ad

ad

Taifa latikiswa •Bunge kuunda kamati teule, Bajeti Nishati yasitishwa.

SERIKALI imeapa kuwasaka waasisi wa vurugu za Mtwara ndani na nje ya nchi ikisema kuwa waliohusika kupanga, kushawishi, kuandaa na kutekeleza vurugu hizo hawataukwepa mkono wa sheria.

Kauli hiyo ya serikali ilitolewa jana bungeni na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Emmanuel Nchimbi, akisema kuwa tofauti za Watanzania lazima ziendelee kuzungumzwa kwa uwazi, kuheshimiana na kuzingatia sheria na taratibu za nchi.
Nchimbi alisema vyombo vya dola vitaendelea kuimarisha amani na utulivu katika eneo la Mtwara ili shughuli ziendelee kama kawaida.

“Tunalo taifa moja la Tanzania ambalo maliasili zake ni za Watanzania wote, tabia inayoanza kujengeka ya kila eneo kutaka inufaike peke yake na mali za eneo hilo italigawa taifa letu vipande vipande,” alisema.
Akieleza athari za vurugu hizo, Waziri Nchimbi alisema kuwa ofisi ya mbunge wa Mtwara Mjini, Hasnain Murji (CCM), iliyoko Mikindani iliharibiwa na kuibiwa vitu mbalimbali.
Nchimbi alisema kuwa ofisi ya mahakama ya mwanzo ya Mitengo ilichomwa na kuteketea pamoja na nyaraka za ofisi huku ofisi ya CCM kata ya Chikongola ikichomwa moto.

Aliongeza kuwa nyumba binasfi ya ofisa mtendaji kata ya Magomeni ilichomwa moto, nyumba za askari polisi wanne zilivunjwa na kuibiwa vitu mbalimbali.

“Nyumba ya mwandishi wa habari wa TBC, Kassim Mikongolo, imechomwa moto na kuteketea; na ofisi ya kata ya Kichongola imeharibiwa na kuibiwa vitu mablimbali. Thamani halisi ya mali zote zilizoungua na kuharibiwa bado haijapatikana,” alisema.
Waziri Nchimbi alisema kuwa mtu mmoja Karim Shaibu alifariki katika vurugu hizo na askari wawili walijeruhiwa kwa bomu la kishindo.

“Kutokana na usalama kuzorota, mkuu wa mkoa wa Mtwara kwa mujibu wa sheria aliomba kwa Waziri wa Ulinzi kuongezewa nguvu kulinda raia wasio na hatia na mali zao,” alisema.
Aliongeza kuwa waziri alikubali na kulielekeza Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) liende mara moja na katika kutekeleza agizo hilo askari 32 wa jeshi hilo walianza safari kutoka Nachingwea kuelekea Mtwara.

Alisema kuwa walipofika njiani katika eneo la Kilimani Hewa, gari lao lilipata ajali ambapo wanajeshi wanne walifariki na 20 kujeruhiwa.

“Wanajeshi hawa wamekufa na kujeruhiwa wakati wakiwa kazini kutekeleza wajibu wa kuwalinda Watanzania wenzao. Damu yao haitamwagika bure,” alisema.

Bunge laahirishwa
Kwa mara nyingine tena Spika wa Bunge, Anna Makinda, jana asubuhi baada ya kauli hiyo ya serikali aliliahirisha Bunge hadi leo ili kutoa nafasi kwa Kamati ya Uongozi kukamilisha kazi yake ya kuamua nini kifanyike kufuatia vurugu hizo.

Pia Spika alisema kuwa mjadala wa hotuba ya bajeti umesitishwa hadi hapo baadaye ili kuepusha kauli ambazo zinaweza kuchochea vurugu zaidi.
“Waheshimiwa wabunge tumeona kuendelea kujadili hapa hatujui kauli zetu zinaweza kukoleza moto juu ya moto vipi, sasa Kamati ya Uongozi tutakaa na kujadili kisha kuona hatua za kuchukua.

“Hivyo kesho tutaendelea na Wizara ya Afrika Mashariki, hii bajeti ya Nishati na Madini tutaendelea nayo baadaye baada ya hali Mtwara kutulia,” alisema.

Hata hivyo, chanzo chetu kilidokeza kuwa kamati hiyo ilimaliza kikao chake kwa pendekezo la kuunda Kamati Teule itakayochunguza sakata zima na kutoa mapendekezo.
Lakini baadhi ya wajumbe walipendekeza kuwa kamati hiyo isiende Mtwara sasa hivi kufanya kazi hiyo kwani haitaweza kupata taarifa sahihi.

“Uamuzi wa ama kamati teule kuundwa au la umeachwa mikononi mwa Spika, lakini kwa jinsi viongozi wetu wanavyopenda kufanya mambo kwa zima moto wanaweza kuamua vinginevyo wakakimbilia kupeleka majeshi na hivyo kusababisha balaa zaidi,” kilisema chanzo chetu.

Mbowe aibana serikali
Kionguzi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe (CHADEMA), alisema ni fikra potofu kudai kuwa mgogoro wa Mtwara unasababishwa na wanasiasa.

