HANS POPPE: KASEJA ALITURINGIA SANA, NA AMECHUMA UTAJIRI WA KUTOSHA SIMBA SC.
MWENYEKITI
wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba
Juma Kaseja hakutaka kukutana na uongozi wa klabu hiyo kujadiliana juu
ya mustakabali wake, licha ya kuitwa kwa miezi miwili na ndiyo maana
wakaamua kuachana naye.
Akizungumza siku ya jana Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la
Wananchi Tanzania (JWTZ), Poppe amesema kwamba tangu Mei wamekuwa
wakimuita Kaseja kwa ajili ya mazungumzo juu ya mustakabali wake katika
klabu hiyo, lakini amekuwa akipiga chenga.
Poppe
alisema mara ya mwisho kukutana ana kwa ana na Kaseja ni wakati wakiwa
Morocco na timu ya taifa, Taifa Stars kwa ajili ya mchezo dhidi ya
wenyeji kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mapema mwezi
huu.
“Nilipokutana
naye, nikamuambia sisi bado tuna nia ya kuendelea na wewe, je wewe
msimamo wako ni upi? Akasema hawezi kujibu kwa sababu ana majukumu ya
timu ya taifa, akimaliza atajibu. Nikamuambia sawa, wewe maliza na ukiwa
tayari njoo ofisini tuzungumze.
Amemaliza
mechi na Morocco, wamerudi hapa, amecheza mechi na Ivory Coast
amemaliza na wiki zaidi ya mbili zimepita hajaja. Sisi tukaona huyu mtu
kwa kuwa amemaliza Mkataba wake hapa na tunamuita haji, anaweza kuwa na
mipango yake mingine, tumuache aendelee nayo,”alisema Poppe.
Alipoulizwa
kuhusu kuachwa kwa sababu ameshuka kiwango, Poppe alisema; “Ni kweli
kama utaona udakaji wake wa sasa, ameshuka mno kiwango na hilo linatupa
wakati mgumu sana mbele ya mashabiki. Na kama utakumbuka Morogoro
walitaka kumpiga.
Sasa
ukitazama kwa mfano lile bao la kwanza alilofungwa katika mechi na
Yanga, lilikuwa bao rahisi sana. Ule mpira ulipita mbele yake ukaenda
kupigwa kichwa (na Didier Kavumbangu). Sasa ile kwa kweli imewaudhi sana
watu,”.
“Lakini
pamoja na yote, tulitaka tuzungumze naye mwenyewe, tujadiliane juu ya
hali halisi, ikibidi hata kumsainisha Mkataba na kumpa fedha anazotaka,
kisha tumpe mapumziko ya muda fulani, ili awe fiti arudi kazini. Lakini
hakutupa fursa hiyo. Tungefanya nini?,”alihoji Hans Poppe.
Askari
huyo wa zamani amesema kwamba Kaseja kama angejitambua yeye ni gwiji wa
klabu, asingethubutu kupiga chenga kikao na uongozi, hususan katika
kipindi hiki kigumu ambacho klabu inahitaji kujipanga upya baada ya
msimu mbovu uliopita ikipoteza taji la ubingwa wa Ligi Kuu.
“Mwisho
kabisa, tukaamua kumteua mtu maalumu wa kuzungumza naye, Evans Aveva.
Aveva kila akimpigia simu Kaseja, anatoa udhuru, mara yuko Kigoma, mara
yupo Korogwe, sasa mtu kama huyu sisi tungefanya nini?”alihoji tena
Poppe.
"Na
pia huyu mtu kama maslahi katika klabu hii amepata makubwa kwa sababu
alikuwa anathaminiwa mno. Juma Kaseja ni kati ya wachezaji ambao
watastaafu soka vizuri tu. Amevuna fedha nyingi sana hapa. Wakati wote
yeye alikuwa mchezaji anayelipwa zaidi kwa upande wa wazawa. Na
unapofika wakati wa usajili, alikuwa anapiga hela ndefu sana
hapa,"alisema Poppe.
Historia
ya Kaseja na Simba SC imefikia tamati mapema wiki hii, baada ya klabu
kuamua kutomuongezea Mkataba kipa huyo iliyemsajili mwaka 2003 kutoka
Moro United ya Morogoro.
Kaseja
amekaririwa na gazeti la Serikali, Habari Leo akisema kwamba
atawaaumbua viongozi wa Simba SC kwa kuanika kila kitu baada ya kutemwa.
Lakini anapotafutwa na vyombo vingine vya habari, amekuwa akikataa
kuzungumzia sakata hilo.

Post a Comment