nchini humo tayari kwa kuanza mzunguko wa pili wa ligi,” alisema Bin Kleb.
Yanga itafungua pazia lake la mzunguko wa pili Januari 25, kwa kuvaana na Ashanti United kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Powered by Blogger.