Mbowe alisema kuwa wasababishaji wakubwa wa vurugu za Mtwara ni serikali yenyewe ambayo haikujipanga kutatua jambo hilo mapema.

“Wakazi wa Mtwara ni jibu la tatizo na si chanzo cha tatizo, serikali katika hili imeshindwa na imekuwa mshiriki mkubwa kwa njia moja au nyingine, hivyo haiwezi kuwa mtatuzi wa tatizo hilo,” alisema.

Alifafanua kuwa ili ufumbuzi wa tatizo hilo uweze kupatikana ni kushirikisha watu makini na taasisi ambazo zinaaminika kwa jamii ya wana Mtwara,” alisema.
Pia alilaani nguvu kubwa inayotumiwa na serikali ya vyombo vya dola kuwatawanya wananchi wa Mtwara akisema kufanya hivyo hakuwezi kusaidia kutatua mgogoro na badala yake busara na hekima ya hali ya juu inatakiwa kutumika.
 
Wabunge waponda
Baadhi ya wabunge waliozungumza  katika viwanja vya Bunge walimlaumu Rais Jakaya Kikwete wakisema amepuuzia mgogoro huo tangu mapema.
Walisema kuwa serikali yake kupitia kwa mawaziri na viongozi wengine wa kiserikali wamekuwa wakipotosha madai ya wananchi wa Mtwara na hivyo kuonekana kama watu wasiotaka rasilimali za kwao zisinufaishe wengine.

“Tatizo la Rais wetu ni kutaka kumfurahisha kila mtu, jambo hili serikali yake ndiyo imelipuuza kwa kuwadharau wananchi wa Mtwara. Sasa huu ndiyo wakati wa yeye kuonyesha kuwa amani ya nchi inarejea,” alisema mbunge mmoja.
Mbunge huyo wa CCM ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe, alisema kuwa malalamiko hayo waliyatoa hata kwenye kikao cha wabunge wa chama hicho na Rais Kikwete.

Alisema walimweleza Rais kuwa amekuwa mpole sana kwa kutowakemea wanaojaribu kuhatarisha amani na usalama wa taifa.
Naye Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), alisema Mtwara walipuuzwa kwa kutokusikilizwa na kuwashanga viongozi kukimbilia kulalamika badala ya kuchukua hatua.

“Tumeambiwa kuwa wanasiasa ndio wanachochea lakini kumbuka wanasiasa ndio haohao wananchi…leo tunaambiwa yanaweza kuwa mataifa ya nje. Kwa nini hatutafuti kiini mapema na kuchukua hatua kabla ya vurugu?” alihoji.
Lugola alishauri kuwa hakuna sababu ya lazima kusafirisha gesi hiyo kuja Dar es Salaam na badala yake mtambo unaweza kujengwa hukohuko Mtwara ili gesi ikawa inafuatwa huko.

“Kwa nini dhahabu inayotolewa kwenye migodi kadhaa au samaki wanaovuliwa Ziwa Victoria havipelekwi Dar es Salaam kwa ajili ya kuchakatwa? Si mitambo imewekwa huko huko na wanaovitaka wanafuata huko?” alihoji.
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), na James Mbatia (NCCR-Mageuzi), walisema kuwa hatua inayochukuliwa na serikali ya kutumia jeshi kuzima vurugu si suluhisho la kudumu.

“Huwezi kuzima moto halafu ukajivuna pasipo kudhibiti chanzo chake, suluhu ya watu wa Mtwara ni mazungumzo, serikali inapaswa kukaa nao na kuwaelewesha faida ya bomba inalotaka kulijenga,” alisema Lissu.
Mbatia naye alisema kuwa serikali imeshindwa kumaliza mgogoro huo, hivyo lazima Bunge liisimamie serikali itemize wajibu wake.

Alisema Mtwara waliahidiwa viwanda miaka mingi lakini siku zinakwenda hawaoni hatua inayofanyika kutimiza ahadi hiyo kama ilivyo kwenye mikoa mingine.
Alisema kwa wakati huu kila taarifa si ya kupuuzwa kwani katika dunia hii ya utandawazi wenye maslahi na gesi hiyo ni wengi na hivyo inawezekana wakajipenyeza hata kuwagawa wananchi wa Mtwara.

Mnyika apinga
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), amepinga hatua ya Waziri Nchimbi kutoa kauli ya serikali wakati wa kipindi cha maswali na majibu kwa Waziri Mkuu akisema ni kuvunja kanuni kwani kiongozi huyo wa serikali alikuwepo.
“Pinda amekwepa kutoa taarifa kwa kuwa anajua kwamba aliahidi wakati akijibu maswali kwenye mkutano uliopita wa Bunge kuwa ufumbuzi wa mgogoro wa Mtwara umeshapatikana na kwamba tatizo lilikuwa ni uelewa tu,” alisema.
Mnyika alisema kuwa kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu ni cha kwake mwenyewe na kanuni ya 38(4) inaruhusu kama kuna jambo la kulitolea taarifa afanye hivyo.
Powered by Blogger.