ad

ad

Ngumi zote zile, Cheka ameambulia milioni tatu!

BONDIA Francis Cheka amelipiga bei gari lake aina ya Noah alilopewa zawadi na waandaaji na kuchukua fedha taslimu Sh 10 milioni.


Cheka alipewa zawadi ya gari hilo lenye thamani ya Sh 12 milioni baada ya kumpiga, Thomas Mashali kwa KO raundi ya 10 katika pambano la raundi 12 kwenye Ukumbi wa PTA, Dar es Salaam, usiku wa Jumatano iliyopita.

Kati ya fedha hizo yaani Sh 10 milioni, Sh 5 milioni amelipa deni la maandalizi yake pamoja na kambi, sehemu nyingine ya fedha hizo amemlipa kocha na watu wengine waliokuwa wanamsaidia na yeye ameambulia Sh 3 milioni tu.
Cheka ambaye alirudi kwao Morogoro jana, Jumatatu kuendelea na shughuli zake alisema: 

"Nimeamua kuuza gari ile nikachukua fedha. Nisingeweza kuchukua gari wakati natakiwa kuwalipa watu fedha zao. Nimefanya maandalizi na kocha (Abdallah Saleh) na wengine waliokuwa wananisaidia kwenye maandalizi yangu, wote natakiwa niwalipe kwa hiyo siwezi kuchukua peke yangu,"alisema Cheka.

"Lakini pia natakiwa kurudisha fedha za watu za maandalizi, unajua ninapokuwa na mechi natakiwa kuwa kambini, nakaa hotelini ambako nalipia chakula, malazi na vitu vingine vyote na si peke yangu ni wengi wanaonisaidia. Kwa hesabu za haraka nilichoambulia ni Sh 3 milioni tu,"alisisitiza.

Alisema, mabondia wamekuwa wanapata maslahi madogo kwa sababu hakuna wadhamini wanaowasaidia. Waandaaji wao wanatoa kiasi hicho kwa makubaliano na fedha zote nyingine wanazokuwa wanapata ni faida yao.
"Hatuna wadhamini, unachokipata ndiyo hicho hicho waandaaji wao wanakupa kiasi ambacho mmekubaliana tu, ingekuwa vizuri wadhamini wangekuwa wanatudhamini mabondia ili kutupunguzia machungu,"alisema Cheka.
Powered by Blogger.