Vibaka waua askari polisi
ASKARI polisi wa kitengo cha usalama barabarani, wilayani
Kahama, Salum Mtepa, ameuawa usiku wa kuamkia jana na watu wanaosadikiwa
kuwa ni vibaka kutoka machimbo madogo ya dhahabu ya Nyangarata na
Mwime, baada ya kumpiga na kitu kizito kifuani.
Tukio hilo lilitokea nyumbani kwake eneo la kata ya Majengo mjini
Kahama usiku wa kuamkia jana baada ya watu hao wanaokadiriwa kuwa wanne
kwenda nyumbani kwa askari huyo mwenye cheo cha Staff Sajenti na kuvunja
kibanda cha biashara kwa lengo la kuiba ndipo askari huyo alipotoka nje
kwenda kupambana nao.
Inadaiwa kuwa baada ya kutoka nje vibaka hao waliokuwa na pikipiki,
watatu kati yao walikimbia akabaki mmoja aliyekuwa na kifaa ambacho
hutumiwa na wachimbaji wa dhahabu katika machimbo madogo madogo kwa
ajili ya kuvunjia miamba ya mawe ambacho hujulikana kwa jina la Moko.
Kwa mujibu wa taarifa ya mkuu wa polisi wilaya ya Kahama, George
Simba, askari huyo alipigwa na kifaa hicho kifuani wakati akijaribu
kupambana na kibaka huyo, hali iliyosababisha avuje damu nyingi ndani ya
kifua na kusababisha kifo chake.
Simba alisema hali ya vibaka katika mji wa Kahama ni mbaya kwani
wameongezeka kutokana na machimbo ya Nyangarata kujaa maji na Mwime
kuisha uzalishaji wake, hali iliyofanya vijana wengi kutoka kwenye
maeneo hayo kutokuwa na fedha.
Alisema hivi sasa wimbi la vibaka hao limekuwa tishio huku akiahidi
kupambana nao pia kuwasaka kwa nguvu zote waliohusika na kifo cha askari
huyo wa usalama barabarani, ingawa hadi jana hakuna mtu yeyote
aliyekuwa amekamatwa kuhusiana na tukio hilo.

Post a Comment