MESSI WA SIMBA AZAWADIWA GARI
KIUNGO nyota wa Simba, Ramadhani Singano ‘Messi’ amepata baraka baada ya kupewa zawadi ya gari na mwanachama wa klabu hiyo.
Mwanachama wa siku nyingi wa Simba, Musley Luwah ambaye amekuwa
karibu na klabu ya Simba tokea akiwa mtoto mwaka 1977, ndiye aliyetoa
zawadi hiyo.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Simba zinaeleza mwanachama huyo
amempa Messi gari aina ya Suzuki Carry 4WD ambalo kiungo huyo mwenye
miaka 21 analitumia kumuingizia fedha.
“Unajua Muslah ni mtu
anayependa sana maendeleo ya Simba, hivyo alivyoona Messi anajituma na
ana nidhamu, akajitolea kumpa gari.
“Aliulizwa anataka gari ya aina gani, yeye Messi akachagua gari hiyo
kwa ajili ya kubebea mizigo ili awe anaingiza fedha. Ameonyesha ana
akili sana maana angekuwa mtu mwingine angechagua gari la kutembelea,”
kilieleza chanzo cha uhakika.
Alipotafutwa Messi kuhusiana na hilo, alitoa ushirikiano ingawa hakutaka kulizungumzia sana suala hilo katika vyombo vya habari.
“Ulichosema ni kweli, Muslah ni mtu anayependa maendeleo ya Simba, pia
amewasaidia watu wengi tu, ila mimi niliposikia gari ndiyo nikaamua
kuchagua hilo la kubeba mizigo badala ya lile la kutembelea.
“Awali niliona kama utani, kweli imekuwa hivyo na ninamshukuru Mungu
maana linaniingizia fedha kiasi. Lakini kwa kuwa sipendi makuu, wengi
hawajui hata kama nina gari, hivyo sipendi kuzungumza sana suala hili
hapa,” alisema.
Juhudi za kumpata Muslah hazikuzaa matunda kwa kuwa ilielezwa yuko
nchini Oman ambako hufanya kazi zake na kuendesha maisha yake lakini pia
hapa nchini ana kampuni zake hivyo atarejea hivi karibuni.
Messi alionyesha uwezo mkubwa katika mechi ya Jumamosi iliyopita
wakati Simba ilipoivaa Yanga katika mechi ya Nani Mtani Jembe na
kushinda kwa mabao 3-1, kiungo huyo akiwa kati ya waliong’ara.
Alisababisha penalti baada ya kunyanyasa beki David Luhende lakini
akasababisha Kelvin Yondani apewa kadi nyekundu baada ya kumtoka naye
akamfanyia faulo na kupewa kadi ya pili ya njano iliyozaa nyekundu.
Post a Comment