Uchaguzi 2015: Magufuli, Lowassa mwisho wa ubishi!
Mwandishi Wetu
Hatimaye
zile mbio za Kampeni za Uchaguzi Mkuu 2015 zilizoanza Agosti 23, mwaka
huu, leo zinafikia tamati ambapo wagombea wawili wenye msisimko wa aina
yake, Dk. John Pombe Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Edward
Ngoyai Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wanafunga
kazi katika Majiji ya Mwanza na Dar.
MAGUFULI MWANZA
Baada
ya kumaliza kuzunguka mikoa yote ya Tanzania Bara na visiwani kisha
kurejea jijini Dar akiunganisha na Mkoa wa Pwani, leo atalitikisa Jiji
la Mwanza katika Viwanja vya Kirumba akifunga kampeni zake hizo.
Hadi
anafunga kampeni zake hizo, Magufuli amefanya karibia mikutano 300
katika majiji, miji na vijiji mbalimbali nchini huku akijinadi kwa ilani
ya chama chake aliyoahidi kuitekeleza kwa dhati kwa kubadili mfumo wa
kiutawala.
Huku
akitumia msemo wake wa ‘Hapa Kazi Tu’ na staili ya kupiga push up
(Magufulika), kote alikopita alieleza baadhi ya vipaumbele vya serikali
yake kuwa ni pamoja na kujenga umoja wa kitaifa, kulinda muungano,
ulinzi na usalama, kuheshimu mihimili ya dola, kuanzisha mahakama maalum
ya mafisadi na majizi, utawala bora, kuheshimu mawazo yote ya kuleta
maendeleo hata yakitoka upinzani na kuimarisha vyombo vya usalama.
Vingine
alivyoahidi ni vita dhidi ya ubadhirifu, kodi ilipwe na wote, kuongeza
ajira kwa kuimarisha viwanda vya ndani, kufufua sekta ya kilimo, mifugo
na tija kwa kujenga viwanda, kudhibiti madini, kupeleka maji vijijini na
mijini, kujenga zahanati kila kijiji, hospitali ya rufaa katika kila
mkoa na kuboresha maslahi ya wauguzi.
Vingine
ni elimu ya bure kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne, kujenga
nyumba za walimu, mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu, kujenga hosteli za
wanavyuo, kuboresha maslahi ya watumishi na kusimamia gesi, kuboresha
barabara, flyovers na reli.
Pia
ameahidi kulinda haki za walemavu, uhuru wa habari, kulinda haki za
wasanii na wanamichezo na nyingine nyingi hasa kulinda rasilimali za
Tanzania.
Mheshimiwa
huyo anatarajia kufunga kampeni zake kwa kishindo akiweka msisitizo
katika vipaumbele hivyo huku akiambatana na timu kamili jijini Mwanza
wakiwemo wasanii na viongozi mbalimbali wa CCM.
LOWASSA JANGWANI
Kwa upande wake, mgombea wa Chadema, Lowassa anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
ataisimamisha Dar katika Viwanja vya Jangwani kuhitimisha kampeni zake
alizofungulia kwenye viwanja hivyo. Lowassa na timu yake amezunguka
mikoa yote Tanzania Bara na visiwani huku akikutana na mafuriko ya
Wana-Ukawa waliokuwa wakijinasibu kuwa wanataka mabadiliko.
Katika
ziara zake, Lowassa alivitaja vipaumbele vya serikali yake kuwa ni
pamoja na elimu bora na bure kuanzia shule za awali hadi chuo kikuu.
Vingine
ni kuwatoa Watanzania katika lindi la umaskini kwa kuboresha kilimo,
viwanda, ujenzi wa reli na barabara na miundo mbinu mingine kama ya
afya, mawasiliano na biashara.
Lowassa
aliahidi kuwa serikali yake itakuwa rafiki wa watu wa hali ya chini ili
kuwainua wamachinga, mama ntilie, bodaboda na wachimbaji wadogowadogo.
Akiwa
Viwanja vya Jangwani, leo Lowassa na viongozi wengine waandamizi wa
Ukawa watahitimisha kampeni zao kuwaomba wapiga kura wamchague Lowassa
na wagombea wengine wote wa Ukawa.



Post a Comment