Yanga yaenda Moro bila Niyonzima
KIKOSI cha wachezaji 20 wa vinara wa Ligi Kuu ya Vodacom, Yanga
Sc, kimeondoka jana mchana kwenda mjini Morogoro, huku nyota wake wa
kimataifa, Haruna Niyonzima, akikosekana.
Yanga imekwenda mjini humo kwa ajili ya mchezo wake wa ligi hiyo dhidi
ya wenyeji, maafande wa Polisi Morogoro utakaopigwa kesho kwenye dimba
la Jamhuri mjini humo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Yanga, Baraka
Kizuguto, alisema kwamba Niyonzima ambaye yuko kwao nchini Rwanda,
anakabiliwa na matatizo ya kifamilia.
Alisema mbali na Niyonzima, wachezaji wengine wanaobaki ni wagonjwa na
majeruhi ambao ni Ladislaus Mbogo, Salum Telela, Omega Seme, Mohammed
Saidi, George Banda na Rehani Kibingu.
Baraka aliongeza kuwa kabla ya kuondoka jana asubuhi walifanya mazoezi ya kawaida chini ya kocha Ernie Brandts.
Alisema wachezaji wote wako katika hali nzuri na wamepania kushinda
mchezo huo ili kuzidi kujiimarisha kileleni, sambamba na kuongeza
matumaini yao katika harakati za kusaka ubingwa.
“Tunajua mchezo utakuwa na ushindani mkubwa, kwani polisi si timu ya
kubeza na hasa ikizingatiwa wanacheza nyumbani, kikubwa ni kwamba
tumejipanga kushinda mechi zetu na kuondoka na pointi tatu,” alisema.
Mechi nyingine za ligi hiyo zitakazopigwa ni Ruvu Shooting
itakayoikaribisha Azam Fc katika dimba la Mabatini, African Lyon
itapepetana na Coastal Union katika uwanja wa Azam Chamazi jijini Dar es
Salaam na Kagera Sugar watakawakaribisha Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa
Kaitaba mjini Bukoba.
Yanga inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 48, ikifuatiwa na Azam Fc
yenye pointi 40 na Simba Sc ikishika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 34.

Post a Comment