Viongozi watakiwa kutatua bomu la ajira kwa vijana
VIONGOZI wa Afrika wameshauriwa kuweka mikakati madhubuti ya kutatua tatizo la ajira kwa vijana ambalo limetajwa kuwa sawa na bomu linalosubiri kulipuka.
Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) nao umeshauriwa kufanyia kazi suala hilo.
Changamoto hiyo ilitolewa mjini hapa wakati wa mikutano ya kutafakari miaka 10 ya APRM na 50 ya Umoja wa Afrika (AU).
Akichangia mada kuhusu utawala bora Barani Afrika, Wakili Maitre Tully kutoka Taasisi ya Kusikiliza Malalamiko ya Wananchi ya Afrika Kusini, alisema sehemu kubwa ya wakazi wa Afrika ya leo ni vijana.
“Takwimu zinaonesha Afrika ina vijana wengi zaidi kuliko sehemu yoyote duniani. Hata hivyo zaidi ya asilimia 60 ya vijana hao hawana ajira,” alisema.
Mmoja wa wajumbe wa Jopo la Watu Mashuhuri la APRM, Balozi Fatma Ndagiza, alitaka vijana wakumbukwe katika mipango ya maendeleo ikiwemo kupewa taarifa juu ya masuala muhimu yanayohusu nchi zao.
Balozi Fatma ambaye alipata kuwa Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, alisema vijana wakipewa taarifa kupitia mitandao ya kijamii watakuwa wamejengewa uwezo wa kujiamini na kushiriki katika maendeleo ya nchi zao.
Akieleza sababu za vijana wengi wa Afrika kukosa ajira, mtaalamu wa masuala ya elimu, Profesa Mbaya Kankwenda, alisema elimu inayotolewa Barani Afrika imeshindwa kuzalisha watu “walio na ujuzi na taaluma” bali “wahitimu”.
Dk. Jean Butera kutoka Rwanda aliwagusa washiriki wengi aliposema elimu itolewayo sasa kwa vijana haitekelezi ajenda ya kuwasaidia vijana wa Afrika bali “ajenda isiyojulikana”.

Post a Comment