ad

ad

Polisi kuhojihoji waandishi kunaashiria nini?

Kwa muda mrefu sasa gazeti hili limekuwa likichapisha habari za Jeshi la Polisi kuwahoji waandishi wa habari kuhusu baadhi ya habari ambazo wamekuwa wakiziandika na hatimaye kuchapishwa au kutangazwa na vyombo vya habari.
Sisi tumegundua kwamba habari zinazolisukuma jeshi hilo la polisi kuwahoji waandishi hao ni zile zilizo mwiba kwa Serikali, licha ya zile zinazohusu matukio ya kihalifu ambazo jeshi hilo linahisi yalisababisha uvunjifu wa amani.

Kwa mfano, habari za maandamano yanayodaiwa kutokuwa na vibali yanayofanywa na makundi mbalimbali kupinga maamuzi au sera mbalimbali za Serikali hufanya jeshi hilo kuwakamata waandamanaji na viongozi wao na kuwafungulia mashtaka.
Katika kufanikisha jambo hilo, jeshi hilo pia huwahoji waandishi wa habari za matukio hayo kwa madai ya kupata ushahidi dhidi ya watuhumiwa. Kwa upande mwingine, jeshi hilo huwahoji waandishi kwa kuwatuhumu kwa uchochezi, kwa maana kwamba habari walizoziandika ziliwachochea wananchi kuvunja sheria.

Habari tuliyochapisha jana kuhusu baadhi ya waandishi wa habari mkoani Mtwara kuanza kuhojiwa na Jeshi la Polisi kuhusu maandamano yaliyofanywa na wananchi kupinga gesi kusafirishwa kwenda Dar es Salaam ni mwendelezo wa utamaduni wa jeshi hilo kuwasakama waandishi wa habari kutokana na habari wanazoziandika.
Ikumbukwe kwamba vurugu hizo zilitokea Januari 26 mwaka huu na kuendelea katika nyakati tofauti, hata kusababisha baadhi ya watu kupoteza maisha, kuchoma moto ofisi za Serikali na nyumba za baadhi ya viongozi, wakiwamo wabunge.

Jeshi la Polisi sasa linawatuhumu baadhi ya waandishi kuhusika na uchochezi unaodaiwa kusababisha vurugu hizo. Waandishi waliohojiwa hadi juzi ni pamoja na watangazaji watatu wa Redio Pride FM wanaodaiwa kuendesha vipindi mbalimbali vya uchochezi na kuwahamasisha waandamanaji kufanya vurugu. Mahojiano hayo yanaelezwa kuendeshwa na makachero kutoka Makao Makuu ya Polisi, jijini Dar es Salaam.

Kama tulivyosema hapo juu, idadi ya waandishi waliohojiwa katika miezi ya hivi karibuni na wanaoendelea kuhojiwa hivi sasa kuhusu habari walizoziandika ni kubwa. Hata hivyo, yafaa tu kusema hapa kwamba lengo la mamlaka zinazosimamia na kuendesha vitendo hivyo dhidi ya waandishi wa habari ni kuwavuruga na kusababisha hofu ili habari zisizoifurahisha Serikali zisiandikwe au kutangazwa.

Kinachoonekana hapa ni ajenda ndani ya Serikali inayolenga kudhoofisha na kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari, ikiwa ni pamoja na kuzuia haki ya wananchi kupata habari. Serikali ingetaka ivinyamazishe vyombo vya habari visiandike na kutangaza habari za wananchi kuandamana kupinga sera au miradi fulani hadi yenyewe itakapotoa taarifa rasmi.
Katika mazingira kama hayo, vyombo vya habari vinatazamiwa tu kunukuu taarifa rasmi za Serikali badala ya kufanya uchunguzi huru na kuwaonyesha wananchi pande zote mbili za shilingi. Hata hivyo, uandishi wa aina hiyo umepitwa na wakati, kwani wananchi wana uelewa mpana zaidi wa kuhoji na kutaka kupata majibu sahihi.

Tungetaka kutoa hadhari kwa waandishi wote wa habari nchini kwamba taaluma yetu iko kitanzini. Mkakati huu wa dola wa kuhoji waandishi kuhusu habari walizoziandika una lengo la kuwataka kwanza wawaone wakuu wa wilaya, mikoa na Usalama wa Taifa kabla hawajachapisha na kutangaza habari zao. Mkakati huo ni wa kishetani. Tuukatae kwa ujumla wetu.
NI MAONI YA Maoni ya Mhariri
Powered by Blogger.