OSTAZ JUMA ADAI KUMRUDISHA TENA DOGO JANJA WATANASHATI
Story ya Dogo Janja kutimuliwa kwenye kampuni ‘inayolegalega’ ya
Watanashati Entertainment jana ilivitawala vyombo vingi vya habari
nchini. Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Ostaz Juma ambaye hivi karibuni naye
alijaribu bahati kwenye muziki kwa kurekodi wimbo uliopotea kwa wiki
chache tu, alisikika akihojiwa kwenye vituo vingi vya radio akielezea
hatua hiyo.
Kuanzia kwenye U Heard ya XXL, Clouds FM, hadi kwenye Showtime ya
RFA, Ostaz alisikika akiongea kwa sauti ya msisitizo, kuhusu uamuzi wake
wa kumuondoa rapper huyo wa Arusha kundini kwa kile alichodai kuwa
amekuwa mtovu wa nidhamu. Wasiwasi wangu juu ya hatua hiyo ilianza
mapema tu jana baada ya maelezo ya Ostaz Juma, Dogo Janja na baba yake
rapper huyo kukinzana.
Ostaz alisisitiza kuwa amemfukuza msanii huyo kwasababu kadhaa, kubwa
likiwa ni suala la nidhamu. Dogo Janja alidai kuwa, hajafukuzwa, bali
kajiondoa mwenyewe. Baba yake Dogo Janja alisema hakuwa na taarifa za
kufukuzwa kwa mwanae kutoka kwenye kampuni hiyo licha ya Ostaz kuiambia
Bongo5 kuwa alishampigia simu kumwelezea uamuzi wake. Baba huyo huyo pia
jana aliiambia RFA kuwa waliyaongea jana na wakayamaliza.
Hata kabla ya siku moja haijaisha, leo Ostaz Juma anasema yamekwisha, na amemrejesha kundini.
“Nimeamua kumrudisha, kwa sababu yale mambo yaliyopelekea mpaka mimi
kutoa maamuzi yale niliyotoa jana, yaani kawa kama mtu mzima mwenye
akili timamu, na mtu yeyote anayelifikiria na akaona kwamba hili ni kosa
akasema kwamba ntajirudi, ni kumpa nafasi ya kumsikiliza,” Ostaz
ameiambia tovuti ya Times FM.
“Kwa hiyo jana tulikaa kama kikao cha familia nyumbani kwangu,
tukazungumza na ni kweli ameona kwamba ni bora aache baadhi ya mambo
ambayo hayakuwa mazuri kwenye jamii, na mimi nachokitaka Dogo Janja awe
mtu bora, awe mzuri katika jamii. Na yeye ameniahidi kwamba,
atawahakikishia watanzania kwamba atakuwa Dogo Janja ambae watanzania
wanamtaka wao.”
Naye Dogo Janja ameiambia tovuti hiyo, “Mi niko mtanashati, kwa
sababu ni mambo ya kifamilia na tumeshakuwa familia moja, na mimi naona
kuhamahama sio swala zuri, na kama nilikuwa na malengo ya kufanya kazi
nzuri, ni bora niendelee kupalilia tu hapahapa. Yamekwisha isha kwa
ufupi.
Kwa namna moja ama nyingine ni ile chuki, marafiki ambao
wamenizunguka, ni watu ambao ni soo, sio watu wazuri. Sasa hivi rafiki
yangu hela tu.”
Maelezo hayo Ostaz Juma na kauli pamoja na msimamo aliokuwa nao jana
na hiki anachokisema Dogo Janja ni ngumu kushawishika kuwa hiki
kinachoendelea ni halisi ama ni njia nyingine ya kuendeleza ugonjwa wa
kutafuta ‘kiki’ uliopata umaarufu kwenye kiwanda cha muziki cha hapa
nyumbani.
Na pengine labda kumshauri tu Ostaz, ni kuwa asipendelee sana
kuconclude mambo na kuongea kwa uhakika kwa vyombo vya habari pale
ambapo migongano midogo inapotokea ambayo ingeweza kumalizika bila hata
nyumba ya jirani kufahamu. Kulikuwa hakuna haja ya jana kutoa kauli ya
kumfukuza na tena kwa msisitizo kama huo na kisha leo kuamka na uamuzi
mwingine.
Hii inaifanya kampuni ya Mtanashati ionekane ipo kienyeji mno na
maamuzi mengine yanafanywa kitoto. Kama ingekuwa ni kampuni
iliyodhamiria kufanya kazi kikampuni, basi isingekuwa rahisi kutimua
watu kienyeji hivyo na hadi leo kuifanya ibakize wasanii wawili tu,
ambao nao hawamake noise yoyote. Pengine ndio maana, Ostaz ameamua
kuingia front pia na kufanya muziki. Muziki ambao kwa wengi unaonekana
kama utani tu na kejeli kubwa kwa fani hiyo.
Hata hivyo hiyo ni ishara kuwa fungate la
Dogo Janja na Mtanashati lina mushkeli mkubwa na nachelea kusema, siku
si nyingi watarudi tena hewani wakiongea kile kile kama kilichofanyika
jana na kisha baada ya siku chache kurudi tena na kusema wameyamaliza.
CHANZO CHA HABARI BONGO 5
CHANZO CHA HABARI BONGO 5

Post a Comment