Mkwasa: Simba hawaifungi Yanga ng'o.
KOCHA wa Ruvu Shooting iliyofungwa na Simba mabao 3-1,
amekiangalia kikosi hicho cha Msimbazi akajiridhisha na kutamka kwamba
hakiwezi hata kidogo kuifunga Yanga Mei 18 kwenye Uwanja wa Taifa.
Mkwasa alisema: "Itakuwa vigumu kwa kikosi hiki cha Simba kuifunga Yanga Mei 18, ni wachezaji wazuri lakini bado ni vijana wadogo, hawawezi kupambana na wachezaji wenye uzoefu kama Yanga,"alisema Mkwasa, kocha na mchezaji wa zamani wa Yanga.
Kauli ya Mkwasa ni sawa na kuwapambanisha, Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondani, Mbuyu Twite, David Luhende na Athuman Idd 'Chuji' wanaocheza safu ya ulinzi ya Yanga dhidi ya chipukizi kama Ramadhani Singano 'Messi', Abdallah Seseme, Haruna Chanongo ambao watasaidiwa na wazoefu kama Amri Kiemba, Mzambia Felix Sunzu na Mrisho Ngassa 'Anko' kwenye safu ya ushambuliaji.
Mkwasa alitoa kauli hiyo baada ya mechi yao dhidi ya Simba walipofungwa mabao 3-1 wikiendi iliyopita ingawa alisisitiza hayo ni maoni yake kulingana na kiwango cha wachezaji walichokionyesha katika mechi hiyo walivyocheza kwa sababu mechi kama hizo za watani wa jadi ni ngumu kuzitabiri.
Mkwasa alisema Simba ilishinda mechi hiyo kwa sababu ya maamuzi ya waamuzi wa mchezo huo. Mechi hiyo ilichezeshwa na waamuzi, Athuman Lazi aliyekuwa katikati akisaidiwa na Milambo Tshikungu na Michael Mkongwa wakati mwamuzi wa akiba alikuwa Hellen Mduma.

Post a Comment