TAARIFA KUTOKA CCM
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Moses Nnauye.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahaman Kinana ataanza ziara ya siku 22
kwenye mikoa ya Ruvuma na Mbeya kuanzia tarehe 15/11/2013 mpaka
mwanzoni mwa mwezi wa Desemba 2013. Huu ni mwendelezo wa ziara za
kichama katika kuimarisha chama, kukagua utekelezaji wa Ilani ya
Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010, kusikiliza kero mbalimbali za wananchi
na kushirikiana nao kuzitafutia ufumbuzi.
Katika ziara zilizopita na vikao kadhaa vya chama Serikali iliagizwa
kushughulikia baadhi ya kero, na tumeshuhudia baadhi ya hoja hizo
zikichukuliwa hatua. Baadhi ya hoja zilizoanza kushughulikiwa na
Serikali ni pamoja na:-
1) Hoja ya kufufua viwanda nchini.
Baada ya ziara kadhaa za Katibu Mkuu, uchambuzi na vikao kadhaa vya
CCM, Chama kiligundua kuwa viwanda vingi vilivyo binafsishwa havifanyi
kazi kama ilivyokusudiwa na vingine kufungwa kabisa na kugeuzwa
magodauni.
Pamoja na athari kubwa kwa uchumi wa nchi yetu, kufungwa na kutofanya
vizuri kwa viwanda hivyo kumechangia sana tatizo la ajira nchini kuwa
kubwa. Hivyo Chama kiliagiza Serikali kufanya tathmini ya viwanda vyote
vilivyo binafsishwa na hali yake kwa sasa na vile visivyofanya kazi kama
ilivyokusudiwa vichukuliwe na Serikali na kutafuta njia sahihi ya
kuvifufua upya.
Serikali imechukua hatua kadhaa katika hili, ikiwemo kufanya tathmini
na mapendekezo kadhaa yamewasilishwa na timu iliyoundwa na Serikali kwa
ajili ya kufanyia uamuzi na kuchukua hatua.
Tunajua zipo hatua kadhaa zimechukuliwa katika jitihada za kufufua
viwanda vya kubangua korosho kama sehemu ya utatuzi wa tatizo la soko na
zao la korosho. Pia Serikali ipo katika hatua kadhaa za kushughulikia
viwanda vingine nchini.
Tunaipongeza serikali kwa hatua hii muhimu ya kutekeleza agizo la
chama. Tunaitaka serikali ikamilishe zoezi hili mapema iwezekanavyo ili
nchi ifaidike na ufufuaji huu wa viwanda nchini.
2) Changamoto kwa wakulima wa pamba
Katika ziara ya Katibu Mkuu mikoa kadhaa ya Kanda ya Ziwa, alitumia
muda mrefu kujifunza na kuzungumza na wakulima wa zao la pamba wa mikoa
hiyo. Pamoja na tatizo kubwa la soko na bei ya pamba, pamekuwa na
changamoto kubwa ya mfumo unaosimamia zao la pamba ikiwemo upatikanaji
wa pembejeo.
Hatua kadhaa zimeanza kuchukuliwa na Serikali ikiwa ni pamoja na
kuvutia uwekezaji kwenye viwanda vya kutengeneza nyuzi, nguo na kukamua
mafuta ya pamba. Tulishuhudia ujenzi wa viwanda kadhaa mjini Shinyanga,
vingi vikijengwa na wawekezaji kutoka China.
Lakini wakati wa Bunge la juzi, Serikali imeamua kutoa ruzuku ya
asilimia hamsini kwa mbegu bora za pamba ili kuwawezesha wakulima kumudu
bei ya mbegu hizo na hivyo kuboresha zao la pamba nchini na maisha ya
wakulima kuwa bora zaidi.(bei ya dukani kwa kilo moja ni Sh. 1,200/=;
Serikali italipia Sh.600/=).
Katika hili la mbegu bora na kilimo cha mkataba tunaitaka Serikali na
hasa wakuu wa wilaya na mkoa kuacha mara moja kutumia nguvu
kuwalazimisha wakulima kulima kwa mkataba na kutumia mbegu bora badala
yake wawaelimishe na kuwashawishi badala ya kutumia nguvu.
Tunaipongeza Serikali kwa kuanza kuchukua hatua za kutekeleza baadhi
ya mapendekezo ya CCM ya namna ya kutatua matatizo yanayowakabili
wakulima wa pamba nchini. Tunaitaka Serikali kuongeza kasi ya utatuaji
wa changamoto hizo ili wakulima wa pamba wafaidike na uchumi wa nchi
kukua kwa kasi nzuri.
3). Migogoro kati ya wakulima, wafugaji na hifadhi juu ya matumizi ya ardhi
Katika ziara mbalimbali za Katibu Mkuu kwenye mikoa kama ya Morogoro,
Njombe, Simiyu, Mara n.k. alishuhudia migogoro mingi sana juu ya
wakulima, wafugaji na hifadhi mbalimbali nchini. Hakuna shaka migogoro
hiyo imegharimu sana maisha ya watu na mali zao na hata uchumi wa nchi
yetu.
Chama kiliagiza migogoro hiyo kushughulikiwa mapema na kupata
ufumbuzi wa kudumu. Chama kinalipongeza Bunge na hasa Wabunge wa CCM na
Serikali yake kwa uamuzi wa kuunda Kamati teule ya Bunge kuchunguza na
kutoa mapendekezo ya hatua kadhaa za kuchukuliwa katika kufikia
suluhisho la kudumu kwa migogoro hii.
Tunawaomba wananchi watoe ushirikiano wa kutosha kwa kamati teule ya
Bunge ili kazi hii ya kamati iwe na matokeo mazuri yatakayosaidia
kumaliza tatizo hili nchini. Wakati Kamati teule ya Bunge ikifanya kazi
yake, tunawaomba wakulima na wafugaji kote nchini kutulia kusubiri
matokeo ya kamati hii teule ya Bunge.
Hivyo basi, ziara hii ya Katibu Mkuu imelenga pamoja na mambo
mengine kuimarisha Chama, kukagua Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kusikiliza
kero za wananchi. Tumeona jinsi ziara zilizotangulia zilivyokuwa na
matokeo mazuri, tunaamini ziara hii pia itakua na matokeo mazuri.
Imetolewa na:-
(Sgd.)
Nape Moses Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
Nape Moses Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
ITIKADI NA UENEZI
12/11/2013

Post a Comment