Gesi yaua Mtwara • Kambi ya Upinzani yacharuka, Waziri alazimisha.
MILIO ya risasi, mabomu ya machozi, maji ya kuwasha na silaha za
jadi ndivyo vilivyotawala jana katika vurugu zilizotokea mkoani Mtwara
na kusababisha mtu mmoja kufariki dunia.
Nyezo hizo ndizo zilizotumika jana katika mapambano baina ya polisi na
wananchi waliokuwa wakiandamana huku wakiharibu mali mbalimbali kupinga
ujenzi wa bomba la gesi kwenda jijini Dar es Salaam.
Mapambano hayo yalianza katika eneo lililo jirani na Kanisa la Agape
mjini Mtwara baada ya wananchi kuanza kuwazomea askari waliokuwa katika
doria kutokana na uvumi wa kusimamishwa kwa shughuli zote mjini Mtwara
kwa ajili ya kusikiliza hotuba ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo, iliyosomwa jana mjini Dodoma.
Mara baada ya hotuba ya Profesa Muhongo, wananchi waliokuwa
wakiifuatilia waliamua kuwatumia watoto wanaokadiriwa kuwa na miaka 11
kufunga barabara ya Mkanalendi iliyopo katika Manispaa ya Mikindani.
Vurugu ziliendelea na kusababisha nyumba ya Mbunge wa Mtwara Mjini
Husnein Murji, Ofisi ya CCM Mtwara Vijijini pamoja na nyumba ya
mwandishi wa habari wa TBC, Kassim Mikongolo, Ofisi ya Mtendaji
Chikongola na Mahakama ya Mwanzo Mitengo kuchomwa moto.
Baada ya matukio hayo wananchi walivamia moja ya nyumba ya wageni
iliyodhaniwa kuwahifadhi askari waliotoka nje ya Mkoa wa Mtwara na
kutaka kuichoma moto.
Vurugu hizo pia zilisababisha baadhi ya watu kuamua kuharibu madaraja
mbalimbali likiwamo lile la Mikindani linalounganisha Mkoa wa Mtwara na
Lindi.
Hatua hiyo indaiwa kufanywa kwa lengo la kuzuia watu hasa polisi kutoingia mkoani humo.
Kifo
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula, Mohammed Kodi,
amethibitisha kupokea maiti moja na majeruhi ambao hata hivyo hakuweza
kutaja idadi yake.
“Ndugu yangu, hivi sasa tupo katika wakati mgumu, siwezi kukuambia ni
wangapi wamejeruhiwa ila kifo kilichotokea ni cha mtu mmoja, nitafute
baadaye,” alisema.
Huduma za kijamii
Huduma za usafiri, maduka, masoko na hospitali nyingine zilifungwa
kuhofia usalama wa watoa huduma kwa jamii au wale waliokuwa wakienda
kupata huduma husika.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na Tanzania Daima walisema majira ya
saa10 jioni askari walijikusanya katika eneo la Mkana Red na kuanza
kuchoma moto vibanda vya wafanyabiashara katika eneo hilo hali
iliyosababisha wananchi kuanza kyujikusanya kwa ajili ya kutaka
kupambana nao.
Polisi hao wanadaiwa baada ya kumaliza zoezi la kuchoma vibanda vya
wafanyabiashara hao walianza zoezi jingine la kuingia nyumba hadi nyumba
kwa kuvunja milango na kuwatoa wananchi waliojifungia ndani kuepuka
kadhia hiyo na kisha kuondoka nao.
Katika sakata hilo waathirika wakubwa walikuwa kina mama na watoto na
waliosalimika walikimbilia katika Msitu wa Naliendele uliopo karibu na
kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
“Wanataka kutudhibiti kwa mabomu kwa ajili ya kudai gesi itunufaishe,
hii si haki, kwa kweli hatutakubali hali hii, ni bora tufe,” alisema
Merina Almas, mkazi wa Mtwara mjini.
Waandishi Mtwara hofu tupu
Hali ya utendaji kazi kwa waandishi wa habari mkoani Mtwara ilikuwa
ya wasiwasi kuanzia jana asubuhi, baada ya nyumba ya mwandishi wa habari
wa TBC, Kassim Mikongolo, kuchomwa moto kwa madai kuwa mke wake ni
askari anayesaidia kuwalinda watu wanaotaka kutoa gesi mkoani humo.
Makao Makuu ya Polisi waongeza nguvu Mtwara
Kutokana na hali kuwa mbaya mjini Mtwara, Mkuu wa Jeshi la Polisi,
IGP Said Mwema, alilazimika kutuma timu ya maofisa wa jeshi hilo kutoka
makao makuu kwenda kuongeza nguvu.
Kiongozi wa timu hiyo ya kuongeza nguvu mkoani Mtwara, Isaya Mngulu,
aliliambia Tanzania Daima kuwa wanakwenda Mtwara kwa kuwa ni jukumu la
Jeshi la Polisi kuwalinda raia na mali zao.
Naye Mkurugenzi wa Haki za Binadamu wa Chama cha Wananchi (CUF), Hamis
Ismail, alisema waliitegemea hali hiyo, kwa sababu serikali ilishindwa
kuchukua hatua ya kuzuia.
“Hali si shwari, kwani hasira iliyochukuliwa na dola pamoja na raia si
sahihi, walitakiwa wasubiri michango ya wabunge wengine,” alisema
Ismail.
Shule, vyuo vyasitisha masomo
Mkuu wa Shule ya Msingi Shangani, Joseph Kandeo, alisema wameamua
kuwarudisha wanafunzi nyumbani kutokana na hali kutokuwa shwari.
“Hali ni tete, hivyo nimeamua kuwarudisha wanafunzi nyumbani kutokana
na hali iliyopo, nimewaambia kama hali itakuwa nzuri wafike shuleni siku
ya Ijumaa na kama hali ikiendelea hivi wafike shuleni siku ya
Jumatatu,” alisema Kandeo.
Chuo Kikuu Kishiriki cha Stella Maris (Stemmuco) pia waliamua kusitisha masomo kutokana na hali kuendelea kuwa mbaya.
Mkuu wa chuo hicho, Dk. Longino Kamuhabwa, alisema asubuhi hali
ilikuwa nzuri na wananchuo walisoma kama kawaida lakini baadaye hali
ilibadilika.
Wananchi wa Mtaa wa Sinani wamelalamikia polisi kumwaga kitu
kinachodhaniwa kuwa ni unga wa sumu unaowasha katika maeneo ya makazi ya
watu.

Post a Comment