Mbunge aibua video za udini.
MBUNGE wa Rombo, Joseph Selasini (CHADEMA) amewasilisha CD za
video alizodai kuwa ni za uchochezi wa kidini na kutaka serikali ichukue
hatua.
Mbunge huyo alitumia nafasi hiyo jana wakati akichangia mjadala wa
hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2013/2014.
Selasini alisema CD hizo moja ni ya wanachuo wa Chuo Kikuu cha Dodoma
(UDOM), wakiwa na wahadhiri wao wa dini moja, wakitoa maneno ya
uchochezi na kupanga namna ya kuwashughulikia wanachuo wenzao wa dini
nyingine ambao wanaishi nao kwenye bweni moja.
Alisema CD nyingine inaonesha kiongozi mmoja wa dini akitoa kauli za
kutaka maaskofu, mapadri na viongozi wengine wa Kikristo wauawe.
”CD hizo zinajulikana, lakini serikali haijachukua hatua. Hii maana
yake suala la ubaguzi wa kidini linachochewa na linahamasishwa na baadhi
ya viongozi wa serikali na CCM,” alisema.
Selasini alisema hakuna sababu ya serikali kupoteza muda kukutana na
viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu kujadili suala hilo la udini
badala yake ichukue hatua kwa wachochezi hao.
Akitolea mfano, Selasini alisema mwaka 2005 aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la
Polisi (IGP), Omari Mahita, alitangaza kukamata shehena ya kontena la
visu na majambia, mali ya Chama cha Wananchi (CUF).
Selesini aliongeza kuwa licha ya CUF kuchafuliwa kwa tuhuma hizo
ambazo hadi sasa hazikufikishwa mahakamani, chama hicho hakikuwahi
kuombwa radhi wala Mahita hakuchukuliwa hatua zozote na serikali.
Pia alisema wapo waliotangaza kwamba CUF ni chama cha Kiislamu,
CHADEMA ni chama cha Kikristo, Wachaga, lakini hakuna aliyechukua hatua
kwa kauli hii ya kibaguzi.
"Hiyo kesi ya majambia ya CUF iko wapi na kama haipo, Mahita
alichukuliwa hatua gani? Leo wapo viongozi wanatangaza CHADEMA ni chama
cha Kichaga, mara cha kigaidi. Hao wanachukuliwa hatua gani?” alihoji
Selasini.
Mbunge huyo alilalamikia vyombo vya dola kuwa vinaachia CD za
uchochezi na badala yake vinachukua picha za video kwenye mitandao ya
You tube na kuwabambikizia kesi watu wasio na hatia.
Wakati Selasini akilalamikia CD hizo ikiwemo ile aliyodai ni ya UDOM,
Mbunge mwingine wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Juma Nkamia (Kondoa
Kusini), alisema hali katika chuo hicho ni shwari na hakuna tatizo la
udini.
”Hapa tunataka kuonesha kwamba UDOM kuna tatizo, si kweli. Kama tatizo
ni baadhi ya maprofesa kwa sababu ya dini zao, basi waondolewe,”
alisema Nkamia.

Post a Comment