ad

ad

Kubezwa, kudharauliwa na kuchekwa ni daraja la mafanikio!

 Katika makala ya leo, nataka kugusa kwa undani zaidi kuhusu baadhi ya watu wanaokata tamaa juu ya mambo fulani maishani baada ya kudharauliwa, kubezwa na hata kuchekwa.
Watu wengi wamekubali maneno na mawazo ya watu kuwa ukweli juu ya maisha yao! Wanavunjwa moyo na dharau wanazooneshwa wazi, hujiona hawawezi pale wanapobezwa na kujisikia vibaya baada ya kuchekwa kwa kila wakifanyacho.
 
Siku zote unapoanza safari yako kuelekea kwenye mafanikio, ni lazima utakutana na changamoto nyingi sana zikiwemo hizo za kudharauliwa, kuchekwa na kubezwa. Lazima watu watakaokupinga wajitokeze. Lazima ukubaliane na hali hiyo huku ukiweka akilini mwako kwamba, njia ielekeayo kwenye mafanikio, haikosi maumivu.
 
Watajitokeza kukupinga na kukudharau kwa uwazi kabisa, wakati mwingine bila hata kukuonea haya machoni, vijembe na maneno makali ya kejeli yatatolewa mbele yako, lengo kubwa likiwa ni kukubeza na kukukatisha tamaa kwa kila unachotaka kukifanya. Furaha yao ni kuona unashindwa na kurudi nyuma! Hao ndiyo binadamu.
 
Kumbuka dunia ina watu wa aina mbili. Kundi la kwanza ni lile la kuwatia moyo watu na kuwapongeza pale wanapofanya mazuri. Kundi la pili ambalo hutazama mabaya ya watu tu, ambalo ni kubwa zaidi. Kazi yao ni kukosoa kila jambo unalolifanya au unalotarajia kulifanya maishani.
Hapa nataka kufafanua kuwa, unaweza kufanya mambo mazuri elfu moja, lakini wasione uzuri huo. 

Ukakosea jambo moja tu, lakini wanasahau yale mazuri elfu moja na kulitazama kosa moja la elfu moja na moja! Hawa ni watu hatari sana katika maisha yetu ya kusaka mafanikio.
 
Kila ukichukua hatua moja kuelekea kwenye mafanikio, wanainua mabango mbele yako na kusema wewe huwezi huku wakitoa hoja dhaifu ambazo ukizitazama kwa haraka unaweza kuziamini na kukata tamaa kabisa juu ya jambo unalotaka kulifanya.
 
Kwa mfano unaweza kuwa na wazo zuri sana la biashara ambayo unaamini inaweza kukupa faida kubwa na hatimaye kukuingiza kwenye ramani ya watu waliofanikiwa lakini watasema huwezi kwa sababu huna elimu ya kutosha.
 
Wakati mwingine watasema huwezi kwa sababu baba au mama yako alishindwa na mambo mengine mengi ya kufanana na hayo. Wengine watasema fulani ambaye alikuwa na nyota ya biashara alifanya akashindwa hivyo na wewe huwezi.
 
Mpenzi msomaji wangu, kuna nyakati fulani maishani huwa nyeusi! Kila mtu anakuwa kinyume na wewe, hata kama unaamini kuwa na uwezo mkubwa ndani yako, lakini watu watakudharau na kukubeza kuwa huwezi kufanya chochote.
 
Ikitokea umeshindwa jambo fulani maishani, wanakucheka bila kificho huku wakisema kuwa tulijua huwezi kufanya jambo hilo. Wanageuka watabiri! Lakini endapo ukilifanikisha kwa kiwango kizuri, hao hao watakuja na kusema tulijua lazima ulitimize maana wewe una akili na uwezo wa hali ya juu mno! Hao ndiyo binadamu, baadhi ya o hawatabiriki!
 
Waache wakudharau, acha wakucheke, ngoja wakubeze kwa maneno yote mabaya lakini mwisho wa siku wewe tarajia ushindi tu.

Kumbuka Mungu alikuumba kwa makusudi makubwa. Elewa hukuumbwa kwa bahati mbaya! Mungu alimaanisha uwe jinsi ulivyo, alikuwekea uwezo mkubwa mno ndani yako na zaidi ya yote akakuwekea kitu ambacho kitakusaidia kujua na kugundua nguvu kubwa uliyonayo ndani yako ambacho ni akili!
 
Lakini pia tambua Mungu alikuumba kwa mfano wake, unamwakilisha wewe chini ya jua, hakuna litakalokushinda kabisa labda wewe ujiwekee mazingira ya kushindwa. Wanaokucheka ni binadamu tu, Mungu yuko pamoja nawe, hata kama unapita katika wakati ambao kila binadamu anaamini hutashinda, wewe  jipe moyo!
 
Jambo la msingi hapo ni wewe kumwamini Mungu, kufanya kazi kwa nguvu, bidii, malengo na maarifa ya hali ya juu huku ukiamiani kuwa mafanikio ni lazima maishani endapo tu utadhamiria kwa dhati kuyatafuta.
 
Hata siku moja, usiwachukie wanaokucheka na kukudharau, kumbuka kukucheka na kukudharau kwao ndiyo madaraja ya wewe kuelekea kwenye mafanikio. Jiamini kuwa wewe ni mtu wa pekee mno katika dunia hii, hakuna aliyeumbwa kufanya unachotaka kukifanya!

Itaendelea Ijumaa wiki ijayo...
Powered by Blogger.