Kajala ajutia kumdharau mama yake.
MSANII maarufu wa filamu nchini, Kajala Masanja juzi alimwaga
chozi kwa madai ya kujutia utovu wake wa nidhamu aliokuwa akimwonesha
mama yake mzazi siku zilizopita.
Kajala ametoka kukumbana na kashikashi katika maisha yake hivi
karibuni, baada ya kusota jela takriban mwaka mmoja kutokana na kesi ya
kutakatisha fedha iliyomwandama yeye na mumewe ambaye yuko jela.
Akizungumza katika kipindi cha ‘Take One’ kinachorushwa kila Jumanne
na Clouds Tv, Kajala alisema alipokuwa jela alimkumbuka mama yake kwa
mambo aliyokuwa akimwambia na kuanza kujuta kutokana na mateso
aliyokutana nayo huko.
“Mimi nilianza kumkumbuka sana mama yangu alivyokuwa akiniusia
kutulia, ila mimi natoroka nyumbani nakwenda ninakotaka na kumuacha
katika huzuni, ila nilipokaa jela niliona nini umuhimu wa mama, namuomba
anisamehe sikujua nilitendalo,” alisema Kajala
Aidha, Kajala alisema katika familia yao, mama yake alikuwa ni mkali
kuzidi baba yake, ambaye kila kitu walichotaka kufanya aliwaruhusu,
ikiwa ni pamoja na kwenda katika majumba ya muziki, lakini mama yao
alikataa na kudai sasa anatambua umuhimu wake.
Aliwashukuru wote ambao walikuwa naye bega kwa bega hadi kufanikisha
kutoka jela, huku shukrani za pekee akizimwaga kwa msanii mwenzake Wema
Sepetu ambaye alimnusuru kufungwa jela miaka saba kwa kumlipia faini ya
sh milioni 13.


Post a Comment