Kinana, Nape wazomewa
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdalrahman Kinana na
Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Nape Nauye, wamezomewa na kulazimika
kumaliza mapema mkutano wao katika mji wa Ruaha wilayani Kilosa baada ya
kushindwa kujibu maswali ya wananchi.
Kuzomewa kwa Kinana na kundi la viongozi wenzake alilofuatana nalo
kulitokana na maswali matatu ya msingi yaliyoulizwa na wananchi,
likiwamo aliloulizwa moja kwa moja yeye kuwa anajisafisha vipi kwa
Watanzania wakati kampuni yake inatuhumiwa na kuhusishwa na utoroshwaji
wa pembe za ndovu kwenda nje ya nchi.
“Mkuu, wananchi hatujaelewa nini unataka kutudanganya wakati wewe
kupitia kampuni yako ya usafirishaji unatuhumiwa kutorosha pembe za
ndovu nje ya nchi. Hapa kuna tatizo sugu la maji safi na salama kwa
miaka mingi na serikali ya chama chako imekuwa inakuja na kutoa ahadi
zisizotekelezeka.
“Sasa umekuja na staili gani mpya kutudanganya? Mji huu ni mkubwa,
ajabu hauna hata zahanati, unasemaje?” alihoji Francis Leonard, huku
akishangiliwa.
Kinana alionesha kuchanganywa na maswali hayo na kujikuta akijibu
pasipo wananchi kuridhika, jambo lililoamsha yowe na minong’ono ya chini
kwa chini wakisema: “Hawana jipya hawa.”
“Kwanza, nikupongeze kijana. Nadhani umetumwa, lakini kwa kifupi ni
kwamba kama kuna mtu mwenye ushahidi na hayo aende mahakamani,”
alifafanua Kinana kabla hajashauriwa kutelemka na kuachana na hoja hizo.
Kutelemka kwa Kinana kukatoa nafasi kwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Wilaya ya Kilosa, Amel Nahadi na Diwani wa Kata ya Ruaha, Rahel
Nyangasi, kujibu swali lililohusu hatima ya usugu wa tatizo la maji na
zahanati katika mji huo.
Amel alisema tatizo la maji lilitokana na wananchi kuiba pampu ya maji
kwenye chanzo, jibu lililopingwa kwa kelele nyingi na wananchi hao
wakilazimisha naye kushuka jukwaani.
“Mkubwa, kwa kuwa mpo hapa na mna vyombo vya usafiri twendeni hapo
kwenye chanzo, huyu mwenyekiti akawaoneshe pampu iliyofungwa na kuibiwa
kwa siku moja. “Tuachane na uongo wakati watu tunaumia…sisi tunataka
maji, leo tuibe pampu kivipi? Kwani eneo hilo halina mlinzi?” ilisikika
sauti ya mtu mmoja na wengine kushangilia.
Baada ya Amel kumaliza, zomeazomea hizo zikahamia kwa Diwani Rahel,
ambaye aliimbiwa wimbo wa ‘fisadi…fisadi…fisadi’, hivyo akalazimika
kujibu kwa kifupi kuwa zahanati inaanza kazi Aprili 15 mwaka huu, kisha
akashuka haraka.
Akionesha kukasirishwa na hali hiyo, Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa
Morogoro, Innocent Kalogelis, alihitimisha mkutano huo akitoa agizo kwa
viongozi wa serikali wa mkoa na wilaya wakiwamo Kamanda wa Polisi wa
mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na Mkuu wa
Wilaya ya Kilosa kuhakikisha
mji huo unatawalika, vinginevyo waondoke.
Kauli ya Kalogelis iliwafanya wakazi wa mji huo kumtamkia kuwa
hawatishwi na utawala wa kiimla wa chama hicho, huku wakimtaka
akajitafakari juu ya matamshi yake.
Katika hali ya kushangaza, baada ya Kinana na viongozi wenzake
kuondoka wakielekea Ifakara, wananchi hawakutaka kutawanyika kwenda
makwao, bali waliendelea kumsubiri Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) mkoani humo, Susan Kiwanga.
Hatua hiyo ilikuwa ni baada ya kusikia kuwa atapita katika ofisi za
chama hicho katani hapo kwa shughuli za kichama akielekea nyumbani kwa
wazazi wake Ifakara.
Akiwa amepigwa butwaa kukuta watu wengi wakimsubiri, Kiwanga aliingia
ofisini kwa muda mfupi na viongozi wa chama wa Kata ya Ruaha na
alipotoka nje wananchi hao walimtaka apande jukwaani awahutubie,
wakitaka kujua yaliyojili bungeni.
“Ndugu zangu kwanza niwashukuru kwa heshima hii, ila mkusanyiko huu
hatuna kibali,” alisema lakini wananchi walipaza sauti wakimtaka apande
jukwaani huku wakimhakikishia ulinzi.
“Tunataka kusikia maneno ya hekima kutoka kwako, tunakuhakikishia kuwa
kama wanataka kushuhudia vurugu leo walete polisi wao…kwanza
tumechoshwa na utawala wao wa kiimla. Sema mama kuhusu hali ya bungeni,”
walimshwawishi.
Kiwanga alikubali ombi hilo, ambapo alisema kwa sasa hali si shwari
bungeni na kwamba utawala wa nguvu ndio umedhihirika baada ya Spika kwa
makusudi kuwabana wapinzani.
CHANZO TANZANIA DAIMA

Post a Comment